Friday 2 May 2014

MAGONJWA SUGU YASIYO YA KUAMBUKIZA ILI UJIEPUSHE NAYO.

.


Magonjwa makuu sita yasiyo ya kuambukiza ni pamoja na: Ugonjwa wa kisukari, Magonjwa ya moyo, Shinikizo kubwa la damu, Saratani, Magonjwa ya figo na Magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Sababu zinazopelekea kuwepo kwa magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza:
Mtindo wa maisha usiofaa unapelekea mtu kupata magonjwa sugu yasiyo ya kuambukiza, mtindo huu wa maisha usiofaa unahusisha mambo yafuatayo: ulaji usiofaa; kutofanya mazoezi ya mwili; matumizi ya sigara na bidhaa zitokanazo na tumbaku; matumizi ya pombe; na msongo wa mawazo.

Ugonjwa wa Kisukari.
Ugonjwa wa kisukari ni hali inayotokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu inayotokana na kongosho linaposhindwa kutengeneza kichocheo cha insulin, au insulin iliyopo katika damu kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
Kichocheo cha insulin ndicho kinachotumika kudhibiti kiwango cha sukari katika damu. Kichocheo hiki ni muhimu sana katika kufanya sukari iweze kutumika mwilini ili kupata nishati lishe.
Ugonjwa wa kisukari unapompata mtu huwa ni wa kudumu, hivyo anahitaji kufuata taratibu za matibabu na maelekezo atakayopewa na mtoa huduma wa afya kwa maisha yake yote.
Aina za kisukari:
Kuna aina kuu mbili za kisukari ambazo ni :
·        Kisukari kinachotegemea insulin ( type 1 diabetes)
·        Kisukari kisichotegemea insulin ( type 2 diabetes)
Kuna aina nyingine ya kisukari ambayo huweza kujitokeza wakati wa ujauzito (Gestational diabetes.)
Kisukari kinachotegemea insulin:
Huwapata zaidi watoto na wenye umri chini ya miaka 35. Katika aina hii ya kisukari seli za kongosho zinazotengeneza insulin huwa zimeharibika hivyo kusababisha ukosefu au upungufu wa insulin mwilini.
Kisukari kisichotegemea insulin
Huwapata zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea. Katika aina hii ya kisukari insulin ya kutosha inaweza ikatengenezwa katika kongosho lakini haifanyi kazi hivyo mwili kushindwa kutumia sukari kwa ufanisi.
Kisukari cha mimba
Ni aina ya kisukari kinachotokea kwa baadhi ya wanawake wakati wa ujauzito.Hali ya ujauzito husababisha ongezeko la baadhi ya vichocheo Kama Progesterone, Estrogen, na free Cortisol ambavyo huongeza kiwango cha sukari katika damu.
Wakati huohuo kichocheo cha Human Placental Lactogen huzuia insulin kufanya kazi kwa ufanisihivyo kusababisha kiwango cha insulin kuongezeka katika damu.
Mwili unaposhindwa kutengeneza insulin ya kutosha kupambana na ongezeko la sukari katika damu kisukari cha mimba hutokea. Mara nyingi hutokea mimba ikiwa na umri wa miezi mitano au zaidi na kwa kawaida huishawiki sita baada ya mwanamke kujifungua.
Viashiria hatarishi vya kupata ugonjwa wa kisukari
Kisukari kinachotegemea insulin
Kurithi katika familia, Magonjwa ya kongosho (kama saratani au uambukizo) ambayo huweza kuua seli za kichocheo kinachotengeneza insulin, kupewa maziwa mbadala (ya kopo au ya wanyama) au kumnyonyesha mtoto kwa muda mfupi, Mtoto akizaliwa na uzito mkubwa kupita kiasi, Unene au uzito mkubwa utotoni.
Kisukari kisichotegemea insulin
Uzito uliozidi au unene uliokithiri, Shinikizo kubwa la damu, Mtindo wa maisha usiofaa hususani kutofanya mazoezi, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, na uvutaji sigara na bidhaa za tumbaku, Kuwepo kwa historia ya kisukari katika familia, Umri zaidi ya miaka 45.
Kisukari cha mimba
Kuwepo historia ya kuwa na kisukari katika familia, Kuwahi kujifungua mtoto mwenye uzito mkubwa, Mimba kuharibika mara kwa mara, Historia ya kisukari cha mimba, Mkojo kuwa na sukari mara kwa mara, Kuzaa mtoto mfu, Uzito au unene uliokithiri, Shinikizo kubwa la damu la muda mrefu, Umri zaidi ya miaka 35.
Dalili za ugonjwa wa kisukari
Dalili za ugonjwa wa kisukari ni pamoja na:Kukojoa mara kwa mara, Kuhisi kiu sana, Kuhisi njaa sana, Kuhisi uchovu wa mwili na kukosa nguvu bila ya kufanya kazi ,Kupungua kwa uzito wa mwili na kuwa mdhaifu, Kutoona vizuri,Kuhisi kizungu zungu ,Baadhi ya viungo vya mwili kama vidole vya mikona na miguu kufa ganzi .
Ushauri wa ulaji Kwa mgonjwa wa kisukari
Kula mlo kamili angalau mara tatu kwa siku, haishauriwi kukaa na njaa kwa muda mrefu.
• Kudhibiti kiasi cha nishati- lishe katika chakula, kiasi kinategemea mahitaji ya mtu binafsi.
• Kuongeza ulaji wa vyakula venye makapi mlo kwa wingi, kiasi kikubwa cha nishati lishe kitokane na vyakula venye makapi mlo kwa wingi ambavyo huyeyushwa na kufyonzwa mwilini taratibu na hivyo kasi ya kuongezeka kwa sukari katika damu hupungua.
• Kupunguza kiasi cha mafuta, epuka mafuta yenye asili ya wanyama na punguza kiasi cha mafuta mengine.
• Epuka sukari na vyakula venye sukari nyingi kama vile soda, keki, biskuti, pipi, na asali, asilimia 80 ya asali ni sukari
• Epuka kunywa pombe, pia haishauriwi kunywa pombe kali kwani huleta madhara kwenye ini, usinywe pombe kabla ya kula chakula kwani huweza kusababisha damu sukatiti ( hypoglycemia
• Kula tunda katika kila mlo, ikiwezekana usimenye tunda na zingatia usalama wa chakula.
• Kula mboga mboga kwa wingi katika kila mlo, chagua mboga mboga ambazo hazina kabohaidreti kwa wingi mfano mboga za majani , nyanya matango, na saladi.
• Kupunguza uzito kama umezidi au dhibiti uzito wa mwili, ni vyema kuwa na uzito unaoshauriwa kulingana na urefu wake.
• Kupanga utaratibu wa kula chakula na matumizi ya dawa, kwa mgonjwa wa kisukari anayetumia dawa ni muhimu kupanga utaratibu maalumu wa kula na kumeza dawa ili kuzuia kupungua kwa sukari katika damu
.
• Epuka kukaa kwa muda mrefu bila kula chakula.

0 comments:

Post a Comment