Wednesday 30 April 2014

MARADHI YA MABUSHA NA MATIBABU YAKE


Mgonjwa  wa  Busha. ( Tunaomba  Radhi  kwa  Picha  )
Mabusha ni hali ya kujaa maji kwenye mfuko wa korodani. Hali hii hutokea kunapokuwa na mkusanyiko wa maji kati ya tabaka mbili za utando unaozunguka korodani.
Inakadiriwa kuwa karibu asilimia moja ya wanaume wote kote duniani huathiriwa na tatizo hili. Kwa hapa nchini, tatizo hili ni maarufu sana maeneo ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi, kiasi cha kuhusishwa na imani kadhaa.


Mabusha husababishwa na nini?


Sababu za kutokea kwa mabusha hutofautiana kati ya watoto wa kiume na wanaume watu wazima.


Muathirika  wa   ugonjwa  wa  Busha.

Kwa watoto wa kiume, mabusha huweza kuanza kutokea kipindi cha ujauzito. Wakati wa ujauzito, korodani za mtoto wa kiume huwa kwenye tumbo lake kabla ya kushuka taratibu kuelekea kwenye mapumbu. Wakati wa ushukaji huo, kifuko kinachozunguka korodani kinachoitwa processus vaginalis hushuka sambamba na kurodani hizo na kufanya korodani kuzungukwa na maji.
Kwa wanaume watu wazima, mabusha husababishwa na mambo makuu mawili; Kwanza, kitendo chochote kinachochochea tando zinazozunguka korodani kuzalisha maji kwa wingi kuliko kawaida, na njia ya pili ni kupungua kwa ufyonzaji wa maji yanayozunguka korodani kwa sababu ya kuziba kwa mirija ya lymph (blockage of scrotal lymphatic system) au kuziba kwa mishipa ya damu inayosafirisha damu kutoka kwenye pumbu kwenda sehemu nyingine za mwili (blockage of scrotal venous system).
Ongezeko la uzalishaji wa maji linaweza kutokana na
• Maambukizi au/na majeraha katika korodani (testicular inflammation au orchitis) au maambukizi katika mshipa ujulikanao kama epididymis yanayoweza kusababishwa na kifua kikuu (tuberculosis) cha makende, au maambukizi yanayosababishwa na vimelea wa filaria (filariasis) wanaosababishwa na kuumwa na mbu aina ya Culex.
• Kujinyonga kwa korodani (testicular torsion) kunakoweza kuzifanya korodani kutenda kazi zaidi ya kiwango chake (hyperactive testis).
• Uvimbe katika korodani (testicular tumors) ambao husababisha uzalishaji wa maji kupita kiasi. 
Kupungua kwa ufyonzaji wa maji hutokana na


• Kufanyiwa upasuaji kipindi cha siku za nyuma katika eneo la kinena, au operesheni ya upandikizaji figo ambazo zinaweza kuathiri mfumo wa lymph na vena na hivyo kupunguza ufyonzaji wa maji kutoka kwenye mapumbu.


• Kuwahi kufanyiwa tiba ya mionzi kipindi cha nyuma nayo uhusishwa na kutokea kwa mabusha.


Kwa hapa kwetu Tanzania, kung’atwa na mbu aina ya Culex anayeeneza vimelea vya filaria kunaelezwa kuwa sababu kuu mojawapo inayopelekea kuwepo kwa tatizo la mabusha na matende hususani maeneo ya Pwani na mwambao.


Dalili za Mabusha

Katika hatua za awali, mabusha hayana dalili zozote (asymptomatic).
Hata hivyo, baada ya muda fulani, mapumbu hujaa na uvimbe huweza kuonekana hata kwa nje. Kwa kadiri uvimbe unavyozidi kuongezeka, dalili zifuatazo zaweza kujitokeza pia;

• Muhusika kujihisi hali ya uzito na kuvuta sehemu za siri kutokana na kujaa na kuongezeka kwa uzito wa mapumbu.

• Mgonjwa huweza kujihisi hali ya usumbufu na kutojisikia vizuri maeneo ya kinena mpaka mgongoni.

• Kwa kawaida mabusha hayana maumivu yeyote. Hata hivyo, iwapo mgonjwa ataanza kujihisi maumivu, hiyo ni dalili ya kuwepo kwa uambukizi katika mshipa wa epididymis (acute epididymitis)

• Uvimbe huwa na tabia ya kupungua iwapo mgonjwa atakaa kitako na huongezeka pindi anaposimama.

