Saturday, 3 May 2014

HUU NDIO ULISHAJI/UNYONYESHAJI WA MTOTO WAKATI MAMA HANA VIRUSI VYA UKIMWI AU HAFAHAMU HALI YAKE YA UAMBUKIZO



Makala hii inatoa maelekezo kuhusu ulishaji wa mtoto wakati mama hana
virusi vya UKIMWI, hajui hali yake ya uambukizo na pia wakati mama anaishi na

virusi vya UKIMWI.
Elimu kuhusu ulishaji watoto katika hali ya kawaida ni msingi
muhimu kwa mama kuelewa jinsi ya kumlisha mtoto wakati ana virusi vya UKIMWI.

Pia, makala hii haitoshi kumfanya mlishaji wa mtoto kuwa na stadi na utaalamu wa
kutosha kwenye eneo hilo.
Ili kuweza kutoa huduma kamilifu kwa hili mama anayeishi na
virusi vya UKIMWI kuhusu kumlisha mtoto, anahitaji mafunzo zaidi
Taarifa ambazo nimeziweka kwenye makala hii ni kumwezesha mama husika
kupata mwanga au kuelewa kwa kiasi jinsi ya ulishaji wa mtoto aliyezaliwa na mama
anayeishi na virusi vya UKIMWI.

Kwa wanawake ambao hawana virusi vya UKIMWI, wale ambao hawajui hali zao za
uambukizo na wale waliopima lakini hawakuchukua majibu; wote wanakuwa katika
kundi moja; ambapo hushauriwa kumlisha mtoto kama kawaida na kufuata taratibu za
kawaida za kunyonyesha.
Maziwa ya mama ndiyo chakula pekee na bora zaidi kwa mtoto mchanga kuliko
maziwa mengine yoyote. Kugundulika uwezekano wa maziwa ya mama
kumwambukiza mtoto virusi vya UKIMWI kumesababisha wataalamu kushauri

utumiaji wa maziwa mbadala au kurekebisha namna ya kunyonyesha ili kupunguza
uwezekano wa uambukizo wa virusi vya UKIMWI kwa mtoto. Ni muhimu
ikumbukwe kuwa chakula cha mtoto chini ya umri wa miezi sita ni maziwa pekee.

Ulishaji wa mtoto wakati mama hana virusi vya
UKIMWI au
hafahamu hali yake ya uambukizo

Kunyonyesha maziwa ya mama

Ni dhahiri kuwa maziwa ya mama ndiyo lishe bora kwa mtoto mchanga kuliko maziwa
mengine yoyote. Kunyonyesha maziwa ya mama kunampa mama pamoja na mtoto
faida nyingi.

• Faida kwa mtoto:
·
Humpatia virutubishi vyote anavyohitaji kwa uwiano ulio sahihi kwa ukuaji wa akili na mwili kwa miezi sita ya mwanzo;
·
Humpatia kinga dhidi ya maradhi mbalimbali kama kuharisha, maradhi ya njia ya hewa na masikio;
·
Huleta uhusiano mzuri na wa karibu kati ya mtoto na mama;
·Watoto walionyonya maziwa ya mama huwa na mwenendo mzuri pamoja na akili zaidi ukilinganisha na wale wasionyonya maziwa ya mama.
·
Maziwa ya mama huyeyushwa kwa urahisi tumboni mwa mtoto na hivyo kusharabiwa na kutumiwa na mwili kwa ufanisi.

·
Faida kwa mama:
·
Mama anaponyonyesha mara baada ya kujifungua husaidia tumbo la uzazi kurudi katika hali ya kawaida mapema. Pia husaidia kupunguza damu
kutoka baada ya kujifungua hivyo huchangia kuzuia upungufu wa wekundu wa damu;
·
Hupunguza uwezekano wa kupata ujauzito katika miezi sita ya mwanzo kama mama atamnyonyesha mtoto maziwa yake pekee mara nyingi (zaidi ya mara 10) kwa siku na pia kama hajapata hedhi katika miezi sita ya mwanzo;
·
Hupunguza uwezekano wa kupata saratani ya mfuko wa uzazi na matiti;
·
Hujenga uhusiano wa karibu kati ya mama na mtoto; na
·
Iwapo mama aliongezeka uzito mkubwa wakati wa mimba, kunyonyesha husaidia kumrudishia mama umbile lake la kawaida.


