Saturday 3 May 2014

HUU NDIO UGONJWA WA KISUKARI AU DIABETES MELLITUS.




Ugonjwa wa kisukari au Diabetes Mellitus hutokea pale tezi kongosho au pancrease inaposhindwa kutengeneza homoni au kichocheo aina ya Insulin, au pale mwili unaposhindwa kutumia 

vizuri kichocheo hicho cha insulin na kusababisha kuongezeka kiwango cha sukari kwenye damu au  kitaalamu hyperglycemia.
 Insulin ni kichocheo au homoni inayotengenezwa na kongosho ili kudhibiti sukari katika damu.

Miongoni mwa magonjwa sugu yanayoendelea kuathiri afya za mamilioni ya watu katika nchi nyingi duniani zikiwemo za bara la Afrika na Tanzania ikiwemo ni ugonjwa wa kisukari.
Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 285 wanasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari duniani ambapo karibu asilimia 90 ya 

wagonjwa hao wana aina ya pili ya kisukari. Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa, idadi ya watu wenye kisukari inaongezeka kwa kasi na wataalamu wanasema kuwa, ifikapo mwaka 2030 idadi hiyo itaongezeka maradufu.

Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wagonjwa wa kisukari katika nchi za Asia na Afrika, na inasemekana idadi hiyo inatokana na kukua miji na mabadiliko ya maisha ya watu katika nchi zinazoendelea, na labda kutokana na kuiga mifumo ya maisha ya Kimagharibi.

Katika miaka 20 iliyopita wagonjwa wa kisukari wameongezeka kwa kiasi kikubwa nchini Marekani ambapo mwaka 2010 watu milioni 26 walikuwa na ugonjwa huo, huku wengine milioni 7 wakiwa hawajagunduliwa.
Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa kuwa na kiwango 

kidogo cha Insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili. Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwa vunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu.

Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari inayoitwa glucose ambayo ni chanzo cha nguvu mwilini huingia katika damu.

Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho au kwa kimombo pancrease kutengeneza kichocheo cha Insulin. Kazi ya Insulin ni kuondoa glucosei katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumiwa kama nishati.

Watu wenye ugonjwa wa kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu.

Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo. Huenda kongosho zao haziwezi kutengeneza insulin ya kutosha, au seli za mwili wao haziathiriwi na insulin kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili.

UGONJWA WA KISUKARI UMEGAWANYIKA
KATIKA MAFUNGU MATATU.

Fungu la kwanza ni Kisukari Aina ya Kwanza au Type 1 Diabetes Mellitus.

Hii ni aina ya kisukari inayowaathiri zaidi watoto na vijana. Aina hii hutokea iwapo seli maalumu zinazotengeneza homoni ya insulin zinapokosekana katika tezi kongosho au zinapoharibika kutokana na sababu yeyote ile, na hivyo kusababisha ukosefu kabisa au upungufu wa kichocheo hicho kwenye damu.

Mambo yanayoweza kusababisha uharibifu wa seli hizi katika tezi kongosho ni pamoja na kushambuliwa tezi kongosho kunakoweza kufanywa na magonjwa ya kinga ya mwili ya mtu mwenyewe au autoimmune diseases, au kushambuliwa na vyanzo visivyojulikana.

Kwa vile, uharibifu katika tezi kongosho hupelekea kutokuwepo kabisa insulin mwilini au insulin kuzalishwa kwa kiwango kidogo sana, wagonjwa wa aina hii ya kisukari huhitaji kupewa dawa za insulin kwa njia ya sindano au pampu kila siku za maisha yao ili waweze kuishi.

Kwa sababu hiyo aina hii ya kisukari huitwa pia Kisukari kinachotegemea Insulin au Insulin Dependent Diabetes Mellitus (IDDM). 

Fungu la pili ni Kisukari Aina ya Pili au Type 2 Diabetes Mellitus.
Hii ni aina ya kisukari inayotokea zaidi ukubwani. Aina hii ya kisukari husababishwa na kupungua utendaji kazi wa homoni ya insulin, au seli kushindwa kutumia insulin ipasavyo.

Hali hii mara nyingi husababishwa na unene uliopitiliza yaani obesity, au hali ya kutoushughulisha kabisa mwili (physical inactivity).

Kwa vile, katika aina hii ya kisukari, insulin huzalishwa kwa kiwango cha kutosha isipokuwa tatizo lipo kwenye ufanisi na utendaji kazi wake, wagonjwa wa aina hii ya kisukari hawahitaji kupewa insulin kwa njia ya sindano.

Ndiyo maana aina hii hujulikana pia kama kisukari kisichotegemea insulin au Non Insulin Dependent Diabetes Mellitus (NIDDM).
 Aina ya tatu ya Kisukari ni Kisukari cha Ujauzito auGestationalDiabetes Mellitus.

