Sunday, 31 August 2014

MAGONJWA NYEMELEZI KWA WANAWAKE-4-5

Mpenzi msomaji, naendelea kuelezea kuhusu magonjwa nyemelezi kwa wanawake, tuwe pamoja...
Vimelea vya Pneumocystis jiroveci huathiri mfumo wa hewa.Fangasi huyu pia huweza kuathiri viungo vingine kama ini, wengu (spleen) na figo katika baadhi ya wagonjwa.
Dalili zake ni kikohozi kikavu, kifua kubana, kupumua kwa shida, homa, kuishiwa pumzi na kutokwa jasho nyakati za usiku.
Baada ya kuangalia na kuchambua magonjwa yanayosababishwa na virusi na fangasi sasa tuone jinsi bakteria wanavyosababisha magonjwa.
Baadhi ya magonjwa yasababishwayo na bakteria ni kama yafuatayo;
Kifua Kikuu (TB):
Ugonjwa huu husababishwa na kimelea kiitwacho Mycobacterium tuberculosis ambacho ni moja katika kundi la Mycobacterium Avium Complex (MAC). Kushuka kwa kinga ya mwili husababisha kulipuka kwa vimelea vya kifua kikuu ambavyo hupatikana, pamoja na viungo vingine, zaidi kwenye mapafu.
Dalili za kifua kikuu ni pamoja na kikohozi na homa (haswa nyakati za usiku) kwa zaidi ya wiki mbili. Kutokwa jasho usiku (mara nyingi jasho huwa jingi mpaka kulowesha shuka), kupungua uzito (zaidi ya kilo moja na nusu ndani ya mwezi), kichomi na kukohoa damu.
Ugonjwa huu pia huweza kusababisha kupata homa ya uti wa mgongo (meningitis) ambayo huambata na dalili kama kuumwa kichwa, kichefuchefu na kutapika ikifuatiwa na kuongezeka kwa joto la mwili na maumivu na kukaza kwa shingo.
Nimonia (Pneumonia):
Huu ni ugonjwa ambao kwa kiasi kikubwa huathiri mfumo wa hewa na haswa mapafu. Baadhi ya vimelea viletavyo nimonia ni kama Pneumococcus, Haemopilus influenza, Mycoplasma (haswa kwa watoto) pia Klebsiella, Staphylococcus aureus, Pseudomonas aeuroginosa (kwa wagonjwa waliolazwa mahospitalini) na wengineo.

MAGONJWA NYEMELEZI KWA WANAWAKE-5




Tumekuwa tukielezea kuhusu magonjwa nyemelezi kwa wanawake, hata hivyo haya maradhi ya leo yanawahusu pia wanaume.
Ugonjwa wa Ngozi:
Huu husababishwa na vimelea vya Staphylococcus aureus.Vimelea hivi huishi katika mwili wa binadamu (kwenye ngozi ya kichwa na kinena (groins) na kwapani) bila madhara.Pia hupatikana kooni na katika utumbo mpana na mkojo.
Vimelea vya Staphylococcus husambaa kwenda sehemu nyingine ya mwili kutoka kwenye usaha, mgusano na ngozi ya mwenye maradhi, kutumia taulo, matandiko,vifaa vya mtu aliyeathirika n.k
Dalili zake ni pamoja na chunusi, majipu, kubabuka kwa ngozi na magamba magamba katika ngozi.
Yapo pia magonjwa yatokanayo na Protozoa ambayo mojawapo ni Toksoplasmosisi ya Ubongo na hujulikana kama Cerebral toxoplasmosis.
Cerebral toxoplasmosis:
 Ugonjwa hutokana na kuamshwa kwa ugonjwa wa awali kutokana na vimelea vya Toxoplasma gondii.
Kitaalamu kimelea hiki huishi ndani ya seli na huathiri ndege,wanyama na lakini pia na binadamu ndiyo maana huugua.
Kimelea hiki kinaathiri mfumo mzima wa fahamu, hupatikana kwenye nyama isiyopikwa vizuri na kinyesi cha paka. Huathiri zaidi ubongo na kusababisha maumivu ya kichwa, kuchanganyikiwa, udhaifu wa viungo, homa, kupoteza fahamu, kupooza na kifafa.
Kriptosporidiosisi:
Huu ni ugonjwa utokanao na vimelea vya Cryptosporidium.Huathiri zaidi mfumo wa chakula na hutokana na kutumia kwa maji au chakula vilivyoathirika na vimelea vya ugonjwa huu.
Dalili zake ni kuharisha sana kiasi cha kusababisha kupungukiwa na maji mwilini (dehydration), maumivu wakati wa haja kubwa, kichefuchefu na kutapika.Wagonjwa wa aina hii huwa na joto la mwili la kawaida.
Kushuka kwa kinga ya mwili husababisha mwili kushindwa kupigana na vimelea vya magonjwa hivyo kusababisha mtu kushambuliwa na magonjwa.
Ifahamike kwamba baadhi ya vijidudu kitaalamu huitwa microorganisms  pia hupatikana katika mwili wa binadamu bila madhara yoyote kama vile kwenye ngozi, mfumo wa chakula, ukeni, uumeni n.k.
 Hata hivyo, vijidudu hivi huweza kuwa chanzo cha magonjwa iwapo kinga ya mwili itashuka.
Sababu mojawapo kubwa ya kushuka kwa kinga ya mwili hasa katika nchi zilizopo chini ya jangwa la Sahara ni Ukimwi/VVU.Hata hivyo, ieleweke kwmba si kila mtu mwenye upungufu wa kinga mwilini ana VVU.
Kuna sababu nyingine nyingi ambazo husababisha kwa njia moja au nyingine kushuka kwa kinga ya mwili.Zifuatazo ni baadhi tu ya sababu hizo;
Utapiamlo, Kuugua mara kwa mara,Sababu za kijenetiki (kurithi),Madhara kwenye ngozi,Msongo wa mawazo na Ujauzito.
Madawa ya Kutibu saratani, Matumizi ya muda mrefu ya antibayotiki (antibiotics),steroidi (steroids) na madawa ya kushusha kinga mwilini (immunosuppressant drugs)) ambayo hutumika wakati wa kupandikiza viungo mwilini kama figo n.k
Magonjwa nyemelezi husababishwa na vijidudu mbalimbali kama bakteria,virusi,fangasi na bakteria.
Magonjwa ya Virusi
Tibu na Ushauri
Aina ya matibabu hutegemea na aina ya ugonjwa na mtu.Iwapo una dalili kati ya zilizotajwa hapo juu ni vyema kumona daktari ambaye atakufanyia uchunguzi na kugundua ni vimelea vya aina gani vimekukumba na atakupa matibabu.
Chakuzingatia ni kuwa kuwepo kwa dalili zilizotajwa hapo juu hakumaanishi kuwa mgonjwa ana Virusi vya Ukimwi.Ukweli ni kwamba dalili hizi hutofautiana kati ya mtu na mtu.
Tunakushauru uwe unapima afya yako kila mara hasa VVU hasa kama kinga ya mwili wako inapungua ili kujua chanzo kwani bila kufanya hivyo unaweza kupata magonjwa nyemelezi.

0 comments:

Post a Comment