Saturday, 3 May 2014

HUU NDIO UGONJWA WA KISUKARI AU DIABETES MELLITUS-2

KISUKARI HUWEZA KUSABABISHA MADHARA YAFUATAYO KWA MHUSIKA IWAPO HAKITATIBIWA INAVYOPASWA.
Kuziba kwa mishipa mikubwa ya damu kutokana na kuzungukwa na mafuta (Atherosclerosis).
Mgonjwa kushindwa kuona vizuri au kushindwa kuona kabisa na kuwa kipofu (diabetic retinopathy)
Kushindwa kufanya kazi vizuri kwa figo,
Mgonjwa kuhisi ganzi na kupoteza hisia mikononi na miguuni kwa sababu ya kuharibika kwa neva (diabetic neuropathy),
Kupungua kwa nguvu za kiume.
Vidonda (diabetic ulcers) hususan vidoleni.
 Hali hii wakati mwingine humpelekea mgonjwa kukatwa viungo vyake.
Mgonjwa kuwa katika hatari ya kupata maambukizi ya vimelea mbalimbali hasa bakteria kutokana na kuharibika na kushindwa kufanya kazi vizuri kwa chembe nyeupe za damu.
Ugonjwa wa kisukari kama hautodhibitiwa unaweza kumsababishia mgonjwa madhara makubwa na kuathiri karibu kila kiungo mwilini.
Kama tulivyosema ugonjwa huo huathiri moyo na mishipa ya damu, macho, figo neva na hata fizi na meno. Ingawa mgonjwa wa 
kisukari anapotibiwa na kujua jinsi ya kudhibiti kiwango chake cha sukari mwilini suala hilo hupunguza na kuzuia madhara ya ugonjwa huo, lakini kwa bahati mbaya hata kisukari kinachodhibitiwa vyema baada ya muda mrefu humuathiri mgonjwa.
Takwimu zinaonyesha kuwa, wagonjwa wenye kisukari hufa zaidi ikilinganishwa na wasiokuwa na ugonjwa huo kutokana na madhara wanayoyapata, sababu kuu ikiwa ni ugonjwa wa moyo.
Zaidi ya asilimia 60 ya wagonjwa wa kisukari hupata mshituko wa moyo huku asilimia 25 wakipata kiharusi.
Njia bora zaidi ya kuzuia hayo yote ni kuhakikisha kwamba kiwango cha glucose katika damu kiko katika hali yake inayotakiwa kila wakati, suala ambalo kwa bahati mbaya huwa gumu kwa wenye ugonjwa huo.
Watu wazima wenye ugonjwa wa kisukari hushambuliwa na maradhi ya moyo mara mbili hadi 4 zaidi kuliko wasiokuwa na ugonjwa huo, na hatari ya kupata mshituko wa moyo ni mara 4 zaidi kwa wagonjwa hao.
Tafiti pia zinaonyesha kwamba, kuharibika mishipa ya damu au kuharibika neva kunaweza kusababisha matatizo ya miguu kwa wagonjwa wenye kisukari, suala ambalo huenda likapelekea kukatwa miguu.
Utafiti unaeleza kuwa zaidi ya asilimia 60 ya miguu inayokatwa bila kuumia sababu kuu huwa ni kisukari. Nchini Marekani ugonjwa huo ni chanzo kikuu cha watu wenye umri kati ya miaka 20 hadi 74 
kuwa vipofu. Inasemekana kuwa, hata kama mgonjwa wa kisukari atatibiwa na kudhibiti vyema kiwango cha sukari mwilini, lakini baada ya miaka kadhaa taratibu ugonjwa huo huathiri macho na moyo wake. Kwa wale ambao hawajali matibabu na kudhibiti kiwango cha glucose mwilini hupata madhara hayo mapema zaidi.
Baada ya kuyaona madhara ya kisukari kwa viungo kadhaa mwilini, suala hilo linatuonyesha umuhimu wa kujikinga na ugonjwa huo na pia umuhimu wa kuutibu na kuudhibiti kwa wale ambao tayari ni wagonjwa.
Matibabu ya kisukari hutegemea aina ya kisukari ingawa kwa ujumla hujumuisha matumizi ya dawa na njia ya kubadilisha mfumo au staili ya maisha. Kwa aina ya pili ya kisukari au Type 2 DM, aina hii ya kisukari huweza kutibiwa ama kwa dawa, kubadili mfumo wa maisha au vyote viwili kwa pamoja.
Katika kubadili mfumo wa maisha, ni muhimu mgonjwa kutilia maanani na kuwa makini na aina ya vyakula anavyokula na kujitahidi kufanya mazoezi na kuushughulisha mwili ili kuepuka kuongezeka uzito kupita kiasi. Kuhusiana na aina ya vyakula inashauriwa sana
1) Kupunguza kula vyakula vyenye mafuta ya kolestroli ambayo ni mafuta mabaya, yaani kula walau chini ya miligramu 300 za kolostroli kwa siku.
2) Kujitahidi sana kula vyakula vya kujenga mwili vya proteini angalau kwa asilimia 10-15 kwa siku. Vyakula hivi ni pamoja na nyama na mboga za majani.
3) Kuwa makini na ulaji wa vyakula vya wanga au carbohydrate. Inapasa kuhakikisha kuwa havizidi asilimia 50-60 ya chakula unachokula kwa siku na visiwe ndicho chakula kikuu kwa siku.
4) Kupunguza utumiaji wa chumvi katika chakula na kuacha kabisa au kupunguza kunywa pombe.
Suala la ufanyaji mazoezi ni jambo muhimu kwa vile mazoezi husaidia sana kupunguza uzito, kuondoa mafuta yanayopunguza utendaji kazi wa Insulin mwilini na hivyo kuongeza ufanisi na utendaji wa homoni hiyo muhimu mwilini.
Vilevile mgonjwa mwenye aina hii ya kisukari anaweza pia kupewa dawa ambazo atatakiwa kunywa kila siku huku akiendelea kufuata ushauri kama tulivyoeleza.
Dawa hizo ambazo huitwa pia dawa za kushusha kiwango cha sukari mwilini (Oral Hypoglycemic drugs) ni kama vile Metformin na Glipizide.
Ifahamike pia kuwa, wapo baadhi ya wagonjwa wa aina hii ya pili ya kisukari (Type 2 DM) ambao pamoja na kutumia dawa za kunywa za kushusha sukari na kufuata ushauri wa daktari kuhusu mfumo wao wa maisha bado njia hizo zinaweza zisishushe sukari inavyotakiwa. Katika hali kama hiyo, wagonjwa hawa huweza pia kudungwa sindano za Insulin kwa muda ili kushusha kiwango cha sukari mwilini.
Katika matibabu ya Aina ya Kwanza ya kisukari au Type 1 DM pamoja na kurekebisha aina ya vyakula na kufanya mazoezi, wagonjwa huhitaji kichocheo cha Insulin ili kudhibiti kiwango cha sukari katika damu.
DAWA ZA INSULIN ZIMEGAWANYIKA KATIKA MAKUNDI MAKUU MATATU.
Kuna zile zinazofanya kazi kwa muda mfupi, za muda wa kati na zinazofanya kazi kwa muda mrefu.
Kulingana na utendaji wa dawa hizo, mgonjwa anaweza kuelekezwa jinsi ya kujidunga mwenyewe sindano za Insulin nyumbani kwa kufuata maelekezo yafuatayo:
Asubuhi: Mgonjwa hujidunga 2/3 ya insulin nusu saa kabla ya kunywa chai.
Usiku: Mgonjwa hujidunga 1/3 ya insulin nusu saa kabla ya chakula cha usiku.
Aidha katika hii 2/3 inayotolewa asubuhi, 2/3 yake huwa insulin inayofanya kazi kwa muda wa kati na 1/3 ni ile inayofanya kazi haraka au kwa muda mfupi.
 
