Saturday 3 May 2014

TATIZO LA MSHITUKO WA MOYO (HEART ATTACK) AU MYOCARDIAL INFARCTION-2

DALILI ZA MSHITUKO WA MOYO
 
Baadhi ya wakati mshituko wa moyo hutokea kwa dalili zilizo wazi na kwa haraka sana. Lakini mara nyingi mshituko wa moyo hutokea polepole huku mtu akipata maumivu ya wastani na kutokujisikia vyema.
 
Mara nyingi watu wanaopatwa na hali kama hiyo huwa hawana uhakika na kile kinachotokea na husubiri kwa muda mrefu kabla ya kuomba msaada au kumuona daktari.
 
Zifuatazo ni dalili ambazo hutokea pale mtu anapopatwa na mshituko wa moyo.
 
1) Maumivu katika kifua: Mara nyingi mtu anapopatwa na mshituko wa moyo huhisi maumivu sehemu za kifua hasa sehemu za katikati ya kifua ambayo huisha baada ya dakika kadhaa au mara nyingine maumivu hayo huisha na kurudi tena. Mtu huhisi kana kwamba kifua kinambana, kimejaa na kinauma.
 
2) Maumivu katika sehemu za juu za kiwiliwili: Mtu huhisi maumivu sehemu za mikono, mgongo, shingo, taya na tumbo.
 
3) Kukosa pumzi au kushindwa kupumua: Hali hii huweza kutokea ikichanganyika na maumivu ya kifua au bila maumivu hayo. Dalili nyinginezo ni pamoja na kutoka kijasho chembemba (cha baridi), kujisikia kichefuchefu pamoja na kichwa kuwa chepesi na 
 
kizunguzungu. Moyo kwenda mbio au kwa ibara nyingine mapigo ya moyo kutokea kwa kasi zaidi kuliko kawaida.
Unashauriwa iwapo utajisikia mumivu ya kifua, hasa pamoja na mchanganyiko wa moja ya dalili tulizozitaja, usisubiri na haraka wasiliana na kituo cha afya ili upatiwe msaada, au elekea haraka 
 
hospitali mwenyewe. Muda unaofaa wa kutibiwa mshituko wa moyo ni saa moja tangu wakati wa kutokea hali hiyo. Kutibiwa mapema dalili za mshituko wa moyo hupunguza hatari ya kuharibika seli za moyo. Hata kama huna uhakika dalili unazohisi ni za mshituko wa moyo au la, ni bora umuone daktari na ufanyiwe uchunguzi.
 
Utafiti waliofanyiwa wanawake 515 ambao walipata mshituko wa moyo umeonyesha kuwa, wengi wao waliripotiwa kuwa na dalili za kujihisi kuchoka, kutolala vyema, kushindwa kupumua, kujisikia maumivu baada ya kula na wasiwasi.
Asilimia 70 ya wanawake hao walihisi dalili zaidi ya moja kabla ya kupatwa na mshituko wa moyo.
 
Karibu theluthi moja ya kesi za ugonjwa wa mshtuko wa moyo hutokea kimya kimya, bila maumivu ya kifua wala dalili nyinginezo. Kesi kama hizo hugunduliwa baadaye katika vipimo. Kesi kama hizo hutokea zaidi kwa wazee, wagonjwa wa kisukari na baada ya kuunganishwa moyo au heart transplant.
 
VIPIMO VYA MSHITUKO WA MOYO.
Kwa kawaida madaktari hufahamu kuwa mtu amepatwa na mshituko wa moyo au anaelekea kupatwa na mshituko huo kutokana na dalili alizonazo na anavyojisikia.
Pia kwa kutegemea historia ya kifamilia na ya kitiba ya mgonjwa pamoja na vipimo.
 
Kipimo kikuu kinachotumika kupima iwapo mtu amepatwa na mshituko wa moyo ni EKG. Hicho ni kipimo kinachoonyesha na kurekodi mwendo na harakati ya moyo. Kipimo hicho huonesha moyo unakwenda kwa kasi ya kiasi gani, mapigo ya moyo na mdundo wake.
 
Kwa hakika kipimo cha EKG huonyesha dalili za kuharibika moyo kutokana na matatizo ya mishipa ya moyo ya ugonjwa wa coronary heart disease na pia dalili za mshituko wa moyo uliotokea huko nyuma na unaotokea hivi sasa.
 
