Friday 29 August 2014

MATATIZO KATIKA MFUMO WA CHAKULA (GASTRO INTESTINAL DISORDERS)



Jinsi tatizo linavyojitokeza
Matatizo yanayotokea katika mfumo huu ni kama vile vidonda, uvimbe na kasoro za kuzaliwa nazo.
Vidonda vinaweza kuwa kinywani, kooni kwenye njia ya kupitishia chakula, tumboni hadi katika mfuko wa haja kubwa na njia yake ya kutolea. Uvimbe pia hutokea maeneo hayo yote tuliyoyaona na uvimbe huu unaweza kuwa kansa au usiwe na kansa.
Kasoro za kuzaliwa nazo ni kama vile kuziba  kwa njia ya kupitishia chakula, hitilafu katika mfumo wa chakula na njia ya haja kubwa.
Matatizo pia huvikabili baadhi ya vipimo visaidizi vya mfumo wa chakula kama ini na kongosho ambavyo pia vikipatwa na matatizo huathiri mfumo mzima wa chakula na mwili kwa ujumla.
Ini likishindwa kufanya kazi mgonjwa huvimba tumbo na miguu, kongosho likiwa na tatizo mgonjwa hupata matatizo ya kuongezeka kwa sukari kwa kuwa uhathiri vichocheo vya insulin.
Ini na kongosho vinaweza kuvimba au kuwa na saratani.
Magonjwa makubwa yanayoathiri mfumo wa chakula ni vidonda vya tumbo, kufunga kupata haja kubwa ambayo ni dalili tu au ishara za magonjwa mbalimbali katika sehemu hiyo na uvimbe katika njia ya haja kubwa.
Matatizo haya ndiyo huwasumbua watu wengi ingawa pia yapo mengi.
Yapo mengine ambayo ni madogomadogo, mfano kuwa na vidonda mdomoni, kooni na maumivu na muwasho katika njia ya haja kubwa.
Dalili za matatizo haya
Matatizo katika mfumo wa chakula kwa ujumla wake huambatana na dalili mbalimbali kuanzia kinywani. Mtu hulalamika vidonda mdomoni, kutoa harufu mbaya kinywani, maumivu ya meno na kushindwa kumeza chakula, kupoteza hamu ya kula na kichefuchefu.
Wengine huhisi mdomo unakuwa mchungu pale wanapoamka asubuhi na mate kujaa mdomoni.
Dalili hizi zinaweza kuhusiana na matatizo ya tumboni upande wa juu ambayo ni kuhisi kiungulia au moto kifuani, maumivu ya chembe ya moyo, maumivu ya mgongo upande wa juu  usawa wa kifua.
Maumivu husambaa hadi usawa wa kitovu na mgonjwa hujihisi kuchoka sana na viungo vinauma.
Mgonjwa mwenye dalili hizi huhangaika kupima malaria, taifodi lakini anatumia dawa kwa muda mrefu bila mafanikio.
Dalili hizi pia huwapata watu ambao wanaanza kupata dalili za awali za ugonjwa wa kisukari, huhangaika nao kupima malaria, utiai, taifodi na kutibu bila mafanikio.
Maumivu pia yanaweza kuanzia kitovuni kushuka chini au maumivu chini ya kitovu na kusababisha kufunga choo. Pia anaweza kupata choo kigumu kikiwa kama cha mbuzi na wakati mwingine mgonjwa anaweza kuharisha, choo kikubwa kinaweza kuwa na harufu mbaya, mkojo unakuwa wa njano sana na wa moto na wakati mwingine maumivu.
Pamoja na maumivu ya tumbo na dalili nyingine, mgonjwa hulalamika mara kwa mara na kutoa hewa kupitia haja kubwa.Maumivu husambaa katika nyonga, kiuno na miguu.
Uvimbe kwenye njia ya haja kubwa pia huambatana na dalili hizo za maumivu ya kiuno na nyonga kutegemea na ukubwa wa uvimbe na aina ya uvimbe. Katika uvimbe huo damu inaweza kutoka wakati wa kujisaidia.
Nini cha kufanya?
Endapo una mojawapo ya dalili hizi ni vema uwahi katika hospitali ya wilaya au mkoa kwa uchunguzi wa kina.
Hizi ni baadhi tu ya dalili za matatizo katika mfumo wa chakula, ukiwahi hospitali ndipo uchunguzi utafanyika kuona chanzo cha tatizo.
Athari za matatizo haya ni mgonjwa kuchoka sana, mwili kudhoofika, kupoteza hamu ya tendo la ndoa, kupungukiwa nguvu za kiume, watoto na vijana kushindwa kutekeleza majukumu yao shuleni na hata kazini. Wahi hospitali.

0 comments:

Post a Comment