Wapenzi wasomaji wa makala zangu ni
matumaini yangu kuwa hamjambo popote pale mlipo mkiwa mnazisoma makala hizi za
afya.
Nimeamua leo kuzungumzia mada
inayohusiana na Afya kwa ujumla. Najua ungependa kwanza tuwaeleweshane Neno 'afya'
linamaanisha nini hasa.
AFYA Kwa mujibu wa ufafanuzi
uliotolewa na kutangazwa na Shirika la Afya Duniani WHO katika mkutano wake wa
tarehe 19-22 Juni 1946 na kusainiwa na wawakilishi wa nchi 61 duniani, Ni kuwa
'afya ni hali ya mtu kuwa vizuri kimwili,
kiakili na kijamii na sio tu kutokuwa na ugonjwa au udhaifu.' Ufafanuzi huo
ulianza kutumika Aprili mwaka 1948 na hadi hii leo
maana hiyo ya afya haijabadika.
maana hiyo ya afya haijabadika.
Ufafanuzi huo unamaanisha kwamba,
tunaposema mtu ana afya sio tu tunakusudia kuwa mwili wake hauna maradhi,
upungufu au udhaifu bali pia mtu huyo anatakiwa asiwe na
matatizo ya kimwili,
kiakili na hata kijamii. Kwa mujibu wa maana hiyo pana ya neno 'afya' tunaona
kuwa watu wengi wanaamini kuwa afya imeganyika katika makundi mawili muhimu ambayo
ni afya ya kimwili na afya ya kiakili.
Afya ya mwili kwa binaadamu ina
maana, kuwa na mwili wenye afya usiokuwa na maradhi, afya ambayo kwa kawaida
hutokana na kuupa mwili mazoezi ya mara kwa mara, lishe bora na mapumziko ya
kutosha.
Katika nchi au maeneo ambayo watu
wanapata lishe bora, huduma nzuri za afya na kuishi katika hali ya kimaisha
inayoambatana na viwango vinavyotakiwa, kwa kawaida vimo na uzito wao
huongezeka. Ukweli ni kuwa, ukiwauliza watu wengi afya ni nini, watasema kwamba
inahusiana na mwili kuwa salama bila ya kuathirika na ugonjwa.
Lakini tukienda ndani zaidi, kitiba
afya ya mwili
inaamanisha ustawi wa mwili hali ambayo mtu anaipata kwa
kutekeleza vipengee vyote vinavyohusiana na afya katika maisha yake.
Uzima wa mwili unaakisi kufanya kazi
vizuri moyo na mfumo wa kupumua, uwezo wa misuli, viungo pamoja na mwili kuweza
kukubali mabadiliko tofauti na muundo wa mwili kwa ujumla.
Masuala mengine ni pamoja na lishe
bora, uzito wa mwili, kutokuwepo uraibu wa madawa ya kulevya, pombe, mahusiano
salama ya kimwili, usafi kwa ujumla na pia kulala na kuamka kwa wakati
unaotakiwa.
Afya ya akili au uzima wa kiakili ni
utambuzi wa mtu na uzima wake kisaikolojia. Mtu ambaye ana afya nzuri ya
kiakili hana matatizo ya kiakili au kichaa. Kwa mujibu wa Shirika la Afya
Duniani WHO, 'afya ya akili ni pale mtu anapoweza kufahamu uwezo wake na
kustahamili
mfadhaiko (stress) unaotakana na dhiki au matatizo ya kawaida ya
kimaisha. Aweze kufanya kazi yenye kuleta mafanikio na kuchangia masuala tofauti
katika jamii yake.'
Ni rahisi watu kuelezea maana ya
ugonjwa wa akili kuliko afya ya akili. Watu wengi wanakubali kwamba afya ya
akili ni kutokuwepo ugonjwa wa akili lakini maana hiyo haitoshi.
Hii ni kwa
sababu kama tutachagua watu 100 ambao hawana kichaa au ugonjwa wa akili
unaoweza kutambuliwa na daktari wa akili, lakini miongoni mwao tunaweza kuona
kwamba afya ya baadhi yao kiakili imeimarika kuliko wengine.