Kipimo kingine ni cha damu ambacho huonesha protini zinazoonekana kwenye damu zinazotokana na seli za misuli za moyo zilizokufa.
Basi tuangalia utafiti uliosema kwamba mshituko wa moyo mara nyingi hutokea saa tatu asubuhi.
 
Wataalamu wa magonjwa ya moyo wamesema kuwa hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo hutokea zaidi mapema asubuhi, hasa saa tatu asubuhi.
Utafiti huo uliotangazwa katika Kongress ya 4 ya magonjwa ya moyo ya Mashariki ya Kati umeonyesha kuwa, watu wanaokabiliwa na hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo, hutokewa na ugonjwa huo mapema asubuhi kwa sababu ya mabadiliko ya homoni, ambayo huongeza hitajio la oksijeni la mishipa ya moyo katika wakati huo, na kusababisha mshituko wa moyo.
 
Uchunguzi huo umeeleza pia kuwa, ripoti zinaonyesha ongezeko la matukio ya mshituko wa moyo katika siku za Jumatatu, suala ambalo huenda likawa linachangiwa na kiasi kikubwa na kula kupita kiasi siku za wikiendi.
 
Wataalamu hao pia wamesema kuwa, mishipa ya juu ya mwili huwa inasinyaa msimu wa baridi, hali ambayo ni kinyume na utendaji wa mishipa ya moyo na husababisha kupungua kiwango cha oksijeni inayohitajiwa na misuli ya moyo.
Wamesema hii ndio sababu, watu hupata mishtuko wa moyo kwa wingi wakati wa mapukutiko (fall) na baridi (winter).


NAMNA YA KUTIBU MSHITUKO WA MOYO
Mshituko wa moyo unahitaji kushughulikiwa haraka. Kama unamshuhudia mtu akipatwa na mshituko wa moyo unapaswa kuomba msaada haraka au kumfikisha kituo cha afya haraka iwezekanavyo.
 
Kama mtu aliyepatwa na mshituko wa moyo amepoteza fahamu, baada ya kuomba msaada kituo cha afya cha karibu, unapaswa kumfanyia CPR mara moja kama unajua kufanya hivyo.
 
CPR ni kitendo ambacho husaidia kufikisha hewa ya oksijeni katika ubongo. Kwanza hakikisha njia za hewa za mgonjwa ziko wazi, yaani hakikisha mdomoni na puani kwake hakuna kitu kinachozuia hewa kupita na msaidie kwa hewa kila baada ya kumkandamiza kifuani au (chest compress)  mara 30.
 
Kama hujui CPR pia unapaswa kuanza kumkandamiza kifuani mgonjwa aliyepoteza fahamu kutokana na mshituko wa moyo, kwani kufanya hivyo huenda kukaokoa maisha yake.
 
Nitaelekeza hapa jinsi ya kumkandamiza kifuani mgonjwa aliyepatwa na mshituko wa moyo na aliyepoteza fahamu.
Weka kiganja cha mkono wako mmoja katika mfupa wa kifua (chestbone) katikati ya matiti na kiganja cha pili juu ya cha kwanza, na kandamiza kwa kiasi cha inchi mbili au sentimeta 5 kuelekea chini.
 
Endelea kukandamiza na kuachia mara 30. Kama unajua namna ya kufanya CPR mfanyie mgonjwa na kama hujui endele kumkandamiza sehemu hiyo ya kifua hadi msaada utakapowasili au hadi mgonjwa atakapopata fahamu au kuonyesha dalili za kupumua.
 
Matibabu ya ugonjwa wa mshituko wa moyo hufanyika hospitali kwa njia tofauti kulingana na hali ya mgonjwa. Kila dakika inavyopita baada ya kutokea mshituko wa moyo, ndivyo tishu ya moyo inavyopoteza oksijeni na kuharibika au kufa.
 
Njia kuu ya kuzuia moyo usiharibike ni kurejesha tena haraka mzunguko wa damu. Mgonjwa wa mshituko wa moyo huweza kutibiwa kwa dawa au njia nyinginezo za tiba kwa kutegemea jinsi gani tishu ya moyo ilivyoharibika.
 
