Sunday, 31 August 2014

CHAKULA NI TIBA NZURI, IJUE SIRI YAKE



Watu wengi tuna desturi ya kula ili tushibe. Katika ulaji huo wakati mwingine tunajitendea ukatili wenyewe kwa kula vyakula visivyo sahihi ambavyo vinapoingia mwilini hugeuka kuwa sumu.
Lakini vyakula pia ni dawa na leo tutajua, japo machache, juu ya namna gani vyakula ni dawa yenye uwezo wa kutibu maradhi, hata yaliyoshindikana hospitalini.
Vyakula ni tiba duniani toka enzi. Miongoni mwa mabingwa wa tiba za vyakula ni watu wa jamii ya Wachina toka Tibet waitwao ‘Tibetans’ au ‘Watibeti’. Hawa walianza kutoa tiba kwa kutumia vyakula miaka mingi sana na hadi leo ukifika Tibet utakutana na tiba hii maarufu kama ‘ Tibetan Food Theraphy’ ambayo imeanza kuenea nchini hivi sasa.
Tiba ya vyakula haihitaji utitiri wa madaktari na wauguzi kwa kuwa mgonjwa na daktari huonana mara moja kwa mwaka au miwili kwa kuwa daktari humsikiliza mgonjwa, humpa maelekezo juu ya kula aina fulani za vyakula ili apone na mgonjwa hufuata maelekezo hayo rahisi na yanayoeleweka kisha mgonjwa hupona.
Katika maelekezo ambayo madaktari wa lishe huwapa wagonjwa kubwa nikwamba mgonjwa anatakiwa aache tabia ya ulafi. Mgonjwa anatakiwa ale wastani wa robo tatu ya ujazo wa tumbo lake kwa uwiano, chakula kiwe nusu na kinywaji kiwe robo, ili tumbo lipate nafuu ya kuyeyusha na kufyonza virutubisho kirahisi toka katika chakula.
Pia maelekezo huwa mengi kwa baadhi ya wagonjwa mfano wengi wetu tunakula mlo mmoja tu na kudhani kulikopa tumbo ni kawaida kumbe ni kusababisha maradhi, kwani hutalitendea haki tumbo kwa kula mara moja kwa siku.
Kwa mfano, ukila matunda na mboga mbichi zisizopikwa (saladi/ kachumbari) basi uyeyushaji na ufyonzaji wa virutubisho huwa rahisi, tumbo huchukua saa 13 tu kukamilisha kazi hiyo. Ila, ukivipika vyakula hivyo basi ujue tumbo litagharimu saa 24 kukamilisha kazi ya ufyonzaji wa chakula hicho.
Tumbo hukutana na kibarua kigumu pale tunapokula vyakula vyenye asili ya usindikaji, nyama, vyakula vilivyopikwa kwa mafuta nk. Kwani hujikuta likihangaika na kazi ya usagaji kwa takriban saa 72 ambayo ni karibu siku tatu.
Hapo ndipo tumbo huweka kando sumu za vyakula hivyo. Sumu zitokanazo na mafuta mabaya, lehemu, chumvi, caffeine na tindikali mbalimbali huanza kulishambulia ini ambalo ndilo ‘Benki kuu’ ya mwili wa binadamu na hapo ndipo mifumo mingine huathirika na mtu kujikuta akiugua maradhi ya moyo na damu kama vile shinikizo la damu, kisukari na kupooza.
Aina nyingi za saratani huanzia hapo hivyo mtu kujikuta akitafuta msaada wa tiba ambayo kwa kiasi kikubwa madawa pamoja na mchanganyiko wa vitamin mbalimbali huhusishwa katika matibabu. Lakini pia maumivu toka tumboni, tumbo kujaa gesi, kukosa haja kubwa kwa muda mrefu na hata kukosa hamu ya kula.
Tumbo huweza kuhifadhi vyakula vyote unavyokula kila siku huku vingine vikikaa tumboni kwa saa 72 bila kuyeyuka kwa sababu utumbo mwembamba tu wa binadamu una urefu wa futi 22 au mita saba, sawa na urefu wa nguzo ya umeme. Utumbo huo umeungana na utumbo mnene. Huu una urefu wa futi 5 au mita moja na nusu.
Hii ni dhahiri kabisa kuwa tunatakiwa tuanze na kujua namna ya kula kwanza kabla hatujazivalia njuga tiba nyingine maana chakula ndiyo dawa ya asili na ya msingi duniani kote.

0 comments:

Post a Comment