Thursday 1 May 2014

MAAMBUKIZI YA FANGASI KATIKA SEHEMU ZA SIRI (VAGINAL CANDIDIASIS)


    
 
Kati ya maambukizi yanayowasumbua
wanawake wengi duniani ni maambukizi
ya fangasi. Inakisiwa asilimia 75 ya
wanawake wote duniani hupata
maambukizi haya katika kipindi cha uhai
wao. Maambukizi ya fangasi katika sehemu za
siri za mwanamke husababishwa na
uwepo wa fangasi wanaojulikana
kitaalamu kama Candida albicans.

Maambukizi haya pia hujulikana kama
yeast infection au thrush. Fangasi
hupatikana kama vimelea vya kawaida
katika mdomo, mpira wa kupitisha chakula
sehemu inayojulikana kama pharynx, katika
kibofu cha mkojo, uume na hata kwenye
uke.

Mfumo mzuri wa kinga wa mwili pamoja
aina fulani za bakteria wanaoishi pamoja
na fangasi hawa husaidia sana katika
kuthibiti maambukizi yanayoyosababishwa
na aina hii ya fangasi.

Nini hutokea?
Kwa kawaida, Candida albicans huishi
kwenye uke na sehemu nyingine (kama
zilivyoelezewa hapo juu) bila kusababisha
madhara yoyote yale isipokuwa pale
mazingira ya eneo husika yanapobadilika
kama vile mabadiliko katika hali ya pH ya
eneo husika (ifahamike ya kwamba pH ya
kawaida ndani ya uke ni 4.0 - 4.5) au
uwiano wake na vimelea
(microorganisms) wengine unapoharibiwa
kutokana na sababu mbalimbali kama vile
matumizi ya madawa aina ya antibiotics,
kupungua kwa kinga mwilini kutokana na
magonjwa mbalimbali n.k.

Maambukizi haya ya fangasi yanaweza
kugawanywa katika sehemu kuu mbili;
1. Maambukizi yasiyo makali yaani
uncomplicated thrush: Katika kundi hili,
mgonjwa hupatwa na maambukizi mara
moja hadi nne kwa mwaka na dalili zake
huwa si mbaya sana na maambukizi haya
husababishwa na fangasi wa jamii hii ya
Candida albicans.

2. Maambukizi makali yaani complicated
thrush: Katika kundi hili, mgonjwa
hupatwa na maambukizi zaidi ya mara nne
kwa mwaka, dalili zake kuwa mbaya zaidi
au kama maambukizi yatakuwa yametokea
kipindi cha ujauzito, ugonjwa wa kisukari,
upungufu wa kinga mwilini. Aina hii
kusababishwa na vimelea vya aina
nyingine tofauti na Candida albicans.
Vihatarishi.

Watu walio katika hatari ya kupata
maambukizi ya fangasi hawa ni wale
wenye;

• Kutumia sana dawa aina ya detergents
kwenye sehemu za siri au douches (vifaa
vinavyotumiwa kusafishia uke kwa
kutumia maji yaliyochanganywa na siki au
antiseptic yoyote ile) kwa sababu hali
husababisha kuharibika kwa uwiano wa
fangasi na aina nyingine ya vinyemelezi
kama bakteria aina ya lactobacilli.

• Kutumia sana madawa aina ya
antibiotics, steroids ambayo yana tabia ya
kushusha kinga ya mwili.

• Mabadiliko ya mfumo wa homoni mwilini
ambayo husababisha mabadiliko katika s
ehemu za siri na hivyo kufanya kuwepo
kwa ukuaji wa kasi wa fangasi hawa.

• Ujauzito (kutokana na kubadilika kwa
mfumo wa homoni mwilini na kupungua
kwa kinga ya mwili). Hata hivyo ieleweke
hapa kuwa si kila mjamzito hupatwa na
maambukizi haya.

• Matumizi ya dawa za kupanga uzazi
(vidonge vya majira)
• Upungufu wa kinga mwilini kutokana na
magonjwa sugu kama kisukari, saratani
aina yoyote ile, ugonjwa aina ya
mononucleosis na nk.

