Thursday 1 May 2014

SEHEMU YA KWANZA; SHINIKIZO LA DAMU LA JUU (HYPERTENSION)






Si rahisi kwa binadamu yeyote kukubali
ushauri wa daktari pale anapogundulika
amepatwa na ugonjwa wa shinikizo la
damu.



Na, mazoea yanaonyesha kuwa inakuwa
ngumu zaidi pale daktari anapo mshauri
mgonjwa husika kutumia dawa maisha
yake yote, ili kudhibiti madhara yatakanayo
na kupanda kwa shinikizo la damu.



Madaktari hutaja baadhi ya madhara
yatokanayo na kutotibiwa au kutodhibitiwa
kwa ugonjwa wa shinikizo la damu.
Madhara hayo ni kama vile kiharusi, moyo
kushindwa kufanya kazi, matatizo katika
mshipa mkubwa wa damu ambapo ukuta
wa ndani huchanika na damu kukusanyika
katika ukuta wa mshipa huo, magonjwa ya
mishipa ya damu, kushindwa kuona na pia
huathiri ubongo.


Lakini hii ndiyo hali halisi hapa Tanzania na
kwingineko duniani ambako kupanda kwa
shinikizo la damu hudhuru mamilioni ya
watu. Huku takwimu kutoka Shirika la Afya
Duniani (WHO) zikionyesha kwamba mmoja
kati ya watatu duniani ameathiriwa na
ugonjwa huu.


Shinikizo la damu ni msukumo wa damu
kwenye kuta za mishipa. Shinikizo la damu
ni muhimu kwa ajili ya kusukuma damu
katika sehemu zote za mwili, lakini shinikizo
la damu la juu huweza kuleta matatizo na
madhara makubwa kiafya.


Shinikizo la damu la juu (Hypertension) au
presha ya damu ya juu (High Blood
Pressure), pia huitwa shinikizo la mishipa
(Arterial Hypertension) ni hali ya ugonjwa
sugu ambapo nguvu ya msukumo wa damu
katika mishipa inaongezeka.


Ongezeko hilo husababisha moyo kufanya
kazi kupita kiasi ili uzungushe damu katika
mishipa ya damu.
Shinikizo la damu linaweza kupimwa na
kifaa maalumu kinachojulikana kitaalamu
Sphygmomanometer/Sphygmometer/Blood
Pressure Meter

.
Kifaa hiki huonyesha muhtasari wa vipimo
viwili. Kwa mfano kinaweza kurekodi
kipimo cha 110/70. Nambari ya kwanza
huonyesha kipimo cha shinikizo la damu
wakati moyo unapopiga (Systole). Nambari
ya pili huonyesha kipimo cha shinikizo la
damu katikati ya mapigo ya moyo (Diastole).


Shinikizo la damu hupimwa kulingana na
milimeta za zebaki (Millimeter Mercury/
mmHg).
Kipimo cha kawaida cha shinikizo la damu
ni 100-140 milimeta za zebaki (mmHg)
kipimo cha juu (Systolic) na 60-90 milimeta
za zebaki (mmHg) kipimo cha chini
(Diastolic). Shinikizo la damu la juu hutokea
kama kipimo kikiwa zaidi ya 140/90
milimeta za zebaki (mmHg) kwa muda
mrefu.


Ugonjwa huu kwa kawaida huitwa muuaji
wa kimya kimya (Silent Killer) kwa maana
kuwa, mtu anaweza akawa na ugonjwa
huo kwa miaka kadhaa lakini bila kujua,
huku ugonjwa huo ukimletea madhara
makubwa.
Shinikizo la damu kwa kawaida
huongezeka katika kipindi cha miaka
kadhaa na huweza kumpata karibu kila
mtu, lakini huwapata zaidi wenye umri wa
zaidi ya miaka 35.


Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni
(WHO) zinasema tayari watu bilioni moja
duniani kote, wanaathiriwa na shinikizo la
damu la juu likisababisha mshtuko wa
moyo (Heart Attacks)  na kupooza/kiharusi
(Strokes).
Watafiti wamekadilia watu kama milioni
nane hufa kila mwaka kwa kupanda kwa
shinikizo la damu.


AINA ZA SHINIKIZO LA DAMU LA JUU


Kuna aina mbili za shinikizo la damu la juu.
Aina ya kwanza ni shinikizo la damu la juu
la asili (Primary/Essential Hypertension) na
aina ya pili ni shinikizo la damu la juu
linalosababishwa na magonjwa mengine
(Secondary Hypertension).


