Saturday, 27 September 2014

MAMBO MATANO YA KUFANYA PINDI UNAPOKUTANA NA MPENZI WAKO ULIYE ACHANA NAE KWA MUDA



Dakika chache za kwanza tunapokutana na wapenzi wetu baada ya kuachana kwa kitambo kifupi zinaumuhimu sana.
Kitambo hiki ni kile ambacho labda mpenzi wako alikuwa kazini au safarini, umepita muda fulani hamjaonana, yamkini moyoni ulitamani kumuona au 

hata kule kuhisi kumkosa (kummiss) kulishaanza kupoa, jiulize mara utakapomuona, labda ni uwanja wa ndege, kituo cha basi, au amefungua mlango tu kuingia nyumbani. Je, unafanya nini? Kile utakachokifanya hapa kina nafasi kubwa katika kuua taratibu penzi na ukaribu wenu (intimacy) au kulijenga kwa kasi kubwa. Ni uchaguzi wako, ingawa unashauriwa kufanya haya yafuatayo:

Jiandae wewe mwenyewe kiakili
Kabla hamjaonana uso kwa uso andaa vema akili yako kumlaki mpenzi wako. Fikiri mawazo mazuri na siyo yaliyo mabaya kumhusu yeye. Usiwaze kummwagia lawama mara tu utakapomwona. Wengine mara tu wamwonapo mpenzi ameingia huanza kukurupuka kuuliza kama kaja na zawadi, na ole wake ukute kasahau huo moto utakao waka hapo! Panga nafsini mwako kitu au tukio la kufurahisha utakalomfanyia mara ukimwona. Mara nyingine unaweza kumuuliza kwa simu muda atakapowasili ili uweze kujiandaa vile unavyodhani.

Jiangalie mwonekano wako
Dakika ya kwanza tu mnapotazamana yaweza kuathiri muendelezo mzima wa siku yenu. Muonekano wako wa uso, tabasamu lako, harufu yako (nzuri au mbaya) vyaweza kumdaka au kumkimbiza mpenzi wako, haswa yule wa kiume. wanaume pia nao wanachakufanya hapa, haupaswi kupokewa ukiwa rafurafu, mchafu, unatoa harufu mbaya ya mwili au ya viatu. Jiangalie, nywele na ndevu zako zikoje, meno yako yanaonekanaje na hata ngozi yako hususan ya usoni. Mwonekano wako huzungumza zaidi vile unavyojiona wewe mwenyewe. Hauhitaji kusema mimi sijipendi, bali kuonekana kwako kutatoa ujumbe. Jaribu uwezavyo kuwa mwenye mvuto mara mtakapokuwa na umpendaye.

Onyesha tabasamu la pendo kwa mpenzi wako
Panga muda wako ili uweze kumsalimu mpenzi wako kwa tabasamu. Acha mpenzi wako ajue kuwa yeye ni wa kipaumbele, na ni muhimu kwako, usimpokee kwa staili ya kumwonyesha humjali. Tabasamu linaweza kusema: “I love you” kuliko hata maneno au zawadi. Tabasamu halina gharama yoyote, 

ni la bure na lipo wakati wowote, kinachokushinda kulitumia ni nini?
Hata kama hujisikii kutabasamu, jitahidi kwa namna yoyote kuonyesha kuwa unaweza pia kutabasamu. Jifanyishe pale mazingira yanapolazimu, hususan katika dakika nne za mwanzo. Ikiwa utajifanyisha vizuri, hisia njema zaweza kuibuka na yale maumivu ya ndani ya moyo kutoweka taratibu.

Salimianeni kwa kukumbatiana na kwa busu
Kuwa na mtu anayetusubiri mara tutakapofika sehemu au mara tutakapofungua mlango ni jambo ambalo wengi wetu tunalipenda, kama kubusu siyo mtindo au pendeleo lako basi tafuta njia nyingine ya miili yenu kugusana mara mnapoonana. Mfano kushikana mikono, kumshika mwenzako nywele au kichwa, nk. Mgusano wa mwili ni muhimu na unashauriwa kwa afya ya penzi lenu.

Tengeneza mazingra mwanana
Jipeni muda wa kupumzika na kupumzisha akili kabla ya kuanza kuzungumzia matatizo yenu. Kila anayeingia nyumbani nakukuta anapokelewa na makelele na mikiki mikiki mara nyingi hutamani kuondoka.
Kila anayekuwa nyumbani kwanza kabla ya mwenzake anawajibika kutengeneza mazingira ya hisia nzuri, ingawa baada ya hapo wote wawili pia mnawajibu wa kuendeleza hisia hizi njema na mazingira ya amani yaliyopo.


Wale ambao wanafanya kazi nje ya nyumbani huhitaji utulivu kidogo mara wanaporudi ili kutuliza akili na hisia zao, wengine watataka dakika 15 wengine dakika 20, watataka kujinyoosha kidogo, au kusikiliza muziki fulani bila maongezi mengi, ingawa pia wapo wanaotaka kucheza na watoto mara wanapofika nyumbani. Chochote na kwa hali yoyote uipendayo, jaribu kujielezea, na mueleze mwenzako aelewe mtiririko wa hisia zako, hii itawasaidia sana.

NAMNA YA KUISHUGHULIKIA NA KUISHINDA HOFU-3-4



Usijiogopeshe kwa vitu ambavyo hutokea kwa nadra sana.
Njia bora ya kuyatengeneza mawazo yetu yanayofikiri sana juu ya hatari ambazo hutokea kwa nadra sana ni kwa kuwaza kuwa wewe hautakuwepo pale hatari hiyo itakapo tokea katika eneo hilo, na hivyo haitakuathiri.

