Saturday 27 September 2014

JINSI YA KUISHINDA HOFU NA NGUVU YA UCHAWI-2



LAKINI jambo baya sana ambalo linawaponza watu wengi ni kwamba wanapogundua kuwa watu fulani ni maadui zao, wao nao huanza kushambulia kwa chuki.
Kufanya hivyo huzifanya nguvu asili zitafutane na kushawishi mawazo yatilie shaka kila kitu kinachojitokeza na hukihusisha na shambulio la mbaya uliyekosana naye adabu.
Hutakiwi kumchukia mtu ambaye unahisi ni adui yako. Unachotakiwa kufanya ni kumpenda na kujipendekeza kwake, ili yeye aone aibu ya kukufanyia ubaya. Usilipe ubaya kwake hata kama ushahidi unaonesha kuwa yeye ndiye aliyekuchongea kwa bosi wako ufukuzwe kazi.
Ukifanya hivi utakuwa umejiokoa na shambulio la adui yako kwa kiwango kikubwa. Nasisitiza upendo! Wanawake mlioolewa wapendeni mawifi zenu, wakwe hata kama mtahisi wana chuki nanyi. Wafanyakazi, wafanyabiashara, pendaneni mkijua kuwa UPENDO ni kinga yenu.
2. UKWELI USEMWE
Hatua inayofuata ambayo saikolojia inahesabu kuwa ni moja ya kinga kubwa zinazoweza kumfanya adui yako asikudhuru ni kumweleza ukweli kuhusiana na mipango yake ya kukuangamiza, hasa ushahidi wa wazi unapokuwepo.
Mtu mbaya anapogundua kuwa amejulikana kuwa yeye ni mbaya, moja kwa moja anakuwa amenyonywa nguvu za kutekeleza mipango yake. Zingatia kipengele cha kwanza cha upendo katika kufikisha ujumbe wako kwake.
 Kwa mfano unapofahamu kuwa wifi yako ndiye anayekuroga, kwanza mpende, kisha mwite na umwambie hivi “wifi yangu nakupenda sana natamani uwe karibu yangu unisaidie katika maisha yangu, lakini sijui kwa nini wewe hunipendi, hivi utajisikiaje kama mimi nikifa au nikiachika?” malizia halafu unyamaze.
Nakueleza ukishamwambia hivyo moja kwa moja atajua kuwa umeshafahamu mipango yake na kitakachotokea akili yake lazima itafute ubaya wako tu ikishakosa ina maana atakuwa amekosa uwezo wa kukufanyia ubaya.
Aidha, hata kama akifanya utashangaa anafanya kwa kiwango cha chini sana kutokana na hofu iliyojengwa kwake na mawazo yake ya kukuonea.
Lakini nasikitika kusema watu wengi hushindwa kunyonya nguvu za maadui zao kwa kueleza ukweli kwa sababu wanatumia jazba na matusi, mfano “wewe kafiri kweli, mema yote haya nakufanyia huoni tu mpaka unataka kuniroga, haya niue na wewe utakufa.” Ukisema hivyo unachochea nguvu zake za kukudhuru.
3. IMANI
Ukitaka kuitafsiri imani kwa maneno mepesi, unaweza kusema ni kukubali na kuyakataa mambo unayoyaona na kuyasikia.  Katika tafsiri hii ichukue akili kama kiini cha maamuzi ya kile unachokiamini.
Siku zote unapotazama kitu epuka sana kufanya kionekane kuwa kinashinda maamuzi na ubinadamu wako.  Kwa mfano umeona damu kwenye mlango wa nyumba yako, kwa nini uwaze kuwa ni uchawi na kwa nini isiwe ni damu ya mijusi iliyomwagika wakati wanagombana? Jiamini wewe na nguvu zako, usiogope mazingira tu.

0 comments:

Post a Comment