Thursday, 8 May 2014

MAAMBUKIZI KATIKA VIUNGO VYA UZAZI (PID)



TATIZO hili kwa kirefu huitwa ‘Pelvic Inflammatory Diseases’. 

Katika hali hii mwanamke hupata maambukizi kwenye viungo vya uzazi vya ndani zaidi ambavyo ni mirija ya mayai na vifuko vya mayai. Maambukizi haya pia husababisha majipu ya ndani kwa ndani kutokea.
Mwanamke mwenye tatizo hili hulalamika maumivu ya chini ya tumbo yanayosambaa kulia na kushoto, kutokwa na majimaji ukeni yanayoambatana na harufu na muwasho, damu kutoka bila mpangilio.
Tatizo hili likiendelea kwa muda mrefu husababisha ugumba, maumivu sugu ya tumbo chini ya kitovu na kupata mimba nje ya kizazi.

CHANZO CHA TATIZO
Maambukizi katika viungo vya uzazi vya mwanamke ‘PID’ husababishwa na bakteria ambao husambaa kutoka ukeni, huenda hadi ndani ya kuta za ndani za kizazi, kwenye mirija na hadi nje ya kizazi na mirija na husababisha atokwe na uchafu mzito unaotoa harufu mbaya .
Maambukizi katika mirija ya mayai huitwa ‘Salpingitis’ na katika vifuko vya mayai huitwa ‘Oophoritis’. 


Matatizo yote haya 
hutokea pamoja na kusababisha tatizo hili la ‘PID’ kwa hiyo mwanamke akipewa majibu kwamba ana ‘PID’ maana yake ameshambuliwa katika maeneo yote hapo juu.
Bakteria wanaosababisha tatizo hili ni Neisseria gonorrhea na Chlamydia Trachomatis. Bakteria hawa husambazwa kwa njia ya ngono.
Vilevile husambazwa au kutokea kutokana na maambukizi mengine ya ukeni na ndani ya kizazi mfano baada ya kuharibika au kutoa mimba na maambukizi sugu ya ukeni.


PID hutokea kwa wanawake 
walio na umri wa chini ya miaka 35. Huwa haitokei kabla ya kuvunja ungo. Hutokea baada ya kuvunja ungo. Pia tatizo hili la PID halitokei wakati wa ujauzito au mama anapokoma hedhi.
Mwanamke ambaye tayari ameshawahi kuugua ugonjwa huu yupo katika hatari ya kurudiwa tena na tatizo hili endapo tiba haitakuwa makini na ndiyo 

Maana baadhi ya wanawake
hulalamikia maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu na kutibiwa mara nyingi bila mafanikio.
Wengine walio katika hatari ya kupata PID ni wale walio katika kipato cha chini wanaoshindwa kumudu gharama za tiba, wanawake wanaoshirikiana kingono na wanaume zaidi ya mmoja na wale ambao wamepata magonjwa ya zinaa.

DALILI ZA UGONJWA
Mwanamke mwenye tatizo la PID hulalamika maumivu ya mara kwa mara ya tumbo chini ya kitovu ambayo wakati mwingine hutibu na kujirudia, hujihisi homa mara kwa mara hasa nyakati za jioni, hutokwa na uchafu ukeni wenye muwasho na kutoa harufu na huwa na rangi ya njano kiasi au rangi ya udongo.
Mwanamke mwenye tatizo hili pia hupata damu ya hedhi bila ya mpangilio wakati mwingine damu hutoka kabla ya tarehe au baada ya tarehe ya kupata hedhi. Hupata maumivu wakati wa tendo la ndoa. Mlango wa kizazi huvimba ambapo anapojisafisha huhisi kizazi kimeshuka kwa kugusa kitu kama gololi ndani ya uke. Maumivu ya chini ya tumbo husambaa kulia na kushoto ya nyonga.

UCHUNGUZI
Vipimo mbalimbali hufanyika kutegemea na hali ya ugonjwa wa mwanamke. Vipimo vya mkojo, damu, Ultrasound na kipimo cha kuangalia ukeni na kuchukua majimaji au uchafu huo kwa ajili ya kupima maabara hufanyika.

USHAURI NA TIBA
Ni vema mwanamke mwenye tatizo hili awahi katika kituo cha afya cha jirani kwa uchunguzi wa awali pia ni vema uwaone madaktari katika hospitali za mikoa kwa uchunguzi wa kina.

0 comments:

Post a Comment