Saturday, 3 May 2014

IFAHAMU TOFAUTI YA UGONJWA WA KASWENDE NA KISONONO


Ndugu msomaji nimeona ni muhimu kuandika tofauti ya ugonjwa wa kaswende na kisonono kwa sababu kumekuwa na idadi kubwa ya wagonjwa ambao wanapotoa maelezo au malalamiko yao wamekuwa wakichanganya ugonjwa wa kaswende na kisonono.

Kawaida daktari anatakiwa amsikilize mgonjwa anavyojieza kuhusu anavyojisikia kwa wakati huo, alianza kuumwa vipi na magonjwa mengine aliyowahi kuumwa hapo nyuma. Maelezo haya kutoka kwa mgonjwa, na majibu mengine atakayojibu baada ya kuhojiwa na daktari humsaidia daktari kujua vipimo vya aina gani akufanyie ili aweze kuelewa una ugonjwa gani na uko katika hatua gani ili kukupa matibabu yanayostahili.

 
Inapotokea mgonjwa akatoa maelezo ambayo si sahihi, inaweza kumfanya daktari atoe matibabu ya ugonjwa totafuti na ule unaaumwa na matokeo yake ni kuendelea kuumwa na kuzababisha usugu wa ugonjwa kwa baadhi ya dawa.
 
Kisonono ni ugonjwa tofauti na kaswende kwa njia mbalimbali kama ifuatatavyo; kwanza kabisa tofauti kubwa ni dalili za magonjwa haya, Kisonono kina dalili ya kutokwa na usaha sehemu za siri ambao huambatana na maumivu makali sana wakati wa kukokojoa kwa wanaume na wanawake husikia mkojo kuchoma sana wakati wanapokojoa.
 
Kwa watoto wanaozalia na mama mwenye ugonjwa wa kisonono, mtoto atazaliwa na ugojwa wa macho kwa kutokwa na matongotongo mengi na macho kuwa mekundu kwa sababu ya kushambuliwa na bakteria wa kisonono. Ukweli Kisonono hutambulika mapemba kuliko kaswende kwa sababu dalili zake ni bayana na zinamlazimisha mgonjwa kwenda hospitali au kununua dawa kutuliza maumivu.
 
Kaswende tofauti na kisonono dalili zake ni za kuota vipele mwilini na hata uambukizaji wake ni zaidi ya kisonono, japo magonjwa yote yanaweza kuambukizwa kwa njia ya kujamiiana, Kaswende inaweza kuambukizwa kwa kugusa majimaji yanayotoka kwenye vipele vya mgonjwa wa kaswende.
Hata kuchangia taulo au shuka na mgonjwa huyo unaweza kupata maradhi hayo iwapo majimaji yanayotoka kwenye vipele hivyo, yamegusa ngozi yako. Wadudu wa kaswende wanaweza kupenya ngozi ya kawaida tofauti na magonjwa kama UKIMWI ambayo yanahitaji kuwepo michubuko ili yaingie mwilini.
Dalili za kaswende ni hatari sana kwani ugonjwa zaidi ya vipele huendelea kukua ndani kwa ndani bila kujua na dalili kubwa zinajitokeza wakati ugonjwa umefikia hatua ya juu.
Dalili hizi ni pamoja kuongezeka kwa vipele sehemu za siri na mwili mzima, kwa kina mama mimba hutoka mara kwa mara na kwa wale watakaojifungua salama basi utakuta mtoto ana kasoro za maumbile. Kaswende imeishawafanya wengi kuishia kuwa vichaa na kuokota makopo barabarani
 
Hata hivyo njia za kuyaepuka magonjwa haya zinafanana sana; Kuacha kufanya ngono ni bora kuliko kupata magonjwa haya mawili, hii itakusaidia kuwa na nafasi ya kujipanga na kutafuta mpenzi au mchumba na wakati utakapofika mnakubaliana maisha ya pamoja na kuwa na mahusiano ya ngono yaliyo salama.
Kuwa na mpenzi mwaminifu ni muhimu sana, kama wote mtatunziana heshima na asiingizwe mtu wa tatu katika mahusiano yenu ya kingono basi ujue kuwa magojwa hayo mtayasikia kwa wengine kwani nyie mkiwa salama itaendelea hivyo maisha yenu yote.
 
Mwisho nasisitiza matumizi sahihi na ya mara kwa mara ya mpira wa baba au wa mama maarufu kama kondomu. Hii imeishawasadia wengi sana, kondomu zinazuia magonjwa ya zinaa na hata mimba zisizotarajiwa. Hivyo basi, tujitahidi kuuliza na kuzijua dalili za magonjwa mbalimbali ili tusiwachanganye madaktari wanapotuhudumia.

0 comments:

Post a Comment