Saturday 27 September 2014

NJIA YA KUPUNGUZA MAUMIVU WAKATI WA KUJIFUNGUWA MTOTO-2



MTAALAMU Joanne Lally kutoka Chuo Kikuu cha Afya ya Jamii cha Newcastle na timu yake waliweza kubainisha mambo mengi ya msingi kuhusu uzazi salama, lakini kubwa kabisa ni faida za kumfariji mzazi mtarajiwa kabla ya wakati wa kujifungua. Kasoro kubwa ya wakunga na walezi wengi wanaohudumia wajawazito ni kuwavunja moyo na kutowajali, jambo ambalo huchangia matatizo wakati wa uzazi.
Nakumbuka nilimuuliza dada Husna (si jina lake halisi) aliyejifungua hivi karibuni mtoto aliyekufa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam, nini kilimpata wakati anajifungua aliniambia hivi: Nilishikwa na uchungu saa saba mchana, wakati huo mume wangu alikuwa kazini. Majirani wakanikimbiza hospitali ya Mwananyamala. Nilifika nikiwa na maumivu makali ambayo sikuwahi kuyapata, nikawa nalia kuomba msaada wa manesi, lakini hawakunijali kabisa.
“Basi nikawa navumilia, uchungu ulipozidi ndo manesi wakaja, wakawa wananiambia sukuma, sukuma kwa nguvu  huku wananitukana, kusema kweli nilizidiwa na uchungu mpaka nikapoteza fahamu nilipozinduka wakaniambia nilijifungua mtoto akiwa amefariki, kusema kweli niliumia sana.” Mwisho wa simulizi ya Husna.
Katika hali ya kawaida Husna na wanawake wengi huenda kujifungua huku wakiwa na historia kwamba kuna uchungu mkali wakati wa kujifungua, lakini ni kwa kiwango gani na wanawezaje kuupunguza? Hili ni swali gumu, na bila shaka  ni wanawake wachache sana waliofundishwa elimu hii na kujiandaa kupunguza maumivu wakati wa kujifungu.
Namkumbuka muuguzi Stacey Rees wa Brooklyn, New York, katika mada zake juu ya uzazi salama alisema, kitu cha kwanza kabisa kukusaidia wakati wa kujifungua ni utulivu wa akili yako.
Hapa ina maana kwamba kila mjamzito anatakiwa kutafuta na kupewa utulivu ndani ya akili yake. Njia pekee itakayomsaidia ni kujifunza namna ya kupata majibu ya matatizo na wasiwasi wake juu ya ujauzito na kujifungua.
Inashauriwa kwamba kila mjamzito anatakiwa kutafuta mkunga au mshauri wake, atakayemuelimisha kuhusu mimba, kumfumbulia matatizo yake na kumpa ushauri juu ya mabadiliko ya mwili, maumivu, ikiwemo nasaha. Ni wazi kwamba maneno ya kusikia huwaogopesha wajawazito.
 “Kama tumbo linakuuma chini ya kitofu inawezekana ukawa na tatizo.” “Unaumia upande gani? Huu, basi mtoto atakuwa amekaa vibaya tumboni.” “Amefariki wakati anajifungua.”
Hizi ni kauli mbaya kwa mjamzito kuzisikia inabidi aondolewe kwa kuambiwa maneno kama haya: “Usiogope, kama maumivu yanatokea mtoto anageuka tu, hata mimi ilikuwa hivyo wakati wa ujauzito wa x.” Aaah, siyo sana ukijitahidi kusukuma wala hutaumia sana.” Nasaha za aina hizi zinajenga sana imani ya mjamzito na kuongeza ujasiri wa kukabiliana na matatizo.   Itaendelea 

0 comments:

Post a Comment