Saturday, 27 September 2014

TIBA YA SARATANI YA MATITI - 4-5




Tunaendelea kujadili ugonjwa wa kansa au saratani ya matiti, ambapo leo tutaanza kuzungumzia tiba ya ugonjwa huo.
Kuna aina tofauti za tiba kwa wagonjwa wanaousumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya matiti. Baadhi ya tiba hizo tayari zinatumika rasmi na nyingine zinafanyiwa majaribio.
Matibabu ya majaribio au Treatment clinical trials ni uchunguzi wa kitiba unaofanyika kwa lengo la kusaidia kuboresha tiba zilizoko au kwa ajili ya kupata ufahamu kuhusiana na matibabu mapya kwa ajili ya wagonjwa wa kansa.
Kwa kawaida mgonjwa hushauriwa na kutakiwa kukubali kabla ya kushiriki katika matibabu hayo ya majaribio. Baadhi ya matibabu ya kansa ya matiti ni kama ifuatavyo: Kwanza kabisa ni:
UPASUAJI
Lengo kuu la upasuaji ni kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi au lymph nodes. Zipo aina kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi linalogundulika kuwa na saratani.
Aina hizo ni pamoja na Lumpectomy ambao ni upasuaji unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo haijaathirika kwa saratani.
Hii hufuatiwa na tiba ya mionzi yaani Radiotherapy kwa muda wa kati ya wiki 6 au 7. Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji huwa na uwezekano wa kuishi sawa tu na mtu anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi lote lililoathirika.
Aina nyingine ya upasuaji ni ile inayohusisha uondoaji wa titi lote lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani ambayo inaitwa Simple ama Total mastectomy. Aina nyingine ni Radical mastectomy ambao ni upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote na sehemu ya tezi liloathirika kwa saratani pamoja na misuli ya sehemu za kifua.

TIBA YA SARATANI YA MATITI - 5



Tunaendelea kuwaletea tiba ya saratani ya matiti baada ya kuelezea ile ya upasuaji. Endelea.
KEMIKALI MAALUM
Ugonjwa wa saratani ya matiti pia hutibiwa kwa njia ya dawa au Systemic theraphy. Tiba ya aina hii inahusisha matumizi ya kemikali maalum za kutibu saratani au Chemotherapy pamoja na kutumia homoni au Hormonal therapy.
Tiba kwa kutumia homoni, hufanywa ili kuua seli za saratani ambazo hazikugundulika hapo awali na ambazo huenda zikawa zimesambaa sehemu nyingine za mwili. Tiba hii hutolewa baada ya upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.
Tiba ya kutumia dawa za kemikali au Chemotheraphy kwa wagonjwa wa kansa ya matiti hutegemea ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye kwapa la mgonjwa ama la.
Tiba hii pia inaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani imeshasambaa mwilini kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji.
Baadhi ya kemikali zinazotumika kutibu saratani ya matiti ni Cyclophosphamide, Methotrexate na Flouracil. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa kujumuisha dawa mbili au tatu kwa wakati mmoja.
Ieleweke pia kuwa, kama ilivyo kwa dawa nyingine za kutibu magonjwa mengine tofauti na saratani, dawa hizi za saratani pia zina madhara mbalimbali kwa mtumiaji.
Madhara haya hutokana na ukweli kuwa, pamoja na kuwa kazi kuu ya kemikali hizi ni kuua seli zenye saratani, lakini pia huua na kuathiri seli za kawaida yaani zisizo na ugonjwa wa saratani kama vile seli zilizo kwenye mdomo, nywele, pua, kucha, utumbo na hata sehemu za siri za mwanamke.
Hata hivyo, tofauti na seli za saratani, seli za kawaida huwa na uwezo wa kuzaliana tena, kukua na kurudi katika hali yake ya kawaida.
Itaendelea

0 comments:

Post a Comment