• Ugonjwa wa ukimwi (HIV/AIDS)
• Matibabu ya homoni (hormonal
replacement therapy) kutokana na sababu
mbalimbali.

• Matibabu ya kusaidia kushika mimba
kwa wale wenye matatizo ya uzazi
(infertility treatment)
• Msongo wa mawazo (stress)
• Utapia mlo (malnutrition)
• Kuvaa nguo au mavazi yanayoleta joto
sana sehemu za siri kwa muda mrefu
kama nguo za kuogelea (swimwear), nguo
za ndani (chupi) zilizotengenezwa kwa
kitambaa aina ya nylon, nguo za ndani
zinazobana sana nk.

• Kujamiana kwa njia ya kawaida mara tu
baada ya kujamiana kupitia njia ya haja
kubwa (anal sex) au matumizi ya vilainishi
vyenye glycerin wakati wa kujamiana pia
yamehusishwa na maambukizi haya.

• Kuvimba kwa tezi la koo (goiter)
• Saratani ya tezi la koo (thyroid cancer)
• Wanawake wenye umri wa miaka kati ya
ishirini na thelathini wapo kwenye hatari
kubwa ya kupata maambukizi haya wakati
wale ambao wameshaacha kupata hedhi
au wale ambao hawajaanza kupata hedhi
kabisa hawako kwenye hatari kubwa.

Kwa wanaume vihatarishi vya
maambukizi haya ni;

• Kujamiana na mwanamke mwenye tatizo
hili au maambukizi haya
• Upungufu wa kinga mwilini

• Matumizi ya madawa aina ya antibiotics
kwa muda mrefu bila ushauri wa daktari
• Magonjwa sugu kama kisukari, saratani
ya aina yoyote ile na nk.

Dalili na viashiria kwa wanawake;
• Kuwashwa sehemu za siri (kwenye tupu
ya mwanamke)
• Kuhisi kuwaka moto sehemu za siri
(burning sensation)
• Kufanya kama vidonda katika sehemu za
siri (soreness)
• Maumivu wakati wa kujamiana
(superficial dyspareunia)
• Maumivu au usumbufu wakati wa
kujisaidia haja ndogo (wakati mtu
anakojoa)
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu kwa
mdomo wa nje wa tupu ya mwanamke
(labia minora)
• Kutokwa na uchafu wa rangi nyeupe au
nyeupe kijivu, unaoweza kuwa mwepesi,
majimaji au mzito na ambao umefanana
na jibini (cottage cheese like discharge)
wenye muonekano unaojulikana pia kama
curd-like appearance.
Kwa kawaida,
uchafu huu haumbatani na harufu yoyote
isipokuwa panapokuwa na tatizo la ziada
kama ugonjwa wa zinaa aina ya Bacteria
vaginosis. Uchafu huu unaotoka hapa
unaweza kuenea kwenye maeneo
mengine yaliyokaribu na tupu ya
mwanamke kama kwenye mitoki (groin
area) au perineum na kusababisha
kuharibika kwa ngozi katika sehemu hizo.
Dalili na viashiria hivi huwa mbaya zaidi
wakati mwanamke anapokaribia kupata
hedhi.

Dalili na viashiria kwa wanaume ni;
• Kuwashwa sehemu za siri
• Kuvimba na kuwa rangi nyekundu
kwenye ncha ya uume
• Kuwepo kwa uchafu wa rangi nyeupe
(kama nilivyoeleza hapo juu) kwenye
sehemu ya juu ya uume.
• Kuwa na vidonda vidogo kwenye uume
(sore on the glans)
Hata hivyo, mara nyingi wanaume
hawaoneshi dalili zozote zile, ni vizuri kwa
mwanamke kumueleza mwenza wake pale
anapopata maambukizi haya ili naye pia
apate kutibiwa.

