Saturday 3 May 2014

HUU NDIO UGONJWA WA ZINAA WA KASWENDE (SYPHILIS)



Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum.  
Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoongoza kwa kusababisha madhara mengi.
 
Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito huleta madhara mengi sana kama vile kujifungua kiumbe ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati wa ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga. 

Ugonjwa wa kaswende huathiri zaidi ya mimba milioni moja duniani kote kila mwaka na kuchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto wanaozaliwa wakiwa tayari wameshakufa katika nchi za maeneo ya 
 
chini ya Jangwa la Sahara. Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto kufariki wakati wa kuzaliwa. Pia asilimia nyingine 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende husababisha watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kupata matatizo ya ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50.
 
Taasisi ya kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania (Tanzania National AIDS Control Programme) au NACP katika ripoti yake ya utafiti uliofanywa chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii 
 
nchini ilitangaza kuwa, maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania bara kati ya mwaka 2003 hadi 2004 yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7 kwa ujumla, kuanzia 
 
mkoani Kilimanjaro ambako maambukizi yalikuwa ya asilimia 0.4 hadi mkoani Tabora ambako yalikuwa ya asilimia 32.
Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana pamoja ambapo pia ugonjwa wa zinaa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu kupata Ukimwi.
 
JE, UGONJWA WA KASWENDE HUAMBUKIZWA KWA NJIA GANI?
 Kama nilivyosema awali,
kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum. Njia za maambukizi za ugonjwa huu ni kama zifuatavyo:
 
1) Kupitia kujamiana bila kutumia kinga au ngono zembe na mtu aliyeambukizwa kaswende.
 
2) Mama aliyepata ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito.
 
3) Kuambukizwa kupitia michibuko au mipasuko kwenye ngozi wakati wa kujamiana au wakati mwingine pale mtu anapogusana na mtu mwenye kaswende ikiwa wote wawili wana mipasuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi zao.
 
Sio rahisi mtu kutambua kama ana michibuko au la kwenye ngozi kwani mingine huwa midogo sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa macho, lakini huweza kuwa njia ya maambukizo. 
 
Baada ya kujua visababishi vya ugonjwa huo sasa tuzibainishe pia dalili zake.
Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kaswende hutegemea aina ya ugonjwa wa kaswende wenyewe.
 
KUNA AINA TANO ZA UGONJWA WA KASWENDE AMBAZO NI;
Ugonjwa wa kaswende wa awali (Primary syphilis)
Ugonjwa wa kaswende wa pili (Secondary syphillis) Kaswende iliyojificha (Latent syphilis)
Kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis)
Kaswende ya kurithi (Congenital syphilis)
Kaswende ya awali (primary syphilis):
 
Dalili ya kwanza ya aina hii ya kaswende ni kutokea kwa kidonda kidogo cha mviringo (chancre kama kinavyojulikana kitaalamu) katika sehemu ambayo bakteria wameingilia na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2 hadi 6).
 
baada ya mtu kupata maambukizi. Kidonda hiki kinaweza kutokea kwenye sehemu ya haja kubwa, shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mdomoni, katika uume, ulimi, vulva, tupu ya mwanamke na sehemu nyinginezo mwilini.
 
Tezi (lymph nodes) ambazo zipo karibu na sehemu iliyotokea kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku 7 hadi 10. Kidonda hiki hakiambatani na maumivu na kwa kuwa kinaweza 
 
kutokea katika sehemu zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu kutambua kama ana aina hii ya kaswende. Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa muda wa wiki 3 hadi 6 kama mtu hatapata matibabu na hutoweka chenyewe bila tiba au baada ya kupata tiba.
 
Robo tatu ya wale ambao hawapati tiba huishia kuingia kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani Secondary syphilis.
 
Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata kaswende ya awali.
Dalili za aina hii ya kaswende ni: vipele ambavyo haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu. Vipele hivi pia vinaweza kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili. Pia muathirika huhisi uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka  nywele, vidonda vya koo, kuvimba kwa matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na kupungua uzito.
 
Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa na hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika. Pia inaweza kujirudia rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu huingia kwenye kundi la aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende yaani (latent syphilis) baada ya miaka miwili.
 
Kaswende iliyojificha (Latent syphilis).
Aina hii inajulikana kama kaswende ambayo inaweza kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara (serological test) na imegawanyika katika makundi mawili.
 
Kundi la kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali au (Early latent syphilis) kwa kimombo.
Hii ni kaswende ambayo hutokea ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya muathirika kuugua kaswende aina ya pili .
Aina hii huwa na dalili zinazojirudia kama za kaswende ya pili.
 
Kundi la pili ni kaswende iliyojificha ya kuchelewa au Late latent syphilis.  
Hii hutokea baada ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya aina ya pili (secondary syphilis). Wakati wa kuugua aina hii ya 
 
kaswende, muathirika huwa hana dalili wala viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu mwingine huwa chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu mwingine.
 
Kaswende ya aina ya nne kama tulivyosema inaitwa kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis).
Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada ya maambukizi ya kaswende.
 
Aina hii inaweza kuathiri viungo kama
macho, ubongo,
mishipa ya fahamu,
viunganishi vya mifupa au joints,
uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu.
 
Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni yenye madhara makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo,
magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu.
Huweza kumfanya mtu kuwa kiziwi na kupungukiwa na kumbukumbu na hata kumsababishia kifo.
 
Pia aina hii ya kaswende inaweza kuathiri mfumo wa chakula, mfumo wa kupumua na mfumo wa uzazi.
 
Kaswende ya aina ya mwisho ni ya  kurithi (Congenital  syphilis).
Aina hii ya kaswende hutokea wakati wa ujauzito au baada ya mtoto kuzaliwa.
 
Nusu ya wototo wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote za ugonjwa huu.
 
Nusu ya watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia muda mfupi kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa.
Dalili za aina hii ya kaswende kwa mtoto mchanga zinaweza kutokea baada ya kuzaliwa au wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.
 
Dalili hizo ni, kutoongezeka uzito au kushindwa kukua, homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua linakuwa bapa, vipele kwenye viganja vya mikono na kwenye  nyayo ambavyo huwa ni vipele vya rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na nyayo na vipele kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa.
 
Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka ukubwa wa ini na bandama, ngozi kuwa ya njano, na upungufu wa damu mwilini (anemia).
 
DALILI ZA UGONJWA WA KASWENDE KWA MTOTO MKUBWA
Ambazo ni,
kuathirika meno (Hutchinson teeth),
maumivu ya mifupa, kupata upofu,
kupungua uwezo wa kusikia au mtoto kuwa kiziwi na kuwa na ukungu kwenye mboni za macho (Clouding of cornea).
 
Dalili nyingine ni kutokwa vidonda vya rangi ya kijivu kwenye sehemu ya haja kubwa na kwenye tupu ya mwanamke, ngozi kuwa na mabaka meusi kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu za haja kubwa, maumivu kwenye mikono na miguu na pia kuvimba jointi za mifupa.
 
Ewe msomaji pale unapoona dalili kama hizo katika mwili wako haina budi uwahi kituo cha afya mapema kabisa ili uweze pumatiwa msaada wa matibabu na ushauri.

0 comments:

Post a Comment