Faida nyingine za maziwa ya mama:
·
Ni safi, salama na hupatikana muda wote katika joto sahihi kwa mtoto na hayahitaji matayarisho;
·
Hayaharibiki ndani ya titi na hata yakikamuliwa huweza kukaa kwa muda wa saa 8 katika joto la kawaida bila kuharibika, na saa 72 kwenye jokofu;
·
Gharama yake ni ndogo ukilinganisha na maziwa mbadala;
· Nchi huokoa fedha za kigeni ambazo zingenunulia maziwa mbadala na dawa;
·
Huokoa muda wa mama na fedha za familia ambazo zingenunua maziwa mbadala au kulipia matibabu;
·
Hayaleti matatizo ya mzio (allergies) kama pumu na magonjwa ya ngozi;
·
Kunyonyesha maziwa ya mama huchangia kutunza mazingira, kwani hayaachi mabaki kama makopo na chupa ambavyo hutumika kwa maziwa mbadala;
·
Maziwa ya mama yana maji ya kutosha hivyo mtoto chini ya miezi sita hahitaji maji;


Mapendekezo ya kumsaidia mama ili anyonyeshe kwa ufanisi
·
Mtoto aanze kunyonya maziwa ya mama mara tu baada ya kuzaliwa (katika saa
moja ya mwanzo);
·
Mama aliyejifungua kwa operesheni, asaidiwe ili aanze kunyonyesha mara
anapopata fahamu. Inaweza kuchukua hadi saa sita kupata fahamu, mtoto
asipewe maji ya sukari au ya kawaida. Mama ambaye hakupewa dawa ya usingizi anaweza kuanza kunyonyesha mapema zaidi;
·
Mtoto anyonyeshwe kila anapohitaji usiku na mchana ili kuendeleza utokaji mzuri wa maziwa ya mama;
·
Mtoto asipewe kitu kingine chochote hata maji, isipokuwa maziwa ya mama mpaka afikie umri wa miezi sita;
·
Mtoto apakatwe kwa namna ambayo anafikia titi vizuri.
·Wakati wa kunyonyesha, chuchu yote na sehemu kubwa ya eneo jeusi linalozunguka chuchu liingie kinywani kwa mtoto.
·
Mtoto afikishapo umri wa miezi sita inashauriwa kuanza kumpa chakula cha
·nyongeza huku akiendelea kunyonya maziwa ya mama.
Mtoto apewe chakula cha nyongeza kwa kutumia kikombe au kibakuli na kijiko;
·
Mtoto anyonyeshwe kwanza, ndipo apewe chakula cha nyongeza (baada ya miezi 6);
·Vyakula vya nyongeza viwe ni vya mchanganyiko wa makundi yafuatayo ya vyakula:

Vyakula vya nafaka, mizizi na ndizi

·Vyakula vinavyotokana na wanyama na jamii ya mikunde

·Mboga-mboga

·Matunda

·Mafuta na sukari (kwa kiasi)

Mtoto aendelee kunyonya mpaka afikie umri wa miaka miwili au zaidi, huku akipewa chakula mara tano au zaidi kwa siku;



Jinsi ya kumpakata na kumweka mtoto kwenye titi
Picha 1 (a)
inaonyesha njia sahihi ya kumshika mtoto ili afikie titi vizuri. Tumbo la mtoto limemwelekea mama na uso umeangalia na umesogelea titi.


Picha 1 (b) inaonyesha njia
ambayo si sahihi ya kumshika mtoto. Hapo mtoto hataweza kuingiza titi kinywani vizuri.


Picha 2 (a) inaonyesha mtoto ambaye titi limeingia vizuri kinywani yaani chuchu pamoja na sehemu nyeusi inayozunguka chuchu imeingia kinywani. Midomo iko wazi na kidevu kimegusa titi. Mtoto atanyonya vizuri.


Picha 2. (b) inaonyesha mtoto ambaye hakuingiza titi vizuri kinywani. Mtoto huyu ananyonya chuchu tu, midomo haikufunguka vizuri na kidevu kiko mbali na titi. Mtoto hataweza kunyonya vizuri.

MUHIMU
Mtoto anayepewa chakula cha nyongeza, ni vyema anyonyeshwe kabla ya kulishwa.

0 comments:

Post a Comment