Vipimo vya uchunguzi
Kabla ya vipimo vya uchunguzi, ni muhimu
kwa daktari kuchukua historia ya
mgonjwa kwa usahihi kabisa. Vipimo
vitahusisha;
1. Uchunguzi wa uke (per Vaginal
Examination (PV exam) – Daktari huvaa
gloves, na kuzilainisha gloves hizi kwa jelly
maalum, mgonjwa hulala kwenye kitanda
na kutanua miguu yake ili njia itanuke na
kumrahisishia daktari kumfanyia
uchunguzi, wakati akiwa tayari, daktari
ataingiza vidole vyake viwili (cha shahada
na cha kati) ukeni kwa dhumuni la
i. Kuhisi kama kuna uvimbe wowote ndani
ya tupu ya mwanamke
ii. Kuangalia kama anapata maumivu
wakati wa kujamiana
iii. Kuangalia kama kuna uchafu wowote
unaotoka, wingi wake, rangi yake, harufu
yake, uzito wake (mwepesi, majimaji au
mzito), na aina ya uchafu unaotoka kama
ni sahihi kutokana na maelezo ya
mgonjwa au ni tofauti
iv. Kuangalia kama sehemu ya siri ipo
kawaida
v. Kuangalia kama kuna uvimbe wowote
wa tezi za sehemu ya siri (mitoki)
vi. Kuangalia nywele za sehemu za siri
zilivyo na jinsi zilivyokaa
vii. Kuangalia shingo ya kizazi, bartholin
glands nk.
viii. Kuangalia sehemu ya haja kubwa kama
kuna skin tags, bawasiri (haemorrhoids)
nk.
ix. Kuangalia kwenye kinembe (clitoris)
kama kuna tatizo lolote lile.
Hayo ni baadhi tu ya malengo na faida za
kipimo hiki kwa vile humuwezesha daktari
kugundua tatizo au maradhi mengine ya
ziada ambayo hayajaanza bado kuonesha
dalili zake kwa mgonjwa au mgonjwa
mwenyewe hafahamu kama hali aliyo nayo
ni tatizo.
Hata hivyo inashauriwa sana
kabla ya kufanya kipimo hiki, daktari
amjulishe mgonjwa aina ya kipimo, lengo
lake na jinsi kitakavyofanyika ili
kumuandaa mgonjwa kisaikolojia. Aidha ni
muhimu pia kumtaarifu wakati anapoanza
kuingiza vidole.

2. Kuchunguza uchafu unaotoka kwa
kutumia hadubini (microscope). Mara tu
baada ya kuchukua sehemu ya uchafu kwa
kutumia swab, kipimo hicho humwagiwa
tone la 10% potassium hydroxide ambayo
huyeyusha chembechembe za ngozi na
kubakisha seli za Candida albicans.
Kuwepo kwa pseudohyphae (mfano wa
aina fulani ya mizizi au miguu ya fangasi
hawa) pamoja na budding yeast cells
(yaani seli za fangasi zinazojigawa kwa ajili
ya kuzaliana) ni uthibitisho wa
maambukizi ya fangasi aina ya Candida
albicans.

3. Kuchukua kipimo na kuotesha kwenye
maabara ili kuangalia aina ya uoto huo
kama ni wa fangasi aina ya Candida
albicans, ama la.
4. Kipimo cha mkojo (Urinalysis)
5. Vipimo vingine hufanyika kulingana na
dalili zinazoashiria uwepo wa magonjwa
mengine kama vile ugonjwa wa kisukari,
HIV/AIDS, ugonjwa wa kuvimba tezi la koo
(goiter), saratani ya tezi koo (thyroid
cancer) nk.

