Wednesday 1 October 2014

UKIMWI, UGONJWA UNAOKWENDA SAMBAMBA NA UGONJWA WA KIFUA KIKUU.



Mchoro unaoonyesha mapafu ya mwanadamu yaliyoathiriwa na maradhi ya Kifua Kikuu. Picha kwa hisani ya Shutterstock. 

Kwa Ufupi
Ni marafiki ambao hawachezi mbali na ndiyo maana siku hizi wagonjwa wengi wanagundulika kuwa nao pamoja.

Asilimia kubwa ya watu wanaougua ugonjwa wa kifua kikuu (TB) duniani wamekuwa wakigundulika pia kuwa na Virusi Vya Ukimwi(VVU).

Hii ni kwa sababu mtu mwenye VVU, huwa na kinga dhaifu jambo ambalo husababisha vimelea vya TB navyo kupata nafasi ya kuushambulia mwili.

Hivyo, mtu mwenye VVU ana uwezekano mkubwa wa kupata TB hai mara 29.6 ukilinganisha na yule asiye na VVU. Kwa mwaka 2012, walikuwepo wagonjwa milioni 1.1 wenye VVU na TB kati yao, karibu asilimia 75 ni watu wanaotoka katika nchi zinazoendelea hasa kusini mwa Jangwa la Sahara .

Pale inapotokea mtu ana maambukizi ya VVU , kinga ya mwili nayo hutetereka na kushuka na hivyo mwili nao hukosa kinga na ugonjwa wa TB hujitokeza.

Ugonjwa wa TB ndio unaongoza kuwaua wagonjwa wa VVU, hesabu ikiwa kwa kila vifo 5, mmoja hufariki kwa TB.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2012, watu 320,000 walikufa kwa VVU uliombatana na TB, ingawa duniani vifo hivyo ni sawa kwa wake kwa waume, ingawa kwa Afrika vifo ni zaidi kwa wanawake kuliko wanaume.

Kwa upande wa Tanzania, watu 120,191 wanakisiwa kupata kifua kikuu kila mwaka, hii ni kutokana na taarifa ya Shirika la Misaada la Marekani (USAID) mwaka 2007.

Kati ya watu hao (120,191), 56,233 ni wale waliogundulika kuwa na ugonjwa huu kupitia makohozi, yaani vifo vinavyotokana na ugonjwa wa kifua kikuu ni 32,000 kila mwaka nchini Tanzania.

Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha kuwa Tanzania ni ya 15 kati ya nchi 22 ambazo zimeathiriwa sana na ugonjwa huu.

Kati ya asilimia 50 ya wagonjwa wa kifua kikuu waliopimwa virusi vya Ukimwi mwaka 2007.

Inakadiriwa kuwa Ukimwi huathiri asilimia 47 ya wagonjwa wote wa kifua kikuu. Ugonjwa sugu wa kifua kikuu (Multi-Drug Resistant Tuberculosis) huathiri watu 1,300 nchini Tanzania kulingana na taarifa ya mwaka 2007.

Wengi wa wagonjwa wa VVU wanakumbana na udharura unaotishia maisha yao hii ni kutokana na kuwapo kwa TB sugu na ile isiyotibika hata kwa dawa mchanganyiko.Kutokana na hilo, ndipo urafiki wa VVU na TB unapotokea na kushirikiana kuushambulia mwili na kama hatua za haraka zisipochukuliwa basi mtu huweza kudhoofu haraka na kupoteza maisha. Takwimu zaidi zinaonyesha kuwa mwaka 2011 wagonjwa 


wa Ukimwi na TB walipoteza maisha kwa magonjwa hayo mawili.

WHO katika mikakati ya kidunia imeweka mikakati ya kusambaza huduma za afya za tb kila mahali kwa ajili ya huduma za matibabu, ushauri na upimaji, na tayari kuna wagonjwa wa TB ambao tayari huduma hizi zimewafikia wagonjwa na kati ya hao wengine wanatumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARVs).

Dalili za TB

Kukohoa kwa zaidi ya wiki mbili, upungufu wa uzito wa mwili wa zaidi ya asilimia 10 ya uzito wa mwili, kupumua kwa shida, maumivu ya kifua, kukohoa damu, homa kali na kutokwa na jasho hasa nyakati za usiku, mwili kuwa mchovu, kuvimba tezi za shingo na kwapani na kuumwa kichwa

Jinsi ya kukabiliana na TB kwa wenye VVU

Jambo la msingi na muhimu ni kuwahi kufika katika huduma za afya mapema uwepo wa VVU na TB mwilini, hatari huwa zaidi kwani mwili hudhoofu na kufariki haraka ukilinganisha na yule mwenye TB bila VVU.

Zingatia matibabu pale unapoanza kutumia dawa za TB na ARVs hakikisha unatumia dawa kama ulivyoelekezwa na wataalamu wa afya, kumbuka usugu wa dawa na kushindwa kwa dawa hizi ni hatari zaidi katika kupambana na TB na VVU. Usiache kutumia dawa za TB ili kuepuka kupata TB sugu na ile isiyotibika kwa dawa mchanganyiko.

Hakikisha pale unapoona unakohoa zaidi ya wiki mbili unafika katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.

Funika mdomo na pua kwa kitambaa pale unapokohoa au kupiga chafya hii inasaidia kuzuia kuenea maambukizi.

Kuepuka mikusanyiko au mrundikano wa watu kama vile kwenye mabweni, kambi za jeshi, baa na kadhalika.

Kuishi kwenye nyumba ambayo ina mfumo mzuri wa kuingiza na kutoa hewa yaani iwe na madirisha makubwa na ya kutosha.

Pia, kuishi katika mienendo bora inayozingatia afya, kula mlo kamili, kunywa maji mengi angalau lita 1.5 kwa siku na mazoezi mepesi kama kutembea kwa dakika 15 kwa siku yanachangia kuujenga mwili na kuwa wenye afya njema. Pata mapumziko ya kutosha angalau lala masaa sita kwa siku, epuka matumizi ya ulevi wa pombe. chanzo.Ukimwi; ugonjwa unaokwenda sambamba na kifua kikuu 


0 comments:

Post a Comment