Saturday, 27 September 2014

MBINU ZA KUJIKINGA NA SARATANI YA MATITI



SARATANI ya matiti ni moja kati ya aina za saratani zenye kuathiri wanawake wengi duniani, Tanzania ikiwemo. Kujikinga na ugonjwa huu hatari ni muhimu zaidi kuliko kupima na kujitambua kama tayari umeshakupata, hivyo katika makala ya leo, utajifunza dondoo muhimu za kufuata ili usipatwe kabisa na saratani hii.
Inakadiriwa kuwa kati ya asilimia 75 na 90 ya magonjwa ya saratani, inaweza kuzuilika kwa kubadili tu staili ya maisha kwa kufuata kanuni za ulaji vyakula sahihi na kujiepusha na vyakula hatari na mtindo wa maisha unaosababisha maradhi mbalimbali, ikiwemo saratani (cancer).
EPUKA SUKARI
Utafiti wa kisayansi umeonesha kuwa aina zote za sukari ni hatari kwa afya na sukari hurutubisha saratani. Sukari aina ya ‘fructose’ ndiyo mbaya zaidi na inatakiwa kuepukwa kadiri iwezekanavyo, hasa kwa mgonjwa wa saratani.
KULA  VITAMIN D
Vitamin D inahitajika karibu katika kila seli mwilini na ni mpiganaji mahiri dhidi ya chembechembe za saratani mwilini. Hivyo, kama wewe ni mgonjwa wa saratani, kiwango chako cha Vitamin D mwilini kinatakiwa kisiwe chini ya ujazo wa 70ng/ml. Unashauriwa kula kwa wingi vyakula na vidonge maalum vinavyoongeza vitamin hiyo (food supplements).
KULA  VITAMIN A 
Kuna ushahidi pia unaoonesha kwamba Vitamin A ina uwezo wa kuzuia ugonjwa wa saratani ya matiti. Ila inashauriwa kupata vitamin A kutokana na vyakula badala ya vidonge. Vyakula vyenye kiwango kingi cha vitamin A ni pamoja na nyama, maini na mayai ya kuku wa kienyeji, maziwa halisi na jibini.
UNENE KUPITA KIASI
Kuwa na unene wa kawaida kutakuja kwenyewe iwapo utazingatia suala la ulaji sahihi. Kuwa na uzito mkubwa kuliko mwili wako hukuweka katika hatari ya kupatwa na magonjwa mbalimbali, ikiwemo hatari ya kupatwa na saratani ya matiti, hivyo hakikisha hunenepi kupita kiasi.
JUISI YA MBOGA ZA MAJANI
Kuwa na utaratibu wa kutengeneza juisi asilia ya mboga za majani na kunywa glasi moja au nusu kila siku, ikiwa kama kinga ya mwili dhidi ya saratani ya matiti. 
POMBE
Jiepushe na unywaji wa pombe kupita kiasi au jiwekee kikomo cha kinywaji kimoja cha pombe kwa siku. Unywaji wa pombe kupita kiasi huchangia kudhoofisha kinga ya mwili na hivyo kukuweka katika hatari ya kupatwa na saratani ya matiti.
Kwa ujumla, ukizingatia haya yaliyoelezwa hapo juu pamoja na kufanya mazoezi, utajihakikishia kinga imara dhidi ya ugonjwa wa saratani ya matiti na kwa wale ambao tayari wamekutwa na ugonjwa huu, watakuwa wanadhibiti athari kuenea mwilini na pengine kupunguza makali bila kutumia dawa.

0 comments:

Post a Comment