Saturday 27 September 2014

UMUHIMU WA KUJIFUNZA SAIKOLOJIA




HUWEZI hata kidogo kutenganisha maisha ya mwanadamu na elimu ya saikolojia, elimu ambayo katika ulimwengu wa sasa wengi wanaisikia lakini ni wachache wanaotambua umuhimu wake, achilia mbali maana ya neno lenyewe.



Injinia wa kwanza aliyeipa nguvu elimu hii ni mwanasaikolojia wa Kijerumani, Wilhelm Wundt ambaye alifungua maabara iliyokuwa ikifanya utafiti na kutibu watu kwa kisaikolojia, zoezi ambalo lilileta matokeo ya kushangaza ulimwenguni. Huo ulikuwa mwaka 1879.
Saikolojia ni ‘mtoto’ wa neno la Kigiriki lijulikanalo kama ‘psyche’ au akili na roho jina ambalo baadaye lilikuzwa na kufahamika kama Psychology, tafsiri ikiwa ni Elimu ya Nafsi na Ufahamu.
Katika nchi zilizoendelea, somo hili linapewa nafasi ya juu katika maisha ya binadamu kutokana na umuhimu wake. Wanasema wataalamu kuwa, kuishi 



bila kujua tabia za vitu na watu, ukuaji wake na kujifunza mabadiliko yake ni sawa na kutembea katika kamba ndogo ya maisha salama.
Saikolojia ni somo ambalo kila kukicha binadamu anatakiwa kufundishwa kwa vile hakuna anachoweza kukifanya kisiguse akili na nafsi yake. Inashauriwa kwamba ni lazima mtu ajifahamu mwenyewe, awafahamu wengine, mazingira anayoishi na mabadiliko yake.



Maswali ya msingi yenye kumuongoza binadamu vizuri katika maisha yake ni haya; Mimi ni nani, kwa nini niko hivi? Wale ni 80 akina nani, kwa nini wako vile na tunapaswa kuwa vipi baadaye, pamoja na kujiuliza kwa nini vitu vipo kama vilivyo.


Imebainika kwamba, mvutano wa nguvu za dunia na za binadamu huongezeka mara dufu kwa mtu ambaye hajui Saikolojia ya Maisha. Dunia kama sayari na mwanadamu kama kiumbe kila mmoja amekuwa akitengeneza nguvu zake za kumuwezesha kuwepo, huku uzalishaji wa nguvu 

hizo kwa upande mmoja ukikinzana vikali na mwingine, hata hivyo madhara makubwa yamekuwa yakiwakuta binadamu ambao ndani yao kuna uhai.
Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba, ufahamu wa nafsi na akili umebaki kuwa kinga muhimu ya mwanadamu katika ulimwengu huu ambao umekuwa ukibadilika mara kwa mara.



Hatari inayokuwepo kwa baadhi ya binadamu siku hizi hasa wa ulimwengu wa tatu, ni ukosefu wa elimu hii muhimu, jambo ambalo limewafanya watu wenyewe kwa wenyewe kuzalishiana nguvu za kuangamizana na kuiacha dunia ikishinda.



Inahuzunisha pia kufahamu kwamba, mbali na binadamu kushindana na mabadiliko ya ulimwengu na nguvu zake, wengi wao wamekuwa wakipambana na nguvu zao wenyewe ndani ya miili yao bila kujijua, kiasi cha kupoteza maisha.


Tafiti za wanasaikolojia zinaonesha kwamba, asilimia kubwa ya matatizo yanayomwangaisha binadamu yanatokana na yeye mwenyewe au jamaa zake, huku ushahidi ukionesha kuwa hata magonjwa ya kutisha kama ya moyo, kansa, kisukari, vidonda ya tumbo na mengineyo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mawazo ya watu wenyewe.



WENGI kati ya watu wanaosumbuliwa na matatizo yanaoitwa ya dunia ni wale wanaopambana na nguvu zao bila kujua. Kwa kutumia akili zao vibaya, hujitesa kwa kufikiri na kutafsiri vibaya matukio ya kila siku yanayotokea duniani.

