Thursday 1 May 2014

UNAHATARISHA AFYA YAKO KWA KUTOKUNAWA MIKONO NA HII NDIO HATARI YAKE


Nikiwa nimeketi mkononi nimeshika
kitafunwa nilichokarimiwa tayari kuanza
kula, nikainua macho na kuangalia mbele
yangu na ghafla nikakutana na maandishi
kwenye kioo cha kompyuta yakihamasisha;
Ongeza ufahamu kuhusu faida za kunawa
mikono kwa sabuni."

Maandishi hayo yakanigusa na
kunikumbusha kuwa nilipokea kile
kitafunwa nikala bila kunawa mikono, zaidi
yakanikumbusha kuwa Oktoba 15, ilikuwa
Siku ya Kimataifa ya Kunawa Mikono, kwa
Kiingereza, 'Global Handwashing Day'.
Ilinitia aibu nikaenda kutimiza kanuni ya
afya kwa kunawa mikono kwa maji safi na
sabuni kabla ya kula, kisha nikaendelea na
mlo wangu huku nikiwaza na kupata
msukumo wa kuandika maelezo haya ili
kukumbushana umuhimu wa kunawa
mikono kabla ya kula.

Si hivyo tu, bali pia kufanya hivyo kwa maji
safi na sabuni baada ya kutoka chooni ili
kuepuka maambukzi ya vimelea vya maradhi
hatari kwa afya zetu.
Vimelea hivi huwapo kwenye mikono
ambayo haikusafishwa kwa maji safi na
sabuni na huingia mwilini kila tunapokula
bila kunawa kwa maji safi na sabuni.
Siku hii hukumbukwa kila Oktoba 15 kwa
lengo la kuhamasisha kujenga kwa
utamaduni wa kunawa mikono kwa sabuni
kwa kila taifa ulimwenguni pia kujua faida
zake.

Kimsingi, siku hii ilianzishwa kwa ajili ya
kuwajengea watoto na wanafunzi
utamaduni wa kunawa mikono, lakini
inaweza kuadhimishwa na mtu yeyote,
ndiyo maana binafsi nimeguswa
kuiadhimisha kwa kalamu, nikikukumbusha
wewe, yule na wote, manufaa na umuhimu
wake katika kunawa mikono kwa maji safi
na sabuni.

Takwimu zinaonyesha kuwa karibu watu
200 milioni katika nchi takriban 100 duniani
hushiriki katika siku hii muhimu kiafya.
Serikali, mashirika ya kimataifa, taasisi za
kijamii, kampuni, mashirika yasiyo ya
kiserikali na kila mmoja wetu anawajibika
pia kushiriki na kuhamasisha kunawa
mikono kwa maji safi na sabuni.
Pamoja na wajibu huu unaweza kujiuliza
kwa nini kunawa mikono kwa sabuni?

Kiafya, kunawa mikono kwa sabuni ndiyo
njia sahihi na nafuu ya kuzuia magonjwa ya
tumbo, kuhara yanayoathiri na kugharimu
maisha ya mamilioni ya watu hasa watoto
katika nchi zinazoendelea kila mwaka.
Hali hiyo inamfanya kila mmoja wetu
kuwajibika kwa namna moja au nyingine na
vifo vya watoto wetu ambao ni taifa la
kesho, wanaopoteza maisha kwa magonjwa
yanayotokana eti na sababu ya kutonawa
mikono kwa sabuni tu.

Ni muhimu tukakumbuka jukumu muhimu
katika maisha la kulinda familia zetu hasa
watoto wetu dhidi ya maradhi hata vifo
vinavyotokana na magonjwa ya uambukizo
yanayowapata kwa kutonawa mikono kwa
maji safi na sabuni.
Katika hali ya kawaida, inawezekana
kunawa mikono kwa maji safi na sabuni ni
zoezi gumu linalohitaji muda mrefu
kujizoesha. Pia ikawa ni vigumu kuueneza
utamaduni huo wa kunawa mikono kwa
maji safi na sabuni, lakini tufanye hivyo kwa
umuhimu wa kuokoa maisha ya watoto
yasipotee.

Kunawa mikono kwa maji safi na sabuni
kabla ya kula na baada ya kutoka chooni ni
utamaduni unaowezekana kujengeka
miongoni mwetu na unaweza kusaidia kwa
kiasi kikubwa kuokoa maisha yetu kuliko
kinga ya dawa. Kitaalamu, tabia hii
inaelezwa kuweza kusaidia kupunguza
nusu ya vifo vinavyotokana na magonjwa ya
kuhara na robo ya vifo kutokana na
magonjwa ya tumbo.

Tufungue milango ya fahamu na kutambua
kwamba tukiwafundisha zaidi watoto wetu
tabia hii njema ya kunawa mikono kwa maji
safi na sabuni kabla ya kula na baada ya
kutoka chooni kutasaidia siyo tu kupunguza
idadi ya vifo na maradhi, bali tunaweza
kujenga jamii ya ustaarabu.

0 comments:

Post a Comment