Saturday 3 May 2014

NANI ANAWEZA KUAMBUKIZWA VIRUSI VYA UKIMWI?


Mtu yeyote aweza kuambukizwa kwani Virusi vya UKIMWI havichagui. Mtoto, kijana, mzee, mwanamke, mwanamume, 
 tajiri, masikini, mnene, kimbaumbau, msomi na siye msomi, wote wanaweza kuambukizwa.

Kuna makundi katika jamii ambayo kutokana nasababu mbalimbali, yapo katika hatari kubwa zaidi ya 
 
kuambukizwa. Makundi hayo ni pamoja na wanafunzi ambao huperembwa na watu wazima kwa imani kuwa hawajaambukizwa.

Pia wanafunzi wanaobalehe/kuvunja ungo wakiwa shule na ambao mara nyingi hushawishika kujaribu kukidhi 
 
matamanio ya kimwili. Pia wanaopata taarifa potofu kutoka kwa wanafunzi wenzao kuhusu masuala ya uzazi na maumbile yao.

Vijana walio nje ya shule pia wako hatarini
kwa kutopata elimu rasmi kuhusu jinsia zao na UKIMWI au wanaopata taarifa potofu kutoka kwa wenzao.
 
Kwa vile hawako shuleni, baadhi yao huwa tayari wana majukumu ya kifamilia na wakati mwingine hujikuta wakishawishiwa na wenzao kuingia katika tabia hatarishi.

Wanaotumia vileo pia wako hatarini kwani wakati mwingine huchangia sindano na wanapokuwa wamelewa hushindwa 
 
kudhibiti tamaa za mwili hivyo hufanya ngono bila kinga. Aidha watu wenye wapenzi wengi si rahisi kwao kuhakikisha kama wapenzi wao wote ni waaminifu.

Wanaotegemea ngono kukidhi mahitaji yao (wanawake) pia wapo hatarini kwani hawana sauti juu ya namna ya kujamiiana.
Kadhalika wanaofanya kazi zinazowalazimu kuwa mbali na familia zao kwa muda mrefu wapo hatarini. Watu wa kundi 
 
hili ni kama wavuvi, wanaofanya kazi migodini, madereva wa malori ya safari ndefu n.k. hukumbana na vishawishi vingi wanapokuwa mbali na wenzi wao.

Ngoma za usiku, magulio na minada ni baadhi ya matukio yanayoambatana na vishawishi vingi, hali ambayo huweza kuwaweka watu wanaozunguka maeneo hayo katika hatari ya kuambukizwa.

Kinachotakiwa ni kuacha ngono na kuwa mwaminifu kwa mpenzi mmoja aliyepima baada ya wewe pia kupima. Au tumia kondomu kwa usahihi katika kila tendo la ngono. 
 
Wewe ndiwe mwenye mamlaka na mwili wako na jukumu la kujilinda liko mikononi mwako.
Kwa hiyo lazima uwe mlinzi wa kwanza wa afya yako. Hakuna anayeweza kuilinda afya yako kuliko wewe 
 
mwenyewe. Pamoja na jukumu hil, kila mmoja anapaswa kumlinda mwenziye dhidi ya maambukizi.

Magonjwa ya ngono na UKIMWI: Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya magonjwa ya ngono na Virusi vya UKIMWI. Mtu anapokuwa na magonjwa ya  ngono ni rahisi sana 
 
kuambukizwa Virusi vya UKIMWI kutokana na michubuko anayokuwa nayo sehemu zake za siri.

Wengine wanapohisi kuambukizwa ugonjwa wa ngono hukimbilia dukani kununua dawa na kumeza kabla ya kupima. Dawa hizo zinaposhindwa kufanya kazi ndipo hukimbilia hospitali wakati hali zao zikiwa mbaya sana.

 Ni hatari kubwa kutumia dawa bila ushauri wa daktari. Muhimu ni kumwona daktari atakayekupima na kukuelekeza dawa na jinsi ya kutumia.

Ni salama zaidi kutibu magonjwa ya ngono hospitalini mapema na kuhakikisha umepona. Usikatishe dozi (kiasi cha dawa ambacho mgonjwa hutakiwa kutumia ili kutibu ugonjwa wake). Kamwe usithubutu kujamiiana kabla ya kumaliza dozi na hakikisha mpenzi wako pia ametibiwa.
 
Mjamzito anapotibu magonjwa ya ngono anapunguza hatari ya kumwambukiza mtoto aliye tumboni Virusi vya UKIMWI.

Wahudumu wa afya na wakunga wa jadi hupatiwa elimu mara kwa mara kuhusu jinsi ya kujikinga dhidi ya maambukizi na serikali inahakikisha taasisi za huduma za afya zinawapatia vifaa kwa ajili ya kujikinga wawapo kazini.
 
Wahudumu wa afya pia wanatakiwa kutumia glavu (mipira ya mikono) wanapozalisha, wanaposafisha vidonda, wanapomwogesha mgonjwa, wanapofua nguo za mgonjwa, wanapompaka mgonjwa dawa, wanapomwosha maiti na wanapo mhudumia mgonjwa mwenye majeraha.

Aidha wahudumu wa afya wanatakiwa kuwa makini wanapomchoma mgonjwa sindano ili kuhakikisha hawajichomi. Wanawe mikono kwa sabuni na maji ya kutosha kabla na baada ya kumhudumia mgonjwa.

Vifaa Kama nyembe, mikasi na sindano vitumike kwa mgonjwa mmoja tu. Ikibidi kutumika tena, vichemshwe ipasavyo.

0 comments:

Post a Comment