Showing posts with label MAGONJWA YA FIGO. Show all posts
Showing posts with label MAGONJWA YA FIGO. Show all posts

Friday, 10 October 2014

FIGO KUSHINDWA KUFANYA KAZI (RENAL/KIDNEY FAILURE)




Figo ni miongoni mwa viungo muhimu sana katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu. Kwa kawaida, mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana kama yale ya maharage, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo, chini kidogo ya mbavu za chini. 





Kazi za figo


Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu kadhaa katika damu na hivyo kusaidia katika kuhifadhi na kuthibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini. Katika kutekeleza hayo, figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika. 



Kazi nyingine za mafigo ni



  • Kurekebisha na kuthibiti kiasi cha vitu mbalimbali katika damu pamoja na kiasi cha maji katika mwili
  • Husaidia kutengeneza kiasili cha erythropoietin ambacho ni muhimu sana katika utengenezaji wa chembe nyekundu za damu.
  • Husaidia uzalishaji wa vitamini D
  • Husaidia pia katika kuthibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure)




Utengenezaji wa mkojo



Kwa kawaida damu inayozunguka mwilini hatimaye huingia kwenye figo kwa ajili ya kuchujwa, kutoa uchafu pamoja na sumu nyingine zisizohitajika mwilini. Kitendo hiki cha utengenezaji mkojo hufanyika katika hatua kuu zifuatazo;



  • Hatua ya kwanza ni uchujaji. Damu kutoka nje huingia ndani ya mafigo na kupita kwenye glomeruli, lenye umbo kama chekeche/chujio ambalo limeundwa na mishipa mingi midogo ya damu iliyojizungusha pamoja. Vitu mbali mbali, maji pamoja na sumu zilizo katika damu inayopita kwenye vimishipa hivi na kisha kuingia katika mirija mingine mikubwa kwa ajili ya uchujaji zaidi. 
  • Mirija inayofuata huendelea kuchuja damu na kunyonya baadhi ya vitu vilivyo chujwa kimakosa kuvirudisha mwilini, mpaka kiasi sahihi cha uchafu kinachotakiwa kuchujwa kinapokuwa kimefikiwa. 
  • Mara baada ya mkojo kutengenezwa na kutolewa kwenye figo, husafiri kuingia kwenye kibofu cha mkojo kwa kupita kwenye mirija ijulikanayo kama ureta. Kutoka kwenye kibofu, mkojo hutolewa nje ya mwili kupitia kwenye mrija waurethra.







Figo kushindwa kufanya kazi (Renal Failure/ Kidney Failure)



Kushindwa kufanya kazi kwa figo hutokea iwapo sehemu ya figo au figo lote litapoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kutoka katika damu na kutengeneza mkojo. Kitendo hiki husababisha kusanyiko la uchafu pamoja na sumu kadhaa katika damu ambazo ni hatari kwa afya ya mhusika. 

Aina za figo kushindwa kufanya kazi

Figo kushindwa kufanya kazi kumeganyika katika makundi yafuatayo



  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) au Acute Kidney Failure (AKF). 
  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa kiasi (Mild renal/kidney insufficiency)
  • Tatizo sugu la figo kushindwa kufanya kazi (Chronic renal failure) 




Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (Acute Renal Failure (ARF) 



Hii ni hali inayotokea kwa ghafla, na kudumu kwa saa chache mpaka siku chini ya 14, na kusababisha ongezeko la kiwango cha creatinine na urea katika damu. Hali hii huwapata karibu asilimia 5% ya wagonjwa waliolazwa hospitali kwa sababu ya matatizo mbalimbali. Aidha hali hii hutokea zaidi kwa wagonjwa mahututi na wale wanaohitaji uangalizi wa kipekee, yaani waliolazwa ICU.



Katika makala hii tutatumia zaidi kifupisho cha ARF.




Visababishi na aina za ARF



Visababishi (au aina) vya ARF vinaweza kugawanywa katika makundi makuu matatu:



  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal causes/failure) 
  • Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure) 
  • Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)





Matatizo yanayoathiri mtiririko wa damu kabla ya kuingia katika figo (Prerenal 

causes/failure) 



Aina hii hutokea kwa takribani asilimia 60 mpaka 70 ya ARF zote. Katika kundi hili, figo hukosa damu ya kutosha kwa ajili ya kuchuja na hatimaye hushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Mambo yanayoweza kusababisha prerenal failure ni pamoja na:



  • Upungufu wa maji mwili unaosababishwa na kutapika kupita kiasi, kuharisha, au kupoteza damu kupita kiasi (kwa sababu ya ajali au kuumia) 
  • Kuvurugika kwa mtiririko wa damu inayoingia kwenye figo kwa sababu ya: 

    • Kushuka kwa ghafla kwa shinikizo la damu kwa sababu ya kupoteza damu nyingi wakati wa upasuaji mkubwa, kuumia au kuungua sehemu kubwa ya mwili, au maambukizi katika mfumo wa damu (sepsis) yanayoweza kufanya mishipa ya damu kutanuka na kushusha shinikizo la damu 
    • Kuziba au kusinyaa kwa mishipa inayopeleka damu kwenye figo 
    • Moyo kushindwa kufanya kazi (heart failure) au shambulio la moyo (heart attack) linalosababisha kushuka kwashinikizo la damu 
    • Ini kushindwa kufanya kazi (liver failure) kunakoweza kusababisha mabadiliko katika mfumo wa homoni zinazoathiri shinikizo la damu pamoja na mtiririko wa damu kwenda kwenye figo.



