Friday, 10 October 2014

VIRUSI ''VIJIDUDU' VIDOGO VINAVYOTIKISA FANI YA TIBA DUNIANI




Miongoni mwa magonjwa mabaya zaidi duniani ni yale yanayoenezwa na virusi, hebu tumchunguze huyu ni kiumbe wa namna gani.
Virusi ni vijidudu vidogo sana kiasi kwamba huingia karibu mara 100 katika seli moja ya mwili wa binadamu.
Virusi husababisha magonjwa mbalimbali ya binadamu, wanyama na mimea. Virusi vinaweza kusababisha magonjwa ya kuambukiza na baadhi ya magonjwa ya saratani.
Wataalamu wa sayansi ya elimu ya virusi wanadai kuwa kuna maelfu ya aina za virusi duniani. Inasemekana kuwa virusi ndivyo viumbe vinavyoongoza kwa wingi duniani.
Virusi havina sifa ya moja kwa moja ya viumbehai kwa sababu huonyesha tabia ya uhai vinapokuwa ndani ya seli ya kiumbe kingine.
Kiumbehai kina sifa ya kula, kuzaliana lakini kirusi hana sifa hizo kinapokuwa peke yake.
Virusi havina uwezo wa kuzaliana vyenyewe kwa vyenyewe kama ilivyo viumbe wengine. Viumbe wengine hukutana pande za kiume na kike ili kuzaliana wakati nyingine hugawanyika.
Vinavyogawanyika huwa ni vile vinavyoundwa kwa seli moja kama vile bakteria na hugawanyika ili kuunda viumbe wengine.
Kwa upande wa virusi, huzaliana baada ya kuingia ndani ya chembechembe hai za viumbe wengine. Virusi hupatikana kila mahali palipo na uhai na inaelezwa kuwa wameanza kuwapo tangu uwapo wa chembechembe zenye uhai duniani.
Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Iyer LM, Balaji S, Koonin EV na Aravind L uliochapishwa katika jarida tafiti za kisayansi la Virus Research, toleo la 117(1) la mwaka 2006.
Virusi husambaa miongoni mwa binadamu kwa njia mbalimbali kama vile kukohoa, kupiga chafya, kushikana mikono au kugusana.
Njia zingine zinazosambaza au kusababisha maambukizi ya virusi ni pamoja na kujamiiana bila kutumia kinga, kugusana na majimaji ya mwili yenye virusi, kula chakula kilichochafuliwa na virusi, kuumwa na wadudu kama vile mbu na kwa njia ya maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambaye hajazaliwa, kipindi cha kuzaliwa au wakati wa kunyonyesha.
Virusi vinapoingia mwilini, hupenya ndani ya aina fulani ya seli na kubadilisha mfumo mzima wa utendaji wa seli kiasi kwamba seli hulazimishwa kuzalisha virusi badala ya kazi yake ya kawaida. Baadhi ya seli zinazoshambuliwa hufa na virusi huingia katika seli zingine zilizo hai na kuzaliana kwa wingi.
Baadhi ya aina za virusi haviui seli bali huilazimisha kubadili mfumo wake wa utendaji na kusababisha ugonjwa wa saratani

Aina nyingine ya virusi husababisha magonjwa yasiyo na madhara makubwa, lakini kuna baadhi ya virusi husababisha maradhi hatari sana yanayoweza kusababisha kifo haraka.

Magonjwa mengi yanayosababishwa na virusi hupona yenyewe bila kuhitaji dawa, lakini kuna magonjwa mengine yasiyopona na yasiyokuwa na tiba wala chanjo.

Magonjwa kama vile ebola, Kichaa cha mbwa na upungufu wa kinga mwilini utokanao na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), ni mifano mizuri ya maradhi hatari yanayosababishwa na virusi.

Magonjwa haya hadi sasa hayana chanjo wala tiba madhubuti yenye kuaminika. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mtu anapougua ebola uwezekano wa kufa ni asilimia 90 na anapougua ugonjwa wa kichaa cha mbwa unaotokana na virusi, uwezekano wa kufa ni asilimia 100.

Wanasayansi hadi sasa, wanaendelea kukuna vichwa kwa ajili ya kutafuta chanjo na tiba ya magonjwa haya hatari yanayoathiri afya na kupoteza maisha ya watu wengi duniani.

Kutokana na maumbile ya virusi na uwezo wake wa kuishi ndani ya seli za mwili na kushikamana nazo, husababisha ugumu wa kuviangamiza kwa dawa bila kudhuru afya ya mgonjwa.