Tunaweza kusema kuwa, afya ya akili
inajumuisha masuala kadhaa kama vile uwezo wa kuishi kwa furaha, uwezo wa
kuvumilia shida na kurejea katika hali ya kawaida baada ya kupatwa na matitizo,
uwezo wa kuwa na uwiano katika maisha, uwezo wa kubadilika kwa urahisi na
kuzoea mazingira mapya, kujihisi salama na kujitambua.
Afya ya mtu na ya jamii kwa ujumla
inaathiriwa na masuala mengi tofauti. WHO inaeleza kwamba, afya mbaya au nzuri
ya watu inategemea mazingira wanayoishi, matukio
yaliyowakumba katika maisha
yao ya zamani na ya hivi sasa. Shirika hilo la Afya Duniani linatujulisha kuwa,
masuala yafuatayo huweza kuathiri afya zetu kwa kiasi kikubwa na
matumizi ya
vituo vya afya katika jamii. Masuala hayo ni mahali tunapoishi, hali ya
mazingira tuishiyo, jenetiki, kipato chetu, kiwango cha elimu zetu na uhusiano
wetu na marafiki na familia. WHO pia inasema, afya zinaainishwa na
masuala makuu matatu,
Uchumi na jamii zetu au mazingira ya
kijamii na kiuchumi.Mahala tunapoishi au yale yanayotuzunguka yaani mazingira
ya kifizikia. Jinsi tulivyo na yale tunayoyafanya, yaani sifa na tabia
binafsi ya mtu.
Kwa kuwa afya nzuri inategema
mukhtadha wa maisha yetu, si sawa kusifu au kuwalaumu watu kutokana na afya
mbaya au nzuri walizonazo.
Sababu kuu zinazochangia hali zetu za
afya kuwa nzuri au mbaya mara nyingi haziko katika mikono wala uwezo wetu.
Kwa
mujibu wa WHO, miongoni mwa sababu hizo ni, hali ya kiuchumi na kijamii ambapo
watu ambao wanaishi katika hali iliyoimarika kisiasa na kijamii, huwa na hali
nzuri za kiafya kuliko wale wanaoishi kwenye jamii yenye hali mbaya ya kisiasa
na kijamii.
Uhusiano huo unabainishwa wazi katika
utafiti uliofanywa nchini Australia unaoonesha kwamba, wanawake wanaoishi
kwenye jamii zenye hali duni kijamii na kiuchumi, mara nyingi hushindwa
kuwanyonyesha watoto wao wachanga, suala ambalo huathiri afya za watoto hao.
Pia utafiti uliofanyika Korea Kusini
umeonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya hali duni ya kijamii na kiuchumi
na hatari ya kupatwa na baadhi ya magonjwa kama mshituko wa moyo.
Elimu ni sababu nyingine inayoathiri
afya zetu. Watu wasiokuwa na elimu ya kutosha kwa ujumla huwa hawana ufahamu
mzuri kuhusiana na masuala yanayoathiri afya zao ikilinganishwa na wale
walioelimika.
Utafiti uliofanywa na wataalamu
katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Feinberg huko Chicago Marekani umebainisha
kwamba, watu wazima waliokuwa na kiwango cha juu cha elimu kuhusiana na masuala
ya afya, wana nafasi kubwa ya kuishi maisha marefu kuliko kinyume chake.
Suala jingine linaloathiri afya ni
ajira. Takwimu zinaonesha kuwa, iwapo una kazi, basi una nafasi nzuri zaidi ya
kuwa na afya bora kuliko mtu asiyekuwa na kazi. Kama una ajira ya kudumu na
kazi nzuri zaidi, hali ya kiafya pia huboreka.
Hivyo ninahitimisha Makala hii ya
AFYA NINI,
kwa usemi wa Mahatma Ghandi kuhusiana
unaosema kwamba, "utajiri wa kweli
ni uzima, na wala sio vipande vya dhahabu au shaba."
0 comments:
Post a Comment