Kwanini uwaze kwamba wewe una bahati mbaya sana na vyote vibaya vitakapotokea vitakukuta wewe tu. Najua inawezekama kabisa lakini nafasi za kuwezekana huko ni ndogo sana. Mfano. Kwanini uwaze kuwa unapotembea msituni peke yako, mti unaweza kukuangukia. 

Au unapokuwa kwenye ndege au meli, ajali yaweza kutokea, au hata unapokuwa safarini kwa gari, jiulize mabasi mangapi yametoka kule unakotokea na kufika salama kule unakokwenda bila shida yoyote, wewe je huwezi kuwa mmoja wa waliokuwa salama?
Kuna mambo mengi ya kuogopesha yanayotokea katika maisha yetu ya kila siku, na kama ukiogopa na kuhofu kila kitu na kutofuata ushauri unaotolewa hapa, basi kila siku utatembea na kuishi kwa hofu tu.

Usiwaze sana juu ya matukio yasiyoweza kuepukika
Yako matukio katika maisha ambayo kamwe hatuwezi kuyaepuka. Matukio haya yanakuja katika maisha yetu, yanapita na kusahaulika. Kitu cha muhimu ni kuishi maisha yako vema na kiusalama zaidi ili usijiweke katika hatari za kiafya na taratibu ukijiandaa kiuchumi na kijamii kwa uzee ulioko mbele yako.

Pia usisahu kutenda mema na kuishi sawa sawa na imani yako inavyokutaka ili uweze kupata maisha mema tena baada ya haya ikiwa unaamini hivyo.

Baada ya kufanya maamuzi haya usiweke sana mawazo yako kwenye mambo yanayohusiana na uzee, kustaafu au kifo. Acha mawazo au fikra hizo zielee zenyewe tu akilini mwako pasipo kuanza kuzichambua kwa kina.

Amua nini utakifanya pale vile unavyo viwazia sana na kuvihofu vitakapotokea
Kama unaona ni kazi ngumu kutowazia sana mawazo ya vile unavyovihofia, na unashindwa kujisahaulisha akilini mwako, basi pata muda wa kuvichambua kwa kina. 

Kwa asili, woga kututisha pale tunapojaribu kuwaza kuhusu mwisho au hatima ya baadhi ya mambo au matukio fulani, kwahivyo jaribu kufikiria nini utafanya pale ambapo hofu zako zitakapotokea. 

Kwakufanya hivi utaona kuwa pale vile unavyovihofia vinapotokea, basi maisha yataendelea kama kawaida, na mambo yatakuwa ya tofauti na vile yalivyo sasa.

Kama unadhani kuna tahadhari ya kuchukua au maandalizi ya kufanya katika vile unavyovihofia basi fanya hivyo kwa umakini mkubwa na mengine yote umwachie Mungu. Baada ya kufanya hili utaona dhahiri kuwa hofu na woga ulionao haukutesi tena.

Wacha kulilia maziwa yaliyokwisha kumwagika
Ni kawaida kulia pale unapopoteza kile ulichokithamini au kukipenda, au pale kile ulichokiwekea jitihada kisipoleta matokeo uliyoyadhania. Hata hivyo, huna haja ya kujiumiza kichwa wala moyo, maana hutobadili chochote kwa yaliyokwisha kutokea. Usiweke mawazo sana katika vile ulivyopoteza au kuvipatia hasara. Ni kweli kwamba yamkini maisha yangekuwa bora zaidi kama kile au vile ulivyopoteza visingepotea, lakini pia hakuna mwenye uhakika na hili. 

NAMNA YA KUISHUGHULIKIA NA KUISHINDA HOFU-4

DALILI ZA KUMGUNDUWA MPENZI MKOROFI, MGOMVI.





Dalili hizi zitakupa kujihadhari mapema mara utakapoziona zinajitokeza mara kwa mara katika mahusiano yenu. 

Kusudi la makala hii ni kuwasadia wale wenyematarajio yakuingia katika mahusiano ya kushi pamoja kwa sababu wengi wamekuwa vipofu katika kuona baadhi ya dalili mbaya zinazoonekana katika hatua za mwanzoni katika mahusiano na mara wanapoendelea mbele na kufanya maamuzi mazito hususani maamuzi ya kuamua kuoana au kuishi pamoja, mabadiliko makubwa yanaanza kutokea na hali inaanza kuleta misuguano mingi na maumivu mengi baina ya wapenzi, na mbaya zaidi wengine hushindwa kabisa kuendelea na mahusiano nahivyo kuamua kulivunja penzi lao.

Yatupasa wote tuliopo katika mahusiano, kabla ya kuendelea na kufanya maamuzi fulani tuwe tunatazama pia dalili za hatari.
Kwa upande mkubwa dalili hizi zimeegemea kuwasaidia zaidi jinsia ya kike kujua au kuwafahamu wanaume. 

Hii ni kwa sababu wanawake ndio ambao wamekuwa wakioyesha kuumizwa zaidi na kukatishwa tamaa na mabadiliko ya tabia za wanaume mara wanapozama katika dimbwi la mapenzi. Ingawa pia wapo pia wanaume wanaoumizwa kutokana na mabadiliko ya tabia za wapenzi wao, nawao pia waweze kuzitazama dalili hizi.

Dalili:
Mpenzi wako anakuwa na wivu sana kwa ule muda unaotumia kuwa na wafanyakazi wenzako, marafiki na hata ndugu zako, ingawa sio kwamba anataka muda huo awe na wewe.