• Iwapo mgonjwa atajisikia homa, kichefuchefu na kutapika, hizo ni dalili za kuwepo kwa uambukizi katika mabusha.

• Kwa kawaida mabusha hayana muingiliano na uwezo na ufanisi wa utendaji wa ngono. Hata hivyo kuna taarifa tofauti za kitafiti kutoka bara Asia na Afrika Magharibi kuwa mabusha yanaweza kuathiri ufanisi wa ngono na kwa kiasi fulani kusababisha mhemko au msongo wa mawazo kwa muathirika.

Uchunguzi na Vipimo

Uchunguzi mzuri wa kitabibu (physical examination) huwezesha kugundua uwepo wa mabusha kwa kiasi kikubwa bila hata kuhitaji vipimo vya ziada. Vipimo uhitajika tu kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha mabusha, madhara yaliyoletwa na mabusha au kujua hali ya korodani.

Vipimo ni pamoja na

• Kupima damu (Full Blood Count) na mkojo (Urine Analysis) kuchunguza uwepo wa maambukizi kama vile vimelea wa filaria na mengineyo.

• Ultrasound ya kinena pamoja na mapumbu: Aina hii ya kipimo hufanywa ili kuchunguza uwepo wa matatizo mengine tofauti na mabusha. Matatizo hayo ni kama vile ngiri, uvimbe, kujinyonga kwa korodani (testicular torsion), majeraha katika korodani, damu kuvuja kwenye kwenye korodani (traumatic hemorrhage) au maambukizi.

Matibabu ya Mabusha

Kwa watoto wadogo, kwa kawaida mabusha hupotea yenyewe ndani ya mwaka mmoja. Iwapo hayajapotea, mtoto uhitaji kufanyiwa upasuaji kama tiba.

Kwa wanaume watu wazima, mabusha pia huweza kupona yenyewe bila kuhitaji tiba. Iwapo mabusha hayajapotea na yanamletea mgonjwa usumbufu (discomfort) au hali mbaya ya kiumbo (disfigurement) hayana budi kufanyiwa upasuaji ili kuyaondoa.

Njia za tiba ni

• Upasuaji: Upasuaji wa mabusha huweza kufanyika bila ya mgonjwa kuhitaji kulazwa (outpatient). Madhara yanayoweza kutokea wakati wa upasuaji wa mabusha ni pamoja na damu kuganda (blood clots), maambukizi au majeraha kwenye korodani. Hii ndiyo njia maarufu zaidi na ya kuaminika ya matibabu ya mabusha duniani kote.

• Kunyonya maji kwa kutumia sindano maalum (Needle aspiration): Njia nyingine inayotumika kutibu mabusha ni kuyanyonya maji kwa kutumia sindano maalum (needle aspiration). Hata hivyo njia hii haitumiki sana sehemu nyingi duniani kwa sasa kwa sababu maji ya mabusha huwa yana tabia ya kujirudia baada ya muda mfupi hata kama yatanyonywa.

Baadhi ya matabibu hupendelea kudunga dawa maalum za kuzuia maji yasijae tena (sclerosing agents) mara baada ya kunyonya na kuyaondoa maji yote.
Njia hii ya kunyonya maji ya mabusha, hufaa zaidi kwa wagonjwa wasioweza kuhimili upasuaji. Madhara yanayoweza kusababishwa na tiba ya namna hii ni pamoja na maambukizi na maumivu kwenye korodani.

Hata hivyo wakati mwingine, bila kujali ni tiba gani imetumika, mabusha huweza kujirudia baada ya matibabu.

Madhara ya Mabusha

Kwa kawaida mabusha hayana madhara yeyote. Aidha mabusha hayawezi kuathiri uwezo wa mtu kuzaa. Hata hivyo mabusha yanaweza kuleta madhara iwapo tu kama yakiambatana na magonjwa mengine kwenye korodani.

Kwa mfano, kama mabusha yataambatana na maambukizi (testicular infection) au uvimbe kwenye korodani (testicular tumor), yanaweza kusababisha kupungua kwa uzalishaji na utendaji kazi wa mbegu za kiume (sperms) na kupelekea tatizo la ugumba kwa wanaume.

Hali kadhalika, iwapo sehemu ya utumbo mkubwa au mdogo imebanwa katika upenyo fulani kwenye sehemu ya ukuta wa tumbo, huweza kusababisha ngiri (strangulated hernia), hali ambayo ni hatari kama isipotibiwa haraka

0 comments:

Post a Comment