Mwanzoni kabisa mwa pre-renal failure huwa hakuna athari yoyote inayotokea kwenye figo, na mara nyingi, figo laweza kurudi katika hali yake ya kawaida iwapo chanzo cha tatizo kitagunduliwa na kushughulikiwa ipasavyo. 



Matatizo ndani ya figo lenyewe yanayozuia na kuathiri uchujaji wa damu au uzalishaji wa mkojo (Renal causes/failure) 



Mambo yanayosababisha madhara katika figo husababaisha karibu asilimia 25 mpaka 40 ya vyanzo vyote vya ARF. Visababishi vilivyo katika kundi hili hujumuisha vile vinavyoathiri uchujaji, mtiririko wa damu ndani ya figo na seli za figo zinazoshughulika na uchujaji na ufyonzaji wa chumvi na maji. 



Visababishi hivyo ni pamoja na:



  • Magonjwa katika mishipa ya damu 
  • Kuwepo kwa damu iliyoganda ndani ya mishipa ya damu inayopita katika figo 
  • Ajali/Kuharibika kwa tishu na seli za figo 
  • Magonjwa ya mzio katika glomeruli na figo kwa ujumla (glomerulonephritis). Magonjwa yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na maambukizi (infection) ya bacteria jamii ya streptococci. 
  • Magonjwa ya mzio katika nyama za figo (acute interstitial nepthritis). Mambo yanayoweza kusababisha hali hii ni pamoja na matumizi ya baadhi ya madawa kama vile Aspirin, Ibuprofen (Brufen), baadhi ya antibiotics, na baadhi ya dawa za kutoa maji mwilini (antidiuretics); magonjwa kama vile saratani ya damu (leukemia), lupus na lymphoma. Magonjwa ya mzio katika nyama za figo husababisha madhara katika seli zinazohusika na uchujaji na ufynzaji wa chumvi na maji. 
  • Magonjwa ya ukosefu wa damu katika mirija ya figo (acute tubular necrosis) ambayo hufanya seli na tishu za mirija hii kufa na hivyo mirija kushindwa kufyonza chumvi na maji kuyarudisha mwilini. Mambo yanayosababisha hali hii ni pamoja na shock (upungufu wa damu kuingia kwenye figo), matumizi ya madawa kama vile baadhi ya antibiotiki, sumu, dawa zinazotumika viwandani na kwenye x-rays na baadhi ya madawa yanayotumika kutibu saratani.




Matatizo yanayoathiri mtiririko wa mkojo nje ya figo (Postrenal causes/failure)



Mambo yanayosababisha hali hii huchangia kati ya silimia 5 mpaka 10 ya vyanzo vyote vya ARF. Postrenal failure wakati mwingine huitwa pia obstructive renal failure kwa sababu husababishwa na mambo yanayozuia utoaji wa mkojo nje ya figo. 



Kuziba kwa ureta moja ama zote mbili kunaweza kusababishwa na:



  • Vijiwe figo (renal stones) 
  • Saratani ya viungo vya njia ya mkojo au viungo vilivyo karibu na njia ya mkojo kiasi cha kuzuia mkojo kutoka nje ya figo 
  • Matumizi ya baadhi ya madawa



Kuziba kwa njia ya mkojo katika eneo la kibofu cha mkojo kunaweza kutokana na:







Tafsiri nyingine ya ARF



Wagonjwa wa ARF wanaweza kupata mkojo kidogo sana au wasipate kabisa., au wanaweza kuwa na ongezeko la creatinine kwa kasi ya kutisha au kwa kasi ndogo sana. Hali hizi zinaweza pia kutumika kutoa tafsiri nyingine ya maana ya ARF. 



Mtu anayetoa kiasi cha mkojo chini ya 400mL kwa siku hujulikana kama ana oliguria, na huchukuliwa kuwa ana hali mbaya ya kutoweza kupona. 



Mtu anayetoa mkojo chini ya 100mLkwa siku husemwa ana Anuria, ambayo kama imetokea ghafla, huashiria kuwepo kwa tatizo la kuziba kwa mirija inayotoa mkojo kwenye figo zote mbili, na mara niyingi hali hii ni ya hatari zaidi. Tafsiri hii husaidia sana katika kuamua aina ya matibabu na muda wa kumpatia mgonjwa matibabu ili kuepusha madhara zaidi yanayoweza kumpata. 



Dalili za ARF



Katika hatua za mwanzo mwanzo, baadhi ya waathirika wanaweza wasioneshe dalili zozote za tatizo hili. Dalili ni kama 



  • Kupungua kwa uzalishaji mkojo 
  • Kuvimba mwili 
  • Kupoteza umakini 
  • kuchanganyikiwa 
  • Uchovu 
  • Kulegea mwili 
  • Kichefuchefu na kutapika 
  • Kuharisha 
  • Maumivu ya tumbo 
  • Kuhisi ladha ya chuma na uchachu mdomoni
  • Na katika hatua za mwisho kabisa, mgonjwa anaweza kupata degedege na hatimaye kupoteza fahamu (coma).