Matibabu
Matibabu ya fangasi huusisha dawa za
kutibu fangasi (antifungal drugs) kama vile
dawa za kupaka za topical Clotrimazole,
topical Nystatin, Fluconazole au topical
Ketoconazole.
Wagonjwa wenye maambukizi yasiyo
makali yaani uncomplicated vaginal
candidiasis wanaweza kutumia dawa za
kupaka (cream) kutoka dawa za fangasi za
jamii ya -azole kama vile Butoconozale,
Miconazole, Clotricomazole nk. Dawa hizi
hutumika kwa muda wa siku 3-7
kulingana na aina ya dawa.
Mgonjwa
anashauriwa kupaka dawa ndani ya uke
pamoja na maeneo yote yanayozunguka
sehemu hiyo. Jinsi ya kupaka dawa hizi ni
kuanzia mbele kuelekea nyuma.
Aidha mgonjwa anaweza kupewa dawa za
kutumbukiza ukeni ambayo atatumia kwa
muda wa siku 3-14 kulingana na aina ya
dawa. Dawa hizo ni pamoja na Miconazole,
Tiaconazole, Terconazole, Nystatin nk.
Kidonge cha kumeza aina ya fluconzolepia
huweza kutolewa. Dawa hizi nilizotaja
hapa juu zina kawaida ya kuharibu ubora
wa mipira ya kondomu zilizotengenezwa
na mpira aina ya latex (latex condoms)
pamoja na vifaa vya upangaji uzazi aina ya
diaphragms.
Ni vizuri kwa daktari kabla ya
kumpa mgonjwa dawa hizi kumfahamisha
kwa ufasaha jinsi ya kuzitumia na
tahadhari anayotakiwa mgonjwa
kuchukua. Inashauriwa kama baada ya
matumizi haya bado mgonjwa ana dalili za
maambukizi au mgonjwa akapata tena
maambukizi haya ndani ya miezi miwili
baada ya matibabu ya awali, basi
anashauriwa kwenda kumuona daktari ili
apate matibabu zaidi.

Kwa wale wenye maambukizi makali yaani
complicated vaginal candidiasis, kabla ya
kupewa tiba, ni muhimu kwanza
kufanyiwa kipimo cha kuotesha sehemu ya
uchafu unaootoka ukeni ili kuwa na
uhakika kama kweli fangasi
wanaosababisha maambukizi haya ni
Candida albicans ama la, kwani fangasi
aina ya Candida glabrata pia wanaweza
kusababisha aina ya maambukizi haya na
huwa siyo rahisi kutibika kwa kutumia
matibabu ya kawaida ya kutibu fangasi
pamoja na pia si rahisi kuonekana kwa
kutumia hadubini (microscope).

Matibabu ya wagonjwa wenye aina hii ya
fangasi hujumuisha matumizi ya dawa za
kupaka au vidonge vya kuweka ukeni kwa
muda mrefu yaani kwa muda wa siku saba
hadi kumi na nne (7-14) au dawa aina ya
fluconazole ambayo hutumika kila baada
ya siku tatu (yaani siku ya 1, siku ya 4 na
siku ya 7). Mara baada ya kumaliza tiba hii,
mgonjwa hutakiwa kuendelea nayo mara
moja kwa wiki kwa muda wa miezi sita.
Ikiwa matibabu haya hayatasaidia basi
mgonjwa anaweza kushauriwa kutumia
mchanganyiko wa fluconazole pamoja na
dawa ya kupaka ya Clotrimazole mara mbili
au moja kwa wiki kulingana na dozi ya
dawa, au fluconazole na dawa nyingine za
kupaka kwa wakati mmoja.

Matibabu ya wagonjwa wenye
maambukizi hatari sana yaani severe
vaginal candidiasis ambayo kwa kawaida
huambatana na dalili kama uke kuwa
mwekundu sana, uke kuvimba, michubuko
ya ngozi ya ukeni (excoriation) na kutokea
kwa mifereji kama vidonda (fissure
formation) huwa ni dawa zozote za
kupaka zilizotajwa hapo juu kwa muda wa
siku 7 mpaka 14 au dawa ya fluconazole
ambayo hutolewa mara mbili, ambapo dozi
ya pili hutolewa siku ya tatu baada ya
kutolewa kwa dozi ya awali (second dose
72hrs after initial dose).

Matibabu ya maambukizi ya fangasi
ambayo hayasababishwi na Candida
albicans kwa mfano Candida glabrata nk ni
matumizi ya dawa za kupaka jamii ya
nonfluconazole azole groups kama vile
Posaconazole, Voriconazole nk zitolewazo
kwa muda wa siku 7 mpaka 14 pamoja na
kidonge cha Boric acid kwa muda wa siku
14. Mtu mwenye maambukizi haya pia
anashauriwa kuonana na daktari bingwa
wa magonjwa ya akina mama.

