Saturday 27 September 2014

MBINU ZA KUWA MTU MAARUFU KATIKA JAMII PART 1-2






KIU ya wanadamu karibu wote ni kuwa maarufu na wenye ushawishi mkubwa katika jamii, lakini kwa bahati mbaya wengi wao hawafahamu wafanye nini ili wafikie ndoto zao.
Leo katika mada hii muhimu nitafundisha mbinu chache zinazoweza kutusaidia kuwa watu maarufu kwenye jamii, mfano wa hao tunaowahusudu ndani na nje ya nchi yetu. Uchawi kamili wa kufikia heshima, mamlaka na ushawishi kwa wenzetu ni huu hapa:
Hakikisha ujuzi wako haumfuniki mkuu wako au watu wengine
Unaweza usiwe ujuzi pekee, lakini hata uwezo wako wa kiakili, mali na uelewa. Hakikisha huutumii kwa majivuno kuonyesha jinsi unavyowazidi wenzako kazini, kwenye biashara, darasani hasa watu waliokuzidi cheo. Siku zote hakikisha kuwa unawatanguliza wenzako, kuthamini mchango wao na kusifu uwezo wao.
Kizuizi kikubwa kabisa kwenye maisha ya umaarufu, heshima na mamlaka kwenye jamii ni kujiona bora kuliko wenzako, jambo linalowafanya watu pamoja na uwezo wao washindwe kuheshimika na kupendwa.
Usiwaamini mno marafiki, jifunze kuwatumia maadui zako
Jihadhari na marafiki, kwani wanaweza kukusaliti haraka zaidi kwani ni rahisi sana kwao kukuonea wivu.  Watu hao ni rahisi sana kubadilika na kuwa wakatili.  Ukianzisha uhusiano na mtu ambaye aliwahi kuwa adui yako utagundua kwamba atakuwa mwaminifu zaidi kwako kuliko rafiki, kwani anakuwa anataka kukuthibitishia kwamba uhusiano wenu ni wa dhati.  Kwa kifupi, waogope zaidi marafiki zako kuliko maadui. 
Katika safari ya kuelekea kwenye kilele cha umaarufu na heshima, kuwa na maadui ni jambo muhimu kwani husaidia kuongeza ari na huthibitisha uwezo wako hasa pale inapotokea maadui zako wamesalimu amri kwako.
Dhamira zako zifanye siri
Hakikisha watu hawakuelewi kwa dhamira zako au sababu ya kile unachokifanya. Kama hawafahamu nini unataka kukifanya, ni dhahiri watakuwa hawana nguvu ya kukufanya lolote. Hakikisha unawapotosha wasijue mipango yako, na wakati watakapofahamu dhamira yako, watakuwa wamechelewa kwani utakuwa tayari umeikamilisha.
Epuka kuwa mtu wa kuropoka juu ya madhumuni yako ya maisha, utawapa nafasi wabaya wako kukuwekea vikwazo vya kukuzuia usifike mahali ulipokusudia.
Usipende kuzungumza sana
Unapotaka kuwavutia watu punguza wingi wa maneno yako, kusema sana kunaweza kuwafanya wanaokusikiliza wakakukinai.  Watu maarufu huweza kuwavutia na kuwaogopesha watu kwa kusema maneno machache.  Jinsi unavyozungumza zaidi, ndivyo unapojenga uwezekano wa kusema kitu cha kipumbavu kitakachokudharaulisha.
Hakikisha unalinda hadhi yao katika jamii
Hadhi katika jamii ndiyo nguzo ya mamlaka.  Kwa kutumia hadhi yako pekee unaweza kuwaogopesha watu na ukafanikiwa mambo yako,  lakini ukipotoka tu, fahamu umeingia matatani na utashambuliwa kutoka pande zote. 
Hakikisha hadhi yao inabaki imara.
Kila mara ujihadhari na mashambulio yanayoweza kutengenezwa kwa lengo la kukuondolea heshima, kuwa mjanja kujitetea kwa hoja na pita njia ya nyuma kuwavurugia wanaotaka kukuangamiza. Epuka kuwahukumu adui zako, acha wahukumiwe na jamii inayokuunga mkono.
Ifanye jamii ikutambue
Kila kitu huamriwa kutokana na mwonekano wake,  kisichoonekana hakina maana yoyote.  Usikubali jamii isikutambue kiasi cha kusahaulika kama upo.  Jitokeze mbele.  Jionyeshe kwa watu katika namna yoyote iwe ya kusaidia au kushirikiana na wenzako katika shida na raha.  Jifanye kivutio katika jamii kwa kujitokeza zaidi, kujijengea umaarufu kuliko watu wengine.