Vipimo na uchunguzi



Kama ilivyoainishwa hapo juu kuwa baadhi ya wagonjwa wanaweza wasiwe na dalili zozote za tatizo hili. Hata wale wenye kuonesha dalili, zinaweza zisiwe mahsusi (non-specific). Uchunguzi wa mwili unaweza usioneshe tatizo lolote lile, au kukawa na dalili chache sana ambazo zinaweza zisimsaidie sana daktari kufikia uamuzi. 



Baadhi ya vipimo vinavyoweza kugundua uwepo wa ARF ni pamoja na



  • Kipimo cha utendaji kazi wa figo (Renal function tests) ambacho husaidia kuchunguza kiwango cha urea (blood urea nitrogen (BUN) katika damu. Aidha husaidia pia kuchunguza ongezeko la kiwango cha creatinine katika damu. 
  • Uchunguzi wa kiwango cha madini mbalimbali katika damu (blood electrolytes) 
  • Uchunguzi wa damu (Full Blood Picture): Husaidia kuonesha uwepo wa maambukizi ya bacteria na/au upungufu wa damu mwilini (anaemia) 
  • Kupima kiasi cha mkojo kinachotolewa na mgonjwa katika masaa 24 
  • Uchunguzi wa mkojo (Urine analysis): Rangi ya mkojo, kiasi cha electrolytes, uwepo wa usaha au damu au casts.
  • Ultrasound ya figo na kibofu cha mkojo 
  • Renal biopsy. 




Matibabu ya ARF



Matibabu ya ARF hutegemea kwanza chanzo chake na pili ukubwa wa tatizo. Kujua chanzo cha tatizo husaidia kufahamu ni aina gani ya matibabu yanayohitajika wakati kufahamu ukubwa wa tatizo huathiri uchaguzi wa aina ya matibabu na hata hitaji la kufanya dialysis. Hata hivyo inashauriwa sana kumpeleka mgonjwa kwa daktari bingwa wa magonjwa ya figo (nephrologist) kwa matibabu zaidi.



Kulingana na chanzo cha ARF, baadhi ya matibabu yanayoweza kufanyika, hutolewa yakiwa na lengo la:



  • Kurekebisha kiasi cha upotevu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa i.v fluids pamoja kurekebisha kiasi cha madini (electrolytes) kilichopotea 
  • Kupunguza au kuzuia ongezeko la maji kwa wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kabisa kutoa maji nje ya mwili 
  • Kuongeza uwezo wa moyo kufanya kazi vizuri au kuongeza shinikizo la damu husaidia kuongeza mtiririko wa damu kwenda kwenye figo 
  • Kurekebisha kiasi cha madini mwilini kitendo ambacho husaidia mwili kufanya kazi zake vema 




Dialysis



Iwapo pamoja na matibabu hayo, figo za mgonjwa zinaendelea kudorora, mgonjwa hana budi kufanyiwa dialysis. Dialysis ni kitendo cha kutoa uchafu na maji yasiyohitajika katika damu. Kitendo hiki hufanywa kwa kupitia mishipa ya damu iliyo chini ya ngozi (hemodialysis) au kwa kupitia tumboni (peritoneal dialysis). Katika hemodialysis mirija hii huunganiswa kwenye mashine ambayo hufanya kazi kama figo. Damu kutoka kwa mgonjwa huingia katika mashine kisha huchujwa ili kuondoa sumu, uchafu pamoja na maji yasiyohitajika kabla ya kurejeshwa tena mwilini. 



Kitendo hiki hufanyika angalau mara mbili mpaka tatu kwa wiki, na kwa kiasi fulani ni ghali na si watu wote wa kipato cha chini wanaoweza kumudu gharama zake.



Katika peritoneal dialysis, uchafu pamoja na maji kutoka katika mzunguko wa damu huingia katika nafasi inayotenganisha tumbo na utando wake (peritoneal space), huchujwa kwenye utando huo kisha hutolewa kupitia sindano maalum (catheter ) iliyowekwa juu ya ngozi na kuingia ndani ya tumbo (peritoneal cavity).



Matarajio



Wagonjwa wengi wenye ARF hupona bila hata kuhitaji dialysis mara tu chanzo cha tatizo kinapogundulika na kushughuikiwa mapema. Hata hivyo wakati mwingine, pamoja na matibabu, baadhi ya figo hushindwa kurudia kufanya kazi kwa ufanisi wake wa awali. Watu kama hawa hawa wanahitaji kufuatiliwa kwa ukaribu na umakini mkubwa. 



Kinga ya ARF



Inashauriwa



  1. kufanya uchunguzi wa figo walau mara moja kila mwaka. Hii husaidia kuchunguza utendaji wa figo na hivyo kuepuka madhara kabla hayajatokea. 
  2. Kunywa maji kwa wingi ili kuyafanya mafigo yatende kazi zake kwa ufanisi.
  3. Kuepuka matumizi ya vitu ama madawa yanayoweza kuathiri nyama, seli au tishu za figo. Ni vema kutumia dawa pale tu unaposhauriwa na daktari.
  4. Watu wenye hatari ya kupata tatizo sugu la kushindwa kufanya kazi kwa figo (Chronic Renal Failure) wanashauriwa kufanya vipimo na cuhunguzi mara kwa mara
  5. Muone mtaalamu wa afya mara tu uonapo dalili za kuwepo kwa shida katika kukojoa au uonapo damu katika mkojo.