Virusi pia vina uwezo wa kujigeuza mara kwa mara katika mfumo wake wa kijenetiki. Hali hii huvisaidia kukwepa udhibiti wa mfumo wa kinga ya mwili, pia hufanya upatikanaji wa dawa na chanjo kuwa mgumu.

Wanasayansi wanapofanya utafiti wa chanjo, hujikuta katika wakati mgumu baada ya muda mfupi kwani virusi huwa vimejigeuza kiasi kwamba chanjo au dawa inayotengenezwa ili kudhibiti virusi, inashindwa kutoa matokeo yaliyokusudiwa. Mara nyingi chanjo ya ugonjwa utokanao na virusi inakuwa na manufaa kwa mgonjwa ambaye hajapata maambukizi ya virusi.

Chanjo pia inashindwa kufanya kazi vizuri katika udhibiti wa virusi vinavyojenga usugu kutokana na kujigeuza haraka katika maumbile na mfumo wake wa kijenetiki.

Wakati mwingine virusi vya kundi fulani katika aina zake vinaweza kujigeuza na kuzalisha kundi jipya lenye mfumo tata wa kijenetiki. Hii ni kwa mujibu wa Jaap Goudsmit katika kitabu chake kiitwacho Viral Sex kilichochapishwa mwaka 1998.
Kwa mfano VVU wanaaminika walitokana na virusi wajulikanao kama Simiani (SIV) ambao walikuwa wanasambaa katika jamii ya sokwe.

Nyani wenye aina hiyo ya virusi hupata athari ya kinga kama ilivyo kwa mwathirika wa VVU na baadaye huugua na kuonyesha dalili sawa na za Ukimwi.

Dawa nyingi zinazotumika katika matibabu ya magonjwa yatokanayo na virusi, husaidia katika udhibiti wa virusi ili visiweze kujiingiza, kujishikiza, kuzaliana au visiweze kushikamana na seli za mwili.

Kwa mfano VVU vina uwezo wa kuzaliana kwa kasi kiasi kwamba seli za kinga ya mwili, hushindwa kukabiliana na ongezeko kubwa la jeshi la virusi mwilini.

Seli nyingi hushambuliwa na kuuawa kwa kasi na kuuacha mwili ukiwa hauna kinga au ulinzi wa kutosha.

Hali hii ya virusi kuonekana kuwa na ujanja wa kujibadilisha haraka kunaonekana kuwakatisha tamaa baadhi ya wanasayansi licha ya kwamba taaluma ya kuvichunguza inakua siku hadi siku.

“Hatutaweza kamwe kutokomeza virusi, lakini kwa kuvielewa vizuri, tunaweza kutengeneza chanjo mpya, dawa za kuvifubaza na kuweka mikakati ya kupunguza athari zake,” anasema Profesa Wendy Barclay wa Chuo cha Elimu ya Juu cha Imperial, jijini London.

Mnamo mwaka 1796, Dk Edward Jenner wa Uingereza alifanikiwa kutengeneza chanjo ya kwanza dhidi ya ugonjwa wa ndui.

Wakati huo ugonjwa wa ndui ambao uliokuwa unasababishwa na virusi, ulikuwa ukisababisha vifo lakini hatimaye ulitokomezwa mwaka 1980 baada ya kupatikana kinga.

Kwa sasa wanasayansi wanahangaika na utafiti wa chanjo ya VVU na ebola. Majaribio ya chanjo ya magonjwa hayo yameanza kufanyika na yako katika hatua mbalimbali.

Mengi ya majaribio hayo kwa sasa yanafanyika katika nchi za Ulaya na ifikapo Januari 2015, yanaweza kuanza kufanyika katika baadhi ya nchi za Afrika. “Kama kila kitu kitaenda vizuri, tunaweza kuanza kutumia baadhi ya chanjo za ebola katika baadhi ya nchi zilizoathirika zaidi mapema mwanzoni mwa mwaka ujao,” anasema Dk Marie-Paule Kieny, mkurugenzi msaidizi wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
Hadi sasa njia yenye manufaa zaidi katika mapambano na udhibiti wa magonjwa yatokanayo na maambukizi ya virusi ni kuepuka njia zile za maambukizi.

Virusi wanaweza kuambukizwa kwa njia mbalimbali lakini mara nyingi ni kwa kugusana moja kwa moja na umajimaji ulio na virusi vya maradhi husika.

Kinga ni bora kuliko kuponya. Magonjwa haya ya virusi yanakuwa magumu kutibiwa, lakini wakati mwingine kuna kuwa na nafasi ya baadhi ya miili ya watu kuweza kuudhibiti pale anapopata misaada mingine ya tiba.

Njia bora zaidi ya kukabili maradhi yatokanayo ni virusi ni kukabiliana na njia za maambukizi.

0 comments:

Post a Comment