Mshituko
wa moyo kwa lugha ya tiba unajulikana kama 'Myocardial Infarction'
inayomaanisha "Myo".. muscles au msuli, 'cardio'.... Heart au moyo na
"infarct"....kufa kwa tishu kutokana na kukosa oksijeni
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo
wapenzi wasomaji na karibuni kujiunga nami katika makala ingine katika blog
yangu.
Katika makala ya leo tutajadili mshituko wa
moyo, ambao ni miongoni mwa magonjwa yanayoongoza kwa kuua watu duniani.
Inakadiriwa kuwa watu milioni 12.5 miongoni mwa 32 milioni wanaopatwa na
mshituko wa moyo hufariki dunia duniani kote.
Nchini Marekani pekee watu laki 4
na 60 elfu hufariki dunia kutokana na ugonjwa huo kila mwaka ambapo ugonjwa huu
huua wanawake zaidi kuliko wanaume kwenye nchi hiyo. Ni mengi niliyowaandalia
katika kipindi hiki na ni matumaini yangu kuwa yatakuwa yenye faida katika
kutunza na kuimarisha afya zetu.
Mshituko wa moyo unatokea wakati
mtiririko wa damu yenye oksijeni unapozuiwa kwa ghafla katika misuli ya moyo.
Iwapo mzunguko huo wa damu hautoendelea haraka, kitendo hicho huifanya misuli
ya moyo kuharibika kwa kukosa oksijeni na hivyo kuhatarisha maisha ya
muathirika.
Kama vilivyo viungo vingine mwilini
hasa misuli, moyo nao huhitajia damu. Bila damu seli za moyo hudhoofika suala
ambalo hupelekea mtu kuhisi maumivu. Mshituko wa moyo hutokea pale mshipa mmoja
wa damu au zaidi inaposhindwa kusafirisha damu yenye oksijeni katika moyo,
kutokana na kuziba mishipa hiyo.
Mishipa ya damu inaweza kuziba kwa
sababu tofauti kama vile, kuta za mishipa ya damu inayopeleka damu kwenye moyo
(coronary arteries) kuwa nene, chembechembe za mafuta kujikusanya katika
mishipa ya damu, kudhoofika na kukonda mishipa ya damu, mishipa ya damu
inaposinjaa na kushikana au spasm na kujitokeza donge la damu katika mishipa ya
damu.
Mshituko wa moyo mara nyingi
husababishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa ya damu au Coronary Heart Disease
(CHD). Hii ni hali ambayo ndani ya mishipa ya damu hutokea kitu kiitwacho
'plaque' na kuzuia damu isiweze kupita katika mishipa ya damu, ambayo ni
matokeo ya muda mrefu.
LAKINI NI WAKATI GANI MTU
HUKABILIWA NA HATARI YA KUPATA MSHITUKO WA MOYO?
Ni pale umri wa mtu unapoongezeka
na kuwa mzee,
mtu anapokuwa na unene wa
kupindukia,
kuvuta sigara,
kuwa na shinikizo la damu au High
Blood Pressure. Kuishi bila kuwa na harakati na kutoushughulisha mwili. Mtu
kuwa na kiwango cha juu cha mafuta katika damu au High Blood Cholesterol.
Kuwa na ugonjwa wa kisukari na kuwa
na msongo wa mawazo, wasiwasi na fikra nyingi.
Mambo mengine yanayochangia kupata
mshituko wa moyo ni baadhi ya magonjwa ya moyo,
kufanyiwa operesheni ya moyo,
kuwa na ndugu katika familia ambao
wana matatizo ya moyo na jinsia ya kiume.
Tunaelezwa kuwa, uvutaji sigara
husababisha mshituko wa moyo unaotokana na kuziba mishipa ya damu kwa asilimia
36,
Ambapo unene husababisha ugonjwa
huo kwa asilimia 20.
Kukaa bila kujishughulisha au
kufanya mazoezi husababisha mshituko wa moyo kwa asilimia 7-12.
Pia wanaume wanakabiliwa na hatari
ya kupatwa na mshituko wa moyo zaidi kuliko wanawake katika kipindi chote cha
maisha hasa kabla ya wanawake hawajafikia wakati wa kukatika hedhi.
Lakini kwa ujumla kwa kuwa wanawake
huishi miaka mingi kuliko wanaume, magonjwa mengine ya moyo husababisha vifo
vya wanawake uzeeni zaidi kuliko wanaume.
0 comments:
Post a Comment