Sunday, 31 August 2014

UVIMBE KWENYE MAYAI YA MWANAMKE ( OVARIAN CYST)



Uvimbe kwenye mayai ya ya mwanamke (ovary) hutokana na mkusanyiko wa majimaji yanaozungukwa na kuta nyembamba ndani ya mayai ya mwanamke.Uvimbe huu ambao hupatikana ndani ya mayai ya mwanamke ndio unaojulikana kama ovarian cyst.

Uvimbe huu hutokea kwa wanawake wa umri wowote ule na mara nyingi huonekana kwa wanawake waliokatika umri wa kushika ujauzito.

Lazima nikiri ya kwamba shauku ya kuandika makala hii inatokana na swali la msomaji wetu mmoja alilouliza “Nimepiga ultra sound nikaambiwa nina kitu cheupe kwenye ovar yangu moja je hili tatizo linaweza kunifanya nisishike mimba? na matibabu yake yakoje? na pia naumwa sana nyonga tiba yake ni nini.

ntashukuru kwa msaada wako.” Mwisho wa kunukuu. 

Sina nia ya kusema ya kwamba tatizo lake ni hili la uvimbe katika mayai ya mwanamke, la hasha, kwa sababu sijaiona ultrasound yake na historia yake aliyotoa msomaji huyu ilikuwa haijitoshelezi.Hivyo, nina imani ya kuwa kwa kupitia makala hii yeye pamoja na wasomaji wengine wanaweza kupata mwanga juu ya tatizo hili la uvimbe katika mayai ya mwanamke.

Mayai ya mwanamke ni nini?

Kwa kawaida mwanamke anakuwa na mayai mawili katika mwili wake.Yai moja upande wa kulia na yai jingine upande wa kushoto kwake.Mayai haya hupatikana pembezoni mwa mfuko wa uzazi (uterus).Mayai haya ya mwanamke huanza kuzalisha mayai ya uzazi yanayojulikana kama ovum.Mayai

haya ya uzazi hukuwa ndani ya mayai ya mwanamke (ovary) kwa kuchochewa na baadhi ya homoni. Katikati ya mwezi, siku ya kumi na nne,masaa 24-36 baada ya kiwango cha kichocheo aina ya Luteinizing Hormone kuwa juu, mayai ya uzazi hutolewa katika kila ovary na hii ndio hujulikana kama ovulation.Mayai haya ya uzazi huishi kwa masaa machache hadi masaa 24 bila kurutubishwa na shahawa kutoka kwa mwanamume.Mabaki ya mfuko

wa mayai ya uzazi yanayojulikana kama follicle ndani ya ovary, hugeuka na kuwa corpus luteum ambao huusika na utoaji wa kichocheo aina ya progesterone kwa wingi.Ni kichocheo hiki cha progesterone ndio kinachosababisha mfuko wa uzazi kujiandaa kwa upachikwaji (implantation) wa yai lililorutubishwa kwa shahawa ndani ya mfuko wa uzazi kwa kuongeza unene kwenye kuta zake.Yai hili husafiri hadi kwenye mfuko wa uzazi kwa

ajili ya kwenda kujipachika.Kama upachikwaji wa yai liliorutubishwa kwa shahawa (au kama yai la uzazi ambalo halijarutubishwa kwa shahawa) hautafanyika, basi ndani ya wiki mbili, corpus luteum huanza kusinyaa na kupotea yenyewe (involute)na kusababisha kushuka kwa kiwango cha vichocheo aina ya progesterone na estrogen.Kushuka kwa viwango vya vichocheo hivi ndio husababisha mfuko wa uzazi kuanza kutoa mabaki ya kuta zake pamoja na yai la uzazi na hii ndiyo pale mwanamke anatoka damu ukeni inayojulikana kama hedhi (menstruation).Unaweza ukajiuliza, ni kwa nini mwandishi ameanza na maelezo ya hedhi? Hapa nilitaka kuonyesha umuhimu wa mayai ya uzazi kwa mwanamke pamoja na kazi yake.


