Monday 27 October 2014

MAUMIVU YA MAGOTI NA VISIGINO

TATIZO hili huwapata watu wote, maumivu ya magoti yanaweza kuwa makali au yakawa kwa mbali, vilevile magoti yanaweza kuvimba.
Maumivu haya yanaweza kuwa mbele ya goti au nyuma ya goti, maumivu yanapotokea mgonjwa hutembea kwa shida na kushindwa kunyanyuka akiwa amekaa.
Maumivu ya visigino huwa katika kisigino chote na hupanda kwa juu, wakati mwingine maumivu huwa kama sindano. Maumivu ya visigino yanaweza kuwa muda wote au yakatokea kwa vipindi, yaani asubuhi unapoamka inakuwa tabu kukanyaga chini lakini ukishakanyaga kwa muda fulani miguu inazoea na mwendo unakuwa wa kawaida na maumivu yanapungua.
CHANZO CHA TATIZO
Maumivu ya magoti hutokana na sababu mbalimbali, inaweza kusababishwa na kusimama au kutembea kwa muda mrefu ingawa siyo sana, ajali yoyote inayoumiza goti iwe barabarani, kuanguka au michezoni, maambukizi ya bakteria katika magoti kutokana na majeraha pia inaweza kuwa ni sababu.
Chanzo kingine ni ugonjwa wa Gauti, umri mkubwa hasa kwa kinamama pia huchangia uwepo wa tatizo hili pale mama anapofikia ukomo wa hedhi ambapo vichocheo vya ‘Estrogen’ vinaanza kupungua mwilini.
Matatizo haya ya magoti yana vyanzo vingi utakapoenda hospitali utapata ufafanuzi.
Maumivu ya visigino pia hutokea tu, huweza kusababishwa na kuumia hasa michezoni au kuvaa viatu vyenye soli ngumu na ukatembea navyo kwa mwendo mrefu.
Maumivu mengine hutokea nyuma ya mguu chini ya goti na kushuka hadi katika kisigino, husababisha misuli ya nyuma ya mguu kuuma au kukamata, wakati mwingine msuli hututumka kama mwanamichezo.
Hii inatokana na kutembea mwendo mrefu kwa kupanda milima, ngazi hasa ghorofani kama ni ghorofa refu sana na wewe kila siku unatumia ngazi.  Pia kuvaa viatu virefu na kutembea navyo mwendo mrefu.
DALILI ZA TATIZO
Maumivu ya magoti na visigino wakati mwingine huwa hayavumiliki. Maumivu huja na kupotea au huwa makali kwa mfululizo, maumivu yanaweza kutokea kwa kupwita kama ndani kuna jipu, goti linaweza kuwa kavu na kuhisi kabisa kama mifupa inagongana au kusuguana, wakati mwingine linakuwa na joto.
Visigino au nyuma ya miguu kunakuwa na maumivu kama kunawaka moto, ukipumzika na kuweka miguu juu utakuta yanapungua taratibu lakini ukikanyaga tu, yanaongezeka kwa kasi.
UCHUNGUZI
Mgonjwa anaweza kufanyiwa vipimo vya damu, x-ray na uchunguzi mwingine ambao daktari ataona unafaa. Uchunguzi hufanyika katika hospitali za mikoa na wilaya.
MATIBABU NA USHAURI
Magonjwa haya huwa yanatibika endapo mgonjwa atazingatia uchunguzi na matibabu kwa kufuatilia kwa kina.
Dawa zipo aina nyingi, kuna za kupaka, vidonge na sindano, hivyo inategemea uchunguzi unasemaje.

0 comments:

Post a Comment