Monday, 5 May 2014

WATU WANENE WACHUNGE KALORI ZAO



LAKINI kabla sijaendelea mbele pengine ningechukua fursa hii kuwafahamisha wasomaji wetu maana ya neno kalori.

Maana ya ˆkalori kwa mujibu wa fizikia, ni kiasi cha nishati zinazohitajika kuongeza joto la gramu moja ya maji kwa celcius moja. Lakini tukiitafsiri kalori kwa mujibu wa lishe na chakula, ni kiwango cha nishati ya chakula au nguvu inayopatikana kutokana na chakula tunachokula.

Kwa msingi huo kwa mfano tunaposema kuwa, mkate una kalori 55, tunamaanisha kwamba, kiasi cha nguvu kinachotokana na mkate ni kalori 55. Kujua maana ya kalori na kiasi cha kalori tunachokula hutusaidia kufahamu ni kiasi gani cha nishati miili yetu inahitaji kwa siku kwa ajili ya mahitaji yake na hivyo kuweza kudhibiti uzito wa miili yetu kwa kutoipatia kalori nyingi zaidi ya mahitaji yake.

Suala hilo pia mbali na kuimarisha afya zetu vilevile huzuia unene wa kupindukia tatizo ambalo linazidi kuongezeka kila siku duniani kote.
Ratili moja ya mafuta (ambayo ni sawa na karibu nusu kilo)  ni sawa na kalori 3,500, kwa hiyo iwapo mtu atapunguza kalori 500 kwa siku, kwa wiki anaweza kupunguza ratili moja na hivyo kupunguza uzito.

Ni vigumu kujua kiasi cha kalori kinachotakiwa kwa siku, kwa sababu kila mtu ana sifa tofauti za kimwili na pia kiwango cha kazi na namna anavyoushughulisha mwili wake.
Bora wanawake wale kalori 1,400 na wanaume kalori 1,800 kwa siku. Pia ni bora tusile kalori 

zinazopungua 1,000 kwa siku, na tuzingatie kazi tunazofanya kwa siku na jinsi tunavyoishughulisha miili yetu.
Hii inamaanisha kuwa, ikiwa mtu anafanya kazi ya kukaa kitini muda mrefu au kazi isiyo nzito na kutoushughulisha sana mwili kama vile kazi za maofisini, ni wazi kuwa kiwango cha kalori anachohitaji kwa siku ni kidogo.

Tofauti na watu wanaofanya kazi zinazohitaji nguvu kubwa na zilizo ngumu kama vile kilimo, ujenzi, ukuli na kadhalila ambazo huufanya mwili utumie nishati nyingi. Hivyo watu wenye kufanya shughuli hizo ni wazi kuwa wanahitaji kula kiasi kingi zaidi cha kalori kwa siku. Vilevile ili kudhibiti uzito wa mwili na kujiepusha na unene wa kupindukia mazoezi yanapaswa kuzingatiwa.

Hii ni kwa sababu wakati tunapofanya mazoezi miili yetu huchoma kalori za ziada mwilini na hupunguza unene na kuudhibiti.  Hata hivyo, hatupaswi kula kalori chache kuliko mahitaji ya miili yetu na ni bora kutopunguza kalori zaidi ya 500 kwa siku.
Hii ni kwa sababu iwapo kiwango cha kalori kitakuwa kidogo kuliko hitaji la mwili, ufanisi wa mwili hupungua na kiwango cha misuli hupungua na inaweza kusababisha utapiamlo na matatizo mengine ya kiafya mwilini.

0 comments:

Post a Comment