Anakuwa na tabia za kukuudhi na kukutawala, ataangalia sana kutoka na kuingia kwako, nyendo zako na hata matumizi yako ya fedha, na kama ukimuuliza kwanini anafanya hivyo, atajiteteta kuwa anakusaidia kufanya maamuzi sahihi.

Taratibu anakutenga na wote waliokaribu na wewe. Pia anajaribu kukutenga na wale wanaoonekana kuwa msaada kwako kama vile, wale unaowisiliana nao kwa simu, wafanyakazi wenzako na hata ndugu zako wa karibu.

Huwa na tabia ya kuwalaumu sana wengine kwa matatizo anayoyapata. Mfano anapokosa kazi, anaposhindwa shuleni nk. Kila kitu ni kosa la mtumwingine na sio yeye.

Hukasirishwa na kuudhiwa na vitu vidogo vidogo na vyakawaida katika maisha ya kila siku, mfano akiambiwa afanye kazi zaidi ya muda wa ofisi, akiombwa amwangalie mtoto, anapopingwa katika kitu kidogo nk.

Anakuwa na tabia za kikatili kwa wanyama (wafugwao) na hata kwa watoto. Haumizwi pale anapoona maumivu au kuteseka kwa wanyama au watoto.
Anaweza kujiona anacheza au kutania bila kujua anaumiza mtoto au mnyama.

Ni wenyetabia ya mabavu hususani katika tendo la ndoa, hawatojali hisia zako, umelala usingizini au unaumwa, bali hujali zaidi kuzitimiza haja zao.

Ni wenye maneno makali yakuumiza, na ya kushusha hadhi, huweza kukuamsha usingizini ili akutukane au kukugombeza. Akianza malumbano hakupi upenyo wa kwenda kulala, anaweza kulalama usiku mzima.

Sio watu wakutabirika, ni watu wenye hisia za kubadilika badilika, mara muda huu anafuraha na kuonyesha mapenzi, mara ghafla kakasirika na kutaka kuadhibu mtu.

Anaweza akawa na historia ya tabia za kikorofi na kigomvi, labda amewahi kuwa na matukio ya kuwapiga marafiki zake, akijitetea kuwa alipitiwa tu na hasira.

Ni mwenye vitisho na tabia za kuashiria fujo, mfano kupenda kutishia akisema “Nitakuzaba vibao” “Nitakuuwa”, “Nitakuvunja Shingo” “ntakufanyia kitu mbaya” n.k.

Mwenyetabia ya kupiga au kugonga vitu kwa hasira, kuvunja vitu vyako, kukurushia vitu wewe au watoto kwa hasira.

Hutumia nguvu anaposisitiza hoja yake, mfano, kukushika nguo au kukukandamiza ukutani na mara nyingine kukusukuma

NJIA 7 ZA KUHUISHA KUMBUKUMBU KWA UMRI WOWOTE



NI jambo la wazi kwamba tunapozidi kuwa wazee huwa tunaanza kugundua mabadiliko kadhaa katika uwezo wetu wa kukumbuka mambo.

Hali hii ni kama kujikuta uko jikoni lakini hukumbuki ni kwa nini ulikwenda humo, au kutoweza kukumbuka jina la mtu unayemfahamu wakati ukiongea na watu wengine.  Unaweza hata kusahau kwenda kwenye miadi kwa vile ulisahau kitu kama hicho. 

Kupungua kwa nguvu ya kumbukumbu kunaweza kutokea katika umri wowote lakini hili hutia wasiwasi zaidi tunavyozidi kuzeeka kwa vile huwa tunahofia kwamba ni aina fulani ya kupungua kwa nguvu ya akili na ufahamu.

Ukweli ni kwamba, kupungua kwa kiasi kikubwa cha kumbukumbu kwa wazee ni suala linalohusu akili kutofanya kazi kikamilifu, majeraha katika ubongo, kuchanganyikiwa, ugonjwa au madhara ya ubongo yanayofanya mhusika kushindwa kwa kiasi kikubwa kuutawala mwili wake (Alzheimer’s Syndrome).

Matatizo mengi ya kupoteza fahamu wakati wa uzee yanaonesha mabadiliko katika muundo na utendaji kazi wa ubongo.  Mabadiliko haya hupunguza nguvu ya ufahamu, humfanya mhusika awe na matatizo katika kujifunza kitu kipya kwa haraka.  

Hata hivyo, kutokana na utafiti  wa miongo kadhaa,  kuna njia mbalimbali tunazoweza kutumia kulinda na kuhuisha akili zetu.  Zifuatazo ni njia saba ambazo unaweza kuzijaribu kukabiliana na tatizo hili.

1. Endelea kujifunza
Kiwango cha juu cha elimu kinahusiana na akili inavyofanya kazi vyema zaidi wakati wa uzee.  Wataalam hufikiri kwamba elimu ya juu zaidi inaweza kusaidia kuifanya kumbukumbu iwe na nguvu kwa vile inamfanya mtu aitumie akili yake kila mara.  

Inaaminika kwamba, kuupa ubongo wako changamoto za kisomi huifanya akili yako kuwa changamfu na kuchochea mfumo wake wa mawasiliano.  

Ili kuipa akili yako uhai zaidi, soma vitabu, cheza michezo angalau ile ya kutumia mahesabu, andika historia ya maisha yako, fanya chemsha bongo mbalimbali, ingia darasani na soma chochote, jiingize kwenye muziki au sanaa yoyote au angalau fanya shughuli za bustani.