Kuna aina ngapi za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke?

Kuna aina nyingi za uvimbe kwenye mayai ya mwanamke lakini aina hizi saba ndio huonekana sana kwa wanawake wengi ambazo ni;
I.Follicular cyst-Hutokea wakati ovulation isipotokea au baada ya corpus luteum kuanza kusinyaa na kupotea yenyewe baada ya kutokupachikwa

kwa yai kwenye kuta za mfuko wa kizazi. Uvimbe huu unakuwa na wastani wa 2.3 inches kwa upana.Upasukaji wa uvimbe huu husababisha maumivu makali sana katikati ya mzunguko wa hedhi yaani siku ya ovulation. Maumivu haya yanayojulikana kamamittelschmerz huonekana kwa wanawake robo moja wenye aina hii ya uvimbe.Kwa kawaida, uvimbe huu hauna dalili zozote na hupotea wenyewe baada ya miezi kadhaa.


II.Corpus Luteum cyst
-Kutokana na kutopachikwa kwa yai la uzazi lililorutubishwa na shahawa kwenye mfuko wa kizazi, corpus luteum husinyaa na kupotea yenyewe, aghalabu inaweza kutokea corpus luteum ikajaa maji na hivyo kusababisha uvimbe wa aina hii.Kwa kawaida, uvimbe huu huonekana kwenye upande mmoja (kushoto au kulia) wa mwanamke na hauna dalili zozote zile.


III.Hemorrhagic cyst
-Uvimbe huu hutokea wakati kukiwa na uvujaji wa damu ndani ya uvimbe wa aina yoyote ule ambao umeshajitengeneza tayari.Huambatana na maumivu makali kwenye upande mmoja wa ubavu wa mwanamke (kushoto au kulia).


IV
.Dermoid cyst- Uvimbe huu ambao sio saratani na pia hujulikana kama mature cystic teratoma, huathiri wanawake wadogo walio katika umri wa kushika mimba na huweza kukua na kufikia inchi 6 kwa upana na ndani yake huweza kuwa na mchanganyiko wa nywele, mfupa, mafuta na cartilage.Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa zaidi (inflamed) au kujizungusha (torsion) na hivyo kuathiri usambazi wa damu kwenda kwenye uvimbe huu na hivyo kusababisha maumivu makali sana maeneo ya tumboni.


V.Polycysitic appearing cyst
- Uvimbe wa aina hii unakuwa ni mkubwa sana na huwa umezungukwa na vijivimbe vyengine vidogo vidogo na huonekana hata kwa wanawake wenye afya njema au wale wenye matatizo ya homoni.


VI.Cystedenoma
-Ni aina ya uvimbe unaotokana kwenye tishu za ovary na hujazwa na majimaji aina ya kamasi.Uvimbe wa aina hii huweza kuwa mkubwa sana hata kufikia inchi 12 au zaidi kwa upana.


VII.Endometriomas /Endometrial Cysts
- Husababishwa na uwepo wa aina mojawapo ya kuta za mfuko wa kizazi unaojulikana kama endometrium kwenye mayai ya mwanamke (ovary).Huathiri wanawake waliokatika umri wa kushika ujauzito na huambatana na maumivu sugu ya nyonga (chronic pelvic pain) wakati wa hedhi.Uvimbe huu unakuwa na damu ya rangi ya nyekundu kahawia(reddish brown) na ukubwa wake ni kuanzia 0.75-8 inches.


Nini husababisha tatizo hili la uvimbe kwenye mayai ya mwanamke?


