Friday 2 May 2014

MAGONJWA SUGU YASIYO YA KUAMBUKIZA ILI UJIEPUSHE NAYO-2

 
 
Shinikizo kubwa la damu
Shinikizo kubwa la damu hutokea pale panapokuwa na ongezeko la nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa inayochukua damu kutoka kwenye moyo kwenda kwenye viungo na tishu mwilini.
Ukubwa wa shinikizo kubwa la damu hutegemea wingi na nguvu ya msukumo wa damu kutoka kwenye moyo na ukubwa wa mishipa inayopeleka damu mwilini.
 
Viwango vinavyoashiria shinikizo kubwa la damu mwilini .
Blood pressure machine (sphignomanometer) hutumika kupima shinikizo kubwa la damu.Kipimo kinachochukuliwa kuwa ni kawaida ni 120/80 mmHg au chini yake.
Kiwango kinapokuwa 140/90 mmHg au zaidi hali hiyo huwa ni shinikizo kubwa la damu.Ikumbukwe kuwa panaweza kuwepo tofauti kati ya mtu na mtu.
 
Viashiria hatarishi vya shinikizo kubwa la damu
Historia ya shinikizo kubwa la damu katika familia, Umri wa zaidi ya miaka 40, Jinsi ya kiume (huwapata wanaume zaidi kuliko wanawake),Uzito uliozidi kiasi, Msongo wa mawazo, matatizo mengine ya kiafya mwilini kama magonjwa ya figo, matatizo ya mishipa ya damu, magonjwa ya moyo, matatizo ya vichocheo mwilini, kisukari au saratani.Matumizi ya baadhi ya dawa na Kutokufuata mtindo bora wa maisha.
 
Dalili za shinikizo kubwa la damu:
Kichwa kuuma mara kwa mara hasa sehemu ya kisogo, Kizunguzungu, Kutokwa kwa damu pumuani, Maumivu ya kifua, Moyo kwenda kasi wakati umepumzika, Kushindwa kufanya mazoezi kwa kushindwa kupumua, Mapigo ya moyo kushuka wakati umepumzika, na Uchovu wa mara kwa mara.
 
Ulaji unaoshauriwa kwa mtu mwenye shinikizo kubwa la damu:
• Kuepuka vyakula venye chumvi nyingi, ikiwa ni pamoja na vile vilivyosindikwa kwa chumvi
• Kutumia viungo mbalimbali kuongeza ladha ya chakula( vitunguu swaumu, tangawizi, mdarasini, )
• Kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi
• Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku ukizingatia kula vyakula vya aina mbalimbali
• Kula matunda na mbogamboga kwa kiasi cha kutosha katika kila mlo
• Kutumia nafaka zisizokobolewa na vyakula vya jamii ya kunde kwa wingi.
 
Mbinu za kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo kubwa la damu
• Kuepuka vyakula venye mafuta mengi, sukari na chumvi nyingi
• Kuepuka mafuta yenye asili ya wanyama
• Kuepuka vyakula vyenye lehemu kwa kiasi kikubwa
• Kupunguza kiasi cha nyama unachokula hasa nyama nyekundu
• Kuepuka kuwa na uzito uliozidi
• Kuepuka matumizi ya pombe sigara na tumbaku
• Kudhibiti msongo wa mawazo na
• Kufanya mazoezi kila siku
 
Shinikizo kubwa la damu wakati wa ujauzito
Mjamzito mwenye shinikizo kubwa la damu ni mhimu kuhudhuria kiliniki mara kwa mara kufuatilia hali yake, kutumia dawa za kupunguza shinikizo kubwa la damu kama atakavyoelekezwa na mtaalamu wa afya, kufuatilia kwa makini ongezeko la uzito wa mwili, Kuepuka utumiaji wa pombe na sigara. Mjamzito afuate ulaji unaoshauriwa kwa watu wenye shinikizo kubwa la damu, bila kusahau ongezeko la mahitaji ya virutubishi kutokana na hali ya kuwa mjamzito.
 
Magonjwa sugu ya njia ya hewa
Aina za magonjwa sugu ya njia ya hewa ni pamoja na ugonjwa wa pumu, saratani ya mapafu, na mengine yanayosababishwa na kemikali zinazotoka katika viwanda vinavyochafua mazingira kwa mfano kiwanda cha saruji, pamba na sigara.
 
Mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Kuvuta sigara, au kukaa karibu na mtu anayevuta sigara, Uchafuzi wa hewa ya ndani na nje, kutokana na vumbi au chavua ya maua, Hewa za sumu na vumbi toka viwandan, Unene uliokithiri, Mara nyingine magonjwa sugu ya njia ya hewa huweza kurithiwa mfano pumu.
 
 
Ushauri wa lishe na ulaji kwa mgonjwa mwenye magonjwa sugu ya njia ya hewa
• Endapo una ugonjwa sugu wa njia ya hewa ni vyema kuzingatia ushauri wa mtaalamu wa afya, matibabu na kufuata kanuni za mtindo bora wa maisha.
• Unashauriwa kula mlo kamili na vyakula vya aina mbalimbali ili upate virutubishi vyote vinavyohitajika kwa afya yako.
• Kula matunda freshi, mboga mboga zenye rangi ya kijani, mboga mboga na matunda yenye rangi ya njano, ili kuimarisha kinga ya mwili wako.
• Unashauriwa pia kula vyakula venye makapi mlo kwa wingi ili kusaidia mfumo wa kusaga chakula kufanya kazi na kutoa uchafu tumboni kwa urahisi, hali hii husaidia kuweza kupumua kwa urahisi.
• kula milo midogo midogo mara kwa mara
• Punguza matumizi ya chumvi ili kuepuka maji kujikusanya mwilini na kusababisha kupumua kwa shida
• Ni muhimu pia kuepuka uzito uliozidi au unene kwani huongeza tatizo la kushindwa kupumua
• Zingatia kuwa na uzito unaofaa kwa kula chakula cha kutosha, mara nyingi mtu mwenye magonjwa sugu ya njia ya hewa huweza kupungua uzito kwa sababu inamlazimu kutumia nguvu (nishati- lishe) kwa kiasi kikubwa wakati wa kupumua.
• Matumizi makubwa ya nguvu husababisha asiwe na nishati- lishe ya akiba ambayo huhifadhiwa mwilini na kufanya mtu huyo kuwa mwembamba
Pamoja na ushauri wa lishe mgonjwa huyu anashauriwa:
• Kuepuka visababishi na vichochezi kama vile vumbi, kuvuta sigara, chavua, hasira, pombe na harufu kali
• Kuhakikisha mazingira na nyumba ni safi na pia iwe na madirisha yanayoruhusu mzunguko wa hewa.
Jinsi ya kuzuia magonjwa sugu ya njia ya hewa
Epuka kuvuta sigara, Epuka kukaa na mtu anayevuta sigara kwa kuzuia mtu kuvuta sigara nyumbani na ofisini, Inapaswa kuzuia uvutaji wa sigara kwenye maeneo ya watu kama hotelini, vituo vya usafiri, kwenye vyombo vya usafiri, hosipitali, shuleni, vyuoni, ofisini, sokoni n.k, Epuka kuchafua mazingira hasa hewa tunayovuta.
 
Uchafuzi wa hewa nje na ndani ya nyumba hudhibitiwa kwa kufanya 
 
yafuatayo
 
a) Nje ya nyumba
• Usiwashe gari na kuiacha kwa muda mrefu bila kuizima kama haitumiki
• Epuka kutumia dawa ya kuua wadudu shambani na kemikali nyingine kuwepo karibu na nyumba yako hasa sehemu za bustani na zile za kukaa watu
 
b) Ndani ya nyumba
• Dhibiti hali ya unyevu hasa jikoni, chooni, na bafuni, hakikisha sakafu, sinki na meza ni safi na kavu.
• Hakikisha vifaa kama kiyoyozi, feni, heater vinasafishwa mara kwa mara.
• Dhibiti vumbi na manyoya ya wanyama kama paka kwa kusafisha kikamilifu sehemu kama sakafu, kabati, magodoro, makochi, mito na matandiko ambayo hayapitishi hewa ya kutosha.
• Shuka na blanketi zifuliwe kwa maji ya moto na mazulia yasafishwe mara kwa mara na yawe makavu ili kuua wadudu
• Hakikisha madirisha ni mapana kuweza kupitisha hewa ya kutosha na yafunguliwe kila siku ili kupitisha hewa
• Hakikisha nyumba ipo wazi ( milango na madirisha) wakati wa kufanya usafi, kupakaa rangi au shughuli nyingine kubwa

0 comments:

Post a Comment