KUMBUKA
Inasisitizwa sana kutojidunga sindano za ugonjwa huo bila kupata maelekezo sahihi ya daktari. Kwa maelekezo zaidi na sahihi ya matibabu kwa kutumia Insulin ni vizuri kuhudhuria kiliniki za kisukari.
Pia njia za kutibu ugonjwa wa sukari hutolewa hospitalini, na hayo ni matibabu maalumu yakoma aina ya hyperosmolar non-ketotic (HONKC).
Mkazo huwekwa katika kusahihisha upungufu wa maji mwilini ambapo mgonjwa hupewa kati ya lita 8 hadi 10 za maji aina ya Normal saline.
Iwapo kuna ugumu katika kusahihisha kiwango cha sukari mwilini kwa kutumia dawa za kunywa, Insulin inaweza kutolewa. Matibabu mengine maalumu ni ya kutibu Diabetic Ketoacidosis(DKA).
Kama ilivyo kwa hyperosmolar non-ketotic coma, matibabu ya DKA nayo hutolewa hospitali chini ya uangalizi maalumu wa madaktari. Hii ni hali ya hatari, ambapo isipotibiwa kwa umakini, inaweza kumuua mgonjwa.
Jambo la muhimu katika matibabu haya ni kusahihisha upungufu wa maji mwilini, kusahihisha kiwango cha potassium katika damu na kurekebisha kiwango cha sukari kwenye damu kwa kutumia Insulin.
Wasomaji wa Blog hii na makala hii
tunapaswa kujua kuwa unene na kuongezeka uzito wa mwili kwa kiwango cha kupindukia ni miongoni mwa sababu kuu zinazopelekea mtu kupata magonjwa mbalimbali kama vile ugonjwa wa moyo, kiharusi, kisukari, shinikizo la damu na mengineyo.
Pia baadhi ya tabia kama vile kuvuta sigara, kunywa pombe, kutumia madawa ya kulevya na ngono za ovyo vile vile husababisha mtu kupatwa na baadhi ya maradhi.
Kwa kuwa suala la unene wa kupita kiasi limekuwa janga la kiafya katika nchi nyingi hasa zinazoendelea na ni suala nyeti ambalo humsababishia mtu magonjwa mbalimbali kikiwemo kisukari.
Namalizia kwa utafiti unaosema kwamba, wale
wanaokoroma wakati wakilala, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupatwa na ugonjwa wa kisukari kuliko wale wanaolala kimya. Kwa mujibu wa uchunguzi huo uliofanywa kwenye chuo kikuu cha Yale nchini Marekani,
Wale wanaokoroma sana wanapolala,
wanakabiliwa na hatari ya kupata kisukari kwa asilimia 50. Wataalamu wanasema pia kuwa, kushindwa kupumua usingizini huenda kukahusiana na kisukari aina ya pili, bila kujali sababu nyinginezo kama vile umri, jinsia, uzito na hata asili anayotoka mtu.
Kukoroma sugu, au kitaalamu sleep apnea ni hali inayosababishwa na kushindwa kufanya kazi njia ya hewa, suala ambalo humfanya mtu aamke mara kadhaa usingizini wakati anapolala.
Hali hiyo inahusiana na baadhi ya mabadiliko ya umetaboli au hali ya ujenzi wa seli na uvunjaji vunjaji wa kamikali zinatokana na chakula mwilini, kwa kimombo 'metabolism'.

0 comments:

Post a Comment