Sunday, 11 May 2014

UGONJWA WA NEPPHROTIC SYNDROME

                                             

Ugonjwa wa Nephrotic syndrome ni hali ya maradhi inayokumba figo na kusababisha kupoteza kiasi kingi cha protini kutoka kwenye damu kuingia kwenye mkojo. Kiasi cha protini kinachopotea ni wastani wa gram 3.5 kwa siku kwa kila mita za mraba 1.73 za mwili.Chujio za

figo (glomeruli) huwa na vitundu vidogo vidogo viitwavyo podocytesambavyo hufanya kazi ya kuchuja uchafu na sumu nyingine kutoka mwilini na kuzitoa nje. Vitundu hivi vina uwezo wa kuzuia protini isichujwe kuingia kwenye mkojo. Hata hivyo, figo zenye Nephrotic syndrome

huwa na podocytes kubwa kiasi cha kuweza kupitisha protini za ukubwa mbalimbali (zikiwepo albumin ambazo ni protini zenye kipenyo kikubwa zaidi). Pamoja na kuharibika huku kwa

chujio,podocytes bado hazina ukubwa wa kuweza kupitisha seli nyekundu za damu ndiyo maana mkojo wa mgonjwa wa Nephrotic syndrome hauna damu ndani yake.
Ukubwa wa tatizo 


Nephrotic syndrome
 huathiri karibu watu wa rika zote. Hata hivyo watoto walio katika umri wa miaka 2 mpaka sita ndiyo waathirika wakuu wa ugonjwa huu. Ugonjwa huu umeonekana kuwapata zaidi watoto wa kiume kuliko wa kike.

Visababishi vya Nephrotic syndrome
Visababishi vya Nephrotic syndrome vimegawanyika katika makundi mawili; yale yanayosababishwa na magonjwa yaliyo ndani ya figo zenyewe (primary nephrotic syndrome), au yale yanayosababishwa na magonjwa yaliyo nje ya figo (secondary nephotic syndrome).


Visababishi vilivyo ndani ya figo (primary nephrotic syndrome)

Kipimo cha biopsy husaidia kutambua magonjwa yanayosababisha Nephrotic syndrome ndani ya figo lenyewe. Kwa watoto wadogo, chanzo kikuu cha Nephrotic syndrome ndani ya figo zenyewe ni ugonjwa unaoitwa

Minimal change disease (MCD
) wakati kwa watu wazima ni Focal segmental glomerulosclerosis (FSGS) pamoja na Membraneous nephropathy (MN). Magonjwa haya yote husababisha uharibifu katika chujio na hivyo kuruhusu upotevu wa protini katika mkojo.

Visababishi vilivyo nje ya figo (secondary nephrotic syndrome)
Kama ilivyo kwa magonjwa yanayosababisha nephrotic syndrome ndani ya figo, magonjwa yanayosababisha nephrotic syndrome nje ya figo (secondary causes) nayo pia husababisha uharibifu katika chujio za figo. Magonjwa haya ni pamoja na

  • Maambukizi katika ini (hepatitis B na C)
  • Ugonjwa wa kisukari
  • Matumizi ya baadhi ya dawa kama vile dawa za kupunguza mcharuko mwili (corticosteroids) pamoja na NSAIDS kama vile Aspirin.
  • Matumizi ya madawa ya kulevya kama vile heroin
  • Baadhi ya kemikali kama madini ya dhahabu
  • Maambukizi ya bacteria kama kaswende na bacteria wanaosababisha ukoma
  • Ugonjwa wa malaria
  • Saratani za aina mbalimbali kama vile saratani ya damu (leukemia)
  • Kung’atwa na nyuki
  • Ukimwi
  • Shinikizo la damu
  • Magonjwa yanayoathiri mwili mzima kama vile Sarcoidosis, systemic lupus erythematosusau Sjogren’s syndrome
Viashiria pamoja na dalili
Ugonjwa huu ni mkusanyiko wa mambo/dalili kuu nne (ingawa mgonjwa anaweza kuwa na dalili nyingine kadhaa).

Mambo hayo ni

  • Kupoteza kiasi kikubwa cha protini katika mkojo (protenuria) zaidi ya gram 3.5 kwa siku
  • Kuwa na upungufu wa protini aina ya albumin katika damu (hypoalbuminemia)
  • Kuwa na ongezeko la mafuta (lipids) katika damu (hyperlipidemia), na
  • Kuvimba (edema) mwili mzima (generalized edema au anasarca)

Ongezeko la mafuta katika damu yaani hyperlipidemia husababishwa na mambo mawili; kwanza upotevu wa protini katika mkojo husababisha upungufu mkubwa wa protini kwenye damu.
Ili kufidia upungufu huo, ini hulazimika kutengeneza protini nyingi kuliko kawaida hali ambayo husababisha ongezeko siyo tu la protini bali viasili vyenye mchanganyiko wa protini na mafuta yaani lipoproteins. Pili, upungufu wa protini husababisha pia

upungufu wa baadhi ya vimeng’enyo muhimu mwilini, kimojawapo kikiwa lipoprotein lipase ambacho huchochea kuvunjika kwa mafuta mwilini. Kukosekana kwa kimeng’enyo hiki hufanya mafuta yasiweze kuvunjwa na hatimaye kusababisha mrundikano wa mafuta katika damu.

