- Ubongo una mfumo wa mawasiliano ya kustajabisha kama makala haya yanavyochambua.
Ubongo ni kiungo cha aina yake katika mwili wa binadamu. Ubongo hutoa kila fikira, tendo, kumbukumbu, hisia na uzoefu wa kidunia.
Kwa mujibu wa jarida la New Scientist, Ubongo wa binadamu umetengenezwa na viini laini vilivyo katika mfumo kama mafuta mazito yaliyoganda.
Ubongo umegawanyika katika sehemu tatu, ya mbele, kati na ya nyuma. Sehemu hizi zinazofanya kazi kwa pamoja japo kila sehemu ina viini vinavyofanya kazi za kipekee katika mwili.
Jarida la Live Science la Mei 6, 2013 linabainisha kuwa ubongo wa binadamu ni mkubwa kuliko ubongo wa kiumbe kingine kwa uwiano wa ukubwa wa mwili.
Ubongo wa binadamu una uzito wa kilo 1.4 sawa na paundi tatu ama gramu 1,300 hadi 1,400 wenye seli za mawasiliano (neurons) bilioni 100 ambazo ndani yake maagizo ya ubongo hupitia kwa kasi katika mfumo wa mapigo au kama msukumo wa umeme.
Msukumo huu husafiri kwa kasi ya zaidi ya kilometa 400 kwa saa. Ubongo hutoa na kupokea mamia ya misisimko ya ujumbe wa fahamu kila sekunde.
Hudhibiti kila kitendo cha mwili, kama kutembea, viungo na misuli ya mwili na kupumua. Kadhalika ubongo unadhibiti shughuli zote za akili, kama kufikiri na kukumbuka mambo.
Ubongo unatumia nguvu nyingi kuliko kiungo kingine chochote mwilini na kwamba huchukua moja ya tano ya chakula anachotumia binadamu.
Tafiti zinabainisha kuwa uwezo wa akili ya mtu mwenye umri wa miaka 100 aliye na kumbukumbu nzuri, unaweza kuwakilishwa na kompyuta zaidi ya 10 zilizo na uwezo wa biti 64. Kompyuta ya kawaida ina uwezo wa kufanya kazi kwa biti 64.
Hata hivyo wanasayansi wengine wanasema ubongo una uwezo wa kufanya mambo mengi zaidi na inakadiriwa kuwa biti 11 trilioni kwa sekunde hii ikijumuisha njia zaidi ya 125 milioni zinazowasilisha taarifa.
Kiwango hiki kinaweza kufikiwa kwa miaka 35. Lakini, uwakilishi huu ni wa uwezo wa kumbukumbu si ule uwezo wote wa mwendelezo wa ubunifu wa mawazo na silika.
Kitabu cha “Facts about Human Brain” kinaeleza kuwa ubongo peke yake hauwezi kupata maumivu lakini ni kituo cha taarifa ya maumivu yanayotokea mwilini. Kwamba mtu anapoumia kidole maumivu yanayosikika ni mapokeo kutoka kwenye ubongo. Pamoja na uwezo mkubwa wa ubongo, bado mtu anaweza kufikiria jambo moja tu kwa wakati mmoja.
Moja ya nne ya ubongo hutumika kudhibiti uimara wa macho. Kwamba tunaona kwa ubongo wetu, macho huwa kama kamera tu.
Mfupa wa Cranium ndio unaoutunza ubongo kichwani na ambao kwa wastani mtu mzima mwanaume ana ubongo wenye uzito wa gramu 1,375.
Kwa mujibu wa taarifa za mitandao, ubongo wa mtunzi wa riwaya ndefu wa Russia bwana Turgenev, ulikuwa na uzito wa gram 2021, wakati ubongo wa Mfaransa maarufu Gambetta ulikuwa na uzito wa gram 1294.
Ubongo wa wanawake ni mdogo kuliko wa wanaume. Ubongo wa Tembo una uzito wa gramu 10,000.
Kwa kulinganisha na mwili, Nyangumi ana ubongo mdogo zaidi kuliko ilivyo kwa binadamu. Hii inampa binadamu nafasi kubwa ya kuwa na maarifa na akili zaidi.
Tangu ilipogundulika kuwa wastani wa ubongo wa “nyani mbilikimo” ni moja ya gramu 27 ya mwili wake na nyani wa “Capuchin” ana wastani wa gramu 1 ya uzito wa gram 17.5 ya mwili wake, wakati wastani wa ubongo wa mtu ni gramu moja kwa gramu 44 ya mwili.
Mwandishi Chudler Eric katika kitabu chake “Brain Facts and Figures,” anasema ubongo hufanya kazi zaidi usiku kuliko mchana.
Kwamba mtu hudhani kazi zote, hesabu na mwingiliano wa majukumu yanayofanywa mchana kutwa hutumia nguvu kubwa ya ubongo kufanya kazi lakini kumbe ni kinyume chake.
Ubongo hutumia nguvu kidogo sana wakati wa mchana. Ajabu mtu anapolala usiku, anaposinzia tu ubongo huanza kufanya kazi kubwa zaidi.
Wanasayansi wameshindwa kutambua ni kwa nini hali hii hutokea hivi kwa ubongo kufanya kazi zaidi mtu anapolala na kumpa usingizi na ndoto nzuri za ajabu.
Utafiti wa Chuo cha “Nursing Assistant Centre” cha Marekani unathibitisha kuwa ubongo wa mtu mzima ni karibu asilimia mbili ya uzito wote wa mwili na kwamba asilimia 75 ya ujazo wa ubongo ni maji. Ubongo wa tembo una uzito wa gramu 6,000 wakati uzito wa ubongo wa paka ni gramu 30.
0 comments:
Post a Comment