Dawa tofauti zinazotumika kutibu mshituko wa moyo ni kama aspirin, dawa zinazoyeyusha damu ili kuondoa damu iliyoganda ambazo huitwa kitaalamu kama clot buster, dawa aina ya heparin na nyinginezo ambazo hutofautiana kutokana na utendaji wake mwilini.
 
Baadhi ya wakati athari za mshituko wa moyo huwa kubwa ambapo mgonjwa hutibiwa kwa njia inayoitwa Angioplasty. Hiyo siyo operesheni bali ni matibabu ya kufungua mishipa ya damu iliyoziba au kudhoofika na kusabisha mshituko wa moyo.
Mara nyingine wagonjwa wa heart attack hutibiwa kwa upasuaji unaoitwa bypass surgery.
Baada ya kujua namna ya kutibu mshituko wa moyo.
 
JINSI GANI TUNAWEZA KUJIEPUSHA NA UGONJWA HUO WENYE MADHARA MAKUBWA KWA MIILI YETU.
 
Kwa wale ambao tayari wameshapatwa na ugonjwa huu pia wanashauriwa kuendelea kutumia dawa walizopewa hospitalini lakini pia kubadilisha mienendo ya maisha yao ili kuzuia kupatwa tena na mshituko wa moyo katika siku zijazo. 
Kwa wale ambao mshituko wao wa moyo umesababishwa na 
 
magonjwa mengineyo waliyonayo kama matatizo mengine katika moyo au maradhi tofauti, wanatakiwa kutibiwa maradhi hayo.
 
Lakini kwa ujumla tunaweza kujiepusha kupatwa na ugonjwa huo kwa kutovuta sigara, kudhibiti hali nyinginezo kama shinikizo la damu, ongezeko la mafuta ya kolestroli mwilini na kisukari.
 
Suala jingine linaloweza kuzuia kupatwa na shinikizo la damu ni kuushughulisha mwili kila mara na kufanya mazoezi, kupata lishe bora, kupunguza uzito uliopindukia wa mwili na kupunguza ua kujiepusha na wasiwasi pamoja na msongo wa mawazo.  
 
Kama wewe ni mvutaji wa sigara, tafadhali acha kuvuta sigara ili ujiepushe kupatwa na heart attack na kama unaishi katika mazingira ambayo kuna mtu au watu wanaovuta sigara, basi washauri wenzako waache kuvuta sigara kwani sio tu tabia hiyo huathiri afya zao bali yako wewe pia. Vile vile matumizi ya tumbaku yana taathira kama ya sigara kwenye moyo. 
 
Tunashauriwa kufanya mazoezi kwa uchache dakika 30 kwa wiki ili kujiepusha na ugonjwa wa moyo.
Mazoezi hayo yanaweza kuwa ya aina yoyote hata kutembea kwa mguu. Hii ni katika hali ambayo, lishe ina nafasi muhimu katika kuwaepusha watu kuwa na unene wa kupindukia na hivyo kutokupata mshituko wa moyo.
 
Dakta Linda Van Horn mtaalamu wa lishe na mjumbe wa Kamati ya Lishe ya Jumuiya ya Moyo ya Marekani ambaye pia ni mhadhiri wa tiba ya kuzuia maradhi katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Northwestern huko Chicago anashauri kuwa, ili kujikinga na mshituko wa moyo tunapaswa kula vyakula vyenye ufumwele kwa wingi na visivyokuwa na mafuta mengi ili kuimarisha afya ya mioyo yetu.
Wataalamu wanasema kuwa, mafuta yasiyo na madhara au unsaturated fats kama vile fati asidi za omega 3 na mafuta ya zaituni huweza kusaidia kupunguza kiwango cha mafuta yenye madhara katika miili yetu, kuzuia damu kuganda na pia kufanya chembe za mafuta zisigande katika mishipa ya damu.
 
Lishe iliyo na ufumwele ambayo mara nyingi hupatikana katika nafaka, baadhi ya matunda na mboga, husaidia kupunguza kolestroli aina ya LDL ambayo ni hatari kwa miili yetu.
 