Kupungua kwa protini hususani protini aina ya albumin katika damu (hypoalbuminemia) husababisha kupungua kwa shinikizo linalosaidia kutunza maji katika mzunguko wa damu (oncotic pressure). Madhara ya kupungua kwa shinikizo hilo husababisha maji kutoka katika mzunguko wa damu na kurundikana katika

sehemu mbalimbali za mwili. Madhara yake ni kufanya kiasi cha maji katika mzunguko wa damu kuwa chini (hypovolemia) kwa sababu maji mengi huingia kwenye nafasi zilizo katika ya seli na seli. Mrundikano wa maji mwilini husababisha

  • kuvimba uso hasa sehemu za macho, hususani nyakati za asubuhi (morning facial puffiness)
  • Kuvimba kwa miguu (hubonyea kama ikiminywa kwa vidole) (pitting edema)
  • Maji katika kifua na mapafu (pleural effusion)
  • Maji kujaa tumboni (ascites), na
  • Kuvimba mwili mzima (anasarca)

Dalili nyingine ni pamoja

  • upungufu wa damu (anaemia)
  • Kupumua kwa shida
  • Kukojoa mkojo mzito kama povu kwa sababu ya protini nyingi kwenye mkojo
  • Dalili zinazoambatana na kisababishi cha nephrotic syndrome kama vile dalili za kisukari, malaria na magonjwa mengine
  • Kiwango cha kawaida cha shinikizo la damu. Wagonjwa wa nephrotic syndrome huwa na BP za kawaida isipokuwa kwa nadra sana BP inaweza kuwa juu.

Vipimo na uchunguzi

Baada ya kusikiliza historia ya mgonjwa na kufahamu mambo yanayomsumbua (dalili), daktari humfanyia mgonjwa uchunguzi wa mwili (physical examination) ili kutambua vishiria zaidi vya tatizo hili.
Vipimo vya maabara hufanyika ili kuchunguza utendaji kazi wa figo, ni kwa kiasi gani yameathirika na pia kufahamu visababishi vya tatizo hili ikiwa ni pamoja na kuchunguza magonjwa mengine ambayo yanaweza kufanana na nephrotic syndrome kidalili.

Vipimo ni pamoja na:

  • kuchunguza kiasi cha albumin katika damu
  • Kuchunguza kiasi cha madini katika damu (comprehensive metabolic panel)
  • Vipimo vya utendaji kazi figo kama vile Blood Urea Nitrogen (BUN), Serum creatinine pamoja na creatinine clearance
  • Kipimo cha mkojo cha urinalysis
  • Kuchunguza kiasi cha mafuta katika damu (blood cholesteroal na triglycerides levels), pamoja na
  • Biopsy ya figo (renal biopsy)

Vipimo vya kutambua visababishi vya nephrotic syndrome ni pamoja;

  • kipimo cha VVU
  • Kipimo cha kaswende
  • Kipimo cha maambukizi katika ini (Hepatitis B na C antibodies/Hepatitis panel)
  • Vipimo vya mfumo wa kinga ya mwili (antinuclear antibody tests, complement levels nacryoglobulins levels) na mcharuko mwili (Rheumatoid factor)
  • Vipimo vya kisukari
  • Kiasi na aina za protini katika damu na mkojo (serum protein elecrophoresis na urine protein elecrophoresis)

Kadhalika, vipimo vya kutambua madhara yaliyosababishwa na nephrotic syndrome ni pamoja na;

  • Kiwango cha vitamin D katika damu
  • Kiasi cha madini chuma kwenye damu
  • Na uwepo wa casts katika mkojo

Matibabu

Malengo ya tiba ya nephrotic syndrome ni kupunguza dalili za ugonjwa, kupunguza madhara ya ugonjwa na pia kupunguza kasi ya uharibifu katika figo. Ili kuthibiti vizuri nephrotic syndrome ni vema sana kutibu chanzo cha tatizo lenyewe. Wakati mwingine mgonjwa anaweza kuhitaji matibabu kwa maisha yake yote.

Matibabu yamegawanyika katika; yale ya kusaidia kupunguza dalili na kumpatia nafuu mgonjwa, yale ya kutibu chanzo cha ugonjwa, na ya kutumia lishe maalum ili kupunguza ongezeko la vitu visivyohitajika mwilini au kurejesha baadhi ya vitu vilivyopungua.