Kama nilivyowahi kusema katika moja ya makala zangu nilizochapisha kwenye toleo la kitabu changu cha pili cha saikolojia ni kwamba hakuna kitu kibaya katika ulimwengu kwa asili, isipokuwa mawazo ya mtu mwenyewe.

Kwa mfano, tukizungumzia kufa ambapo watu wengi wanaamini kwamba ni jambo baya, kuna wengine wanaona ni zuri ndiyo maana wapo wanaojiua, na kama tukisema vita ni hatari, bado kuna watu wanafurahia vita kwa vile si wote wanaowahurumia wafao vitani hata kama wataona maiti zao barabarani kwa wingi.

Kama nilivyosema, duniani kuna nguvu mbili, ambazo ni za watu wenyewe na za ulimwengu, hii ina maana kuwa hata mawazo ya mwanadamu ni nguvu na mtu anaposumbukia kuwaza jambo fulani kwa undani kiasi cha kuumiza moyo wake anakuwa anashindana na nguvu zake mwenyewe.

Ifahamike kuwa kadiri mwanadamu anavyozidi kuongeza nguvu ya kufikiri, iwe kwa kukua kimwili, kusoma na kujifunza mambo mengi zaidi, kwa asili anakuwa anaongeza nguvu ambazo asipokuwa makini anaweza kufa akishindana nazo badala ya kuzitumia katika kumsaidia kimaisha.

Kwa mfano, watu kutoka kabila la Wabarabeigi wanaopatikana mkoani Manyara, nchini Tanzania wanaishi maisha ya kuwinda wanyama na kula mizizi ya porini, hawawezi kukaa wakifikiri jinsi ya kupata gari kwa kuwa kwao gari halina maana. Kwao maendeleo ni kuwinda na kuzaliana.
Kwa maana hiyo linapokuja suala la maisha magumu litatokana na ukame na 

wala si ukosefu wa mitaji au kazi. Hawa hawawazi magari kwa sababu hawajajifunza umuhimu wake, hawajui umuhimu wa kuwa na zahanati, hospitali na wala bei ya mafuta haiwasumbui. Lakini kwa Wachaga waliozoea umeme wakikosa huduma hiyo kwao hilo litakuwa ni tatizo kubwa litakalowakosesha usingizi.

Vivyo hivyo, kwa watu waliozoea kutibiwa kwa sindano na vidonge, wakikosa tiba hizo itakuwa rahisi kwao kufa, kwa sababu akili zao zinatafsiri ukosefu huo kama tatizo kubwa kwao, lakini haiwi hivyo kwa Wasukuma wanaoishi maporini kusikokuwa na hospitali za rufaa wala umeme.

Tafsiri ya hili ni nini? Ni fikra zitokanazo na kujua mambo na namna ya kuyawaza. Watu wengi siku hizi wanajua utajiri, wanafahamu nini maana ya afya, wanaelewa umuhimu wa maendeleo lakini siyo wote wenye uwezo wa kukutana na changamoto hizo na kupata matokeo sahihi ya kile wanachokifahamu.

Kwenda hospitali kupimwa na kuambiwa kuwa una Kansa, Ukimwi, Kisukari, Pumu, TB na magonjwa kama hayo, siyo jambo linalowasaidia wengi kwa vile hawajui hatua ya kuelekea kwenye ujuzi huo wa mambo. Hapa ndipo elimu ya saikolojia inapohitajika ili iweze kumsaidia mtu anayejua mambo hayo namna ya kuyakabili, kuyaendeleza na kupata mafanikio.

Jambo la kusikitisha ni kwamba watu wengi wanaofahamu mambo hawafaidiki nayo na pale wanapojaribu kutumia ujuzi wao walioupata shuleni, wanajikuta wanaingia kwenye mapambano ya nguvu ya vile wanavyovifahamu.

Watu wengi leo hawalali usiku kucha wakipambana na yale waliyoyafahamu, utakuta mtu kakonda kwa sababu katambua mpenzi wake si mwaminifu, anakesha akilia bila kujua afanye nini kumaliza tatizo.
Mtu mwingine anakonda kwa sababu ni maskini, hana mtaji na ajabu nyingine kuna wanaosumbukia hata kasoro za maumbile yao ambazo wameumbwa nazo! 


0 comments:

Post a Comment