Tuesday 9 December 2014

UTAFITI: UMBEA UNA FAIDA KIAFYA NA WANAUME NI WAMBEA ZAIDI YA WANAWAKE




Katika jamii yoyote mtu mwenye tabia ya umbea huchukiwa, hutengwa na hata wakati mwingine hupigwa kwa kuonekana kuwa ni chanzo cha migogoro na huku viongozi wa dini wakimwona mtu wa aina hiyo kuwa ni mtenda dhambi.



Watu wanaopenda tabia ya umbea huenda wakawa wamepata mtetezi. Ripoti iliyotolewa hivi karibuni kuhusu tabia ya watu kupenda kutumia muda mwingi kusema mambo ya watu wengine, inasema tabia ya umbea ina manufaa kiafya.


Ripoti hiyo iliyotolewa na watafiti kutoka chuo kikuu cha Rhode Island cha Marekani, inasema kuwa watu wanaonufaika zaidi za tabia hiyo ni wale wanaopenda kuongea mambo mabaya wa watu wengine kuliko wenzao wanaopenda kuzungumza kuhusu mambo mazuri.


Wataalamu hao wamebaini kuwa iwapo mtu atatumia dakika 20 kuzungumzia mambo mabaya ya watu wengine, anaweza kuimarisha afya yake kwa kupunguza msongo wa mawazo, woga na mashaka kwa asilimia 96 kwa muda wa masaa manne mfululizo.


Hata hivyo, wamebainisha kuwa mtu akitumia muda huo huo kuzungumza mambo mazuri ya watu wengine, atapunguza msongo wa mawazo kwa asilimia 72 ikimaanisha kuwa watu wenye kuzungumza mambo mabaya ndio wenye kunufaika zaidi.


Watafiti hao, wakifafanua hali hiyo wameelezwa kuwa mtu anapoongea habari nzuri zinazowahusu watu wengine huuchochea ubongo kutaka kujiunganisha na mtu anayezungumzwa, wakati yule anayezungumza habari mbaya huwa kinyume chake.


Mtu anayezungumza habari mbaya anatabia ya kutokuhifadhi alichokisema, bali huendelea na mambo yake kama kawaida, wakati anayezungumza habari nzuri hukaa nazo moyoni kwa kipindi cha muda fulani.


Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Lusajo Kajula anasema binadamu wote huongea kuhusu watu wengine, lakini umbea ni zaidi ya maongezi.


Lusajo anasema asili ya mwanadamu ni kuzungumza japokuwa wakati mwingine hujikuta akiishia kutoa mifano halisi ya maisha ya watu wengine na hivyo kuingia katika mgogoro wakati mtu aliyesemwa anaposikia.


Umbea ni kawaida na hauzuiliki, tatizo ni yaliyomo ndani ya umbea ambayo mara nyingi hutegemea na mawazo mtu aliyonayo. Kama ana mawazo hasi, ataongea mambo mabaya,” anasema Kajula.


Hata hivyo, Kajula anapingana na dhana iliyopo miongoni mwa watu kuwa mwanamke ndiyo anayependa zaidi tabia ya kuzungumza mambo ya watu wengine kuliko mwanaume.

0 comments:

Post a Comment