Vihatarishi vya tatizo hili ni;

•Historia ya awali ya ovarian cyst.
•Kuwa na mzunguko wa hedhi usiotabirika (irregular menstruation cycle)

•Kuwa na mafuta mengi kwenye sehemu ya juu ya mwili (kwa wale wanawake wanene)

•Ugumba

•Kuvunja ungo/Kubaleghe mapema ( kuvunja ungo ukiwa na miaka 11 au chini yake)

•Kukosekana kwa uwiano sawa wa vichocheo mwilini au ugonjwa wa aina ya hypothyroidism.
Tamoxifen – Dawa ya kutibu saratani ya matiti.Hii ni moja ya madhara ya dawa hii.


Dalili na viashiria 

a)Maumivu makali, ambayo hayana mwanzo maalum, yanayochoma, maumivu haya yanaweza yakawa yanakuja na kupotea au yakawepo moja kwa moja.Pia mtu anaweza kupata usumbufu (discomfort) kwenye maeneo ya chini ya kitovu, kwenye nyonga, uke(vagina), kwenye mapaja na mgongoni kwa chini.

b)Kuhisi tumbo kuwa zito, limejaa au limevimba.

c)Maumivu kwenye matiti
d)Hedhi isiyotabirika

e)Maumivu ya muda mrefu kwenye nyonga wakati wa hedhi na ambayo huweza kuhisiwa sehemu ya chini mgongoni.Maumivu haya yanaweza kuanza muda mfupi tu baada ya kuanza hedhi, wakati wa hedhi au mwisho wa hedhi.


f)Maumivu ya nyonga baada ya kufanya kazi ngumu/mazoezi au baada ya kufanya mapenzi/kujamiana.

g)Kichefuchefu
h)Kutapika

i)Kutokwa na matone ya damu kwenye tupu ya mwanamke au kutokwa na damu kupitia ukeni.

j)Ugumba.
k)Uchovu

l)Mabadiliko ya haja ndogo-Kukojoa mara kwa mara, au kujikojolea, au kushindwa kutoa mkojo wote kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kupata haja ndogo.

m)Mabadiliko ya haja kubwa-Kupata haja kubwa kwa shida sana kutokana na presha kwenye maeneo ya nyonga.
n)Nywele kuwa kubwa sana
o)Kuongezeka kuota kwa nywele kwenye uso au sehemu nyingine za mwili

p)Kuumwa kichwa

q)Kuongezeka uzito
r)Maumivu ya kwenye mbavu

s)Kufanya uvimbe chini ya ngozi

t)Kuvimbiwa (bloating)

Vipimo vya uchunguzi


Endovaginal Ultrasound-Ultrasound inayofanywa kwa kuingiza mpira maalum kupitia ukeni/tupu ya mwanamke na kuangalia mfuko wa uzazi na mayai ya mwanamke. Kwa kutumia kipimo hiki, ni rahisi kwa daktari kugundua kama uvimbe kwenye mayai ni wa aina gani kama ni maji tu (fluid filled sac)complex (maji pamoja na mchanganyiko wa vitu vigumu), au ni vitu vigumu pekee(completely solid).

•Abdominal Pelvic Ultrasound- Ultrasound ya kawaida.Husaidia kujua ni aina gani ya uvimbe uliopo kwenye mayai ya mwanamke.Mara nyingi, uvimbe kwenye mayai ya mwanamke huonekana kama maputo (bubbles).
•CT Scan
•MRI

Serum CA-125 Assay-Kipimo cha damu kuangalia kiashiria cha CA-125 (Cancer Antigen 125).Kupatikana kwa kiashiria hiki huonyesha ya kwamba mwanamke ana saratani ya mayai ya mwanamke aina ya Epithelial Ovarian Cancer.Pia huweza kuonekana kwenye magonjwa mengine ambayo sio saratani kamaendometriosis, 
uterine fibroids nk.