Ukiwa kazini pendekeza au jitolee kufanya kazi zinazo jumuisha ujuzi ambao huwa huutumii kila mara.
Kumbuka kwamba kujenga na kuendeleza nguvu ya ubongo wako ni jambo ambalo linaendelea maishani, hivyo hakikisha unaendelea kujifunza mambo mapya kila siku.

2. Tumia ufahamu wako wote
Unavyotumia ufahamu wako wote katika kujifunza jambo fulani ndivyo akili yako itakavyokuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu.

Katika utafiti mmoja, wazee walionyesha taswira kadhaa zilizoambatana na harufu fulani.  Hawakuulizwa ni nini walikiona, lakini baadaye walionyeshwa taswira kadhaa, bila ya harufu, na baadaye wakaulizwa ni nini walikuwa wamekiona hapo mwanzo.
Waliweza kukumbuka picha zote zilizokuwa na harufu husika, hususan zile zilizokuwa na harufu za kuvutia.

Hii ilionyesha kwamba akili yenye kunasa harufu ilikuwa imefanya kazi inayotakiwa wakati wazee hao walipotazama picha hizo zikiwa sambamba na harufu husika.  Mnaso wa harufu pamoja na picha uliwasaidia kukumbuka kwa mara ya pili walipoletewa picha zile zile ingawa kwa mara hiyo picha hazikuambatanishwa na harufu.

Hivyo hakikisha unatumia nguvu zako zote za ufahamu hasa katika mambo ambayo ni mapya kwako.    Kwa mfano, jaribu kufikiria vitu vinavyohusika katika utayarishaji wa chakula kwenye mgahawa wakati unaposikia harufu au ladha yake.

Vilevile, fanya hivyo kwa vyombo vipya unavyovitumia, kwa kuona unaweza kuvikumbuka kwa ufahamu upi, ikiwa ni pamoja na harufu yake au sauti zake.

3. Jiamini 
Dhana za kufikirika  kuhusu uzee zinaweza kusababisha kupungua au kwisha kwa kumbukumbu.  Watu wenye umri wa wastani au wazee huweza kupata matatizo ya kumbukumbu  iwapo wataamini kwamba kuzeeka ni kupungukiwa na nguvu ya kukumbuka mambo mbalimbali.

Watu wanaoamini kwamba kumbukumbu yao ni dhaifu ni dhahiri watajikuta wana upungufu huo.    Iwapo utaamini kwamba unaweza kuimarisha kumbukumbu zako na kufanyia kazi imani hiyo, utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuimarisha akili yako. 


Njia 7 za kuhuisha kumbukumbu kwa umri wowote - 2




3. Jiamini
Dhana za kufikirika  kuhusu uzee zinaweza kusababisha kupungua au kwisha kwa kumbukumbu.

 Watu wenye umri wa wastani au wazee huweza kupata matatizo ya kumbukumbu  iwapo wataamini kwamba kuzeeka ni kupungukiwa na nguvu ya kukumbuka mambo mbalimbali.

Watu wanaoamini kwamba kumbukumbu yao ni dhaifu ni dhahiri watajikuta wana upungufu huo.

 Iwapo utaamini kwamba unaweza kuimarisha kumbukumbu zako na kufanyia kazi imani hiyo, utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuimarisha akili yako.

4. Upunguzie mzigo ubongo wako
Ikiwa hutaki kutumia nguvu katika kukumbuka ulipoweka funguo zako au siku aliyozaliwa mjukuu wako wa kike, ni vyema ukajikita katika kujifunza mambo mengine mapya na muhimu. 

Katika hili tumia kalenda mbalimbali, ratiba za mipango mbalimbali, ramani, orodha za bidhaa madukani, mafaili au vitabu vya anwani ili kupata habari unazozitaka.

Panga mahali maalum nyumbani kwako utakapoweka miwani yako, pochi ya fedha, funguo na vitu vingine unavyovitumia mara kwa mara.

 Ondoa mrundikano wa vitu usivyotumia ofisini mwako ili uweze kuviona vitu ambavyo utataka kukumbuka vilipo.

5. Kirudie kitu unachotaka kukijua
Ukitaka kukumbuka kitu ambacho umekisikia, kukisoma au kukifikiria, basi kirudie kwa kukitaja kwa sauti au kukiandika. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unaimarisha kumbukumbu yako.

Kwa mfano, iwapo utakuwa umeambiwa jina la mtu fulani, basi litumie wakati unaongea naye.  Kwa mfano: “Hivi John, ulikutana na Camille wapi?”

Iwapo utaweka kitu chako sehemu fulani ambapo si pa kawaida, basi jiambie kwa sauti ulipokiweka.

  Vilevile, ukiambiwa kitu, usisite kumwambia mtu akirudie tena kukuambia lengo likiwa ni kuufanya ubongo wako unakiri barabara.

6. Panga muda wa kujifunza
Kurudia kitu kwa kukitaja ni njia nzuri ya kujifunza ikifanyika kwa muda fulani.

 Si vyema kurudia kutaja kitu mara nyingi katika muda mfupi kama vile unakariri kwa ajili ya mtihani. 

Badala yake, rudia kujifunza masuala muhimu ya kitu husika kwa muda mrefu zaidi kama vile mara moja katika saa moja, na baadaye kila baada ya saa chache kisha kila siku.

Kupanga muda wa kujifunza ni vyema zaidi unapojaribu kupata habari ngumu kama  vile maelezo ya jukumu la kazi mpya.