Inakadiriwa asilimia 90-95 ya watu wenye
shinikizo la damu la juu wanaathiriwa na
shinikizo la damu la juu la asili, yaani wana
ugonjwa huu bila kuwa na chanzo cha
kisayansi kinachofahamika.
Shinikizo la damu la juu linalosababishwa
na magonjwa mengine kama ya figo,
mishipa, moyo, mfumo wa homoni huathiri
asilimia 5-10 iliyobaki ya watu wenye
shinikizo la damu la juu.


Sababu nyingi huathiri ugonjwa wa
shinikizo la damu kama wingi wa maji
mwilini, wingi wa chumvi mwilini, homoni,
kiwango cha mishughuliko, hali ya joto au
hali ya baridi, hali ya hisia, hali ya figo,
mfumo wa neva, na mishipa ya damu.


MGAWANYIKO WA SHINIKIZO LA DAMU
KULINGANA NA RIKA/HALI

1.  Watoto waliozaliwa karibuni (Neonates)
& watoto wachanga (Infants).
Sio kawaida kwa watoto waliozaliwa
karibuni kuwa na shinikizo la damu la juu
na ni asilimia 0.2-3 tu ya watoto wachanga
ambao wanapata. Shinikizo la damu
halipimwi mara kwa mara kama watoto ni
wadogo na wana afya mzuri.
Kuna masuala tofauti ya kuangalia, kama
vile kipindi cha ujauzito, umri baada ya
utungaji mimba, na uzito wakati wa
kuzaliwa kabla ya kuamua kama kipimo cha
shinikizo la damu ni cha kawaida kwa
mtoto mchanga.


2. Watoto (Children)

Ni kawaida kwa watoto na vijana kupata
shinikizo la damu la juu (Asilimia 2-9
hutegemea na umri, jinsia na asili) na
huambatana na afya mgogoro/dhaifu.
Hivi sasa kuna pendekezo la kuwapima
shinikizo la damu watoto wenye zaidi ya
miaka mitatu na kuangalia kama wana
shinikizo la damu la juu kila wanapoenda
kupima afya zao.
Shinikizo la damu la juu kwa watoto
huthibitishwa ikiwa wastani wa kipimo cha
juu (Systolic Pressure) au kipimo cha chini
(Diastolic Pressure) vilivyopimwa nyakati
tatu tofauti ni asilimia 95 au zaidi kulingana
na jinsia, umri na kimo cha mtoto.


3.  Vijana (Adolescents)
Kwa vijana, inapendekezwa kwamba
shinikizo la damu la juu la na dalili za
shinikizo la damu la juu zichunguzwe na
kuainisha kwa kutumia vigezo vya watu
wazima.


4.  Watu wazima (Adults)
Kwa watu wenye umri wa miaka 18 au
zaidi, shinikizo la damu la juu linaweza
kuwa kama kipimo hicho ni zaidi kuliko
kipimo cha kawaida kinachokubalika
ambacho ni 139/89 milimeta za zebaki
(mmHg).



5.  Kipindi cha ujauzito (Pregnancy)
Shinikizo la damu la juu hutokea takribani
asilimia 8-10 ya ujauzito. Tunasema
mwanamke ana shinikizo la damu la juu
ikiwa shinikizo la damu yake ni zaidi ya
140/90 milimeta za zebaki (mmHg)
lililopimwa kwa nyakati tofauti
zinazotofautiana masaa 6.
Wanawake karibu wote wenye shinikizo la
damu la juu wakiwa na mimba
walishakwisha umwa na shinikizo la damu
la juu la kawaida.
Hali hiyo ikitokea katika ujaizito ni dalili ya
kwanza ya kifafa cha mimba kabla
hakijashikika kabisa.


Maradhi hayo hutokea katika kipindi cha
miezi mitatu ya pili ya ujauzito (Second
Trimester) na majuma machache baada ya
kujifungua.
Uaguzi wa maradhi hayo ni pamoja na
shinikizo la damu kuongezeka na dalili za
protini ndani ya mkojo.
Maradhi hayo hutokea takribani asilimia 5
ya ujauzito yakisababisha takribani asilimia
16 ya vifo vya wenye ujauzito.

MAKALA HII ITAENDELEA SEHEMU YA PILI TUTAANZA KUANGALIA NINI SABABU ZA SHINIKIZO LA DAMU NA JINSI YA KUEPUKANA NA SABABU HIZO!!!!!!!

0 comments:

Post a Comment