Saturday, 27 September 2014

NJIA 7 ZA KUONGEZA UWEZO WA KUMBUKUMBU



NI jambo la wazi kwamba tunapozidi kuwa wazee huwa tunaanza kugundua mabadiliko kadhaa katika uwezo wetu wa kukumbuka mambo.
Hali hii ni kama kujikuta uko jikoni lakini hukumbuki ni kwa nini ulikwenda humo, au kutoweza kukumbuka jina la mtu unayemfahamu wakati ukiongea na watu wengine.  Unaweza hata kusahau kwenda kwenye miadi kwa vile ulisahau kitu kama hicho.
Kupungua kwa nguvu ya kumbukumbu kunaweza kutokea katika umri wowote lakini hili hutia wasiwasi zaidi tunavyozidi kuzeeka kwa vile huwa tunahofia kwamba ni aina fulani ya kupungua kwa nguvu ya akili na ufahamu.
Ukweli ni kwamba, kupungua kwa kiasi kikubwa cha kumbukumbu kwa wazee ni suala linalohusu akili kutofanya kazi kikamilifu, majeraha katika ubongo, kuchanganyikiwa, ugonjwa au madhara ya ubongo yanayofanya mhusika kushindwa kwa kiasi kikubwa kuutawala mwili wake (Alzheimer’s Syndrome).
Matatizo mengi ya kupoteza fahamu wakati wa uzee yanaonesha mabadiliko katika muundo na ufanyaji kazi wa ubongo.  Mabadiliko haya hupunguza nguvu ya ufahamu, humfanya mhusika awe na matatizo katika kujifunza kitu kipya kwa haraka.
Hata hivyo, kutokana na utafiti  wa miongo kadhaa,  kuna njia mbalimbali tunazoweza kutumia kulinda na kuhuisha akili zetu.  Zifuatazo ni njia saba ambazo unaweza kuzijaribu kukabiliana na tatizo hili.
1. Endelea kujifunza
Kiwango cha juu cha elimu kinahusiana na akili inavyofanya kazi vyema zaidi wakati wa uzee.  Wataalam hufikiri kwamba elimu ya juu zaidi inaweza kusaidia kuifanya kumbukumbu iwe na nguvu kwa vile inamfanya mtu aitumie akili yake kila mara.
Inaaminika kwamba, kuupa ubongo wako changamoto za kisomi huifanya akili yako kuwa changamfu na kuchochea mfumo wake wa mawasiliano. 
Ili kuipa akili yako uhai zaidi, soma vitabu, cheza michezo angalau ile ya kutumia mahesabu, andika historia ya maisha yako, fanya chemsha bongo mbalimbali, ingia darasani na soma chochote, jiingize kwenye muziki au sanaa yoyote au angalau  fanya shughuli za bustani.
Ukiwa kazini pendekeza au jitolee kufanya kazi ambayo inajumuisha ujuzi ambao huwa huutumii kila mara.
Kumbuka kwamba kujenga na kuendeleza nguvu ya ubongo wako ni jambo ambalo linaendelea maishani, hivyo hakikisha unaendelea kujifunza mambo mapya kila siku.
2. Tumia ufahamu wako wote
Unavyotumia ufahamu wako wote katika kujifunza jambo fulani ndivyo akili yako itakavyokuwa na uwezo wa kutunza kumbukumbu.
Katika utafiti mmoja, wazee walionyesha taswira kadhaa zilizoambatana na harufu fulani.  Hawakuulizwa ni nini walikiona, lakini baadaye walionyeshwa taswira kadhaa, bila ya harufu, na baadaye wakaulizwa ni nini walikuwa wamekiona hapo mwanzo.
Waliweza kukumbuka picha zote zilizokuwa na harufu husika, hususan zile zilizokuwa na harufu za kuvutia.
Hii ilionyesha kwamba akili yenye kunasa harufu ilikuwa imefanya kazi inayotakiwa wakati wazee hao walipotazama picha hizo zikiwa sambamba na harufu husika. 
Mnaso wa harufu pamoja na picha uliwasaidia kukumbuka kwa mara ya pili walipoletwa picha zile zile ingawa kwa mara hiyo picha hazikuambatanishwa na harufu.   
HAKIKISHA unatumia nguvu zako zote za ufahamu hasa katika mambo ambayo ni mapya kwako.    Kwa mfano, jaribu kufikiria vitu vinavyohusika katika utayarishaji wa chakula kwenye mgahawa wakati unaposikia harufu yake au ladha yake.
Vilevile, fanya hivyo kwa vyombo vipya unavyovitumia, kwa kuona unaweza kuvikumbuka kwa ufahamu upi, ikiwa ni pamoja na harufu yake au sauti zake.
3. Jiamini
Dhana za kufikirika  kuhusu uzee zinaweza kusababisha kupungua au kwisha kwa kumbukumbu.  Watu wenye umri wa wastani au wazee huweza kupata matatizo ya kumbukumbu iwapo wataamini kwamba kuzeeka ni kupungukiwa na nguvu ya kumbukumbu.
Watu wanaoamini kwamba kumbukumbu yao ni dhaifu ni dhahiri watajikuta wana upungufu huo. Iwapo utaamini kwamba unaweza kuimarisha kumbukumbu yako na kufanyia kazi imani hiyo, utakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kuimarisha akili yako.
4. Upunguzie mzigo ubongo wako
Ikiwa hutaki kutumia nguvu katika kukumbuka ulipoweka funguo zao au siku aliyozaliwa mjukuu wako wa kike, ni vyema ukajikita katika kujifunza mambo mengine mapya na muhimu. Katika hili tumia kalenda mbalimbali, ratiba za mipango mbalimbali, ramani, orodha za bidhaa madukani, mafaili au vitabu vya anwani ili kupata habari unazozitaka.
Panga mahali maalum nyumbani kwako utakapoweka miwani yako, pochi ya fedha, funguo na vitu vingine unavyovitumia kila mara. Ondoa mrundikano wa vitu usivyotumia ofisini mwako ili uweze kuviona vitu ambavyo utataka kukumbuka vilipo.