Ni aina ya kisukari kinachotokea pindi kunapokuwa na ongezeko la kiwango cha sukari katika damu (hyperglycemia) wakati wa ujauzito. Aina hii ya kisukari huathiri karibu asilimia 2 hadi 5 ya mama wajawazito wote ingawa wengi wao hupata nafuu na kupona kabisa mara tu baada ya kujifungua.

Hata hivyo karibu asilimia 20 mpaka 50 ya mama wajawazito wanaopata aina hii ya kisukari huweza kuendelea kuwa na ugonjwa huo hata baada ya ujauzito na hatimaye kuwa na aina ya pili ya kisukari maishani.

KISUKARI HUSABABISHWA NA NINI.
Sababu za kisukari hutofautiana kulingana na aina ya ugonjwa huo.
Kwanza tutatuzungumzia yanayosababisha mtu apatwe na aina ya kwanza ya kisukari.

Aina ya kwanza ya kisukari ina uhusiano mkubwa sana na kurithi. Aidha aina hii pia husababishwa na maambukizi virusi kama vile 

Coxsackie virus type B4.

Visababishi vingine ni pamoja na sumu inayotokana na kemikali za 
 baadhi ya vyakula (food borne chemical toxins), na kwa baadhi ya watoto wachanga maziwa ya ng'ombe yanaweza kuchochea kinga ya mwili wa mtoto uushambulie mwili wenyewe na hivyo kusababisha uharibifu katika tezi kongosho.

Aina ya pili ya kisukari kwa ujumla husababishwa zaidi na jinsi mtu anavyoishi na pia matatizo ya kijeneteki. Aidha kuongezeka uzito na unene kupita kiasi (obesity) vilevile huchangia kutokea aina hii ya kisukari.

Sababu nyingine ni pamoja na kuongezeka umri, maisha ya kivivu na kutofanya mazoezi na pia ugonjwa wa tezi kongosho (pancreatitis) ambao hufanya insulin inayozalishwa kuwa na ufanisi mbovu au ya kiwango cha chini.

DALILI ZA UGONJWA WA KISUKARI NI ZIPI?
DALILI HIZO NI:

Kukojoa mara kwa mara hali inayojulikana kitaalamu kama polyuria.
Mgonjwa kuhisi kiu kali na kunywa maji kwa kiwango cha kupitiliza (polydipsia).

Mgonjwa kuhisi njaa na kula mara kwa mara (polyphagia).
Kuchoka haraka Kupungua uzito Vipele mwilini ambavyo kitaalamu huitwa diabetic dermadromes.

Na wagonjwa wa kisukari pia huwa katika hatari ya kupata maambukizi katika kibofu cha mkojo, ngozi na kwa wanawake sehemu za siri.

Aidha kuna dalili maalumu ambazo hutokea kwa wagonjwa wa kisukari iwapo mgonjwa atapatwa na mojawapo ya madhara (complications) ya ugonjwa huo.

Madhara hayo ambayo hujulikana kwa kifupi DKA hutokea kwenye aina ya kwanza ya kisukari na huwa na dalili zifuatazo: Mgonjwa kutoa harufu ya acetone (inayofanana kidogo na harufu ya pombe).

Mgonjwa hupumua kwa haraka na kwa nguvu,
kujihisi kichefuchefu,
kutapika,
kuhisi maumivu ya tumbo na kupoteza fahamu.

Kupoteza fahamu mgonjwa kunakoitwa Hyperosmolar Non-ketotic coma hutokea kwenye kisukari cha aina ya pili ambapo mara nyingi husababishwa na upungufu wa maji mwilini.
Baada ya mtu kuwa na dalili za ugonjwa wa kisukari matibabu huanza baada ya kufanyiwa vipimo na kuthibitisha kwamba kweli ana ugonjwa huo.
Baada ya vipimo tunaweza kusema mtu fulani ana kisukari iwapo:

1)           Kiwango cha sukari kwenye damu kinatakuwa sawa na 126mg/L, kipimo ambacho kwa kawaida hufanyika kwa mtu ambaye hajakula chakula chochote. Kwa jina jingine kipimo hiki huitwa Fasting Blood Glucose (FBG).

2)          Kiwango cha sukari kwenye damu kinapokuwa sawa na 200mg/L kwa mtu ambaye amelishwa gram 75 za glucose ndani ya masaa mawili. Kipimo hiki pia huitwa Oral Glucose Tolerance Test (OGTT). Au iwapo mgonjwa atafanyiwa kipimo kinachoitwa glycoslytated hemoglobin (Hb A1C) na kuwa chanya

ITAENDELEA SEHEMU YA PILI....

0 comments:

Post a Comment