Baadhi ya vyakula vyenye uwezo wa kuimarisha afya ya mioyo yetu ni samaki hasa aina ya sardine na salmon. Samaki hao wana kiwango kikubwa cha omega 3 pamoja na calcium na niacin ambazo ni virutubisho muhimu kwa afya zetu. Chakula kingine ni shayiri yenye ufumwele kwa wingi na pia huupatia mwili nguvu kwa haraka na kuzuia njaa kwa muda mrefu.
 
Utafiti umeonyesha kwamba kunywa kikombe kimoja tu cha kahawa kwa siku kunapunguza hatari ya kupatwa na mshituko wa moyo.
 
Utafiti huo uliotolewa katika Kongamano la Jumuiya ya Mshituko wa Moyo la Kimataifa nchini Marekani, umeeleza kwamba kunywa kikombe kimoja cha kahawa ya kawaida na isiyokuwa na kafeini kila siku huzuia kupatwa na mshituko wa moyo kwa asilimia 30.
 
Hata hivyo wataalamu wameonya kuwa kutumia sana kinywaji hicho matokeo yake yanaweza kuwa kinyume. Utafiti mwingine umeonosha kuwa, kufanya mazoezi kwa muda mrefu hakuhusiana na kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo.
 
Huko nyuma kulikuwepo tafiti zilizoonesha wasiwasi wa afya ya mishipa ya moyo kwa baadhi ya wanamichezo wa Olimpiki.
 
Tafiti hizo zilisema kwamba, kupanuka kwa mioyo ya wanamichezo kunakoitwa kitaalamu "athlete's heart" huufanya moyo kuwa dhaifu sana na kushindwa kuvumilia mazoezi mazito. Lakini kwa mujibu wa uchunguzi uliochapishwa kwenye jarida la Marekani la Kitengo cha Magonjwa ya Moyo, mazoezi mazito hayana hatari kwa afya ya moyo.
 
Kiwango cha damu inayosukumwa katika miili ya wanamichezo hakibadiliki wakati wa mazoezi. Mbali na kupanuka kidogo baadhi ya sehemu za moyo, misuli ya moyo hubakia sawa wakati wa mazoezi.
 
Wanasayansi wamehitimisha kwamba, mioyo ya wanamichezo ina afya nzuri na inaweza kuvumilia kirahisi mazoezi ya kiwango cha juu. Pia wamesema kwamba, baadhi ya dawa kama vile 
 
erythropoietin (EPO) zinazotumiwa na wanamichezo hao ili kuzipa nguvu chembe chembe nyekundu za damu, kunaufanya utendaji kazi wa moyo udhoofu, suala ambalo limekuwa likiwaathiri wanamichezo hao na wala sio mazoezi mazito ya mwili wanayoyafanya.
Sio vibaya ukijua kuwa,
 
 
moyo ulioko katika kifua cha mwanadamu hupiga mara 100,000 kwa siku,
husukuma galoni mbili za damu kwa dakika,
 
galoni 120 kwa saa na hufanya hivyo kwa masaa 24 kwa siku, miezi na miaka yote mwanadamu anayoishi duniani.
 
Mfumo wa mishipa ya damu ambayo
husafirisha damu katika mwili wa binadamu ina urefu wa maili 60,000. Ukubwa huo ni mara mbili zaidi ya mzunguko wa dunia!

Suala la kustaajabisha zaidi na unalopaswa kujua kuhusiana na kiungo hiki muhimu katika mwili wa binadamu ni kwamba moyo huanza kupiga katika mwili wa mtoto mchanga pale anapoumbwa tumboni, hata kabla ubongo haujaumbwa.
Moyo huanza kupiga kabla hata ya mfumo wa fahamu wa kati kuumbwa!
Kuna nadharia maarufu kwamba mfumo wa kati wa fahamu (CNS) hudhibiti na kusimamia vitendo vyote vya mwanadamu kuanzia kwenye ubongo lakini utafiti umeonesha kwamba mfumo wa fahamu hauanzishi mapigo ya moyo.
 
 Kiuhakika mapigo ya moyo huanza yenyewe na kuna wanaosema kuwa bado haijafahamika mapigo ya moyo huanzishwa na nini.
Wataalamu wanasema kuwa moyo ni kituo cha ufahamu (consciousness) na wala sio ubongo kama wengi tunavyodhani.
Daima tuzilinde afya zetu!

0 comments:

Post a Comment