Tuesday 30 September 2014

UGONJWA WA ZINAA WA TRICHOMONIASIS








Leo pia tutaendelea kuyajadili magonjwa ya zinaa ambapo tutazungumzia ugonjwa wa Trichomaniasis, ambao huwaathiri sana wanawake kuliko wanaume. I.


Ugonjwa wa Trichomoniasis ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya jamii ya protozoan vinavyojulikana kama Trichomonas vaginalis. Ugonjwa huu huathiri mrija wa kupitisha mkojo unaojulikana kama urethra na tupu ya mwanamke. Trichomoniasis pia hujulikana kwa majina mengine kama Trichomonas vaginitis au Trich.

Trichomoniasis huathiri watu milioni 170 kwa mwaka duniani kote ambako nchini Marekani pekee watu milioni 8 huambukizwa ugonjwa huo. Ugonjwa huu huonekana sana kwa wanawake kuliko wanaume labda kutokana na wanaume kutoonyesha dalili zozote wakati wa maambukizi au kutokana na majimaji ya kwenye tezi dume kuwa na madini ya zinc ambayo huathiri vimelea hivi vya Trichomonas vaginalis vinavyosababisha ugonjwa huo. 

Trichomoniasis hupatikana kwa njia ya kujamiana bila kutumia kinga na mtu aliyeathirika ugonjwa huo. Wanawake wengi wamekuwa wakisumbuliwa na ugonjwa huu, na ili kuufahamu vyema ni bora kwanza tuelezee nini hutokea wakati wa maambukizi au Pathofiziolojia ya ugonjwa huo.
Umbile la vimelea vya Trichomonas vaginalis ni sawa na chembechembe moja ya damu nyeupe kwa upana, ingawa wakati mwingine ukubwa unaweza kutofautiana kulingana na mazingira. Kuwepo kwa umbile kama mikono 

kwa nje kwenye kimelea hicho inayojulikana kama flagellum, husaidia vimelea hivi kuingia kwenye tishu za mrija wa kupitisha mkojo pamoja na tupu ya mwanamke na hivyo kuharibu seli aina ya epithelium na kusababisha vidonda 

katika tishu hizo. Hii ndiyo sababu, watu wanaopata ugonjwa huu huwa kwenye hatari kubwa ya kupata ugonjwa wa Ukimwi (HIV) na magonjwa mengineyo ya zinaa. Je, wagonjwa huwa na dalili zipi?
Dalili za Trichomoniasis huanza kuonekana kuanzia siku ya 4 hadi ya 28 baada ya mtu kupata maambukizi ya ugonjwa huu. Kwa wanawake, Trichomoniasis huathiri shingo ya kizazi (cervix), mrija wa mkojo, tupu ya mwanamke, kibofu cha mkojo na tezi zinazojulikana kama Bartholin glands na Skene glands. Kwa wanaume 

vimelea hivi vya Trichomonas vaginalis hupatikana katika sehemu za siri za mwanamume, sehemu ya nje ya mrija wa kupitisha mkojo (anterior urethra), kwenye tezi dume, kwenye mirija ya kuhifadhi na kutoa mbegu za kiume (epididymis) na hata kwenye mbegu zenyewe. Dalili kwa wanawake zinaweza kuwa: 1) Uchafu unaotoka kwenye tupu ya mwanamke ambao huwa wa rangi mchanganyiko ya njano na kijani, au rangi ya kama kijivu na huwa mzito sana. 2) Maumivu wakati wa kujamiana. 3) Kutoka harufu kwenye tupu ya mwanamke. 4) Maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo. 5) Shingo ya kizazi kuwa nyekundu hali ambayo hugundulika wakati daktari anamfanyia mgonjwa uchunguzi. 6) Kuwasha sehemu za siri, ambako huwatokea baadhi ya wanawake na sio wote. 7) Maumivu chini ya kitovu ambayo pia huwapata baadhi ya wanawake.
Ingawa wanawake ndio huonyesha dalili na viashiria vya ugonjwa huu, lakini mara nyingine wanaweza kuwa na vimelea hivi hata kwa muda wa miaka kadhaa hata kama vipimo vya uchunguzi havitaonyesha kama wameathirika na vimelea vya ugonjwa huo.


Wanaume huwa hawaonyeshi dalili zozote lakini baadhi huonyesha dalili ambazo ni za kuwasha ndani ya uume, kutokwa na uchafu au majimaji kwenye uume na kuwashwa au kuhisi kichomi baada ya kujisaidia haja ndogo au baada ya kutoa mbegu za kiume. Baada ya mtu kuhisi dalili hizo anashauriwa kwenda hospitalini au katika vituo vya afya ili kufanyiwa uchunguzi na vipimo. Trichomoniasis hugundulika kwa kutumia kipimo cha hadubini ambapo 

