Sunday, 31 August 2014

FAHAMU UGONJWA WA KIBOFU CHA MKOJO



WIKI iliyopita tulizungumzia ugonjwa wa uvimbe sehemu ya kizazi kwa wanawake, leo tunachambua ugonjwa wa kibofu cha mkojo ambao huwa ni tatizo kubwa kwa wanaume.Wanaume, hasa wenye umri mkubwa wanaweza wakawa na ugonjwa wa saratani hii ya ‘prostate’. Ni tezi iliyo kwenye viungo vya uzazi vya wanaume chini ya kibofu panapopitia mrija wa mkojo.
Saratani zipo za aina nyingi na moja ya saratani hizo ni hiyo ya kibofu cha mkojo. Aina hiyo ya saratani inaweza kusababishwa na mazingira ikiwemo matumizi ya maji yasiyo salama.
Kabla ya kuelezea saratani hii ya kibofu cha mkojo au prostate nieleze kwamba kibofu cha mkojo kinapatikana sehemu ya chini ya maeneo ya tumbo na ni kiungo ambacho kina uwazi ndani ulio kama mfuko na kazi yake kubwa ni kukusanya na kuhifadhi mkojo unaotolewa na figo kabla ya kutolewa nje wakati muhusika anapoamua kukojoa.
Kibofu cha mkojo kina tabaka tatu za tissue ambazo ni mucosa, lamina propia na muscularis.
Tabaka la mucosa – ukuta wa ndani kabisa ambao ndiyo unakutana na mkojo wa binadamu, lina kuta nyingi sana za seli au chembechembe zinazojulikana kama transitional epithelium cells ambazo pia hupatikana kwenye sehemu ya mirija inayojulikana kama ureters, urethra na kwenye figo. Seli hizi zinazuia uvujaji wa mkojo kwenda kwenye sehemu nyingine ya mwili.
Ureter huingiza mkojo kutoka kwenye figo na urethra hutoa mkojo kutoka kwenye kibofu cha mkojo wakati wa kukojoa.
Tabaka la lamina propia – ukuta wa katikati ambao ni mwembamba sana kati ya kuta  hizi tatu na  ambao mishipa ya damu na neva inapatikana hapa- ni muhimu sana wakati wa kupanga makundi ya saratani ya kibofu cha mkojo wakati wa tiba.
Tabaka la muscularis -  ukuta wa nje ambao ndani yake kuna misuli maalumu na ndiyo ukuta mnene kati ya hizi tatu. Una kazi kubwa ya kupumzisha kibofu cha mkojo ili uingie ndani na ukishajaa basi hukaza kibofu na kufanya mkojo kutoka nje.Nje ya kuta hizo tatu, kibofu cha mkojo kimezungukwa na  mafuta ambayo hukinga kibofu kutokana na mtikisiko wowote na kukitenganisha na viungo vingine.
Turudi kwenye mada, kazi ya ‘prostate’ ni kudhibiti kibofu na mtiririko wa mkojo lakini pia ni muhimu katika tendo la ndoa kwani humwezesha mwanamume kuwa na nguvu ya kufikia kilele. ‘Prostate’ ya kawaida kwa mwanamume mtu mzima ina ukubwa kama punje ya karanga na ukubwa huu huongezeka kadiri mtu anavyokua. Katika umri wa miaka 40 tezi huanza kutanuka na kadiri inavyotanuka, hubana mrija wa kupitisha mkojo na kufanya mkojo utoke kwa shida na kusababisha tatizo katika tendo la ndoa.
Urothelial carcinoma (transitional cell carcinoma) – Hii ndiyo aina ya saratani inayotokea kwa wingi na hutokea kwenye seli za transitional epitheliumo na asilimia 95 ya saratani zote za kibofu cha mkojo huwa ni aina hii.
Squamous cell carcinoma – aina hii hutokea baada ya maradhi ya kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu kama vijiwe vya kibofu cha mkojo .
Adenocarcinoma – hutokea baada ya shambulizi kwenye kibofu cha mkojo kwa muda mrefu. Huchukua asilimia mbili ya saratani zote za kibofu cha mkojo.

DALILI
Dalili za kwanza za mgonjwa kuwa na tatizo katika kibofu cha mkojo  ni kwenda haja ndogo mara kwa mara, hasa usiku na mara nyingine mtu huweza kujikojolea.
Pia mkojo hutoka kidogokidogo ama kwa kukatika katika na wakati mwingine mwanamume hupata maumivu wakati wa kukojoa na hata kutoka damu.
Maumivu huenea kwenye sehemu za mgongo, kiuno na sehemu za juu ya mapaja na kupunguza uwezo wa tendo la ndoa au kupata maumivu wakati wa kufikia kilele.
Matatizo mengine ni kupata maambukizi ya magonjwa kwenye kibofu, njia ya mkojo na figo na mkojo hubaki kwenye damu na kuwa sumu. Utafiti waonesha kuwa asilimia 25 ya wanaume wenye umri wa miaka 30 na kuendelea wana chembechembe za ‘prostate cancer’.
‘Prostate cancer’ ndio aina kuu ya saratani inayowashambulia sana wanaume japokuwa inaweza kutibika mgonjwa akiwahi hospitali.
Matibabu na ushauri
Matibabu ya saratani hii hutegemea uchunguzi. Inashauriwa kutibu ugonjwa wa kichocho mapema na kukwepa vihatarishi vya kupata ugonjwa huu.Ulaji wa matunda, mboga za majani na unywaji maji ya kutosha angalau lita moja kwa siku unaweza kupunguza tatizo la saratani ya kibofu. Inashauriwa watu waepuke matumizi ya tumbaku.

0 comments:

Post a Comment