Utafiti unaonyesha kwamba kujifunza kitu kilekile kwa muda maalum uliopangwa huimarisha kumbukumbu kwa watu walio na afya za kawaida na wale wenye matatizo ya utambuzi.

7. Jiwekee vidokezo vya kumbukumbu
Vidokezo hivi ni maneno yatakayokukumbusha haraka mahali ulipoweka vitu vyako, hebu angalia neno hili:  CHIKALANGU linaweza kukukumbusha mahali ulipoweka pochi yako ya fedha, yaani: CHI (chini ya) KA (kabati) LA (la) NGU (nguo).

Kidokezo hicho kitakukumbusha kwamba ulipoweka pochi yako ni “Chini ya kabati la nguo”.

Vilevile maneno “Free Moza Day” yanaweza kukukumbusha siku aliyozaliwa mjukuu wako yaani tarehe 26 Juni, ambayo ni siku Msumbiji ilipopata uhuru.



MBINU ZA KUONGOZA FAMILIA KATIKA HALI DUNI YA KIMAISHA-3


REJESHO la makala haya kutoka kwa wasomaji wangu limeniaminisha kuwa somo hili limekuwa msaada mkubwa kwa watu wengi.
Nichukue nafasi hii kumshukuru kila mmoja ambaye tumekuwa naye tangu tulipoanza mada hii wiki mbili zilizopita ila nikusihi mdau wangu tuungane tena kumalizia sehemu ya mwisho ya somo hili kwa kuangalia dondoo zilizobakia.

MAWAZO YA KILA MWANAFAMILIA YAHESHIMIWE
Katika kipindi kigumu cha maisha ni rahisi sana kukumbwa na udikteta wa mawazo kiasi cha kuamini kuwa, hakuna anayeweza kuleta mawazo sahihi ya kukabili changamoto zaidi yako wewe kiongozi.
Katika hali ya kawaida, wakati huu ndiyo mbaya zaidi kwenye upofu wa maamuzi kwa sababu akili huchoshwa na msongo mkali wa mawazo jambo linaloweza kuzalisha haraka uamuzi usiofaa.
Ukiwa kama kiongozi wa familia na uko kwenye msoto wa maisha na giza la hali ngumu limezidi kutanda, ni vema kuwashirikisha wanafamilia wote, mjadili namna ya kupambana na dhiki na ikiwezekana mawazo ya kila mmoja yazingatiwe bila kujali huyu ni mwanamke au mtoto.
JENGA HALI YA KUAMINIANA
Kuna baadhi ya viongozi wa familia duni ambao wakati wa dhiki ndiyo huongeza kasi ya kulewa wakijitetea kuwa, wanapoteza mawazo kwa pombe za ofa.
Ukweli ni kwamba, familia inaweza isikuamini kama kweli unakwenda baa au klabuni kununuliwa pombe kila siku, badala yake itakuona kama unafuja kinachopatikana kwa ulevi na kwamba umeitelekeza familia yako.
Kiongozi wa familia lazima ajenge hali ya kuaminiana kwa kila mtu, isiwe hawa wanalala njaa, mwingine anaonekana na nguo mpya.
FURAHIA USHINDI HATA MDOGO
Ikiwa familia imepambana na kupata sehemu ndogo ya mafanikio, kiongozi anatakiwa kufurahia ushindi huo na wapiganaji wenzake ndani ya familia, iwe kwa kununua kuku na kupiga wali ‘spesho’ au kununuliana nguo mpya kwa lengo la kujipongeza kwa mafanikio.
Kitendo hiki hutia moyo watendakazi na kuwafanya waongeze bidii wakiamini kupata kuna faida ya kila mtu. Kamwe kiongozi asiungane na familia yake kwenye shida tu halafu sehemu ya mafanikio ikipatikana ajitenge na kwenda kutumia na watu wengine kwenye nyumba za starehe, jambo hili huvunja moyo sana.
KINGA MIGAWANYIKO
Familia duni haipaswi kugawanyika kwa namna yoyote. Wazazi wengi wamekuwa na tabia ya kuzigawa familia kimatabaka au ulevi wa kupenda. Utakuta watoto wawili wanampenda zaidi baba kuliko mama na hawa wanamuunga mkono mama zaidi ya baba kwa sababu za kipuuzi.
Kiongozi wa familia hatakiwi kuendekeza usaliti kwenye familia bali kujenga umoja na usawa usiokuwa na mgawanyiko ili kuleta tija katika vita ya kujikomboa kimaisha.
THAMINI MCHANGO WA KILA MTU
Kila mtu anavyochangia pato kwenye familia anatakiwa kuheshimiwa bila kuangalia kiasi. Endapo mtoto mkubwa ni mbeba zege na huchangia shilingi 1,000 kila siku basi aheshimiwe na kutiwa moyo.
Viongozi wengi wa familia hasa wazazi wamekuwa na desturi ya kuwapenda zaidi watoto au ndugu wanaochangia pato kubwa na kuwadharau wale wanaoleta fedha kidogo au kuhudumia familia kwa hali zao peke yake. Hilo si jambo zuri.
Mpaka kufikia hapa nitakuwa nimemaliza mada hii, kwa wakazi wa Dar wanaweza kujipatia elimu hii kupitia vitabu vyangu vya Saikolojia na Maisha ambavyo wanaweza kuvipata kwa kuwasiliana nami.

MBINU ZA KUONGOZA FAMILIA KATIKA HALI DUNI KIMAISHA


KATIKA moja ya masomo yangu ambayo yanapatika katika vitabu vyagu vya Saikolojia No1,2&3, niliwahi kuandika mada inayohusu mambo yanayochangia familia nzima kuwa maskini. Leo sitarudia hayo lakini nitafundisha somo la mbinu za kuongoza familia katika hali ya umaskini.
Ni imani yangu kuwa, wadau wakubwa wa mada zangu ni watu wazima licha ya kuwa, wengine wana umri mdogo lakini naamini wanafahamu ugumu wa maisha unaozikabili familia mbalimbali.
Inawezekana wapo wenye mali na fedha nyingi ambao nao watapata fursa ya kusoma mada hii na kukosa mashiko ya hoja, kwa vile tu maisha yao ni mazuri na hivyo kukosa sababu kujifunza pamoja nami.
Waswahili husema; ya Mungu mengi na tabia ya upepo kugeuka. Raha ya leo si tumaini la kesho kwa vile usiku ni mrefu na mchana una mengi ya kuona na kujifunza.
Kwa kauli hizi, mwenye fedha leo hana mkataba na Mungu yawezekana kesho akaugua, akafilisika au akatetereka kimaisha na kumfanya aone tofauti hii na ile katika maisha yake kiasi cha kutapatapa: “Nitafanyaje kuiongoza familia yangu katika hali hii?”
Naamini kwenye maisha tunahangaika sote, wakati mwingine tunajiuliza; tutawalisha nini watoto wetu, tutawasomeshaje, tutawauguzaje, tutaihudumiaje familia yetu? Je, umewahi kujiuliza maswali haya? Hebu tazama dokezo kumi zifuatazo ili zikusaidie namna ya kuiongoza familia yako katika hali ngumu.
Kuishinda nafsi na akili yako
Mtu anayeongoza familia maskini lazima ashinde kwanza msukumo wa nafsi na akili zake ambao mara nyingi huwa unakimbilia kutoa majibu ya kumfanya mtu akate tamaa ya kuishi au kuzishinda changamoto.
Hakikisha, hata kama umefukuzwa kazi, umekosa fedha ya kula, huna kodi ya nyumba, unadaiwa mkopo, usikubali mawazo ya: “umekwisha, unadhani utafanyaje?” Ukikubali mawazo hayo, kwanza utaiona familia yako kuwa ni mzigo na hutaweza kuiongoza.
Nashauri uchukue hatua madhubuti ya kupingana na hali ya kukata tamaa na kujipa moyo wa kukabiliana na matokeo yoyote yatakayotokea katika maisha yako ya umaskini na familia yako. Ukifanya hivyo utafanikiwa kuituliza akili na mhemko wa hisia zako utapungua na hivyo kupata uwezo wa kukalibili changamoto.
Kinga utajiri wa wengine usiathiri familia yako
Familia nyingi maskini mara nyingi hukwazwa na tamaa ya kuishi sawa na matajiri. Watoto wa maskini hutamani kuvaa, kula, kustarehe kama wenzao wa nyumba ya pili anamoishi tajiri fulani.
Hali hiyo inapotokea, jitahidi sana, kuwafanya watoto na familia yako wavione vitu hivyo kama ni vibaya (jenga propaganda hasi) ili uwakinge wasijihukumu unyonge.
Saikolojia hii itawasaidia sana kupuuza tamaa za kuwa kama watoto wa matajiri na hivyo kutoa nafasi ya familia kupambana na hali ngumu ya maisha mpaka kitakapokuwa kimeeleweka.
Familia za maskini husifiwa kwa kupenda maharagwe na kande siyo soseji, kuku choma na chips funga. “Nawapenda sana ndugu zangu, yaana hamchagui vyakula; kama Juma (Mfano tu) ndiyo kabisa anapenda sana mboga za majani ndiyo maana ana afya njema.”

