Ugonjwa wa kaswende ni ugonjwa wa zinaa
unaosababishwa na bakteria aina ya Treponema pallidum.
Ugonjwa huu ni kati ya magonjwa ya zinaa yanayoongoza
kwa kusababisha madhara mengi.
Maambukizi ya kaswende wakati wa ujauzito huleta madhara
mengi sana kama vile kujifungua kiumbe ambacho kimeshakufa, mtoto kuathirika na
ugonjwa huu wakati wa kuzaliwa, mtoto kupata matatizo wakati
wa ukuaji wake, degedege na kuongezeka kwa vifo vya watoto wachanga.
Ugonjwa wa kaswende huathiri zaidi ya mimba milioni
moja duniani kote kila mwaka na kuchangia theluthi mbili ya vifo vya watoto
wanaozaliwa wakiwa tayari wameshakufa katika nchi za maeneo ya
chini ya Jangwa
la Sahara. Asilimia 30 ya mimba zinazoathiriwa na kaswende huishia watoto
kufariki wakati wa kuzaliwa. Pia asilimia nyingine 30 ya mimba zinazoathiriwa
na kaswende husababisha watoto wanaozaliwa na ugonjwa huu kupata matatizo ya
ukuaji, degedege na kuongezeka vifo vya watoto kwa asilimia 50.
Taasisi ya kudhibiti Ugonjwa wa Ukimwi nchini Tanzania
(Tanzania National AIDS Control Programme) au NACP katika ripoti yake ya
utafiti uliofanywa chini ya Wizara ya afya na ustawi wa jamii
nchini
ilitangaza kuwa, maambukizi yote ya kaswende wakati wa ujauzito Tanzania bara
kati ya mwaka 2003 hadi 2004 yaliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.7 kwa
ujumla, kuanzia
mkoani Kilimanjaro ambako maambukizi yalikuwa ya asilimia 0.4
hadi mkoani Tabora ambako yalikuwa ya asilimia 32.
Magonjwa ya Ukimwi na kaswende mara nyingi huambatana
pamoja ambapo pia ugonjwa wa zinaa wa kaswende huongeza uwezekano wa mtu
kupata Ukimwi.
JE, UGONJWA WA KASWENDE HUAMBUKIZWA KWA NJIA GANI?
Kama nilivyosema
awali,
kaswende husababishwa na bakteria aina ya Treponema
pallidum. Njia za maambukizi za ugonjwa huu ni kama zifuatavyo:
1) Kupitia kujamiana bila kutumia kinga au ngono zembe na
mtu aliyeambukizwa kaswende.
2) Mama aliyepata ugonjwa wa kaswende wakati wa ujauzito
anaweza kumuambukiza mtoto wake wakati wa ujauzito.
3) Kuambukizwa kupitia michibuko au mipasuko kwenye ngozi
wakati wa kujamiana au wakati mwingine pale mtu anapogusana na mtu mwenye
kaswende ikiwa wote wawili wana mipasuko kwenye sehemu mbalimbali za ngozi zao.
Sio rahisi mtu kutambua kama ana michibuko au la kwenye
ngozi kwani mingine huwa midogo sana isipokuwa ile inayoweza kuonekana kwa
macho, lakini huweza kuwa njia ya maambukizo.
Baada ya kujua visababishi vya
ugonjwa huo sasa tuzibainishe pia dalili zake.
Dalili na viashiria vya ugonjwa wa kaswende hutegemea aina
ya ugonjwa wa kaswende wenyewe.
KUNA AINA TANO ZA UGONJWA WA KASWENDE AMBAZO NI;
Ugonjwa wa kaswende wa awali (Primary syphilis)
Ugonjwa wa kaswende wa pili (Secondary syphillis) Kaswende
iliyojificha (Latent syphilis)
Kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis)
Kaswende ya kurithi (Congenital syphilis)
Kaswende ya awali (primary syphilis):
Dalili ya kwanza ya aina hii ya kaswende ni kutokea
kwa kidonda kidogo cha mviringo (chancre kama kinavyojulikana kitaalamu) katika
sehemu ambayo bakteria wameingilia na hutokea kati ya siku 10 hadi miezi
mitatu (kwa kawaida kuanzia wiki 2 hadi 6).
baada ya mtu kupata
maambukizi. Kidonda hiki kinaweza kutokea kwenye sehemu ya haja kubwa,
shingo ya kizazi kwa wanawake (cervix), mdomoni, katika uume, ulimi, vulva,
tupu ya mwanamke na sehemu nyinginezo mwilini.
Tezi (lymph nodes) ambazo zipo karibu na sehemu iliyotokea
kidonda hiki kawaida huwa zinavimba baada ya siku 7 hadi 10. Kidonda hiki
hakiambatani na maumivu na kwa kuwa kinaweza
kutokea katika sehemu
zilizojificha kama kwenye shingo ya kizazi, sio rahisi mtu kutambua kama ana
aina hii ya kaswende. Kidonda hiki kinaweza kuwepo kwa muda wa wiki 3 hadi 6
kama mtu hatapata matibabu na hutoweka chenyewe bila tiba au baada ya kupata
tiba.
Robo tatu ya wale ambao hawapati tiba huishia kuingia
kwenye kundi la kaswende ya aina ya pili yaani Secondary syphilis.
