Saturday 3 May 2014

MENOPAUSE: USIHOFU, NI UTU UZIMA WA MWANAMKE NA MABADILIKO YAKE








NIMEKUWA nikitafuta maneno sahihi ya Kiswahili yenye maana sawa na maneno mawili ya Kiingereza - menopause na climacteric, lakini juhudi zangu zinaonekana kutozaa 
matunda.
Menopause (hedhi kukoma mfululizo kwa miezi sita au zaidi), ni hatua ya mwisho ya mabadiliko yanayotokea kwa 
mwanamke; aghalabu kwa sababu ya utu uzima. Hii ni hatua inayotanguliwa na kipindi cha mpito chenye mabadiliko mengi kutoka katika mfumo unaotabirika wa kuona hedhi 
unaoambatana na tezi za uzazi (ovaries) kutoa angalau yai moja kila mwezi na kufikia hali ya hedhi isiyo na mpangilio thabiti ambayo mara nyingi inaambatana na tezi za uzazi 
kushindwa kutoa yai na kuhitimishwa na kukoma kwa hedhi.
Climacteric ni mabadiliko ya kimwili na kifiziolojia yanayotokea kwa akina mama, kwa sababu ya utu uzima, yanayoanza pale hedhi ya mama inapoanza kubadilika na 
kuwa ya mpangilio usio thabiti, kupitia katika hali ya hedhi kukoma (menopause) na kuhitimishwa na mabadiliko yanayotokea baada ya ukomo huu.
Katika hali ya kawaida ya fiziolojia ya mama, wengi hufikia menopause katika umri wa takriban miaka hamsini hivi.
Baadhi ya akina mama wanafikia menopause kwa sababu tofauti kama vile operesheni ya kuondoa tezi za 
kutengeneza mayai, tiba mbalimbali kama vile ya kansa kwa kutumia mionzi au kwa akina mama wachache, hii inaweza kutokea kwa sababu ya mabadiliko yasiyotarajiwa ya kufikia hali hii katika umri mdogo bila sababu za wazi.
Takriban asilimia kumi ya akina mama hufikia menopause kabla ya umri wa miaka arobaini na tano. Kwa kuwa sababu mbili za mwanzo kati ya tatu nilizozitaja siyo za asili, mama hana kipindi cha mpito na hivyo hufikia mabadiliko ya  
menopause mara moja.
Ushahidi uliopo unaonyesha kuwa muda wa binadamu kuishi umeongezeka sehemu nyingi duniani isipokuwa baadhi ya sehemu za Afrika ya Kusini mwa jangwa la Sahara. Binadamu wanaishi miaka mingi zaidi sasa kuliko huko 
nyuma.
Kwa mfano, inakadiriwa kuwa miaka 100 kabla ya kuzaliwa Kristo, binadamu aliishi wastani wa miaka 18 tu na kwa nchi kama Marekani umri huu ulikuwa umeongezeka na kufikia takriban miaka 49 mwanzoni mwa karne iliyopita.
Tangu mwanzoni mwa karne hii, umri huu umeongezeka na kufikia karibu miaka 80 kwa wanawake na miaka 74 kwa wanaume. Ikumbukwe kwamba katika nchi nyingi duniani, 
wastani wa kuishi wa wanawake ni mrefu zaidi ya wanaume kwa sababu mbalimbali zilizo nje ya wigo wa makala hii na kwa sababu hii akina mama wengi wanaweza kuishi na kufikia menopause sasa kuliko ilivyokuwa huko nyuma.
Takwimu za muda mrefu kama hizi kwa nchi kama Tanzania ni nadra kupatikana; lakini kitu kilicho wazi ni kwamba , akina mama wengi nchini mwetu wanaufikia umri huu sasa 
kuliko huko nyuma kwa sababu idadi ya watu imeongezeka na hali ya maisha kuboreka ikiwemo baadhi ya huduma za afya zinazozuia vifo vingi vya utotoni.
Sensa ya watu na makazi iliyofanyika mwaka 2002 ilionyesha kuwa takriban asilimia nne ya Watanzania walikuwa ni akina mama wenye umri wa menopause. Kwa 
kutumia takwimu za sensa hii na umri tarajiwa wa mama kuingia katika menopause, karibu akina mama nusu milioni 
walifikia hali hii mwaka huo.
Vilevile, idadi ya wanawake wenye umri wa miaka hamsini na zaidi ilizidi ya wanaume, na hivyo kutoa ushahidi kuwa hata nchini mwetu wastani wa umri wa kuishi wa wanawake 
ni zaidi ya ule wa wanaume.
Zamani, jamii nyingi na hata madaktari walifikiri kuwa ukomo wa kuona hedhi unatokana na tezi za kutengeneza mayai kuchoka baada ya miaka mingi ya kazi na kwamba 
tezi hizi zilitoa sumu katika mwili wa mama na hivyo kuathiri viungo mbalimbali ikiwemo ubongo; sumu ambayo ilisababisha matatizo ya mfadhaiko na hata kichaa.
Ingawa ni kweli kuwa menopause husababishwa na tezi za kutengeneza mayai kuishiwa nguvu za kutengeza mayai na virutubisho vinavyohitajika katika mwili wa mama vinavyoitwa homoni, hali hii haina uhusiano na matatizo ya 
 akili. itaendelea sehemu ya pili....

0 comments:

Post a Comment