Saturday 27 September 2014

JIFUNZE MIONGOZO ZAIDI YA KUKULETEA UTAJIRI


DUNIA imekuwa ndogo kutokana na ukuaji wa sayansi na teknolojia. Katika utafutaji wa maisha yenye mafanikio, ukuaji huu wa teknolojia hauwezi kukwepeka. Hata hivyo,  mbinu na njia za kukuongoza katika kukuletea utajiri zimekuwa zikibadilika na kuongezeka kila siku, hali inayosababishwa pamoja na mambo mengine, mazingira uliyopo.
Zifuatazo ni mbinu au njia zaidi ambazo endapo zitafuatwa zitakuwezesha kuufikia utajiri mapema zaidi kuliko unavyotarajia.
1: Badilisha mtazamo wako kuhusu pesa
Watu wengi kwa ujumla wao wangependa kuwa na uhusiano na watu wenye pesa, ingawa baadhi yao pia hawapendi. Licha ya kuwa wapo wanaowachukia watu wenye hela, lakini wao wenyewe binafsi wanatumia muda mwingi kuzitafuta. Sababu kubwa inayofanya watu washindwe katika mikakati yao ya upatikanaji wa fedha ni kutojua kwao asili ya hela na jinsi zinavyofanya kazi.
Fedha, kama ilivyo kwa mtu, ni kitu kinachoishi. Unapoamka asubuhi na kwenda kazini, unauza bidhaa ambayo ni wewe mwenyewe kwa maana ya ajira yako. Unapogundua kwamba kila siku asubuhi mali zako zinaamka na zinafanya kazi kama unavyofanya wewe, unafungua njia kubwa kabisa ya maisha yako.
Kila senti unayohifadhi ni kama mwajiriwa. Baada ya muda, lengo lako ni kuwafanya waajiriwa kuwa wengi na wanaofanya kazi sana na kwa jinsi ilivyo, watasababisha uwe na fedha za kutosha zaidi. Utakapokuwa umefanikiwa vizuri, sasa hautakuwa na haja ya kuuza nguvu zako tena, unaweza kuishi nje ya ajira ukiwa unategemea uwekezaji wako.
2: Jenga uelewa wa nguvu ya hela ndogo
Kosa moja kubwa linalofanywa na watu wengi ni kuwa wanafikiria kuanza na fedha nyingi kama ilivyo kwa jeshi la Napoleon. Wanasumbuliwa na ugonjwa wa kimawazo wa kusema ‘hazitoshi’, kwamba kama hawataanza na kiasi labda cha shilingi laki moja au tano katika uwekezaji, hawataweza kuwa matajiri.
Kitu kimoja ambacho watu hawa hawajui ni kwamba yale majeshi yenye askari wengi yalianza kujengwa na askari mmoja, hiyo ikitegemea pia uwezo wao kifedha.
Rafiki yangu mmoja anamuoa mwanamke mmoja aliyefanya kazi kama muosha vyombo na baadaye akawa muosha vyupa. Mwanamke huyo aliweka kila hela aliyopata ingawa kwa wakati ule hakuwa na fedha zozote. Hivi sasa anatisha, akaunti yake inasoma mabilioni ya shilingi, lakini ikumbukwe kuwa alianza na uwekezaji mdogo tu. Sisemi kwamba na wewe unatakiwa kupitia njia hii, lakini ninachotaka upate somo kuwa chochote kidogo, kina thamani kubwa.
3: Kwa kila senti unayoweka, unanunua uhuru wako
Unapoweka jambo hili katika mahesabu, unatambua kwamba ni kwa jinsi gani kutumia shilingi 20,000 hapa na 40 kule kunavyoweza kuleta tofauti kubwa baada ya muda.
Kama tujuavyo kwamba fedha zina uwezo mkubwa wa kufanya kazi popote ulipo, kwa kadiri unavyozihifadhi, ndivyo zitakavyokua kwa haraka. Ukiwa na fedha nyingi, ndivyo unavyopata uhuru zaidi, uhuru wa kukaa nyumbani na watoto wako, uhuru wa kustaafu mapema, uhuru wa kusafiri popote duniani na hata uhuru wa kuamua kuacha kazi.
Kama unacho chanzo cha mapato, inawezekana kabisa kuanza kutengeneza utajiri leo. Unaweza kuwa unaweka shilingi elfu tano au kumi kwa sasa, lakini kila wekezo la fedha hizo, ni msingi imara sana wa uhuru wako kifedha.
4: Unawajibika kwa maisha yako yalipo
Miaka kadhaa nyuma, rafiki yangu mmoja aliniambia asingeweza kuwekeza katika kilimo na ufugaji kwa sababu atalazimika kusubiri kwa miaka kumi ili aweze kuwa tajiri, alidai asingeweza kuzifaidi fedha zake. Ujumbe kwa neno hili ni kwamba jamaa aliamini atakuwa hai baada ya miaka kumi.
Swali hapa ni kama utakuwa katika nafasi nzuri kimaisha utakapofika wakati huo au la. Pale ulipo leo ni matokeo ya jumla ya maamuzi uliyofanya siku za nyuma. Kwa nini usipange jinsi maisha yako yatakavyokuwa siku za baadaye na sasa hivi?

0 comments:

Post a Comment