Kwa vile maambukizi ya fangasi hutokea
sana kwa wanawake wajawazito, hivyo
basi wanashauriwa kutibiwa kwa kutumia
dawa za kupaka tu kwa muda wa siku 7.
Aidha dawa aina ya Itraconazole haipaswi
kutumiwa na mwanamke mjazito au
anayekusudia kushika mimba. Dawa ya
Ketoconazole haipaswi kutolewa bila
ushauri wa daktari kwani ina madhara ya
kusababisha ugonjwa hatari wa Ini
(Fulminant hepatitis). Usugu wa fangasi
dhidi ya dawa za jamii ya azole groups
hutokea baada ya matumizi ya dawa za
vidonge (vya kumeza) za kutibu fangasi
kwa muda mrefu.

Maambukizi ya fangasi pia huonekana
sana kwa wagonjwa wenye Ukimwi. Tiba
ya maambukizi haya ni sawa na tiba ya
watu ambao hawana ugonjwa wa Ukimwi.
Hata hivyo, kwa wale wagonjwa wa
ukimwi ambao wamepata maambukizi ya
fangasi mara kwa mara wanashauriwa
kunywa dawa aina ya fluconzole mara
moja kwa wiki kama kinga dhidi ya
maambukizi haya au kama njia ya
kupunguza fangasi hawa. Kadhalika dawa
za kutibu fangasi aina ya Itraconazole,
Voriconazole, Posaconazole huingiliana
sana katika utendaji kazi na dawa za
kurefusha maisha za ugonjwa wa Ukimwi
(Antiretroviral drugs, ARVs) aina ya
Protease Inhibitors, PIs (rotinavir nk.) na
Nonnucleoside Reverse Trancriptase
Inhibitors, NNRTI (maraviroc nk).

Wakati mwingine, maambukizi ya fangasi
yanaweza kuambatana na magonjwa ya
zinaa (Bacterial vaginosis nk), hivyo dawa
zitatolewa kulingana na dalili na historia ya
mgonjwa.

Kinga ya maambukizi ya fangasi
• Kuosha sehemu ya siri kwa kutumia
kitambaa kisafi kila siku na kuosha kuanzia
mbele kuelekea nyuma, epuka kurudia
ukishafika nyuma.

• Epuka matumizi ya sabuni zenye
manukato, bubble baths, vaginal
deodorant products, feminine hygiene, na
bath powder.
• Vaa chupi ambazo hazibani sana na
zilizotengenezwa kwa kutumia pamba au
hariri (silk), epuka synthetic underwear.
• Epuka mavazi yoyote ya kubana kama
jeans za kubana nk.
• Badilisha nguo za ndani (chupi) kila
zinapopata unyevunyevu.
• Fua chupi zako kwa maji yenye nyuzi
joto 90 na kuendelea.

• Tumia pedi wakati tu unapozihitaji (kama
umeingia kwenye mzunguko wako wa
hedhi)
• Kula mlo wenye virutubisho vyote kamili
(balanced diet)
• Epuka kufanya mapenzi na mpenzi wako
ambaye amepata maambukizi ya fangasi.
• Epuka kuoga maji moto sana (hot baths)
tumia maji ya uvuguvugu, hii kwa wale
ambao wanaishi kwenye ukanda wa joto
(tropical climate).
• Matumizi ya vifaa vya ngono (sex toys),
vifaa vya upangaji uzazi (diaphragms,
cervical caps) yanaweza kuleta kujirudia
kwa maambukizi ya fangasi kama
havitaoshwa na kukaushwa vizuri baada
ya kutumiwa.
• Baadhi ya tafiti zilizofanyika,
zimethibitisha ya kwamba unywaji wa
maziwa ya mtindi (yoghurt) yenye live
culture, husaidia kupunguza maambukizi
ya fangasi.chanzo.

0 comments:

Post a Comment