Thursday, 8 May 2014

VYAKULA HIVI HUDHANIWA NI SALAMA, LAKINI SIYO!



KUNA vyakula vingi ambavyo vimekuwa vikitangazwa kibiashara kuwa ni bora kiafya lakini siyo kweli. Baadhi ya vyakula hivyo vinaelezwa katika makala haya kama ifuatavyo:
NYANYA ZA KOPO
Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, vyakula vingi vya kwenye makopo huwa na kiwango kingi cha kemikali aina ya BPA ambayo imegundulika kuwa na uhusiano wa magonjwa ya saratani ya matiti na kibofu cha mkojo, ugonjwa wa kisukari, ugonjwa wa moyo na matatizo ya kuzaa watoto wenye kasoro kiakili au kimwili.
Ili kujiepusha na hatari ya kupatwa na madhara hayo, watu wanashauriwa kuacha kutumia nyanya za kopo na vyakula vingine na badala yake watumie nyanya asilia. Iwapo hapana budi, nyanya au chakula kingine cha kusindika kinachoweza kutumiwa ni kile kilichohifadhiwa kwenye chombo aina ya ‘glasi’ na siyo ‘bati’.

NYAMA ZA KUSINDIKA
Ukweli ni kwamba, nyama za kwenye makopo nazo si salama kiafya na zinatakiwa kuepukwa kabisa na hii ni kwa mujibu wa utafiti wa kitabibu uliofanywa mwaka 2011 kwa stadi 7,000, uliochunguza uhusiano kati ya ugonjwa wa saratani na nyama.
Imeelezwa kuwa utafiti huo ulifanywa na Mfuko wa Dunia wa Utafiti wa Saratani kwa kutumia fedha za walipa kodi, ikiwa na maana kwamba utafiti huo haukuegemea upande wowote, ulikuwa huru na wa haki. Hivyo matokeo ya utafiti wake ni ya kuaminika.

Utafiti huo umetoa ushahidi 
mkubwa kuwahi kutolewa na umethibitisha matokeo ya tafiti zilizowahi kufanywa zikielezea kuwa nyama za kwenye kopo au nyama za kusindika huchangia hatari ya mtu kupata saratani, kiasi chochote utakachokula unahatarisha afya yako, hata kama ni kidogo.
Hivyo kama wewe ni mpenzi wa nyama, basi kula nyama ya kawaida na ile itokanayo na ng’ombe wa ‘kiswahili’ ambao hufugwa kwa kula nyasi asilia. Na siyo nyama ya wale ng’ombe wanaolishwa nafaka na madawa ya kuwafanya wanenepe na kutoa maziwa mengi. Vinginevyo jiepushe kabisa na ulaji wa nyama.

MAFUTA YA KUPIKIA
Miongoni mwa vyakula hatari tunavyoweza kuwa tunakula kila siku, ni vile vinavyopikwa na mafuta yaliyokwisha ondolewa virutubisho wakati wa kuyatengeneza.

Usifanye makosa kwa kujidanganya unatumia mafuta safi, mafuta yatokanayo na mimea (vegitable oils) yamekuwa si salama tena kama ambavyo tumekuwa tukiambiwa.
Ni kweli kwamba 
miongoni mwa vyakula bora kiafya ni pamoja na vyakula vitokanavyo na mimea, lakini mafuta yanayotengenezwa kutokana na mimea baadhi yamekuwa si salama kutokana na namna yanavyotengenezwa kuwa mafuta ya kupikia.
Ili kutengeneza
na kupata mafuta meupe, mmea hupitia katika mchakato fulani kiwandani ambao kwa njia moja au nyingine hupunguza ubora na faida zinazoweza kupatikana katika mafuta yatokanayo na mmea.
Mafuta 
unayotumia kupikia vyakula mbalimbali, baada ya kutoka kiwandani lazima yawe bado na virutubisho ambavyo vinaweza kuhimili joto la kupikia kwa mara nyingine tena ili kuepuka kugeuka na kuzalisha kemikali za sumu kutokana na joto kali.
Hatari iliyopo 
ya kupikia mafuta yaliyopoteza ubora wake wakati wa kutengenezwa ni kuongeza hatari ya kubadilisha Kolestrol nzuri kuwa mbaya baada ya kutokea kitu kinachoitwa ‘oxidation’ wakati wa kupika. Mafuta mengi ya kupikia ndiyo yalivyo, licha ya kuandikwa kuwa ‘hayana kolestrol’.
YAPI NI MAFUTA BORA?
Imegundulika kuwa kwa jamii yote ya mimea, mafuta ya nazi ndiyo chaguo bora la mafuta ya kupikia, kwa sababu yenyewe huwa hayaharibiki wala kubadilika ubora wake wakati wa kupika. Aidha, mafuta ya nazi ni ya kipekee na ni mafuta yenye faida mwilini. Mafuta ya ‘Olive’ ni mazuri  kiafya, lakini nayo huharibika haraka wakati wa kupika, hivyo ni mazuri kwa kumwagia juu ya saladi au mboga bila kuchemsha.
TAHADHARI
Mboga na matunda mengi hivi sasa hulimwa kwa kutumia kile kinachoitwa ‘kilimo cha kisasa’. Bahati mbaya sana, wakulima wengi hutumia mbolea zenye kamikali pamoja na madawa ya kuulia wadudu. Mbolea hizo na madawa mengine huweza kuifanya nyanya au chungwa kuwa kubwa kuliko kawaida. Unaweza kudanganyika ukadhani hayo ndiyo matunda bora, lakini nayo ni hatari sana kwa afya yako. Kula matunda na mboga zilizolimwa kwa kutumia mbolea asilia (organic farming).

0 comments:

Post a Comment