Tuesday 8 July 2014

MAUMIVU YA MGONGO HAYATAKI DAWA!



TATIZO la kuumwa mgongo (sehemu ya chini) ni kubwa miongoni mwa watu wengi, inakadiriwa kati ya asilimia 75-85 ya watu duniani hupatwa na matatizo ya mgongo katika maisha yao. Mara nyingi matatizo ya kuumwa mgongo, huwa hayatokani na maradhi, bali hutokana na kazi wanazozifanya au mazingira wanayoishi watu.
Aidha, asilimia 50 ya watu wenye matatizo ya kuumwa mgongo ni wafanyakazi wenye kazi za kukaa au kuinama kwa muda mrefu bila kubadili mkao na hali hiyo huwa ndiyo sababu ya kushindwa hata kwenda kazini.
Kama nilivyoanza kusema hapo awali, mara nyingi tatizo la kuumwa mgongo huwa la muda mfupi na halitokani na maradhi, lakini linapoachwa kwa muda mrefu huwa tatizo kubwa la kiafya na husababisha matatizo mengine.
Kosa kubwa linalofanywa na watu wengi ni kukimbilia kumeza dawa za kupunguza maumivu (pain killers) badala ya kuliondoa tatizo kwa njia nyingine za kawaida kama tutakavyojifunza katika makala haya ya leo.
Ubaya wa kumeza dawa za kutuliza maumivu ni kusababisha matatizo mengine mwilini mbali na hilo la mgongo, kwani dawa za kutuliza maumivu huwa na madhara mengi. Inaelezwa kuwa dawa hizo huweza kusababisha hata kifua kikuu (Tuberculosis).
Kuna utafiti mmoja wa nchini Marekani umeonesha kuwa, siyo vidonge vya kupunguza maumivu tu vyenye madhara,  bali hata sindano za maumivu nazo zina madhara. Mwaka jana, zaidi ya watu 22 waliotumia dawa ya sindano (steroid injections) kutuliza maumivu makali ya mgongo waliyokuwa nayo, walipatwa na ugonjwa wa uti wa mgongo.
NINI CHA KUFANYA UUGUAPO MGONGO?
Kwa kuwa kitendo cha kukaa kwa muda mrefu bila kubadili mkao na utembeaji usio sawa (kama hutatembea umenyooka mwili) ndiyo chanzo kikuu cha maumivu ya mgongo, upatapo maumivu, kitu cha kwanza kufanya ni mazoezi ya kunyoosha viuongo, na hasa mgongo.
Ni kosa kubwa kukimbilia vidonge au sindano za kutuliza maumivu, badala yake unatakiwa kufanya mazoezi sahihi ya kunyoosha mgongo na vilevile kujiepusha na kukaa kwa muda mrefu bila kuinuka.
DONDOO MUHIMU KUJIEPUSHA NA TATIZO
Hakikisha ukaapo unakaa sawa, bila kupinda mgongo kwa muda mrefu na ufanye ‘mazoezi madogo madogo’ kabla, katikati ya kazi na baada ya kazi.
Hakikisha kiwango chako cha Vitamin D mwilini kiko sawa kwa kupata mwanga wa jua wa kutosha kwa siku au kula vidonge vinavyoongeza Vitamin D (Vitamin D supliments)

Kama unafanya kazi ya kukaa kwa muda mrefu, hakikisha mara kwa mara una vuta punzi nyingi kuingia ndani na kutoa pumzi nje kwa sekunde kadhaa, mara kwa mara. Hii husaidia kuamsha mishipa ya eneo la tumbo na mgongo.
Fanya ‘masaji’ ya mgongo mara kwa mara, hii husaidia kunyoosha mishipa ya mgongo na kuondoa maumivu haraka. Lala kwenye kitanda kilichonyooka au sakafuni ili kunyoosha mgongo.

Kwa akina dada, usipende kuvaa viatu virefu huku umekaa kwa muda mrefu wakati wa kufanya kazi zako.
Kunywa maji mengi kila siku, hii husaidia kufanya mtiririko wa damu mwilini kuwa mwepesi katika mishipa.
Kwa kuzingatia dondoo zilizotajwa hapo juu, bila shaka wakati mwingine utakapopatwa na maumivu ya mgongo, utazingatia hayo na utajiepusha na kukimbilia dawa za maumivu. Kumbuka, kinga ni bora kuliko tiba na maumivu yakizidi sana, tafadhali pata ushauri wa daktari.

2 comments: