Saturday 27 September 2014

MBINU ZA KUONGOZA FAMILIA KATIKA HALI DUNI KIMAISHA


KATIKA moja ya masomo yangu ambayo yanapatika katika vitabu vyagu vya Saikolojia No1,2&3, niliwahi kuandika mada inayohusu mambo yanayochangia familia nzima kuwa maskini. Leo sitarudia hayo lakini nitafundisha somo la mbinu za kuongoza familia katika hali ya umaskini.
Ni imani yangu kuwa, wadau wakubwa wa mada zangu ni watu wazima licha ya kuwa, wengine wana umri mdogo lakini naamini wanafahamu ugumu wa maisha unaozikabili familia mbalimbali.
Inawezekana wapo wenye mali na fedha nyingi ambao nao watapata fursa ya kusoma mada hii na kukosa mashiko ya hoja, kwa vile tu maisha yao ni mazuri na hivyo kukosa sababu kujifunza pamoja nami.
Waswahili husema; ya Mungu mengi na tabia ya upepo kugeuka. Raha ya leo si tumaini la kesho kwa vile usiku ni mrefu na mchana una mengi ya kuona na kujifunza.
Kwa kauli hizi, mwenye fedha leo hana mkataba na Mungu yawezekana kesho akaugua, akafilisika au akatetereka kimaisha na kumfanya aone tofauti hii na ile katika maisha yake kiasi cha kutapatapa: “Nitafanyaje kuiongoza familia yangu katika hali hii?”
Naamini kwenye maisha tunahangaika sote, wakati mwingine tunajiuliza; tutawalisha nini watoto wetu, tutawasomeshaje, tutawauguzaje, tutaihudumiaje familia yetu? Je, umewahi kujiuliza maswali haya? Hebu tazama dokezo kumi zifuatazo ili zikusaidie namna ya kuiongoza familia yako katika hali ngumu.
Kuishinda nafsi na akili yako
Mtu anayeongoza familia maskini lazima ashinde kwanza msukumo wa nafsi na akili zake ambao mara nyingi huwa unakimbilia kutoa majibu ya kumfanya mtu akate tamaa ya kuishi au kuzishinda changamoto.
Hakikisha, hata kama umefukuzwa kazi, umekosa fedha ya kula, huna kodi ya nyumba, unadaiwa mkopo, usikubali mawazo ya: “umekwisha, unadhani utafanyaje?” Ukikubali mawazo hayo, kwanza utaiona familia yako kuwa ni mzigo na hutaweza kuiongoza.
Nashauri uchukue hatua madhubuti ya kupingana na hali ya kukata tamaa na kujipa moyo wa kukabiliana na matokeo yoyote yatakayotokea katika maisha yako ya umaskini na familia yako. Ukifanya hivyo utafanikiwa kuituliza akili na mhemko wa hisia zako utapungua na hivyo kupata uwezo wa kukalibili changamoto.
Kinga utajiri wa wengine usiathiri familia yako
Familia nyingi maskini mara nyingi hukwazwa na tamaa ya kuishi sawa na matajiri. Watoto wa maskini hutamani kuvaa, kula, kustarehe kama wenzao wa nyumba ya pili anamoishi tajiri fulani.
Hali hiyo inapotokea, jitahidi sana, kuwafanya watoto na familia yako wavione vitu hivyo kama ni vibaya (jenga propaganda hasi) ili uwakinge wasijihukumu unyonge.
Saikolojia hii itawasaidia sana kupuuza tamaa za kuwa kama watoto wa matajiri na hivyo kutoa nafasi ya familia kupambana na hali ngumu ya maisha mpaka kitakapokuwa kimeeleweka.
Familia za maskini husifiwa kwa kupenda maharagwe na kande siyo soseji, kuku choma na chips funga. “Nawapenda sana ndugu zangu, yaana hamchagui vyakula; kama Juma (Mfano tu) ndiyo kabisa anapenda sana mboga za majani ndiyo maana ana afya njema.”

Mbinu za kuongoza familia katika hali duni kimaisha-2



KWANZA nianze makala haya kwa kukushukuru wewe msomaji wangu ambaye umekuwa nami katika somo hili tangu wiki iliyopita ambapo tulianza kwa kuangalia baadhi ya dokezo zitakazoweza kumsaidia mtu kuiongoza familia duni kimaisha.
Pongezi za kila mmoja anayeguswa na mada zangu zinanifanya nijivunie kila siku kwani naamini ndizo zinazonitia nguvu ya kuendelea na kazi hii ya kuwasaidia watu elimu ya jinsi ya kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
Baada ya shukrani hizo naomba tufuatane tena katika vipengele vichache vilivyosalia katika somo hili muhimu katika maisha.
hamasisha kila mmoja apigane
Huwezi kushinda vita kama askari wako wa mstari wa mbele hawapigani vita kwa umoja. Maisha magumu katika familia yanahitaji sana umoja, ifundishe familia yako kushiriki katika kupambana na maisha.
Keti na mkeo/mume, watoto, ndugu na jamaa unaoishi nao na kuwaambia kila mmoja anatakiwa kufanya kazi zinazolingana na uwezo wake. Mwenye uwezo wa kubeba mawe na kuponda kokoto aende kazini na mpepeta pumba mashineni asiache kufanya hivyo kwa kutegemea fulani atawajibika kwa ajili ya kumtafutia maisha.
Kwenye familia nyingi hasa vijana wamekuwa na tabia ya kukaa vijiweni na kupiga soga wakitegemea baba arudi kutoka kuuza madafu halafu wao wapate chakula. Hilo si jambo jema, lazima kila mtu afanye kazi. Moyo wa kufanya kazi hauji kimiujiza bali ni kwa mtu kuhamasishwa na kufundishwa.
TIA MOYO NA HAMASA
Mara nyingi familia duni hukumbwa na aina fulani za mikosi na wakati mwingine mipango iliyokuwa inategemewa kuleta ufumbuzi wa tatizo hukwama bila sababu za msingi.
Inapotokea hali ya namna hiyo kiongozi wa familia lazima achukue jukumu la kuitia moyo familia yake kwa kupanda mbegu ya matumaini mapya.
“Mwanangu hela yako imepotea? Usijali Utapata nyingine, usihuzunike sana,” ndivyo unavyotakiwa kusema.
Kwenye maisha duni epuka kuwa mtu wa kuongeza fikra hasi kwa mtu ambaye hana tumaini lingine, kwani utamvunja moyo sana na kumsababishia hali ya kukata tamaa kutafuta jibu la tatizo kwa njia nyingine.
BADILI UMASKINI WAKO NA UTAJIRI
Niliwahi kusema katika moja ya makala zangu kuwa hata matajiri tunaowaona wanahitaji msaada wa maskini. Kiongozi wa familia duni kimaisha lazima alijue hili na awe tayari kuifundisha familia yake kutumia umaskini wao kuleta utajiri.
Katika hali ya kawaida matajiri hawapendi kufanya kazi dhaifu au duni, hutegemea kuajiri na kuwalipa wengine fedha ili wafanye usafi wa mazingira nyumbani au hata ofisini.
Kuna mfano wa kijana mmoja wa Kifaransa aitwaye Devis, huyu kaka mwaka 1996 alikuwa maskini wa kutupwa na alikuwa akipata riziki yake kwa kufanya usafi kwenye nyumba ya tajiri. Akiwa kwenye kazi aliokota kitu kama chuma, hakujua ni kitu gani ila alikipenda na kukiweka mfukoni.
Aliporudi nyumbani, rafiki yake alikiona kuwa si kitu cha kawaida, akamshauri wakipeleke kwa sonara. Walipofika huko waligundua kuwa kumbe kilikuwa ni jiwe la dhahabu. Hivyo, akaliuza kwa bei kubwa na tangu hapo akaanza kufanya biashara.
Miaka mitano baadaye alifanikiwa kumiliki mgahawa uliopendwa sana na wateja na hivyo kumletea kipato kikubwa.
Naamini mpaka hapa tutakuwa tumejifunza mengi na pengine kuhitaji elimu zaidi, lakini nafasi yangu imemalizika, naomba tukutane tena wiki ijayo tumalizie somo hili zuri.

0 comments:

Post a Comment