daktari humfanyia mgonjwa uchunguzi kwa kuingiza kifaa maalum katika tupu ya mwanamke na kuchukua kipimo kwa kutumia pamba maalum. Hatua ambazo hufanywa kitaalamu na bila kusababisha maumivu kwa mgonjwa na kisha kupelekwa maabarani ili kuangalia kama kuna vimelea vya Trichomonas vaginalis. Kwa kufanya uchunguzi huu, daktari pia anaweza kuangalia kama kuta za ndani za tupu ya mwanamke au shingo ya kizazi zimeathirika 

kwa kuwa na vidonda ambavyo ni vyekundu. Kwa mwanamume, daktari huchukua kipimo cha uchafu unaotoka kwenye uume au hupangusa sehemu za siri za mwanaume kwa wale ambao hawatoi uchafu au majimaji yoyote kwa kutumia pamba na kupeleka maabara kuyafanyia uchunguzi. Pia kipimo kilichochukuliwa na daktari kinaweza kuoteshwa kwenye maabara (culture) na kuangalia kama kuna uoto wa vimelea vya Trichomonas vaginalis baada 

ya siku tatu. Daktari pia anaweza kuangalia kiwango cha tindikali (PH) kwenye tupu ya mwanamke kwa kutumia karatasi maalum ya kipimo hiki ijulikanayo kama PH paper, ambapo kiwango kitakuwa alkaline kama ameathiriwa yaani PH zaidi ya 5. Kwa kawaida PH ya tupu ya mwanamke inakuwa ni ya tindikali (acidic) ya kuanzia PH 3.8 mpaka 4.5, na magonjwa yanayobadilisha PH hii ni pamoja na Trichomoniasis, na Bacteria Vaginosis. Mabadiliko ya hali hiyo humfanya mwanamke kuwa kwenye hatari ya kupata maambukizi tofauti.

Kipimo kingine ni cha damu ili kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA). PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume. Uzalishaji wake huongezeka wakati seli za tezi dume zinapokua kuelekea kuwa kensa hali inayojulikana kitaalamu kama BPH, au wakati tezi dume inapopata maaambukizo (prostitis), na katika saratani ya tezi dume. Kipimo hiki kinapaswa kufanywa kwa wanaume wanaopata ugonjwa wa Trichomianisis mara kwa mara au wale wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea na ambao wamepata ugonjwa huu, na wanapaswa wafanyiwe kipimo hiki angalau mara moja kwa mwaka. Kipimo kingine ni cha Pap smear ambapo 

chembechembe au seli za shingo ya kizazi huchukuliwa na kuchunguzwa kwa kutumia hadubini. Kipimo hiki pia hutumiwa katika uchunguzi wa wanawake ili kujua kama wamepata saratani ya shingo ya kizazi au la. Wanawake wenye zaidi ya miaka 18 au wale wenye upungufu wa kinga mwilini wanashauriwa kufanya kipimo hiki pia angalau mara moja kwa mwaka ili wajue afya zao. Pia waliothirika na Trichomaniasis wanapaswa kufanyiwa kipimo cha kuangalia maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi, kipimo cha mkojo na kipimo cha damu kuangalia wingi wa damu, chembechembe tofauti za damu na chembechembe bapa (platelets).


Tunasonga mbele tukiendelea kujadili ugonjwa wa zinaa wa Trichomoniasis kwa kuelezea tiba ya ugonjwa huo. Tiba ya Trichomaniasis ni kutumia dawa aina ya metronidazole au flagyl. Kwa wanawake wajawazito, dawa hii haitumiki kwa wale wenye ujauzito wa chini ya miezi mitatu au kwa wale ambao wananyonyesha. Ni vizuri kumuona daktari kabla ya kutumia dawa hii. Wale walioathirika na ugonjwa huu wa zinaa, wanashauriwa kupata tiba pamoja 

na wenza wao. Madhara ya dawa ya metronidazole ni pamoja na mzio au mcharuko mwili kwa maana ya allergic reaction, kichefuchefu, kukauka midomo, kuharisha, kuhisi ladha kama ya chuma mdomoni na kushuka kiwango cha chembechembe nyeupe za damu (leukopenia) ambazo hutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali na hivyo upungufu wake kumfanya mtu awe katika hatari ya kupata maambukizi tofauti tofauti. Msishituke wapenzi wasikilizaji, hali hizo za allergic kwa dawa hutokea mara nyingi iwapo masharti ya dawa hayakufutwa vyema au mtu anapokunywa dozi

ya dawa zaidi ya alivyoelekezwa na daktari. Ni muhimu kufahamu kuwa, unapohisi hali kama hizo katika matibabu yoyote inakupasa kuacha kutumia dawa zilizokudhuru na kumuona daktari haraka. Baada ya kujua matibabu, yafuatayo ni madhara ya ugonjwa wa zinaa wa Trichomoniasis. Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa ambayo huongeza hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa ukimwi kama tulivyosema huko nyuma. Pia Trichomaniasis husababisha mwanamke kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo. Ugonjwa huu vilevile huwaongezea wanawake hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi na kwa wanaume huwaongezea hatari ya kupata saratani ya tezi dume

0 comments:

Post a Comment