Wednesday 17 September 2014

MAGONJWA YANAYO ADHIRI LISHE KWA BINADAMU



 KIMSINGI magonjwa yote yanaathiri lishe. Hata hivyo, makala hii inazungumzia magonjwa matano ambayo athari yake juu ya lishe ni kubwa, magonjwa hayo ni kuharisha, surua, maleria, minyoo na ukimwi (AIDS). 

Kuhara: 
Ugonjwa wa kuharisha unasababishwa na vidudu kwa njia ya chakula au maji. Yaani mtu akinywa au kula chakula chenye vijidudu vyenye kuambukiza ugonjwa wa kuharisha, mtu huyo atapata ugonjwa huo. 
Kuharisha hasa kwa kipindi cha zaidi ya wiki moja ni sababu kubwa ya lishe duni kwa watoto wadogo na pia kwa watu wazima. Hii ni kwa sababu, kuharisha kuna punguza uwezo wa mwili kunyonya chakula kilichosagwa katika utumbo. 

Pia kuharisha kunapoteza virutubisho na kunamfanya mtu kukosa hamu ya kula chakula. Kadiri mtoto (au mtu mzima) anayeharisha anavyozidi kukosa mlo kamili ndivyo atakavyozidi kuharisha na anaweza kupoteza maisha kwa kipindi kifupi. 
Namna ya kuikabili hali hiyo ni kuwa, wagonjwa wapelekwe hospitali haraka iwezekanavyo. Vile vile, kina mama wawanyonyeshe watoto wao maziwa ya mama na hasa yale ya kwanza (Colostrum) kwa sababu huongeza kinga kwa mtoto. 
Sambamba na hatua hizo, wagonjwa wa kuharisha wapatiwe chakula bora ili miili yao iweze kupata virutubisho na hivyo kuziba pengo la vile vilivyopotea na hatimaye miili hiyo iweze kujikarabati (kujitengeneza upya). 
Mbali na hatua hizo, wananchi waimarishe usafi wa vyakula, maji hasa ya kunywa na mazingira kwa ujumla. 

Surua: 




Ugonjwa wa surua huongeza mahitaji ya vitamini A mwilini. Kwa hiyo, mtu mwenye ugonjwa huo mara nyingi mwili wake huwa na upungufu wa vitamini A. Upungufu wa vitamini A mwilini una madhara mengi kiafya. Moja ya madhara hayo ni kutokuona vizuri au upofu kabisa. 
Surua huharibu kinga ya mtoto (au mtu mzima kama atapata ugonjwa huo) na ndiyo maana watoto wengi hushikwa na maradhi mengine baada ya kuugua surua. 
Ili kukabiliana na janga la Surua, watoto wadogo lazima wapelekwe hospitali (au Kliniki) ili wapatiwe chanjo siyo tu ya surua bali pia hata ya magonjwa mengine. 
Sawia na juhudi hizo, wagonjwa wa sura wapatiwe mlo mzuri na wakutosha na wenye ziada ya dozi ya vitamini A. 

Maleria: 




Maleria ni ugonjwa unaoharibu chembe chembe za damu (RBC) na hivyo unasababisha upungufu wa damu mwili. RBC hutumika kusafilisha hewa ya kuunguzia chakula mwilini. Kwa hiyo, upungufu wa damu huathiri lishe. 
Maleria ni ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi hasa barani Afrika. Kwa mama mwenye mimba, maleria (kama haikutibiwa) inaweza kuiharibu mimba hiyo au inaweza kusababisha kuzaliwa mtoto mwenye uzito mdogo. 
Kuna njia mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa maleria. Miongoni mwa njia hizo ni kumdhibiti mbu. Usafi wa mazingira na utumiaji wa vyandarua ni miongoni mwa njia zinazoweza kumdhibiti mbu kwa ufanisi zaidi na kwa gharama ndogo ambayo pia haiharibu afya ya binadamu. 
Ikumbukwe kuwa kuna vyandarua vilivyotiwa dawa ya kuua mbu. Mashirika mbalimbali yanawahimiza wananchi kutumia vyandarua hivyo, njia za kisayansi huwa na faida pia hasara. 
Hivyo basi, utumiaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa nao unamadhara yake. Njia bora ni kuyaweka mazingira katika hali ya usafi na kutumia vyandarua ambavyo havikutiwa dawa. 
Pia ni vema kujiepusha na utumiaji wa dawa ya mbu ya kuchoma au ya kupuliza (spray) au ile ya kujipaka. Mabingwa wa mazingira wanatufundisha kuwa njia za kibaolojia ni nzuri kuliko zile za kikemikali. Japo ukweli huo unaweza kuwaudhi wenye viwanda vya madawa ya mbu! 
Sambamba na hatua za hapo juu, wagonjwa wa maleria lazima wapelekwe hospitali ili wakapatiwe tiba sahihi. 
Vile vile lazima wapatiwe chakula bora na ziada ya vyakula vyenye kuongeza damu mwilini. Mfano wa vyakula hivyo ni maharage, njegele, soya, nyama, samaki, mayai, maziwa n.k. Ili damu iweze kutengenezwa mwilini. Vyakula vingine kama vile matunda na mboga za majani ni muhimu. 



Minyoo ya tumboni: 




Tumbo la binadamu linaweza kuwa makazi mazuri ya minyoo. Minyoo hupunguza hamu ya kula kwa aliyenayo. Pia huleta upungufu wa virutubisho mwilini. Yaani minyoo inatumia virutubisho ambavyo ni haki ya mwili. 
Vile vile minyoo husababisha upungufu wa damu mwilini na inaweza kuharibu viungo vingine muhimu mwilini kama vile ini. 
Ili kukabiliana na minyoo, wananchi wadumishe kanuni za afya hasa ile ya utumiaji wa vyoo. Pia watu, watoto wawe wanapimwa mara kwa mara (mfano kila baada ya miezi mitatu) ili kuangalia minyoo, kwa sababu hata kama alipata matibabu sahihi minyoo inaweza kumwingia tena hasa kama hali ya mazingira ni duni. 



Ukimwi: 




Watu wenye ukimwi mara nyingi hupoteza uzito. Hii ni kwa sababu ugonjwa huo hupunguza hamu ya kula na pia huufanya mwili kushindwa kunyonya na kutumia vizuri chakula kilicho sagwa mwilini. 
Kwa hiyo wagonjwa hao wabembelezwe ili waweza kula chakula. Chakula bora kinaongeza nguvu kwa wagonjwa wa ukimwi japo kwa kipindi fulani.  

0 comments:

Post a Comment