Saratani ni aina ya ugonjwa
unaosababisha ukuaji wa seli za mwili kubadilika na kukua bila mpangilio
maalum.
Saratani ya matiti hutokea
kwenye titi ambalo kwa
kawaida lina sehemu ya kutengeneza maziwa ijulikanayo
kama lobules na aina fulani ya mishipa inayounganisha hizi lobules na chuchu za
titi. Sehemu kubwa iliyobakia ya matiti inajumuisha mafuta na tishu ambazo
kitaalamu
tunazoita connective and lymphatic tissue. Saratani
ya matiti inayotokea kwenye lobuleshuitwa lobular carcinoma na
ile inayotokea kwenye ducts huitwa ductal carcinoma.
Baadhi ya saratani ya matiti
zinaongeza ukubwa kutokana na kuwa na vishikizi aina ya receptors zinazojulikana
kama estrogen receptorskwenye seli zao ambazo husababisha ukuaji wa
saratani ya matiti.
Kuna wanawake wengine wana
viashiria vya asili vinajulikana kamaHER2 positive breast cancer ambacho
husaidia seli kuongezeka, kugawanyika na kujirekebisha
pale zinapoharibika.
Kiashiria hiki kinaaminika ndicho kinachosababisha wanawake hawa kuwa na
saratani ya matiti yenye madhara zaidi na kuwa na uwezekano mkubwa
wa kujirudia
kwa saratani baada ya tiba tofauti na wale ambao hawana kiashiria hiki
cha HRE2.
Vihatarishi vya Saratani
Kuna mambo kadhaa ambayo
yameonekana kuwa na uhusiano, ama wa moja kwa moja au kwa kupitia vitu
vingine,
wa kusababisha saratani ya matiti, au kumfanya mtu au kundi la watu kuwa katika
hatari ya kupata ugonjwa huu kuliko wengine. Mambo hayo ni pamoja na
1.
Jinsia: Ingawa, saratani ya
matiti huweza kutokea kwa wote wanawake na wanaume, imeonekana kuwa wanawake ni
waathirika wakubwa zaidi wa saratani hii ikilinganishwa na wanaume.
2. Umri: Uwezekano
wa kupata saratani hii huendana na umri wa mtu. Kadiri umri wa mtu
unavyoongezeka ndivyo pia uwezekano wa kupata saratani hii unavyozidi kuwa
mkubwa. Wanawake walio na umri wa
kuanzia miaka 50 wapo kwenye hatari kubwa
(mara 2 au 3 zaidi) kuliko walio na umri wa miaka 45.
3. Uasili wa
mtu (ethnicity):
Saratani ya matiti hutokea zaidi kwa wanawake wazungu kuliko
wanawake wa kiafrika au wenye asili ya afrika (weusi).
4. Uzazi:
Wanawake
ambao hawajazaa au kunyonyesha wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani ya
matiti. Wanawake wanaopata ujauzito kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 nao
pia wapo kwenye hatari kubwa ya kupata saratani hii.
5. Historia ya
ugonjwa huu katika familia:
Wanawake walio katika familia zenye historia
ya ugonjwa huu wana uwezekano mkubwa wa kupata
saratani ya matiti ukilinganisha
na wale ambao hawana historia ya ugonjwa huu katika familia zao. Kwa mwanamke
aliye na ndugu (mama, dada au mtoto)
ambaye aliwahi kupata saratani hii kabla
ya umri wa miaka 50, uwezekano wa mwanamke huyu kupata ugonjwa huu ni mara
mbili ya yule ambaye hana historia hii.
6. Umri wa
kuvunja ungo:
Wanawake wanaovunja ungo (kupata hedhi) kabla ya umri wa miaka 12
wapo kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu.
7. Kuacha
kupata hedhi:
Kwa kawaida wanawake huacha kupata hedhi wafikapo miaka 45,
hali ambayo kitaalamu hujulikana kama menopause. Wanawake
wanaochelewa kuacha
kupata hedhi, kwa mfano wale wanaoendelea kupata hedhi
wakiwa na zaidi ya miaka 45, wapo kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata saratani
ya matiti.
8. Historia ya
saratani ya matiti:
Wanawake ambao wamewahi kupata ugonjwa huu kwenye titi la
upande mmoja hapo kabla, wana uwezekano mkubwa wa kupata tena saratani kwenye
titi la upande mwingine hapo siku za usoni.
9. Ulaji wa
vyakula venye mafuta mengi:
Tafiti zinaonesha kuwa, wanawake
wanaopendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi wapo kwenye hatari zaidi ya
kupata ugonjwa huu.
10.
Kuongezeka uzito:
Tafiti
nyingine zimeonesha kuwa, wanawake wanene wana uwezekano mkubwa wa kupata
saratani ya matiti ukilinganisha na wale wa uzito mdogo au wa kati.
11.
Uvutaji sigara:
Kuna matokeo yenye
kukinzana kuhusu uhusiano wa uvutaji sigara na hatari ya kupata saratani ya
matiti.
Wakati baadhi ya tafiti zinaonesha uhusiano wa karibu kati ya uvutaji
sigara na uwezekano wa kupata saratani ya matiti, tafiti nyingine zinaonesha
majibu
yenye kutofautiana kuhusu uhusiano wa uvutaji wa sigara na saratani ya
matiti. Hata hivyo, kwa ujumla, wanawake wanaojizuia kuvuta sigara wanakuwa na
afya njema zaidi kuliko wale wanaovuta sigara.
12.
Unywaji pombe:
Imeonekana kuwa
wanawake wanaokunywa pombe zaidi ya chupa moja kwa siku wana uwezekano wa
kupata saratani ya matiti kwa asilimia zaidi ya ishirini.
13.
Historia ya tiba ya mionzi:
Wanawake
ambao wamewahi kupata tiba ya mionzi hususani wakati wa ukuaji wa matiti, wapo
kwenye hatari zaidi ya kupata ugonjwa huu. Hali hii
husababishwa na ukweli kuwa
mojawapo ya madhara ya mionzi ni kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya aina
yoyote.
14.
Matumizi ya dawa za kupanga uzazi:
Kuna
ushahidi kuwa saratani ya matiti ina uhusiano na matumizi ya muda mrefu ya
vidonge vya kupanga uzazi.
15.
Kuwepo kwa kiwango kikubwa cha homoni mwilini:
Kwa wale
wanaotumia tiba ya homoni inayojulikana kamahormone replacement therapy, kwa
sababu
nyingine yeyote ile, au wale wenye kiwango kikubwa cha homoni kama vile
oestrogen na progesterone mwilini mwao wapo kwenye hatari zaidi ya kuugua
saratani ya matiti.
16.
Kuwa na matiti makubwa:
Wanawake
wenye matiti makubwa (dense breast tissue) wana uwezekano
mkubwa wa kupata saratani ya matiti. Hali hii hutokana na ukweli kuwa wakati
mwingine ni vigumu sana kwa madaktari kutambua kama wana saratani au la
kutokana na ukubwa wa matiti yao.
Saratani
husambaa vipi?
Kwa kawaida saratani husambaa kwa njia tatu zifuatazo;
Kwa kawaida saratani husambaa kwa njia tatu zifuatazo;
1.
Kupitia tishu – Saratani husambaa kwenye tishu za kawaida ambazo
zimezunguka eneo la saratani.
2. Kupitia
mfumo wa limfu(lymphatic system) - Saratani huvamia mfumo wa lymph
na kufuata mishipa yake hadi sehemu nyingine za mwili.
3. Kupitia
damu – Saratani inaweza kusambaa kupitia damu kwa kuvamia mishipa ya damu ya
vena na capillaries (veins and capillaries) na
kusafiri kutumia damu hadi sehemu nyingine za mwili.
Dalili za Saratani ya Matiti
Dalili ya awali inayoweza
kutambulisha saratani ya matiti ni kuwepo kwa uvimbe kwenye titi ambao huwa na
hali tofauti na sehemu nyingine za titi. Hata hivyo, si kila uvimbe
kwenye titi
unaashiria uwepo wa saratani ya matiti. Uvimbe huu huwa mgumu, unaochezacheza
kwenye titi,
ambapo wakati mwingine unaweza kuwa na maumivu makali au kusiwe na
maumivu yeyote. Uvimbe huu huwepo zaidi ya mzunguko mmoja wa hedhi kwa wale
ambao hawajaacha kupata hedhi.
Dalili nyingine ni pamoja na
1.
Kuwepo kwa uvimbe kwenye sehemu za kwapa
2. Sehemu ya
titi kuingia ndani inayoashiria uvimbe usioonekana au usioweza kuhisiwa
3. Mabadiliko
kwenye chuchu, kama vile chuchu kuzama ndani au kuwa na nundu ndogo ndogo,
chuchu kuwasha, kuhisi kama kuchoma, kidonda kwenye chuchu au chuchu kuwa na
kovu ambalo huashiria saratani ya sehemu hiyo
4. Kubadilika
kwa umbo la titi, ngozi ya titi kuwa kama ganda la chungwa (peu de
orange), ngozi kuwa na rangi nyekundu, na kuongezeka kwa joto kwenye titi.
Dalili hizi huashiria kusambaa kwa saratani mwilini.
5. Dalili
nyingine ni chuchu kutoa maji yasiyo ya kawaida ambayo hayana rangi. Aidha
wakati mwingine, chuchu hutokwa damu au majimaji yenye rangi nyingine tofauti.
Ugunduzi wa
Saratani ya Matiti
Pamoja na mgonjwa kufanyiwa
uchunguzi wa kitabibu na wataalamu wa afya kuweza kutambua uwepo wa tatizo
hili, anaweza pia kufanyiwa vipimo vifuatavyo ili kusaidia kutambua ugonjwa
huu.
1.
X-ray ya matiti au Mammogram ambayo
ina uwezo wa kuonesha ulipo uvimbe kwenye matiti
2. Ultra-Sonography ni
kipimo kinachosaidia kutambua iwapo uvimbe uliopo ndani ya matiti umejaa maji
ama la ili ufanyiwe vipimo zaidi
3. Kipimo
kinachofanywa kwa kuchukua sehemu ya uvimbe(Aspiration) kwa kutumia
aina fulani ya sindano (fine needle) na kisha kupeleka maabara
sehemu iliyochukuliwa kwa ajili ya kutafitiwa zaidi ili kugundua uwepo wa
saratani. Kwa kitabibu kipimo hiki hujulikana kama Fine Needle
Aspiration and Cytology (FNAC)
4. Kipimo
kingine ni upasuaji mdogo unaofanywa kwenye titi lililoathirika kwa ajili ya
kuchukua sehemu ya titi (surgical biopsy) na kisha kuipeleka
maabara kwa ajili ya uchunguzi zaidi.
5. Sentinal
lymph node biopsy - Kipimo hiki hufanywa ili kujua kama saratani imesambaa hadi
kwenye tezi.
Aidha kwa nchi zilizopiga
hatua ya kimaendeleo, mgonjwa anaweza pia kufanyiwa vipimo kama
- PET Scan: Hii ni aina mpya ya kipimo ambacho kinahusisha CT Scan na PET kwa pamoja. Kipimo hiki kina uwezo wa kutambua uwepo wa saratani ya matiti,
- iwapo saratani hiyo imesambaa ama bado, na kama itakuwa imeshasambaa, basi ni sehemu gani ya mwili iliyoathirika.
Aidha kipimo hiki, kina uwezo
wa kutofautisha tezi au lymph nodes zilizovimba zina uhusiano na
saratani (Metastatic
lymph nodes) au hazina uhusiano na saratani (Benign lymph
nodes).
Baadhi ya matabibu hupata
taabu kutofautisha kati ya kuvimba kwa tezi kunakosababishwa na saratani na
kule
kunakosababishwa na vitu vingine tofauti na saratani. Hali hii hutokea kwa
wagonjwa wa saratani wenye tezi zilizovimba ambao hudhani kuwa kuvimba huko ni
sababu ya saratani (metastatic lymph nodes).
Kipimo hiki pia husaidia
madaktari kuwatibu wagonjwa wa saratani kwa kutumia mionzi kwa usahihi
zaidi ( Precise
Radiotherapy) au kutumia mionzi inayolekezwa
na kipimo hiki (PET Scan guided radiotherapy). Aidha, PET
Scan huweza pia kutumika kuonesha maendeleo ya mgonjwa wa saratani
baada ya kupata tiba ya mionzi(Radiotherapy) au dawa za kutibu
saratani (Chemotherapy).
- Kipimo kingine hujulikana kama DCE MRI (Dynamic contrast MRI). Hiki nacho ni kipimo kipya kwenye ugunduzi na tiba ya saratani. Aina ya kipimo hiki
- hutofautina na kipimo cha MRI ya kawaida kwani DCE MRI ina uwezo wa kutoa maelezo ya ziada namna uvimbe wa saratani unavyopata damu yake kupitia
- mishipa ya damu (blood vessels of the tumor) na hivyo kukua na kuongezeka zaidi. Uwezo mwingine wa DCE MRI ni kutoa maelezo mengine sawa na PET Scan.
Hata hivyo, vipimo hivi
vya PET Scan na DCE MRI kwa sasa havipatikani
nchini Tanzania.
Tiba ya saratani ya matiti
Upasuaji
Upasuaji
Lengo kuu la upasuaji ni
kuondoa saratani kwenye titi pamoja na tezi(lymph nodes). Zipo aina
kadhaa za upasuaji unaoweza kufanywa kwenye titi lililogundulika kuwa na
saratani. Aina hizo ni pamoja na
1.
Lumpectomy:
Huu ni upasuaji
unaofanywa kuondoa sehemu ya saratani pamoja na sehemu ya titi ambayo
haijaathirika kwa saratani. Hii hufuatiwa na tiba ya
mionzi (radiotherapy) kwa
muda wa kati ya wiki 6 au 7.
Mgonjwa anayefanyiwa aina hii ya upasuaji anakuwa
na uwezekano wa kuishi muda mrefu sawa na anayefanyiwa upasuaji wa kuondoa titi
lote lililoathirika.
2. Simple ama
Total mastectomy:
Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote
lililoathirika kwa ugonjwa wa saratani.
3. Radical
mastectomy:
Aina hii ya upasuaji uhusisha uondoaji wa titi lote na kundi
la tezi liloathirika kwa saratani, pamoja na misuli ya sehemu za kifua (chest
wall muscles). Hata hivyo, upasuaji wa aina hii ni nadra sana kutumika siku
hizi.
4. Modified
radical mastectomy:
Ni aina ya upasuaji unaohusisha uondoaji wa titi lote
lililoathirika pamoja na kundi lote la tezi (lymph nodes) chini
ya mkono (axilla) bila kuhusisha uondoaji wa misuli ya kifua.
Kwa ujumla, lumpectomy na mastectomy,
zote zinahusisha uondoaji wa kundi la tezi ambalo lipo karibu na uvimbe wa
saratani (regional lymph nodes).
Tiba ya
mionzi
Mionzi inaweza kutumika
kuharibu seli za saratani zilizobaki kwenye matiti, kifua (chest wall),
au/na eneo la chini ya mkono mara baada ya upasuaji kufanyika.Mionzi pia
inaweza kutumika kupunguza ukubwa wa uvimbe wa saratani kabla ya kufanyika kwa
upasuaji.
Tiba ya saratani kwa njia ya
dawa (Systemic therapy)
Tiba ya aina hii inahusisha matumizi
ya kemikali maalum za kutibu saratani (chemotherapy) pamoja na
matumizi ya homoni (hormonal therapy).
Tiba kwa kutumia homoni (Adjuvant
hormonal therapy) hutumika ili kuua seli za saratani ambazo
hazikugundulika hapo awali na ambazo yawezekana zimesambaa sehemu nyingine za
mwili. Tiba hii hutolewa baada ya kufanyika kwa upasuaji wa kuondoa uvimbe wa
saratani.
Aina hii ya tiba hutegemea na
ukubwa wa uvimbe, matokeo ya vipimo vya kimaabara vya saratani (histological
results), na iwapo saratani imesambaa hadi kwenye tezi za kwenye
kwapa la
mgonjwa ama la. Tiba hii pia yaweza kutolewa kwa mgonjwa ambaye saratani
imeshasambaa mwilini kwake kwa muda mrefu, na ambaye hawezi kufanyiwa upasuaji.
Baadhi ya kemikali
zinazotumika kutibu saratani ya matiti nicyclophosphamide, methotrexate, na
flouracil. Kwa kawaida dawa hizi hutolewa kwa kujumuisha dawa 2 au 3 kwa
wakati mmoja.
Ieleweke pia kuwa, kama
ilivyo kwa dawa nyingine za kutibu magonjwa mengine tofauti na saratani,
kemikali (dawa) hizi za saratani pia zina madhara mbalimbali kwa
mtumiaji.
Madhara haya huletwa na ukweli kuwa, pamoja na kuwa kazi kuu ya kemikali hizi
ni kuua seli zenye saratani,
hutokea pia kuua na kuathiri seli za kawaida yaani
zisizo na ugonjwa wa saratani kama vile seli zilizo kwenye mdomo, nywele, pua,
kucha, utumbo na hata sehemu za siri za mwanamke.
Hata hivyo, tofauti na seli
za saratani, seli za kawaida huwa na uwezo wa kujizaa tena, kukua na kurudi
katika hali yake ya kawaida wakati zile za saratani hazina uwezo huo. Madhara
ya dawa hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.
Dalili za saratani kusambaa
mwilini ;
1.
Maumivu ya mifupa
2. Maumivu
kwenye titi
3. Vidonda
kwenye ngozi
4. Kuvimba
mkono karibu na eneo la saratani
5. Kupungua
uzito.
0 comments:
Post a Comment