Matibabu kwa ajili ya kupunguza dalili ni pamoja na

  • kuthibiti na kuhakikisha kiasi cha maji katika mwili kipo katika viwango sahihi. Hili hufanyika kwa kupima mara kwa mara kiasi cha mkojo kinachotolewa pamoja na shinikizo, kupunguza unywaji maji kufikia angalau lita moja kwa siku na kutumia dawa za kupunguza maji mwilini kama vile frusemide.
  • Njia nyingine ni kupima utendaji kazi wa figo mara kwa mara
  • Kushusha kiasi cha mafuta mwilini kwa kutumia dawa ili kuzuia madhara zaidi katika mishipa ya damu
  • Dawa za kuzuia damu kuganda pia zaweza kutumika

Matibabu ya chanzo cha nephrotic syndrome
ni pamoja na

  • ili kupunguza mcharuko mwili na pengine kumaliza kabisa tatizo hilo, dawa za jamii ya cosrticosteroids kama vile prednisolone hutumika ili kuthibiti na kushusha kwa muda kinga ya mwili
  • Kushusha na kuthibiti shinikizo la damu kuhakikisha lipo 130/80mmHg au chini yake. Lengo kuu ni kuzuia uharibifu zaidi katika figo. Kufanikisha hili, dawa za jamii ya Angiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors kwa mfano captopril au angiotensio receptor blockers (ARBs) hutumika. Dawa za jamii ya ACE inhibitors pia husaidia kupunguza upotevu zaidi wa protini katika mkojo.
  • Kutibu na kuthibiti kisukari iwapo mgonjwa ana kisukari

Matibabu kwa njia ya lishe hujumuisha

  • kupunguza matumizi ya chumvi katika chakula kufikia angalau gramu 1000 mpaka 2000 kwa siku. Epuka matumizi ya vyakula vya makopo, nyama za kuoka, na vyakula vya magengeni au madukani (fast foods). chumvi kidogo husaidia kupunguza mrundikano wa maji mwilini na uvimbe
  • Kula lishe yenye kiasi cha wastani cha protini inayotokana na wanyama kama vile nyama ya ng’ombe isiyo na mafuta, samaki au ndege (kuku, bata). Kiasi kinachoshauriwa ni walau gramu moja ya protini kwa kila kilo moja ya mlo unaokula.
  • Ingawa baadhi ya tafiti zinaonesha hakuna faida ya kula chakula chenye mafuta na lehemu kidogo kwa mgonjwa wa nephrotic syndrome, lakini kiujumla wataalamu wengi wanashauri kuepuka kula vyakula vyenye mafuta kwa wingi, hasa yale yenye lehemu (cholesterol). Ni vema kuepuka vyakula vyenye mafuta yasiyofaa (saturated fats) kama vile jibini, siagi, vyakula vya kuokwa, nyama yenye mafuta, kiini cha yai, na ngozi ya ndege kama kuku. Inashauriwa kula zaidi vyakula vyenye mafuta yanayofaa (unsaturated fats) kwa mfano mafuta ya mizeituni (olive oil), mafuta ya karanga, maparachichi, samaki pamoja na vyakula vya jamii ya njugu. Aidha dawa za kupunguza kiasi cha mafuta (statins) nazo husaidia sana. Lengo kuu la matibabu haya ni kupunguza uwezekano wa kupata maradhi ya moyo na mishipa ya damu kwa ujumla.
  • Inashauriwa pia kuongeza ulaji wa matunda na mboga za majani.
  • Na pia matumizi ya vidonge vya kuongeza vitamini D

Madhara ya nephrotic syndrome

Ugonjwa wa nephrotic syndrome huathiri karibu kila sehemu ya mwili. Baadhi ya madhara ya ugonjwa huu ni;

  • Upungufu wa damu mwilini
  • Kuziba kwa vena (mishipa ya damu inayorudisha damu kwenye moyo) (venous thrombosis) hususani vena za figo (renal veins).
  • Maambukizi ya bacteria mbalimbali (kwa mfano Haemophilus influenzae na Streptococcus pneumoniae) kwa sababu ya upungufu wa protini zinazosaidia kutengeneza seli za mfumo wa kinga ya mwili (immunoglobulins).
  • Kujaa maji katika mapafu (pulmonary edema)
  • Figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla (ARF) kwa sababu ya upungufu wa maji katika mzunguko wa damu.
  • Matatizo ya mifupa kwa sababu ya upungufu wa vitamini D
  • Ukuaji wa kusuasua ambao husababishwa na upotevu wa protini nyingi katika mkojo, matumizi ya dawa za kupunguza mcharuko mwili na hata ulaji wa shida kwa sababu ya mgonjwa kujihisi kichefuchefu cha mara kwa mara.
  • Upungufu wa homoni ya thyroid (hypothyroidism) kwa sababu ya upotevu wa protini (thyroid binding globulin) inayosaidia utengenezaji wa homoni hiyo.
  • Upungufu wa madini ya calcium, na hata
  • Ugonjwa wa homoni wa Cushing’s syndrome.
  • Moyo kushindwa kufanya kazi (congestive cardic failure)
  • Utapiamlo
Matarajio
Matokeo ya ugonjwa huu hutofautiana kati ya mgonjwa na mgonjwa kulingana na chanzo chake. Kwa wengine ugonjwa unaweza kuja kwa ghafla na kupona baada ya muda mfupi wakati kwa wengine huwa sugu na kuchukua muda mrefu kupona au pengine kuhitaji mgonjwa kubadilishwa figo. Kwa ujumla, watoto wenye nephrotic syndrome iliyosababishwa na ugonjwa wa minimal change disease wana matokeo mazuri baada ya kutibiwa na dawa za kupunguza mcharuko mwili (steroids) wakati watu wazima wenye nephrotic syndrome iliyosababishwa na ugonjwa wa focal segmental glomerulosclerosis mara nyingi huishia kupata uharibifu mkubwa katika figo hatimaye figo hufa kabisa (End stage renal disease, ESRD).

Kinga 
Ni muhimu kufahamu vyanzo vinavyosababisha nephrotic syndrome. Kuweza kuthibiti vyanzo hivyo, kwa mfano maambukizi kama ya Ukimwi, malaria, kaswende, ukoma, na mengineyo, husaidia kupunguza uwezekano na kujikinga dhidi ugonjwa wa nephrotic syndrome.

KUHARIBIKA KWA CHUJIO ZA FIGO ( ACUTE BLOMERULONEPHRITIS)



Kuharibika kwa chujio amaGlomerulonephritis ni aina ya ugonjwa wa figo unaoathiri sehemu maalum ya figo (chujio) inayohusika na uchujaji wa maji pamoja na uchafu kutoka katika damu. Sehemu hii huitwaglomelurus au chujio kama tutakavyokuwa tukitumia katika mada hii.
Visababishi
Mara nyingi chanzo halisi cha kuharibika kwa chujio za figo(glomerulonephritis) huwa hakijulikani. Hata hivyo wakati mwingine uharibifu huu unaweza kusababishwa na kushambuliwa na mfumo wa kinga ya mwili. Uharibifu katika chujio husababisha damu pamoja na protini kuingia katika mkojo.
Tatizo hili hukua kwa haraka na figo linaweza kupoteza uwezo wake wa kuchuja maji na uchafu kwa kasi ndani ya muda mfupi wa kati wiki chache mpaka miezi kadhaa. Aina hii ya kuharibika kwa chujio za figo kwa haraka hujulikana kitalaamu kama rapidly progressive glomerulonephritis.
Ukubwa wa tatizo na vihatarishi vyake
Takribani robo ya watu wanaopatwa na tatizo sugu la glomerulonephritishuwa hawana historia ya kuwa na ugonjwa wowote wa figo hapo kabla.
Kuna mambo kadhaa yanayoweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kupataglomerulonephritis. Mambo hayo ni pamoja na:
  • Matatizo katika mfumo wake wa damu au lymph
  • Kuwahi kutumia vimiminika vilivyotengenezwa kwa kemikali zahydrocarbon
  • Wenye historia ya saratani
  • Maambukizi ya bakteria aina ya streptococcus, virusi, majipu au maambukizi katika moyo
  • Mambo mengine yanayoweza kuongeza hatari ya kupatwa naglomerulonephritis ni pamoja na:
  • Magonjwa ya mishipa ya damu kama vile vasculitis au polyarteritis
  • Matumizi yaliyopitiliza ya dawa za kutuliza maumivu za jamii ya Non steroidal anti-inflammatory drugs kama vile aspirin
  • Magonjwa ya mfumo wa kinga ya mwili kama vile Anti-glomerular basement membrane antibody disease na IgA nephropathy
  • Makovu katika chujio (Focal segmental glomerulosclerosis) au hali ya chujio kuwa na kuta nene kuliko kawaida (Membranoproliferative GN)
  • Magonjwa yanayoathiri viungo mbalimbali vya mwili kama vileHenoch-Schonlein purpura, Goodpasture’s syndrome au Lupus nephritis
  • Ugonjwa wa kimetaboliki wa Amyloidosis
Dalili
Dalili kuu za glomerulonephritis ni kuwa na damu katika mkojo (hali inayoufanya mkojo kuwa na rangi kama nyeusi, kutu au samawati; mkojo kuwa kama wenye povu jingi (kwa sababu ya kuwa na protini nyingi kuliko kawaida) na kuvimba uso, macho, miguu au tumbo (hali inayojulikana kamaedema)
Dalili nyingine ni pamoja na
  • Maumivu ya tumbo
  • Kutapika damu
  • Kuharisha au kupata choo kikubwa chenye kuchanganyika na damu
  • Kukohoa pamoja na kupumua kwa shida
  • Kukojoa kupita kiasi
  • Homa
  • Maumivu ya misuli na viungo, uchovu, maumivu ya mwili mzima pamoja na kukosa hamu ya kula
  • Kutokwa na damu puani
Baada ya muda, figo hushindwa kufanya kazi na mgonjwa huanza kuwa na dalili za mtu mwenye ugonjwa sugu wa figo.