Aina hii hutokea wiki 4 hadi 10 baada ya mtu kupata
kaswende ya awali.
Dalili za aina hii ya kaswende ni: vipele ambavyo
haviwashi katika viganja vya mikono au nyayo za miguu. Vipele hivi pia vinaweza
kutokea mwili mzima au sehemu mbalimbali za mwili. Pia muathirika huhisi
uchovu, kuumwa kichwa, homa, kunyofoka nywele, vidonda vya koo, kuvimba kwa
matezi mwili mzima, maumivu ya mifupa na kupungua uzito.
Kaswende ya aina hii hujitokeza kwa wiki kadhaa na
hutoweka hata bila kupata tiba kwa mtu aliyeathirika. Pia inaweza kujirudia
rudia katika kipindi cha mwaka mmoja hadi miwili na mtu huingia kwenye kundi la
aina ya tatu ya ugonjwa wa kaswende yaani (latent syphilis) baada ya miaka
miwili.
Kaswende iliyojificha (Latent syphilis).
Aina hii inajulikana kama kaswende ambayo inaweza
kuthibitika tu kwa kutumia vipimo vya maabara (serological test) na imegawanyika
katika makundi mawili.
Kundi la kwanza ni kaswende iliyojificha ya awali au
(Early latent syphilis) kwa kimombo.
Hii ni kaswende ambayo hutokea ndani ya kipindi cha mwaka
mmoja baada ya muathirika kuugua kaswende aina ya pili .
Aina hii huwa na dalili zinazojirudia kama za kaswende ya
pili.
Kundi la pili ni kaswende iliyojificha ya kuchelewa au
Late latent syphilis.
Hii hutokea baada ya mwaka mmoja wa kuugua kaswende ya
aina ya pili (secondary syphilis). Wakati wa kuugua aina hii ya
kaswende, muathirika
huwa hana dalili wala viashiria vyovyote vile na uwezo wake wa kuambukiza mtu
mwingine huwa chini au hawezi kabisa kumuambukiza ugonjwa huu mtu
mwingine.
Kaswende ya aina ya
nne kama tulivyosema inaitwa kaswende ya baadaye (Tertiary syphilis).
Asilimia 30 ya wagonjwa wa kaswende ambao hawakupata tiba
hapo awali huingia kwenye kundi hili na hutokea miaka 15 hadi 30 baada ya
maambukizi ya kaswende.
Aina hii inaweza kuathiri viungo kama
macho, ubongo,
mishipa ya fahamu,
viunganishi vya mifupa au joints,
uti wa mgongo, moyo na mishipa ya damu.
Kwa ajili hiyo aina hii ya kaswende ni yenye madhara
makubwa kwani huweza kusababisha upofu, magonjwa ya moyo,
magonjwa ya akili na magonjwa ya mishipa ya fahamu.
Huweza kumfanya mtu kuwa kiziwi na kupungukiwa na
kumbukumbu na hata kumsababishia kifo.
Pia aina hii ya kaswende inaweza kuathiri mfumo wa
chakula, mfumo wa kupumua na mfumo wa uzazi.
Kaswende ya aina ya mwisho ni ya kurithi (Congenital syphilis).
Aina hii ya kaswende hutokea wakati wa ujauzito au baada
ya mtoto kuzaliwa.
Nusu ya wototo wanaozaliwa huwa hawaonyeshi dalili zozote
za ugonjwa huu.
Nusu ya watoto wenye maambukizi ya kaswende hufariki dunia
muda mfupi kabla ya kuzaliwa au baada ya kuzaliwa.
Dalili za aina hii ya kaswende kwa mtoto mchanga zinaweza
kutokea baada ya kuzaliwa au wiki 2 hadi miezi 3 baada ya kuzaliwa.
Dalili hizo ni, kutoongezeka uzito au kushindwa kukua,
homa, kukasirika haraka, kutochongoka kwa pua yaani pua linakuwa bapa, vipele
kwenye viganja vya mikono na kwenye nyayo ambavyo huwa ni vipele vya
rangi ya madini ya shaba kwenye uso, viganja vya mikono na nyayo na vipele
kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu ya haja kubwa.
Dalili nyingine ni kutokwa na majimaji puani, kuongezeka
ukubwa wa ini na bandama, ngozi kuwa ya njano, na upungufu wa damu
mwilini (anemia).
DALILI ZA UGONJWA WA KASWENDE KWA MTOTO MKUBWA
Ambazo ni,
kuathirika meno (Hutchinson teeth),
maumivu ya mifupa, kupata upofu,
kupungua uwezo wa kusikia au mtoto kuwa kiziwi na kuwa na
ukungu kwenye mboni za macho (Clouding of cornea).
Dalili nyingine ni kutokwa vidonda vya rangi ya kijivu
kwenye sehemu ya haja kubwa na kwenye tupu ya mwanamke, ngozi kuwa na mabaka
meusi kwenye mdomo, sehemu za siri na sehemu za haja kubwa, maumivu kwenye
mikono na miguu na pia kuvimba jointi za mifupa.
Ewe
msomaji pale unapoona dalili kama hizo katika mwili wako haina budi
uwahi kituo cha afya mapema kabisa ili uweze pumatiwa msaada wa matibabu
na ushauri.
0 comments:
Post a Comment