Friday, 10 October 2014

VIUNGO VYA MBOGA VINAVYOWEZA KUOKOA MAISHA YAKO



AFYA bora ndiyo msingi wa maisha ya kila binadamu, bila kuwa na afya bora hakuna maisha. Kwa sababu maradhi hukaa mbali na mtu mwenye afya bora na maradhi hukaa karibu na mtu mwenye afya mbovu. Lakini je, utawezaje kuwa na afya bora? Siri kubwa iko kwenye vyakula na staili ya maisha.
Katika makala ya leo, nakuorodheshea viungo muhimu vya chakula ambavyo vinaweza kuweka tofauti kubwa katika afya yako kama ukiwa unavitumia kwenye mlo wako wa kila siku. Unaweza kupata tiba na kinga ya maradhi mbalimbali kutoka jikoni mwako, baada ya kusoma makala ya leo;
BIZARI
Hiki ni kiungo jamii ya tangawizi, chenye rangi ya njano. Unaweza kutumia tangawizi mbichi ikiwa katika umbo lake la mzizi, au unaweza kuikausha na kutumia unga wake kwa kuungia mboga. Inajulikana kama ‘Mfalme wa Viungo’ kutokana kuwa na faida nyingi mwilini.
Baadhi ya faida hizo ni pamoja na uimarishaji wa mifupa, maungio ya viungo, ngozi, kinga ya mwili, usagaji chakula tumboni pamoja na uimarishaji wa njia ya uvutaji hewa. Hali kadhalika bizari imeonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuzuia na kutibu ugonjwa hatari wa saratani ambao unaua watu wengi duniani.
Utafiti wa kina ambao umekuwa ukifanywa kwa karne tano zilizopita, umegundua kuwa bizari ina kirutubisho aina ya ‘curcumin’ ambacho kina uwezo mkubwa wa kuzuia magonjwa mengi, yakiwemo ya kolestro, kisukari na huzuia kuongezeka kwa virusi vya HIV mwilini, kwa wale walioathirika na ugonjwa huo. Ushauri ni kwamba, kuanzia leo unapopika mboga, weka na bizari kupata ladha na faida zilizotajwa hapa.
LOZI (Almonds)
Lozi ni chakula jamii ya karanga na korosho, kina sifa moja kubwa ya kuwa na virutubisho vingi kuliko jamii nyingine ya karanga. Lozi (almonds) imethibitika kuwa na uwezo wa kupunguza maumivu mwilini na kuzuia magonjwa mengine kwa haraka zaidi. Ni chanzo kikubwa cha madini ya potasiamu, kasiamu, manganizi, phosphora, chuma na Vitamin E.
Lozi inapunguza kolestro mwilini, shinikizo la damu na inasaidia katika kupunguza uzito bila kuleta madhara mwilini. Vile vile ulaji wa lozi kavu kama karanga kila siku, siyo tu kutakukinga na maradhi kama ugonjwa wa moyo, lakini pia huondoa mara moja matatizo ya tumbo kujaa, kuumwa kichwa au mwili kuvimba. Vilevile lozi zinaaminika kuongeza nguvu za kiume.
VIUNGO VINGINE
Viungo vingine muhimu vya mboga vyenye faida kubwa mwilini ni pamoja na kitunguu saumu, mboga za majani aina ya brokoli (brĂ³coli), pilipili kali, vitunguu vya kawaida na nyanya.
Hivi ni viungo ambavyo huweza kutumika kama kinga ya magonjwa hatari na huweza kutumika pia kama dawa ya kuleta ahueni kwa magonjwa hatari ambayo mtu anakuwa tayari ameyapata.
MAJI SALAMA
Mwisho, kwa sababu binadamu anaishi kwa kuvuta hewa chafu na kula vyakula vyenye kemikali za sumu kutokana na uchafuzi wa mazingira, unywaji wa maji salama na ya kutosha kila siku ni muhimu katika kuusafisha mwili ili kuondoa sumu hizo.
Matatizo mengi ya kiafya yanachangiwa na mengine yanasababishwa na upungufu wa maji mwilini, matokeo yake watu wengi hujisikia kuumwa na kwenda hospitali kupewa dawa kwa matatizo ambayo wangeweza kuyaepuka kwa kunywa maji ya kutosha tu kila siku. Kwa maneno mengine, kwa kunywa maji ya kutosha kila siku, kutakuwezesha kuwa na afya bora.

0 comments:

Post a Comment