Uchunguzi na vipimo
Kwa kawaida tatizo la uharibifu wa chujio za figo hutokea tatratibu sana hali inayoweza kufanya ugunduzi wake kuchelewa pia. Wengi wa wagonjwa wenye tatizo hili hugunduliwa pale wanapokwenda hospitali kwa ajili ya uchunguzi wa matatizo mengine. Mara nyingi hali hii hujidhihirisha kwa kuwepo na hitilafu katika kipimo cha urinalysis.
Mambo makuu matatu yanaweza kuonesha kuwepo kwa uharibifu katika chujio za figo. Mambo hayo ni upungufu wa damu (anemia), shinikizo la damu kuwa juu na ishara za kupungua kwa utendaji kazi wa figo.
Vipimo vinavyoweza kufanywa hujumuisha vipimo vya mkojo, damu pamoja na picha kama vile Ultrasound, CT au SPECT/CT.
Vipimo vya mkojo kama vile urinalysis husaidia kuonesha:
  • Utendaji kazi wa figo yaani Creatinine clearance pamoja na Urine creatinine
  • Uchunguzi wa mkojo kwa kutumia hadubini
  • Kiasi cha protini katika mkojo
  • Kiasi cha tindikali ya urea katika mkojo
  • Chembe nyekundu za damu (RBC) katika mkojo
  • Specific gravity ya mkojo na kiasi cha chumvi kwenye mkojo (yaaniurine osmolality)
Vipimo vingine ni pamoja na CT scan, ultrasound ya figo, X-ray ya kifua auIntravenous pyelogram (IVP)
Vipimo vya damu husaidia kuonesha:
  • Kiasi cha protini ya albumin katika damu
  • Utendaji kazi figo kuchunguza kiasi cha BUN na creatinine katika damu
  • Viasili vinavyohusika katika mfumo wa kinga ya mwili kama vile Anti-glomerular basement membrane antibody, Anti-neutrophil cytoplasmic antibodies (ANCAs), Anti-nuclear antibodies au Complement levels.
Ili kuthibitisha uwepo wa tatizo hili na aina yake, kipimo cha biopsy (renal biopsy) hutumika.
Matibabu
Matibabu ya glomerulonephritis hutegemea sana na kisababishi cha tatizo hili, aina yake pamoja na ukubwa wa tatizo lenyewe yaani wingi wa dalili pamoja na uzito wake. Dalili ya muhimu sana kuithibiti ni ongezeko la shinikizo la damu ingawa kwa kawaida huwa ni ngumu sana kuthibiti shinikizo la damu kuwa katika kiwango cha kawaida.
Mgonjwa anashauriwa pia kupunguza kiasi cha chumvi katika chakula chake na pia kiasi cha protini na maji anayokunywa ili kusaidia utendaji kazi wa figo.
Dawa zinazoweza kutumika kwa mgonjwa mwenye tatizo hili ni pamoja na:
  • Zile za kushusha na kuthibiti shinikizo la damu hususani za jamii yaAngiotensin-converting enzyme (ACE) inhibitors kama vilecaptopril, Lisinopril au Enalapril; na zile za jamii ya Angiotensin receptor blockers kama vile losartan, Valsartan na Irbesartan.
  • Zile za jamii ya Corticosteroids kwa ajili ya kupunguza na kuondoa mcharuko mwili
  • Zile za kupunguza nguvu ya mfumo wa kinga ya mwili
Iwapo dawa za kupunguza nguvu ya kinga ya mwili zimeshindwa kufanya kazi na kuna uthibitisho kuwa glomerulonephritis imesababishwa na mashambulizi ya seli za kinga ya mwili katika figo, mgonjwa anaweza kufanyiwa tiba inayoitwa plasmapheresis. Katika tiba hii, sehemu ya damu yenye seli za kinga ya mwili zijulikanazo kama antibodies huondolewa kwa kubadilishwa na maji maji (plasma) yasiyo na antibodies zozote zile. Kuondoa antibodies husaidia kupunguza mcharuko mwili na uharibifu zaidi katika chujio za figo.
Iwapo figo zitashindwa kufanya kazi kabisa, mgonjwa anaweza kuhitaji kufanyiwa dialysis au kupandikizwa figo mpya.
Matarajio
Kuharibika kwa chujio za figo kunaweza kuwa ni tatizo la muda na lenye kurekebishika au linaweza kudorora na kuwa la kudumu. Kudorora kwa chujio za figo kunaweza kusababisha kupungua kwa utendaji kazi wa figo au ugonjwa sugu wa figo kushindwa kufanya kazi (chronic renal failure), au kufa kabisa kwa figo zote (end-stage renal disease).
Madhara
Pamoja na kusababisha shinikizo la damu kuwa juu, uharibifu katika chujio za figo unaweza pia kusababisha mlinganyo usio sawa wa madini katika damu (electrolytes imbalance) kama vile ongezeko la madini ya potassium(hyperkalemia); maambukizi yanayojirudia katika njia ya mkojo, uwezekano wa kupata maambukizi ya mwili, mrundikano wa maji mwilini hali inayoweza kusababisha moyo kushindwa kufanya kazi (congestive heart failure) au maji kujaa katika mapafu (pulmonary edema); au ugonjwa wa figo ujulikanao kama Nephrotic syndrome (utaelezwa katika makala zijazo).
Kinga
Inawezekana kuzuia uharibifu wa chujio za figo kwa baadhi ya watu ingawa, kwa ujumla ni ngumu kufanya hivyo. Baadhi ya mambo ya kufanya ili kuepuka kupatwa na tatizo hili ni pamoja na kuepuka matumizi ya vimiminika vyenye kemikali za hydrocarbons, matumizi ya madini ya zebaki pamoja na matumizi ya muda mrefu ya dawa za jamii ya nonsteroidal anti-inflammatory drugs (NSAIDs) kama vile Aspirin.