MBINU ZA KUWA MTU MAARUFU KATIKA JAMII-2



NAKUMBUKA wiki iliyopita tuliangalia vipengele vichache vinavyoweza kumuwezesha mtu akawa maarufu kwenye jamii, pamoja na notisi yangu ya kuacha kuandika kwenye mraba huu, leo naomba niendelee na mada hii nzuri ya kijasusi yenye uwezo wa kumwinua mtu kutoka chini na kuwa juu kabisa kiheshima. Sasa tusonge mbele…!
Waache watu wakufanyie kazi kwani sifa utapata wewe
Kuwa mjanja, hakikisha unatumia busara na ujuzi wa watu wengine katika kuendeleza masilahi yako.  Msaada huu hautaokoa muda na nguvu zako tu, bali utakupa umaarufu wa kufanya kazi vyema na kwa kasi.
  Mwisho wa yote, watu wanaokusaidia watasahauliwa na badala yake ni wewe utakayekumbukwa.
Kama wewe ni mwanasiasa kwa mfano, usifanye kila kitu wewe, tafuta watu wenye ushawishi kwenye jamii zao, watume wafanye utakayo, mwisho wa siku ushindi utakuwa wako.
Wafanye  watu wakufuate kwa kuweka vivutio
Ukimlazimisha mtu mwingine kufanya kitu, ujue wewe ndiye mshika usukani.  Siku zote ni vyema zaidi kumleta mpinzani wako kwako, jambo ambalo litamfanya aiache mipango yake yote. Mvutie kwa kumwonyesha mafanikio yako makubwa, kisha mmalize, kwani wakati huo wewe utakuwa umeshika mpini wa kisu.
Daima, hakikisha kuwa mafanikio yako yanakusaidia kuvuta watu kwa namna yoyote, iwe ya kusaidia, kununua siri, kutoa motisha na hata kuwachonganisha wanaokuchukia  ili washuke na wewe upate nafasi ya kung’ara zaidi kwenye jamii.
Shinda kwa vitendo, si kwa maneno
Ushindi wowote wa muda mfupi unaotokana na maneno ni ushindi bandia.  Chuki na nia mbaya unazoweza kuziibua zina nguvu zaidi na hudumu zaidi kuliko mabadiliko ya muda ya maoni fulani.
Ni rahisi zaidi kwa watu wengine kukubaliana nawe kwa kuonyesha vitendo bila hata kusema chochote.  Onyesha kwa mifano si kwa maneno mengi.
Waepuke watu wasio na furaha, wasio na bahati
Unaweza kufa kutokana na matatizo ya mtu mwingine, kwani hali ya mtu mwingine inaambukiza kama ugonjwa. Unaweza kuhisi unamsaidia mtu aliye matatizoni, kumbe unajipalia matatizo na balaa.  Fanya uhusiano na watu wenye furaha na wenye bahati siyo wenye mikosi na matatizo yasiyokwisha.
Jifunze kuwafanya watu wakutegemee
Ili kuendelea kujitegemea lazima kuwe na watu wanaokuhitaji kwenye maisha yao.  Kumbuka watu wanavyozidi kukutegemea, ndivyo unavyozidi kuwa huru zaidi.  Wafanye watu wakutegemee ili waweze kupata furaha na ustawi usiogope wala usizuie watu tegemezi.
Ukitaka kuwa maarufu usikubali kuwafanya wenzako waweze kuishi bila wewe. Epuka kuwapa mbinu za kujitegemea kwani wakifanikiwa utapoteza umaarufu kwao na bila shaka watakudharau.
Chagua wema na ukarimu utakaowavunja nguvu maadui zako
Jambo moja jema hufukia mabaya mengi yaliyofanywa na mtu.  Wema na ukarimu unaofanywa kwa moyo mkunjufu humvutia hata mtu aliyekuwa na wasiwasi na wewe.
Wema huo uliopangwa unapowavutia watu, ni wazi unaweza kuwalaghai na kuwatumia jinsi utakavyo.  Zawadi yoyote inayotolewa kwa muda unaotakiwa inaweza kufanikisha lengo lako la kumtumia umtakaye kwa faida yako.
Epuka kukumbusha wema wako mbele ya jamii, acha kuutumia wakati wa kuomba msaada
Unapotafuta msaada kutoka kwa rafiki, usitake kumkumbusha misaada au vitendo vyema ulivyomfanyia.
Ukimwambia hivyo anaweza akakupuuza.  Badala yake, mweleze kitu kipya katika kuomba msaada huo au katika uhusiano wenu, kitu ambacho kitamnufaisha.  Kisisitize kitu hicho kwake.  Atakusaidia kwa furaha mara atakapoona kuna kitu ambacho naye kitamnufaisha.
Jifanye rafiki wa mpinzani wako, lakini fanya kazi naye kama jasusi
Ni muhimu kumfahamu vyema mpinzani wako, ufahamu huo utaupata pale utakapoamua kuwa rafiki wa adui yao na kutumia ukaribu huo kumchunguza mbinu zake ili baadaye umshinde kwa udhaifu wake utakaoujua.
Mwangamize kabisa adui yako
Viongozi wote maarufu tangu enzi za Musa wamefahamu kwamba adui anayeogopewa ni lazima aangamizwe kabisa. 
(Wakati fulani wamelitambua hilo kwa matatizo.)  Iwapo ukuni mmoja ukiachwa unawaka, hata kama una moto mdogo kiasi gani hatimaye moto utalipuka.  Mambo mengi hupotea kwa kufanywa nusunusu badala ya kuyamaliza kabisa: Ukimshambulia adui usimwache hai, akinusurika atalipiza kisasi kwa nguvu kubwa.

0 comments:

Post a Comment