Urine for pregnancy test-Kipimo cha kuangalia ujauzito kwani matibabu ya uvimbe kwenye mayai hutofautiana kwa mwanamke mwenye ujauzito na yule ambaye hana ujauzito.Pia husaidia kujua kama mwanamke ana mimba iliyotunga nje ya mfuko wa kizazi(ectopic pregnancy) au la, kwani uvimbe kwenye mayai ya mwanamke huweza kuonyesha dalili zinzoshahabiana na dalili za mimba iliyotunga nje ya mfuko wa kizazi.


Culdocentesis- Kipimo kinachofanywa kwa kuchukua maji kutoka katika mfuko unaojulikana kama pouch of douglas ulio katikati ya puru (rectum) na shingo ya kizazi ili kuangalia kama kuna maambukizi katika uke (Pelvic Inflammatory Disease) au mgonjwa ana mimba iliyotunga nje ya mfuko wa uzazi.


Hormone levels-Kuangalia kiwango cha vichocheo aina ya Luteinizing Hormone, Follicle Stimulating Hormone, Testosterone, Estardiol na nk.

Complete Blood Count-Kipimo cha kuangalia wingi wa damu na seli tofauti za damu.
•Doppler Flow Studies

Tiba ya uvimbe kwenye mayai ya mwanamke
1.Tiba ya Dawa

Tiba hii huusisha matumizi ya dawa za upangaji uzazi (oral contraceptives) kwa muda wa wiki 4-6.Matumizi ya dawa hizi kwa muda mrefu huzuia kutokea tena kwa uvimbe kwenye mayai ya mwanamke.Dawa hizi hufanya kazi kwa kuzuia mayai ya mwanamke (ovary) kutoa mayai ya uzazi (ovums).Aidha, dawa hizi hazipunguzi uvimbe huu kwani uvimbe hupotea wenyewe baada ya muda.Dawa za maumivu hutolewa kwa wale wenye kupata maumivu makali sana.Matumizi ya dawa za matatizo ya uzazi(fertility drugs) husababisha tatizo la ovarian hyperstimulation ambalo huambatana na uvimbe kwenye mayai ya mwanamke, uvimbe wa aina hii hupotea baada ya mwanamke kupata hedhi au baada ya kujifungua.


2.Tiba ya Upasuaji

Exploratory Laparatomy- Mgonjwa hupasuliwa kwenye maeneo ya tumboni ili daktari aweze kuondoa uvimbe uliopo ndani.Upasuaji hufanyika kwa wanawake wenye;
•Uvimbe ambao unajulikana kama complex ovarian cyst na ambao haupotei wenyewe
•Uvimbe unaosababisha dalili na viashiria nilivyotaja hapo awali na ambao pia haupotei wenyewe
•Uvimbe mkubwa kuanzia 5cm-10cm na
•Wanawake ambao wamefikisha umri wa kutopata hedhi tena au wanakaribia umri huo (miaka 42-58).

Laparascopic Surgery
-Upasuaji unaofanywa kwa daktari kupasua sehemu ndogo kwenye maeneo ya tumboni na kuingiza mpira maalum ambao una kamera kwa mbele na huenda kuondoa uvimbe ulio kwenye mayai ya mwanamke.Upasuaji huu hauachi kovu la aina yoyote ile linalotokana na upasuaji, hivyo tiba ya aina hii hupendwa sana na wanawake.


Je kuna madhara ya uvimbe kwenye mayai ya mwanamke wakati wa ujauzito?

Tatizo la uvimbe kwenye mayai ya mwanamke wakati wa ujauzito pia hutokea. Mara nyingi wanawake wajawazito wenye uvimbe kwenye mayai ya yao huwa na uvimbe ambao sio saratani.Kawaida uvimbe kwenye mayai ya mwanamke wakati wa ujauzito hauna madhara yoyote yale kwa mwanamke mjamzito au kwa kiumbe kilicho ndani ya tumbo kama ukiwa bado mdogo.