Mbinu za kuongoza familia katika hali duni kimaisha-2



KWANZA nianze makala haya kwa kukushukuru wewe msomaji wangu ambaye umekuwa nami katika somo hili tangu wiki iliyopita ambapo tulianza kwa kuangalia baadhi ya dokezo zitakazoweza kumsaidia mtu kuiongoza familia duni kimaisha.
Pongezi za kila mmoja anayeguswa na mada zangu zinanifanya nijivunie kila siku kwani naamini ndizo zinazonitia nguvu ya kuendelea na kazi hii ya kuwasaidia watu elimu ya jinsi ya kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
Baada ya shukrani hizo naomba tufuatane tena katika vipengele vichache vilivyosalia katika somo hili muhimu katika maisha.
hamasisha kila mmoja apigane
Huwezi kushinda vita kama askari wako wa mstari wa mbele hawapigani vita kwa umoja. Maisha magumu katika familia yanahitaji sana umoja, ifundishe familia yako kushiriki katika kupambana na maisha.
Keti na mkeo/mume, watoto, ndugu na jamaa unaoishi nao na kuwaambia kila mmoja anatakiwa kufanya kazi zinazolingana na uwezo wake. Mwenye uwezo wa kubeba mawe na kuponda kokoto aende kazini na mpepeta pumba mashineni asiache kufanya hivyo kwa kutegemea fulani atawajibika kwa ajili ya kumtafutia maisha.
Kwenye familia nyingi hasa vijana wamekuwa na tabia ya kukaa vijiweni na kupiga soga wakitegemea baba arudi kutoka kuuza madafu halafu wao wapate chakula. Hilo si jambo jema, lazima kila mtu afanye kazi. Moyo wa kufanya kazi hauji kimiujiza bali ni kwa mtu kuhamasishwa na kufundishwa.
TIA MOYO NA HAMASA
Mara nyingi familia duni hukumbwa na aina fulani za mikosi na wakati mwingine mipango iliyokuwa inategemewa kuleta ufumbuzi wa tatizo hukwama bila sababu za msingi.
Inapotokea hali ya namna hiyo kiongozi wa familia lazima achukue jukumu la kuitia moyo familia yake kwa kupanda mbegu ya matumaini mapya.
“Mwanangu hela yako imepotea? Usijali Utapata nyingine, usihuzunike sana,” ndivyo unavyotakiwa kusema.
Kwenye maisha duni epuka kuwa mtu wa kuongeza fikra hasi kwa mtu ambaye hana tumaini lingine, kwani utamvunja moyo sana na kumsababishia hali ya kukata tamaa kutafuta jibu la tatizo kwa njia nyingine.
BADILI UMASKINI WAKO NA UTAJIRI
Niliwahi kusema katika moja ya makala zangu kuwa hata matajiri tunaowaona wanahitaji msaada wa maskini. Kiongozi wa familia duni kimaisha lazima alijue hili na awe tayari kuifundisha familia yake kutumia umaskini wao kuleta utajiri.
Katika hali ya kawaida matajiri hawapendi kufanya kazi dhaifu au duni, hutegemea kuajiri na kuwalipa wengine fedha ili wafanye usafi wa mazingira nyumbani au hata ofisini.
Kuna mfano wa kijana mmoja wa Kifaransa aitwaye Devis, huyu kaka mwaka 1996 alikuwa maskini wa kutupwa na alikuwa akipata riziki yake kwa kufanya usafi kwenye nyumba ya tajiri. Akiwa kwenye kazi aliokota kitu kama chuma, hakujua ni kitu gani ila alikipenda na kukiweka mfukoni.
Aliporudi nyumbani, rafiki yake alikiona kuwa si kitu cha kawaida, akamshauri wakipeleke kwa sonara. Walipofika huko waligundua kuwa kumbe kilikuwa ni jiwe la dhahabu. Hivyo, akaliuza kwa bei kubwa na tangu hapo akaanza kufanya biashara.
Miaka mitano baadaye alifanikiwa kumiliki mgahawa uliopendwa sana na wateja na hivyo kumletea kipato kikubwa.
Naamini mpaka hapa tutakuwa tumejifunza mengi na pengine kuhitaji elimu zaidi, lakini nafasi yangu imemalizika, naomba tukutane tena wiki ijayo tumalizie somo hili zuri.

MAWAZO HUCHANGIA UGUMBA KWA WANAWAKE



TAFITI umebaini kuwa wanawake wengi wenye viungo salama lakini hawazai, wana kiasi kikubwa cha homoni ya Cortisol inayoletwa na uchovu. 
Aina hii ya homoni ndiyo inayosimamisha mchakato wa uzalishaji wa mayai kwa wanawake wanaoshiriki mchezo wa riadha.
 
Hivyo basi, uwiano huu wa kasoro za ukuzaji mayai kati ya wakimbia riadha na wanawake wagumba unaweka usawa baina ya uchovu mkubwa wa mazoezi ya viungo na ule uchovu unaotokana na msongo wa mawazo ya ugumba. 


Ukweli pekee ambao nimeukusudia kuuzungumza leo ni kuhusiana na wanawake wasiokuwa na matatizo ya uzazi ambao utafiti  ulioandikwa katika jarida la Minerva Ginecologica la nchini Italia unaonesha mawazo ndiyo unaochangia kwa kiasi kikubwa wanawake hao wasipate watoto licha ya kwamba kibaiolojia hawana matatizo. 


Imebainika kuwa, wanawake wengi hujisogeza wenyewe katika nguvu ya kukosa watoto kutokana na ukubwa wa kiu yao ya kupata watoto hao. 
Hawa hujiweka katika uzalishaji mkubwa wa homoni ya Cortisol ambayo huchipuka kwa kasi kutokana na msukumo wa kiu kubwa na ya haraka ya kutaka kukumbatia mwana.


Kutokana na ukubwa wa tatizo hili, imebainika kuwa wagumba wengi wasiokuwa na kasoro katika viungo vyao vya uzazi wanaweza kupona au kupata watoto bila hata kupewa tiba ya miti shamba au vidonge. Tiba kubwa iliyobainishwa ni kupatiwa nasaha zitakazowaondolea mawazo tasa, wasiwasi na kutojiamini.


Ukweli wa tiba hii ya ushauri imethibitishwa hivi karibuni na kituo kimoja nchini Marekani kinachojishughulisha na utafiti wa kuzalisha watoto, ambapo majibu yake yalichapishwa katika majarida na mitandao mbalimbali.


Kwa mujibu wa taarifa ya kituo hicho asilimia 75 ya wanawake waliokosa watoto ambao walifika kituoni hapo na kupewa ushauri walifanikiwa kuzaa baada tu ya kuhudhuria kliniki na kupewa ushauri uliowatoa katika msongo wa mawazo.


Nasaha ambazo zimekuwa zikitolewa na wataalamu hao si ngumu, bali ni zile zilizojaa maneno yenye kugeuza fikra hasi zenye kuondoa kiu kali ya kupata watoto kwa utashi na nyakati zilizopangwa na wahusika. 


Pia, wagumba hufundishwa namna ya kuepuka migogoro ya kimapenzi na kutoumizwa kupita kiasi na kejeli za watu kuhusiana na matatizo yao, huku wakijengewa imani kuwa kuzaa ni suala linalowezekana kwao, hivyo kuwafanya watupilie mbali hofu na mawazo ya wao ni wagumba. 


