Thursday 1 May 2014

WATU BILIONI 2 WANAUMWA HOMA YA INI (HEPATITIS B) DUNIANI, CHUKUA HATUA




Virusi vya Hepatitis baada ya kulishambulia ini.
Ni ugonjwa unaoambukizwa kwa njia ya virusi ambavyo vikishaingia mwilini hushambulia ini kabla ya kugeuka maradhi sugu.
Virusi hivyo vinaitwa HBV (Hepatitis B Virus).
Virusi hivyo husambazwa kwa njia ya damu au majimaji mengine ya mwilini, mfano mate au jasho.

Watu takribani 1,000,000 wanapoteza maisha kila mwaka duniani kote kutokana na ugonjwa wa Homa ya Ini (Hepatitis B).
Watu zaidi bilioni mbili wanaishi na Virusi vya Homa ya Ini (HBV) duniani kote. Hii ni sawa na asilimia 28.5 ya watu wote duniani.
 Zaidi ya watu milioni 400 duniani ni waathirika sugu wa Hepatitis B.


HEPATITIS B INAVYOSAMBAZWA
Katika maeneo hatari zaidi duniani, Virusi vya Hepatitis B (HBV) kwa kawaida husambazwa kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto wakati wa kuzaliwa, au kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine hususan nyakati za utotoni.
Kama ilivyo kwa Ukimwi, Virusi vya Homa ya Ini pia huambukizwa kwa njia ya kujamiiana,
Tafiti za kitaalamu zinaonesha kuwa Virusi vya Hepatitis B ni hatari kuliko hata vya Ukimwi kwa sababu vinaweza kuishi nje ya mwili wa binadamu (yaani nje ya mfumo wa damu) kwa siku saba. Virusi vya Ukimwi (HIV) havina uwezo wa kuishi nje ya mfumo wa damu hata kwa dakika moja.
Kutokana na usugu wa HBV, maana yake ni kwamba kama kirusi kipo kwenye ngozi, kitaendelea kuwa hai kwa siku saba na katika kipindi hicho mtu anaweza kuambukizwa kwa njia ya damu au jasho.
Kwa wastani Kirusi cha Hepatitis B kikishaingia mwilini, hupevuka ndani ya siku 75, hata hivyo upo uwezekano wa kupevuka kati ya siku 30 hadi 180. Ndani ya siku 30 mpaka 60, mtu mwenye HBV anaweza kugundulika kama atapimwa.

DALILI
Watu wengi huwa hawaonyeshi dalili yoyote. Kwa maana hiyo mtu anaweza kuishi na HBV na kusababisha maambukizi kwa wengin bila kugundulika.
Hata hivyo, watu wengine husumbuliwa na homa kali na dalili ambazo hudumu kwa wiki kadhaa. Dalili hizo ni ngozi na macho kugeuka njano. Hii kwa kawaida huitwa Jaundice, yaani homa ya nyongo au manjano.
Dalili nyingine ni mgonjwa kujisaidia mkojo mchafu (mweusi), uchovu wa mara kwa mara, kichefuchefu, kutapika, maumivu ya tumbo na kichwa.
Kwa wagonjwa wengine, Virusi vya Hepatitis B hukua mpaka kusababisha ini kuharibika kabisa kwa ini (cirrhosis of the liver) au saratani ya ini (liver cancer).

KUNDI LIPI NI HATARI ZAIDI?
Asilimia 80-90 ya watoto wachanga ambao huambukizwa katika kipindi cha mwaka wa kwanza tangu kuzaliwa, Ugonjwa wa Ini (Hepatitis B) hukua mpaka kufikia kuwa sugu na hatimaye kifo.
Asilimia 30-50 ambao huambukizwa kabla ya kufikisha umri wa miaka sita, Hepatitis B hukua mpaka kuwa sugu na baadaye ni kifo.
Asilimia 90 ya watu wazima wanaopata HBV, virusi hivyo hutoweka ndani ya miezi sita. Yaani uimara wa ini husababisha virusi hivyo kupotea.
Asilimia tano kushuka chini ya watu wazima wanaopata maambukizi ya HBV, virusi hivyo vya Hepatitis B kugeuka sugu na hatimaye kifo.
Asilimia 15-25 ya watu wazima ambao walipata maambukizi utotoni na hatimaye Hepatitis B kuwa sugu, hufariki dunia kutokana na matokeo ya ini kuharibika kabisa (cirrhosis of the liver) au kwa saratani ya ini (liver cancer).

KINGA IPO
Kinga dhidi ya Hepatitis B iligunduliwa tangu mwaka 1982.
Inashauriwa kwamba kinga ni lazima kwa kila mtoto anayezaliwa.
Ili kupata kinga ya asilimia 100 ni lazima mtu apate chanjo mara tatu.
Chanjo ya kwanza ikishatolewa, ya pili hufuata baada ya mwezi mmoja nay a tatu baada ya miezi sita baada ya dozi ya kwanza.
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), linasisitiza kuwa ni lazima kwa kila aliye na umri chini ya miaka 18 achanjwe mara tatu kinga ya Hepatitis B.
Ni vizuri kwa kila mmoja kwenda kupima na akikutwa yupo salama aweze kuchanjwa.
Hata kwa walio na umri zaidi ya miaka 18, wanaweza kuchanjwa na kuwa salama dhidi ya maambukizi ya Hepatitis B.

TANZANIA IPO KUNDI LA KIFO
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), Kusini ya Jangwa la Sahara ndiyo eneo hatari zaidi. Tanzania ni moja ya nchi zilizopo katika eneo hilo. Kiwango cha hatari Kusini ya Jangwa la Sahara kinalingana na kile cha Mashariki ya Bara la Asia.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa watu wengi walipata maambukizi nyakati za utotoni na kwamba kati ya asilimia tano mpaka 10 ni waathirika sugu.

0 comments:

Post a Comment