Ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema pamoja na akili timamu, akiwa tumboni lazima alishwe lishe bora na mlo sahihi. Mwenye jukumu la kutoa lishe bora na sahihi kwa kiumbe kilichomo tumboni ni mama. Anatakiwa kujua aina ya vyakula anavyopaswa kula. Vivyo hivyo, anatakiwa kujua aina ya vyakula vya kuviepuka.
Katika makala ya leo, tunaangalia orodha ya vyakula vilivyokatazwa. Mama mja mzito haruhusiwi kuvila vyakula vifuatavyo kwa faida ya kiumbe kilichomo tumboni na kwa faida yake mwenyewe:
NYAMA MBICHI
Epuka kula samaki au nyama mbichi au iliyopikwa lakini haikuiva vizuri. Utajiepusha na uwezekano wa kula bakteria na vijidudu vingine hatari kwa afya ya mtoto tumboni. Mjamzito anapokula nyama, anatakiwa kuhakikisha imeiva sawasawa.
‘SOSEJI’ NA ‘SANDWICHI’
Mjamzito haruhusiwi kula ‘soseji’, ‘sandwichi’ za nyama na vyakula vingine vilivyotengenezwa kwa nyama. Inaaminika kuwa nyama zinazoandaliwa kwa ajili ya kutengenezea vyakula kama hivyo, huwa vimewekewa vihifadhi vyakula (preservatives) ambavyo vinaweza visiwe vizuri kwa afya ya mtoto.
SAMAKI WENYE ZEBAKI (MERCURY)
Wajawazito wamekatazwa kula samaki wenye kiasi kingi cha madini ya zebaki. Ulaji wa zebaji kwa wajawazito umehusishwa na uzaaji wa watoto taahira. Mfano wa samaki hao ni pamoja na Papa, Chuchunge na dagaa wakubwa.
MAYAI MABICHI
Ulaji wa mayai mabichi au vyakula vilivyochanganywa na mayai mabichi, mjamzito haruhusiwi kuvila. Kuna baadhi ya ‘Ice Cream’ na ‘mayonaizi’ hutengenezwa kwa kuchanganywa na mayai mabichi. Mjamzito amekatazwa kuvila vyakula hivyo.
MAINI
Maini yana kiwango kikubwa cha madini aina ya chuma. Hata hivyo, yana kiasi kikubwa cha Vitamin A ambacho huweza kuwa na madhara kwa mtoto kikizidi.
MAZIWA MABICHI
Maziwa mabichi huweza kuwa na bakteria ajulikanae kama ‘Listeria’, ambaye huweza kusababisha kuharibika kwa mimba. Unapokunywa maziwa, hakikisha yamechemshwa au kama ni ya paketi hakikisha ni yale yaliyoandikwa ‘Pasteurized’ na siyo ‘Unpasteurized’.
KAFEINI (CAFFEINE)
Ingawa baadhi ya utafiti unaonesha kuwa unywaji wa kiasi kidogo cha kafeini hauna madhara, lakini kuna utafiti mwingine unaonesha kuwa unywaji wa kafeini una uhusiano na kuharibika kwa mimba. Kafeini ni aina ya kirutubisho kinachopatikana ndani ya kahawa.
Iwapo mjamzito atakunywa kahawa, basi anywe kiasi kidogo sana kisichozidi kikombe kimoja kwa siku. Kwa kawaida kahawa hukausha maji mwilini, hivyo unywaji wake husaidia kukauka maji mwilini ambayo ni muhimu sana kwa mjamzito.
Utafiti mwingine unaonesha kuwa kafeini inahusishwa pia na uharibikaji wa mimba, uzaaji wa watoto ‘njiti’ na watoto wenye uzito mdogo. Ni vizuri kunywa maji ya kutosha, maziwa na juisi na kuepuka kunywa vinywaji vyenye kahawa.
POMBE
Hakuna ushahidi unaothibitisha kuwa unywaji wa pombe kiasi kidogo wakati wa ujauzito hauna madhara, kwa maana hiyo matumizi ya pombe hayaruhusiwi kabisa wakati wa ujauzito, hata kama ni kidogo.
Unywaji wa pombe wakati wa ujauzito huweza kuathiri ukuaji mzuri wa mtoto. Kutegemeana na kiasi atakachokunywa mjamzito, pombe inaweza kumsababishia mtoto ugonjwa hatari utokanao na pombe (Fetal Alcohol Syndrome).
0 comments:
Post a Comment