Lakini pamoja na nchi zilizoendelea kuwa na vituo vya kutolea nasaha kwa waathirika, bado wanasaikolojia wanakiri kwamba mtu mwenyewe anaweza kujiepusha na uchovu unaoletwa na mawazo kwa kurahisisha tatizo lake kutoka kutowezekana na kuwezekana kutatuliwa. Akili ya mtu ndiyo 

inayopima na kuongoza utambubuzi wa ukubwa wa tatizo na si kwamba kuna matatizo makubwa na madogo kama watu wanavyofikiria.
Mtu aliyejiwekea ukuta wa kutozaa kutokana na msongo wa mawazo yake ili aweze  kuzaa ni lazima aondoe mawazo ya kwamba yeye ni mtu asiye zaa, kwani hakuna mtu wala vipimo vilivyompa majibu ya kwamba ni mgumba.


Jambo jingine la kufanya ni kupuuza maneno ya kukatisha tamaa kutoka kwa watu wengine. Hii ina maana kuwa lawama zozote kutoka kwa mume/ mke au wanafamilia zinazohukumu kosa la mtu kutokuza lazima zipuuzwe na zisipewe nafasi ya kutia simanzi moyoni.
Sambamba na hilo kuna suala la wanawake kuzingatia kalenda zao kwa 

kujichunguza na kubaini muda muafaka wa kukutana kimwili na wanaume ili kupata matokeo mazuri ya utungishaji mimba. 
Kwa mantiki hii kuna wanandoa wengi wameshindwa kupata mtoto kwa kutozingatia siku zenye uwezekano wa kupata mimba ambazo ni siku ya 11 hadi ya 16 tangu siku ya kumaliza hedhi.

JINSI YA KUISHINDA HOFU NA NGUVU YA UCHAWI-2



LAKINI jambo baya sana ambalo linawaponza watu wengi ni kwamba wanapogundua kuwa watu fulani ni maadui zao, wao nao huanza kushambulia kwa chuki.
Kufanya hivyo huzifanya nguvu asili zitafutane na kushawishi mawazo yatilie shaka kila kitu kinachojitokeza na hukihusisha na shambulio la mbaya uliyekosana naye adabu.
Hutakiwi kumchukia mtu ambaye unahisi ni adui yako. Unachotakiwa kufanya ni kumpenda na kujipendekeza kwake, ili yeye aone aibu ya kukufanyia ubaya. Usilipe ubaya kwake hata kama ushahidi unaonesha kuwa yeye ndiye aliyekuchongea kwa bosi wako ufukuzwe kazi.
Ukifanya hivi utakuwa umejiokoa na shambulio la adui yako kwa kiwango kikubwa. Nasisitiza upendo! Wanawake mlioolewa wapendeni mawifi zenu, wakwe hata kama mtahisi wana chuki nanyi. Wafanyakazi, wafanyabiashara, pendaneni mkijua kuwa UPENDO ni kinga yenu.
2. UKWELI USEMWE
Hatua inayofuata ambayo saikolojia inahesabu kuwa ni moja ya kinga kubwa zinazoweza kumfanya adui yako asikudhuru ni kumweleza ukweli kuhusiana na mipango yake ya kukuangamiza, hasa ushahidi wa wazi unapokuwepo.
Mtu mbaya anapogundua kuwa amejulikana kuwa yeye ni mbaya, moja kwa moja anakuwa amenyonywa nguvu za kutekeleza mipango yake. Zingatia kipengele cha kwanza cha upendo katika kufikisha ujumbe wako kwake.
 Kwa mfano unapofahamu kuwa wifi yako ndiye anayekuroga, kwanza mpende, kisha mwite na umwambie hivi “wifi yangu nakupenda sana natamani uwe karibu yangu unisaidie katika maisha yangu, lakini sijui kwa nini wewe hunipendi, hivi utajisikiaje kama mimi nikifa au nikiachika?” malizia halafu unyamaze.
Nakueleza ukishamwambia hivyo moja kwa moja atajua kuwa umeshafahamu mipango yake na kitakachotokea akili yake lazima itafute ubaya wako tu ikishakosa ina maana atakuwa amekosa uwezo wa kukufanyia ubaya.
Aidha, hata kama akifanya utashangaa anafanya kwa kiwango cha chini sana kutokana na hofu iliyojengwa kwake na mawazo yake ya kukuonea.
Lakini nasikitika kusema watu wengi hushindwa kunyonya nguvu za maadui zao kwa kueleza ukweli kwa sababu wanatumia jazba na matusi, mfano “wewe kafiri kweli, mema yote haya nakufanyia huoni tu mpaka unataka kuniroga, haya niue na wewe utakufa.” Ukisema hivyo unachochea nguvu zake za kukudhuru.
3. IMANI
Ukitaka kuitafsiri imani kwa maneno mepesi, unaweza kusema ni kukubali na kuyakataa mambo unayoyaona na kuyasikia.  Katika tafsiri hii ichukue akili kama kiini cha maamuzi ya kile unachokiamini.
Siku zote unapotazama kitu epuka sana kufanya kionekane kuwa kinashinda maamuzi na ubinadamu wako.  Kwa mfano umeona damu kwenye mlango wa nyumba yako, kwa nini uwaze kuwa ni uchawi na kwa nini isiwe ni damu ya mijusi iliyomwagika wakati wanagombana? Jiamini wewe na nguvu zako, usiogope mazingira tu.