5. Kirudie kitu unachotaka kukijua
Ukitaka kukumbuka kitu ambacho umekisikia, kukisoma au kukifikiria, basi kirudie kwa kukitaja kwa sauti au kukiandika. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unaimarisha kumbukumbu yako.
Kwa mfano, iwapo utakuwa umeambiwa jina la mtu fulani, basi litumie wakati unaongea naye.  Kwa mfano: “Hivi, John, ulikutana na Camille wapi?”
Iwapo utaweka kitu chako sehemu fulani ambapo si pa kawaida, basi jiambie kwa sauti ulipokiweka. Vilevile, ukiambiwa kitu, usisite kumwambia mtu akirudie tena kukuambia lengo likiwa ni kuufanya ubongo wako unakiri barabara.

6. Panga muda wa kujifunza
Kurudia kitu kwa kukitaja ni njia nzuri ya kujifunza ikifanyika kwa muda fulani. Si vyema kurudia kutaja kitu mara nyingi katika muda mfupi kama vile unakariri kwa ajili ya mtihani.
Badala yake, rudia kujifunza masuala muhimu ya kitu husika kwa muda mrefu zaidi kama vile mara moja katika saa moja, na baadaye kila baada ya saa chache, na kisha kila siku.
Kupanga muda wa kujifunza ni vyema zaidi unapojaribu kupata habari ngumu kama vile maelezo ya jukumu la kazi mpya.
Utafiti unaonyesha kwamba kujifunza kitu kilekile kwa muda uliopangwa maalum huimarisha kumbukumbu kwa watu walio na afya za kawaida na wale wenye matatizo ya utambuzi.
  


2 comments: