Sunday, 31 August 2014

FAHAMU AINA ZA KIHARUSI (STROKE)-2




WIKI iliyopita tulielezea ugonjwa wa kiharusi na aina zake na tukafafanua kwa nini unawapata watu. Endelea kuelimika.
Iwapo mgonjwa ataathirika sehemu ya ubongo kwenye shingo kuelekea kwenye uti wa mgongo (brainstem), mgonjwa anaweza kuwa na dalili za kuhisi mabadiliko ya harufu, ladha, kusikia na  kuona, kulegea kwa misuli ya macho (ptosis),  kupungua kwa ufahamu na kulegea kwa misuli ya uso, ulegevu wa ulimi (kushindwa kutoa nje au kusogeza upande upande).
Pia atakuwa na upungufu wa uwezo wa kumeza, ulegevu wa misuli ya shingo na kushindwa kugeuza shingo upande mmoja, kushindwa kusimama sawasawa na kuona vitu kwa hali ya utofauti, mabadiliko ya upumuaji na kiwango cha moyo kudunda.
Iwapo sehemu mojawapo ya mfumo mkuu wa neva kitaalamu huitwa central nervous system  imeathirika, mgonjwa atakuwa na dalili za kupoteza ufahamu kwa upande mmoja wa mwili na kulegea kwa misuli ya uso, kuhisi ganzi mwilini na kupungua kwa ufahamu wa hisia na kutetemeka mwili.
Mgonjwa anaweza kukumbwa na matatizo ya kupoteza fahamu, maumivu makali ya kichwa na kutapika hasa kwa wale wenye kiharusi cha kuvuja damu (hemorrhagic stroke) ambacho husababisha ongezeko la shinikizo na mgandamizo wa ubongo ndani ya fuvu kutokana na kuvuja kwa damu.
TIBA
Mgonjwa kabla ya kutibiwa ni lazima afanyiwe vipimo kama vile cha ECG, ECHOCARDIOGRAM  ambacho huwezesha kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo ( na kama kuna damu iliyoganda kwenye moyo ambayo inaweza kufika kwenye ubongo.
Holter monitor husaidia kutambua hitilafu katika mapigo ya moyo (arrhythmia) zinazotokea kwa vipindi na Angiogram huwezesha kugundua matatizo kwenye mishipa ya damu, na ni mishipa ipi ya damu iliyoziba.
Vipimo vya damu huwezesha kutambua uwepo wa lijamu mwilini (hypercholesterolemia) na mabadiliko mengine katika damu.
Mgonjwa hutibiwa kwa kutumia dawa za kuyeyusha damu iliyoganda (thrombolytics) au kwa kuondoa damu iliyoganda kwa njia mbalimbali (thrombectomy). Dawa nyingine kama vile junior Aspirin na Clopidogrel hutolewa kwa ajili ya kuzuia chembe sahani kukusanyika na kuganda.
Matibabu ya kiharusi kinachotokana na damu kuvujia kwenye ubongo (Hemorrhagic stroke)  huhitaji tathmini ya upasuaji wa neva ili kuchunguza na kutibu sababu ya damu kuvuja. Haishauriwi kabisa kumpa mgonjwa wa aina hii ya kiharusi dawa za kuyeyusha damu iliyoganda au za kuzuia kuganda maana huhatarisha maisha ya mgonjwa badala ya kumsaidia. Kwahiyo ni vizuri kwa wataalamu kufanya uchunguzi wa kutosha ili kuwa na uhakika na tatizo.
Mgonjwa wa kiharusi inafaa kumuelimisha ili arudishe ujuzi wake wa maisha ya kila siku. Inashauriwa wataalamu wa viungo wanahitajika ili kumpa mazoezi mgonjwa.
Hatari ya ugonjwa huu ni kwamba asilimia 75 ya wanaonusurika kifo huwa walemavu wa akili au kimwili na kusababisha kuathirika kwa ufanyaji kazi wao .
Ulemavu wa kimwili ni pamoja na ulegevu wa misuli, kujihisi ganzi sehemu mbalimbali za mwili hususan zilizoathirika, kutoona vizuri, vichomi na kadhalika.
USHAURI
Wagonjwa wanashauriwa kutibu au kuzuia tatizo la shinikizo la damu, kisukari na wanapewa ushauri wa kufanya mazoezi kila siku, kuacha kuvuta au kunywa pombe kupita kiasi, kula chakula kisichokuwa na mafuta mengi na kisicho na chumvi nyingi.
Tumia dawa za kupunguza mafuta mwilini (statins) kwa mfano Simvastatin.
Watu waepuke unene kupita kiasi (obesity) na wajichunge wasipate  cholesterol nyingi kwenye damu ambayo huchangia kuziba kwa mishipa ya damu mwilini.

0 comments:

Post a Comment