Madhara ya uvimbe kwenye mayai wakati wa ujauzito

a)Uvimbe kuwa mkubwa sana na hivyo kusababisha maumivu makali kwa mjamzito, kama uvimbe huu utapasuka au kujinyonga wenyewe (twist on itself), basi kuna uwezekano wa mimba kuharibika na hivyo kutoka (miscarriage) au kujifungua mtoto mapema zaidi (pre- term labor).
b)Kupasuka kwa uvimbe huu hakuleti madhara ya maambukizi yoyote yale.

c)Dawa za kupunguza maumivu hutumiwa kwa wanawake wajawazito ambao hupata maumivu makali kutokana na kupasuka kwa uvimbe huu.

d)Matumizi ya dawa za usingizi wakati wa kujifungua kwa mwanamke mjamzito mwenye uvimbe kwenye mayai yake bado ni salama
e)Uvimbe huu ukiwa mkubwa na kujinyonga wenyewe au kukandamiza mfuko wa kizazi na hivyo kukandamiza kiumbe kilichomo ndani yake.

Mwanamke mjamzito atahitaji upasuaji ili kuondoa uvimbe huu.Upasuaji hautamuathiri mama wala kiumbe kilicho ndani ya tumbo.Lakini kama unavyojua, wakati wa upasuaji kunaweza kutokea madhara yoyote yale, hivyo mwanamke mjazito wenye uvimbe kwenye mayai hushauriwa kuepuka upasuaji kama anaweza.


f)Kama uvimbe huu utahitaji kufanyiwa upasuaji ili uondolewe, muda mzuri wa kufanyiwa upasuaji kwa mwanmke mjazito ni kuanzia wiki ya 13-28 ya ujauzito wake


g)Uvimbe mdogo huweza kuondolewa kwa njia ya upasuaji ya Laparascopic surgery kama nilivyoeleza hapo juu, kwa uvimbe mkubwa, utahitaji kuondolewa kwa kufanyiwa upasuaji kwenye maeneo ya tumboni.


h)Kutokana na uvimbe mkubwa kwenye mayai ya mwanamke kuwa na madhara mengi, mwanamke mjazito atahitaji uangalizi wa karibu kutoka kwa daktari.


i)Kama mwanamke mjazito mwenye uvimbe kwenye mayai yake atatimiza miezi tisa ya ujauzito wake bila matatizo yoyote, anashauriwa ajifungue kwa njia ya upasuaji ili wakati wa upasuaji uvimbe ule nao pia uondolewe ili kumuepusha kufanyiwa upasuaji tena.

2 comments:

  1. Asalaam aleykum warahmatullah wabarakat, samahani ndugu yangu katika imaan, mi nina tatizo la siku za hedhi, nimeanza kuona tatizo hili mwezi uliopita, ambapo nilipata period tofauti na nilivyozoea, inatoka kidogo mno ikiwa na kitu kama maji ya bamia yanavutika, na pia tumbo linauma, mwezi huu pia imekua hivyo, na damu hii haitoki mpaka nichutame kama ni nimeenda chooni kupata haja ndogo ndo naona damu tena tone moja tu kisha haitoki mpaka nitakapokwenda uani, na huja kama kawaida siku tatu kisha nimemaliza je hili ni tatizo au kawaida??

    ReplyDelete
  2. Asalaam aleykum warahmatullah wabarakat, samahani ndugu yangu katika imaan, mi nina tatizo la siku za hedhi, nimeanza kuona tatizo hili mwezi uliopita, ambapo nilipata period tofauti na nilivyozoea, inatoka kidogo mno ikiwa na kitu kama maji ya bamia yanavutika, na pia tumbo linauma, mwezi huu pia imekua hivyo, na damu hii haitoki mpaka nichutame kama ni nimeenda chooni kupata haja ndogo ndo naona damu tena tone moja tu kisha haitoki mpaka nitakapokwenda uani, na huja kama kawaida siku tatu kisha nimemaliza je hili ni tatizo au kawaida??

    ReplyDelete