Thursday 9 October 2014

NJIA 4 ASILIA ZA KUDHIBITI PRESHA YA KUPANDA (HIGH BLOOD PRESSURE)



LICHA ya kusababisha vifo vingi duniani ikiwemo Tanzania, shinikizo la damu (High Blood Pressure), inaelezwa na wataalamu kuwa ndiyo chanzo cha magonjwa mengine hatari ya moyo, kiharusi na figo. Hata hivyo ugonjwa huu unaweza kuzuilika na kutibika kwa njia asilia, mbali na matibabu ya kawaida.
POTASIAMU MWILINI
Ulaji wa mboga na matunda yenye kiwango kingi cha Potasiamu (Potassium) ni sehemu muhimu sana katika mikakati na mipango anayoweza kuwa nayo mtu ya kudhibiti au kushusha kiwango cha shinikizo la damu alichonacho, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa wa Tiba za Kinga, Dk. Linda Van Horn wa Chuo Cha Tiba cha Feiberb.
Profesa huyo anasema kuwa ulaji wa Potasiamu kati ya miligramu 2000  na 4000 kwa siku kutasaidia kushusha kiwango cha shinikizo la damu kwa kiasi kikubwa. Vyakula vinavyoaminika kuwa na kiwango kingi cha Potasiamu ni viazi vitamu, maharagwe, nyanya, juisi ya machungwa pamoja na karanga na korosho.
KUWA MAKINI NA CHUMVI
Baadhi ya makundi ya watu yanayougua ugonjwa wa shinikizo la damu, ulaji wa chumvi kiasi chochote huwa na athari mbaya kwao, hasa wale wenye historia ya kifamilia ya kuugua ugonjwa huu.
Kwa kuwa siyo rahisi mtu mwenye shinikizo la damu kujitambua kama chumvi ina muathiri zaidi, inashauriwa kila mtu kupunguza matumizi ya chumvi katika vyakula vya kila siku.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya lishe ya moyo na mapafu, Dk. Eva anasema kuwa kiwango cha chumvi cha wastani anachotakiwa kutumia mtu kwa siku kisizidi miligramu 1,500. Kipimo hicho ni zaidi kidogo ya kijiko kimoja cha chai ambacho huwa na miligramu 1200. Kwa maana nyingine, matumizi ya mtu kwa siku nzima katika milo yote hayatakiwi kuzidi kijiko kimoja na nusu cha chai.
ULAJI WA CHOKOLETI
Aina nyingi za chokoleti (Chocolate) zina aina ya kirutubisho (flavanols) kinacholainisha mishipa ya damu na kuwezesha damu kutembea vizuri mwilini. Katika utafiti mmoja, asilimia 18 ya wagonjwa wa presha waliokula chokoleti walionesha kupata ahueni kwa presha kushuka. Kiasi cha chokoleti moja kinatosha kwa siku, muhimu iwe inayotengenezwa kutokana na Cocoa.
TATIZO LA KUKOROMA USIKU
Kwa mujibu wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Alabama nchini Marekani, watu wengi wenye tatizo la kukoroma usiku, wana homoni ijulikanyo kama ‘aldosterone’ ambayo huongeza shinikizo la damu na inakadiriwa kuwa nusu ya watu wote wenye tatizo la kukoroma wana presha.
Mbali ya kukoroma kama dalili moja wapo ya kuwa na presha kwa baadhi ya watu, kusikia uchovu sana na kizunguzungu asubuhi nako ni dalili moja wapo, hivyo inashauriwa kumuona daktari akushauri kuondoa tatizo la kukoroma ili kujiepusha na matatizo yatokanayo na shinikizo la damu.
Kama hujui hali yako kuhusu  presha, ni vyema ukamuone daktari na kupima sasa.

0 comments:

Post a Comment